Hakuna mtu anayeweza kusimama kwa ujasiri na kujipiga kifua mara nyingi nakusema nimeyaweza haya yote kama jeshi la mtu mmoja. Mtu huyu anayesema haya basi hajui maisha ni muunganiko na hakuna mtu awezaye kujisifu na kusema kafanya yote mwenyewe bila kuhitaji watu wengine. Utasema umefanikiwa kibiashara lakini je bila wateja kuja katika biashara yako ungefanikiwa ? Kila kitu unachokifanya na kufanikiwa jua kuna pahala umehitaji msaada au umetegemea watu wengine. Mf umenunua gari na kuweza kujisifu kuwa unamiliki gari lakini ukiangalia kwa ndani si wewe uliyefanya ubunifu huo wa gari bali pana watu ambao wametengeneza na wewe umepata matokeo tu ya ubunifu wao. Huwezi jidai hapa kusema unaweza kila kitu mwenyewe bila kuhitaji wengine au kutegemea wengine. Maisha yetu ni muunganiko wa vitu na vyote vyakaa katika umoja siku zote. Kuna msemo rahisi na huwa tunausikia sana “Umoja ni Nguvu”. Umoja ni nguvu kwa maana ya maisha unahitaji nguvu kutoka kwa watu wengine, utawahitaji wengine na utawategemea wengine ili katika umoja huo upate matokeo makubwa. Watu ambao wanaona ni wao wamefanikiwa kwa nguvu zao basi husahau mchango wa watu wengine ambao walijitoa kwa ajili yake. Huwezi kusimama mwenyewe katika safari ya maisha. Ikiwa hata maiti husaidiwa basi ni zaidi ya mtu aliye hai ambaye kila hatua ya maisha yake inahitaji watu na kutegemea watu. Hili lilionwa toka zamani katika maisha ya wastoa kama Marcus Aurelius ambaye katika maandiko ya notibuku yake anaonesha namna ya kutambua mchango wa kila mtu katika maisha yake kuanzia utoto hadi utu uzima ikihusisha vipindi mbalimbali vya maisha. Hili linamshawishi kuandika kuwa tumeumbwa kwa ajili ya wengine. Marcus Aurelius anasema “Meditate often on the interconnectedness and mutual interdependence of all things in the universe. For in a sense, all things are mutually woven together and therefore have an affinity for each other – Marcus Aurelius. Hii ikiwa na tafsiri iso rasmi “Tafakari nyakati zote juu ya muunganiko wetu sisi binadamu na mategemeano ya kila kitu katika asili. Jua kuwa kwa namna moja tunaunganishwa na kutegemeana kwa ukaribu kati ya mtu mmoja na mwingine”. Ni maneno mazito na fikirishi sana. Ubinafsi wa watu na kuona wanaweza kufanya kila kitu ndiko kunachelewesha watu wengi kufanikiwa. Watu ambao wanakuwa wazito kuhitaji msaada au kutegemea watu wengine hawajajua maisha kwa upana. Kwa kuwa hakuna ambaye kapewa kila kitu ndani yake isipokuwa vingine vingi vipo kwa watu wengine. Hili ndilo ambalo linatualika kutegemeana na kuhitajiana maisha yetu ya kila siku ili yaende. Ishi siku zote katika kuwa sehemu ya muunganiko wa kutegemeana na kuhitajiana. Kuna vitu vingine utavipata kwa wengine ukiwa tayari kujitoa na kujua maisha ni mategemeano na kuhitajiana. Tumeumbwa kuhitajiana kama ulivyo mwili na viungo vyake vinavyofanya kazi katika kusaidiana na kushirikiana. |
BADILI FIKRA.FIKIRI TOFAUTI .BADILI MAISHA.JITAMBUE .JIFUNZE ELIMU YA SAIKOLOJIA,TEOLOJIA , FEDHA ,UTAMBUZI(SELF HELP EDUCATION),FALSAFA YA MAISHA,MAISHA NA MAFANIKIO,BIASHARA / UJASIRIAMALI.FURAHIA WASAA WAKO NA MAISHA NA MAFANIKIO BLOGU.THIS IS THE COMMUNITY CAPACITY BUILDING BLOG.ENJOY THE BLOG.STRETCH YOUR MIND. YOU CAN CHANGE YOUR LIFE FOR EVER. YOU CAN ACHIEVE EXCELLENCE.YOU CAN MAKE A DIFFERENCE.
Saturday, January 23, 2021
TUNATEGEMEANA NA TUNAHITAJIANA KILA SIKU ILI MAISHA YAENDE.
Saturday, January 2, 2021
JINSI UMASKINI UNAVYOHARIBU AKILI NA JINSI YA KUEPUKA MTEGO WA UMASKINI.
Umasikini siyo tu ni mzigo na kikwazo kwa mtu kuwa na maisha bora na yenye uhuru, bali pia ni laana ambayo inamfanya anase kwenye maisha ambayo hawezi kujinasua.
Utafiti ambao umewahi kufanywa nchini Marekani na India unaonesha kwamba umasikini huwa unaharibu akili ya mtu.
Utafiti huo ulionesha kwamba wale wanaoishi kwa umasikini, wana upungufu wa alama 13 za kipimo cha akili (IQ) ukilinganisha na wale ambao hawaishi kwenye umasikini.
Kwa lugha rahisi na ya kueleweka vizuri ni kwamba umasikini unawafanya watu kuzidi kuwa wajinga.
Swali unaloweza kujiuliza ni kwa namna gani umasikini unaharibu akili za watu na kuwafanya kuwa wajinga?
Jibu liko wazi, masikini anakuwa ametingwa zaidi na mawazo ya hali ngumu anayokuwa anapitia, hivyo akili yake inakuwa imechoka muda wote. Inapokuja kwenye uhitaji wa kufikiri mambo makubwa na magumu, masikini hawezi kufikiri kwa usahihi, kwa kuwa akili yake tayari imeshachoka.
Chukua mfano wa watu wawili, wana elimu sana na wanafanya kazi ya aina moja. Mtu A ni tajiri na B ni masikini. Mtu A ameamka asubuhi, kapata kifungua kinywa kizuri, kaingia kwenye gari yake binafsi na kwenda kazini. Mtu B ameamka hana hata kifungua kinywa, anaenda kazini kwa kutumia usafiri wa umma ambao ni wa shida na hajui siku hiyo atakula nini, wakati huo huo kuna watu wanamdai na wanamtafuta sana. Watu hao wawili wanapewa jukumu moja la kukamilisha, ambalo linahitaji utulivu wa akili ili kulikamilisha, unafikiri yupi atalikamilisha kwa umakini?
Unajionea mwenyewe hapo, jinsi ambavyo umasikini unakuwa mzigo ambao unaharibu akili ya mtu na kumfanya awe mjinga.
Umasikini unapunguza uwezo wa mtu kufikiri na kufanya maamuzi kwa sababu muda mwingi akili yake inakuwa imetingwa na fikra na hofu mbalimbali.
Mbaya zaidi sasa, na hapa ndipo ilipo laana ya umasikini, ni pale uwezo mdogo wa kufikiri unapomfanya mtu afanye maamuzi mabovu zaidi na yanayomfanya abaki kwenye umasikini.
Tuendelee na mfano wa mtu B, ambaye anafikiria siku yake inaishaje, maana mshahara umeshaisha na mwezi ndiyo kwanza uko katikati. Anasikia kuna mtu anatoa mkopo wa haraka ila una riba kubwa. Kwa sababu anachohofia zaidi ni fedha na hawezi kufikiri kwa usahihi, anajikuta anachukua mkopo huo. Anakuja kulipa mkopo kwa riba kubwa, kitu kinachopunguza kipato chake zaidi.
Maamuzi mengi ambayo mtu anasukumwa kuyafanya akiwa masikini huishia kuwa maamuzi ya kumuumiza zaidi na kumfanya abaki kwenye umasikini.
Unaondokaje kwenye mtego na laana hii ya umasikini?
Umejionea hapo jinsi umasikini unavyoharibu akili na kumnasa mtu kwenye umasikini zaidi.
Kama bado hujafikia uhuru wa kifedha, kama bado unategemea kipato unacholipwa kwa kufanya kazi au biashara ndiyo uendeshe maisha yako, haijalishi kipato hicho ni kikubwa kiasi gani, upo kwenye hii hatari.
Hivyo hatua muhimu kwako kuchukua ni kujijengea uhuru wa kifedha. Na hapa kuna maeneo sita muhimu ya kufanyia kazi ili kuondoka kwenye mtego na laana ya umasikini.
Eneo la kwanza ni kuongeza kipato chako. Kipato chochote unachoingiza sasa hakiwezi kukutosha, gharama za maisha zinachukua sehemu kubwa ya kipato chako. Hivyo pambana kuongeza kipato chako. Kama umeajiriwa anzisha biashara ya pembeni. Kama upo kwenye biashara ongeza huduma na bidhaa zaidi na wafikie wateja wengi zaidi. Kwa kipato chochote unachoingiza sasa, pambana kukikuza zaidi.
Eneo la pili ni kudhibiti matumizi yako. Matumizi huwa yana tabia ya kukua kadiri kipato kinavyokua. Usipoyadhibiti, ongezeko la kipato ulilopambana nalo halitaleta tofauti kwenye maisha yako, badala yake litakuwa limekuchimbia kwenye umasikini zaidi. Dhibiti matumizi yako kwa kuhangaika na yale ya msingi pekee, hasa kama unaanzia kwenye umasikini wa chini kabisa.
Eneo la tatu ni kuwa na akiba ya dharura ya miezi 6 mpaka 12. Kama unaishi maisha ya mkono kwenda kinywani, yaani unafanya kazi, unaingiza kipato na unakitumia chote, basi upo kwenye hatari ya umasikini kuharibu akili yako zaidi. ukipata dharura yoyote ile, iwe ni kazi kusimama au biashara kuyumba, utaanguka vibaya mno. Hakikisha unakuwa na akiba ya kukuwezesha kuendesha maisha yako kwa miezi sita mpaka 12 hata kama hutakuwa na kipato kabisa. Unapokuwa na akiba ya aina hii, unapata utulivu mkubwa ndani yako na kuweza kufanya maamuzi sahihi kwako. Mfano kama umefukuzwa kazi na huna akiba, utalazimika kufanya kazi yoyote hata kama haikulipi, kwa sababu unataka kipato cha kuendesha maisha. Lakini kama umefukuzwa kazi na una akiba ya miezi 12 ya kuendesha maisha, unaweza kusubiri kwa muda mpaka upate kazi nzuri, maana akiba ya kuendesha maisha ipo.
Eneo la nne ni uwekezaji. Huwezi kufanya kazi muda wote na kila muda ambao hufanyi kazi hunufaiki. Unapaswa kuwa na njia ya kuingiza kipato hata kama hufanyi kazi moja kwa moja. Na njia ya kufanya hivyo ni kuwa na uwekezaji ambao unazalisha faida na kukua thamani kadiri muda unavyokwenda. Unapokuwa na uwekezaji unaozalisha faida kubwa ya kukuwezesha kuendesha maisha yako hata kama hufanyi kazi moja kwa moja, unakuwa umefikia uhuru wa kifedha.
Eneo la tano ni kulipa madeni ambayo unayo. Kama umekopa, pambana kulipa madeni yako kwa kutumia ongezeko la kipato ulilofanyia kazi.
Eneo la sita ni kuacha kukopa. Usikope tena, rahisisha maisha yako, punguza yasiyo muhimu na kama kitu huwezi kukimudu jipe muda. Vitu vingi unavyoingia kwenye madeni ili kuwa navyo ni vitu ambavyo siyo muhimu sana kwako. Ukiacha kuiga maisha ya wengine na kuchagua kuishi maisha yako, hutahangaika na mikopo inayokusumbua.
Zingatia maeneo hayo sita ili kuweza kuondokana na mtego na laana ya umasikini.
Ndimi KOCHA MWL. JAPHET MASATU , DAR ES SALAAM
( WhatsApp + 255 716 924 136 ) / + 255 755400128 / + 255 688361539
EMAIL : japhetmasatu@gmail.com
Friday, January 1, 2021
JINSI YA KUINUKA BAADA YA KUANGUKA KAMA UMEJAJAIRI.
Karibu kwenye makala ya ushauri wa changamoto mbalimbali zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa tunayotaka.
Kwenye makala ya leo tunakwenda kupata ushauri wa jinsi ya kuinuka na kuendelea na safari baada ya kuanguka kwenye kujiajiri.
Kabla ya kupata ushauri huo, tupate maoni ya msomaji mwenzetu ambaye ametuandikia kuomba ushauri kwenye hilo.
Niliacha kazi nilioajiriwa ili niweze kujiajiri kwenye Kilimo na Ufugaji, toka 2017 lakini mambo mwanzo yalienda sawa ila ,kwa sasa 2020 Nimeanguka kwenye kilimo na mtaji kwa ujumla. Naomba ushauri nifanyeje? - Mdachi K. J.
Msomaji mwenzetu ametushirikisha changamoto yake ya kuanguka kwenye kujiajiri baada ya kuachana na ajira, ambapo mwanzoni mambo yalikwenda vizuri ila baadaye yakabadilika.
Hii ni changamoto ambayo kila ambaye amewahi kupambana kufanikiwa ameshaipitia na ni sehemu ya kupikwa ili uweze kupokea mafanikio makubwa zaidi baadaye.
Anguko ambalo mwenzetu amepata ni darasa kubwa sana kwake kwenye safari ya mafanikio na hasara aliyopata ni ada ya kupata darasa hilo.
Kwa sasa anajua mambo gani akifanya ataanguka na hivyo anapaswa kuepuka kufanya mambo hayo.
Hivyo ushauri wa kwanza na muhimu kabisa kwa yeyote ambaye anapitia magumu au kuanguka ni kutokukata tamaa wala kuangalia kama kitu kibaya. Badala yake ona ni darasa umepitia na kukomazwa ili kuyapokea mafanikio makubwa zaidi baadaye.
Waswahili wanasema kufanya kosa siyo kosa, bali kurudia kosa. Kuna mengi ambayo mtu unakuwa umefanya mpaka ukaanguka. Pia ipo kauli inayosema ujinga ni kufanya jambo lile lile kwa namna ile ile kisha kutegemea matokeo tofauti.
Kwa kuwa hujakata tamaa, unaendelea na kile ambacho ulikuwa umechagua kufanya. Kwa sababu ukilipa ada, lazima uendelee na masomo. Lakini usiendelee kwa kurudia makosa ambayo umeyafanya, ukifanya hivyo utakuwa umepoteza ada yako.
Ushauri wa pili kwenye hili ni kukaa chini na kutafakari kila ulichofanya kwenye mradi wako ulioshindwa. Anza na yale uliyokuwa unafanya wakati mambo yanakwenda vizuri. Kisha nenda kwenye yale ambayo ulikuwa unafanya na mambo yakaenda vibaya. Kisha jua ni mambo gani ambayo hutarudia tena kuyafanya unapoanza mradi wako upya.
Kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja huwa ni chanzo cha kushindwa kwenye yote. Kila kitu kipya unachoanzisha kinakuhitaji mno hasa mwanzoni. Sasa kama unafanya mambo mengi, unatawanya sana nguvu zako na hivyo kila jambo halipati umakini wa kutosha kitu kinachopelekea kushindwa.
Ushauri wa tatu hapa ni kuchagua kitu kimoja tu ambacho utaanza nacho na kuweka umakini wako wote kwenye kitu hicho. Achana na mengine yote, acha kuhangaika na kila fursa inayokuja kwako na kushawishiwa ni bora zaidi. Sikiliza rafiki yangu, fursa bora kwako ni ile uliyoichagua na uko tayari kuifanyia kazi kwa moyo wako wote.
Kama umeamua kulima kitunguu, lima hicho, achana na hadithi kwamba nyanya zinalipa zaidi na kufanya kitunguu na nyanya kwa wakati mmoja. Kama umeamua kufuga kuku fanya hivyo, achana na kelele kwamba sungura au bata mzinga wanalipa zaidi.
Unapokuwa chini, hiyo ndiyo sehemu pekee unayoweza kuanzia. Na uzuri ukiwa chini huna tena pa kuangukia.
Ushauri wa nne hapa ni kuanzia pale ulipo, kuanzia chini kabisa, kuanza kwa hatua ndogo kabisa unayoweza. Kwa kuwa umeshapoteza kila kitu na kwa kuwa umeamua kuanza na kitu kimoja, anza na chochote kilicho ndani ya uwezo wako kwa sasa. Hata kama ni kidogo kiasi gani, wewe anza na pambana kukua kwa kuanzia hapo. Usisubiri mpaka upate uwezo mkubwa wa kuanza, anzia popote pale ulipo sasa. Kama utaanza na sehemu ndogo ya kulima fanya hivyo, kama utaanza na ufugaji kidogo fanya hivyo. Anza kidogo na utazidi kuona fursa za kukua zaidi.
Maisha lazima yaendelee na kama umeanguka kabisa, kuna machaguo mawili, kurudi kwenye ajira itakayokupa msingi wa kuanza tena au kuishi kama mtawa ili kuweza kupambana hapa mwanzoni.
Ushauri wa tano ni kuamua maisha yako yataendeleaje, kwa kuwa umepoteza kila kitu, ina maana hata gharama za kuyaendesha maisha yako huwezi kuzimudu. Hapa unaweza kuchagua kurudi tena kwenye ajira ili upate fedha ya kuendesha maisha yako huku ukijijengea msingi imara zaidi. Au unaweza kuchagua kuishi kama mtawa, kwa kipindi cha mwanzo ambacho unaanza upya, punguza kabisa gharama zako za maisha. Yaani gharamia yale ya msingi tu, mfano chakula na cha kawaida kabisa. Hapa hununui kitu chochote kile cha anasa, yaani ambacho siyo muhimu kabisa. Kwa kufanya hivi unapunguza sana gharama za maisha yako huku pia ukipata muda mwingi wa kuweka kwenye kile unachofanya.
Usimamizi wa uhakika na wa karibu kwenye kitu chochote kile ni muhimu ili kiweze kukua. Kitu chochote kinachoshindwa huwa kinakosa usimamizi na udhibiti mzuri.
Ushauri wa sita ni kuhakikisha unakuwa na usimamizi na udhibiti wa karibu wa kile unachofanya. Yaani hakikisha upo kila wakati na kwa kila hatua inayochukuliwa. Usimuamini yeyote, hata kama anakushawishi na kukuridhisha kiasi gani. Jua kwenye jambo lolote lile, mhusika ana uchungu zaidi na hivyo atafanya maamuzi sahihi zaidi kuliko ambaye ni mjumbe tu. Kama utakuwa na wasaidizi ni vizuri, ila hapa mwanzoni, hakikisha upo mwenyewe kwa kila hatua. Baadaye utaweza kuweka mfumo mzuri, lakini mwanzoni, kila kitu ni wewe.
Maarifa sahihi kwenye kile unachofanya ni muhimu, kuna makosa mtu unaweza kuwa unafanya bila ya kujua na yanakukwamisha na kukuangusha. Wengi huwa wanafanya kwa mazoea kitu kinachokuwa kikwazo kwao.
Ushauri wa saba ni kupata maarifa sahihi juu ya kile unachofanya, chagua vitabu sahihi kusoma kwenye kile ulichochagua kufanya. Kama ni kilimo soma vitabu vya kilimo hicho, kadhalika kwenye ufugaji. Epuka sana maarifa ya kusisimua yanayoshirikisha mitandaoni, wewe nenda kwenye vitabu, jifunze kwa kina na jua hatua sahihi za kuchukua. Pia soma vitabu vinavyokupa maarifa ya jumla na hamasa ili upate nguvu ya kuendelea na safari yako, kwa sababu haitakuwa rahisi kwako.
Ndimi KOCHA MWL. JAPHET MASATU
(WhatsApp + 255 716924136 ) / 0755400128 / 0688361539
Sunday, October 4, 2020
UCHAMBUZI WA KITABU , MINDSET ( SAIKOLOJIA MPYA YA MAFANIKIO )
Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu Mindset: the new psychology of success kilichoandikwa na mwanasaikolojia Carol S. Dweck.
Hiki ni kitabu kinachoelezea mitazamo ambayo watu tunayo na jinsi inavyoathiri maisha na mafanikio yetu.
Kupitia kazi zake, tafiti mbalimbali na maisha ya wengine Carol anawagawa watu kwenye makundi makuu mawili;
Kundi la kwanza ni wale wenye MTAZAMO MGANDO ambao anauita FIXED MINDSET.
Huku kundi la pili wakiwa wale wenye MTAZAMO WA UKUAJI ambao anauita GROWTH MINDSET.
Tofauti hii moja na ndogo tu kwenye mtazamo, ndiyo inaleta tofauti kubwa kwenye maisha kati ya wale wanaofanikiwa sana na wale wanaokuwa na maisha ya kawaida.
Mtazamo ambao mtu unakuwa nao, uwe ni mgando au wa ukuaji, unatokana na imani ambazo umekuwa nazo kwa maisha yako yote. Imani hizo hujengeka mapema tangu ukiwa mdogo, kulingana na mazingira yanayokuzunguka.
Kile ambacho wengi tunaita haiba, ni mtazamo wa kuendesha maisha ambao mtu unakuwa umeuchukua na kwenda nao maisha yake yote. Na kitu ambacho kimekuwa kikwazo kwa wengi kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yao, ni aina ya mtazamo wanaokuwa nao.
Kwenye kitabu hiki, Carol anakwenda kutuonesha jinsi mitazamo tuliyonayo inavyojengwa, jinsi inavyokuwa kikwazo kwa mafanikio na pia jinsi ya kubadili mtazamo ambao mtu unao na kuwa na mtazamo bora zaidi.
Kitabu kimesheheni tafiti mbalimbali pamoja na mifano ya wale waliofanikiwa na kushindwa kwenye michezo, biashara na hata elimu, kutokana na aina ya mtazamo ambao mtu anakuwa nao.
Kitabu pia kinatusaidia jinsi ya kuwajenga watoto kwenye mtazamo sahihi ambao utawawezesha kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yao.
Tofauti kuu za mitazamo miwili kwa ufupi.
Mitazamo miwili ambayo watu wanayo, yaani mgando na ukuaji huwa inaleta tofauti nyingi kwa watu, lakini kubwa kabisa na zinazopelekea baadhi kufanikiwa na wengi kushindwa ni hizi;
1. UWEZO WA KIAKILI.
MGANDO; huona uwezo wa akili una ukomo na hivyo hawakazani kujiendeleza.
UKUAJI; huona uwezo wa akili hauna ukomo na hivyo hujiendeleza kwa kujifunza.
2. CHANGAMOTO.
MGANDO; huzikimbia changamoto.
UKUAJI; huzikaribisha changamoto.
3. VIKWAZO.
MGANDO; huona ndiyo mwisho wa safari yao na kukata tamaa.
UKUAJI; huona ni njia ya kufika wanakotaka na hivyo hung’ang’ana.
4. JUHUDI.
MGANDO; huona juhudi hazihitajiki, maana uwezo wao una ukomo.
UKUAJI; huweka juhudi kubwa wakijua zitabadili uwezo wao.
5. KUKOSOLEWA.
MGANDO; huepuka kila aina ya ukosoaji na hawajifunzi.
UKUAJI; hupokea ukosoaji na kujifunza.
6. MAFANIKIO YA WENGINE.
MGANDO; huona wivu pale wengine wanapofanikiwa na kuona ni hatari kwao.
UKUAJI; hufurahia mafanikio ya wengine na kujifunza kutoka kwao.
7. MAFANIKIO.
MGANDO; mafanikio yao hufikia kilele mapema na hawafanyi makubwa.
UKUAJI; wanafikia mafanikio makubwa na kuendelea kufanikiwa zaidi.
UTABIRI UTAKAOKUSAIDIA KWENYE MAISHA YAKO ?
Utabiri wa wataalamu ni wa uongo na umekuwa na upotoshaji mkubwa, je unawezaje kupanga mambo yako na kuchukua hatua zitakazokuwezesha kufanikiwa zaidi?
Kuna aina moja tu ya utabiri unaopaswa kuufanya mwenyewe na kuuishi kila siku. Utabiri huo ni huu kwamba kuna mabadiliko yanakuja, kwamba kila unachofanya sasa, kitaondoka na kupotea kabisa, hivyo kila mara uwe na maandalizi sahihi ya kuweza kukabiliana na mabadiliko hayo.
Kama umeajiriwa, kila siku ishi kwa kufikiri kesho unaweza kuamka na ajira yako isiwepo, kisha jiulize maisha yako yataendaje?
Kama unafanya biashara, kila siku ishi na utabiri kwamba kesho biashara hiyo haitakuwepo kabisa, halafu ona maisha yako yataendaje katika hali hiyo.
Utabiri huu unakufanya uwe na njia mbadala za kukabiliana na maisha yako ili chochote kinachotokea, isiwe mshangao kwako, badala yake iwe ni kitu ulichotegemea na kinachofuata ni kuchukua hatua ulizokuwa umepanga.
Kwa kuishi kwa namna hii, hutatikiswa na chochote, hutababaishwa na utabiri wa wengine na maisha yako yataendelea kwenda vizuri bila ya kutegemea nini kinaendelea.
Tuesday, September 29, 2020
USIWE MTU MWEPESI WA KUUDHIWA NA WATU , HATUA 09 ZA KUSHINDA DHIDI YA MAUDHI AU ADHA.
Habari mwanafalsafa, wadau wangu wa MAISHA NA MAFANIKIO BLOG ,
Karibu katika mwendelezo wa safari ya kujifunza falsafa ya Ustoa. Falsafa hii imekuwa ni falsafa yenye msingi mzuri wa kuzalisha maisha matulivu na bora. Wiki hii nimejiwekea utaratibu wa kuendelea kujifunza falsafa hii ya ustoa kupitia mwandishi Dr. Chuck Chakrapani ambaye kaandika mfululizo wa kazi nyingi za kistoa kwa kukusanya nukuu na misemo ya wastoa kama Seneca, Epictetus na Marcus. Kitabu cha awali nilishirikisha kama mapendekezo katika moja ya mijadala ya kifalsafa kupitia substack kiitwacho “STOIC INSPIRATIONS”. Ni kitabu kizuri sana kukisoma
Mbali na hicho kitabu kuna kingine ambacho nimekipitia na ndio msingi wa kuandika makala hii unayoisoma. Kitabu hiki kinaitwa “UNSHAKABLE FREEDOM” kwa tafsiri iso rasmi inatafsiriwa kama “UHURU USOTIKISWA”. Uhuru ni hitaji mama la mtu yeyote yule sehemu yoyote Duniani. Uhuru unalindwa na uhuru wa maisha ni katika kujua mambo yapo makundi mawili; Mosi, ni yale yalo katika uwezo wako na pili yalo nje ya uwezo wako. Kitabu hiki kinagusa namna unavyoweza kuwa na uhuru usotikiswa. Kuudhiwa ni njia rahisi inayoweza kuharibu uhuru wetu katika maisha na usipokuwa na msingi wa falsafa utaishi kuamua ovyo.
Kuudhiwa kunaweza kukufanya ujisikie vibaya, upandwe na hasira na tatu unakupotezea utulivu wa akili na wakati mwingine mwili. Ila si vile ambavyo Marcus Aurelius anatushauri kuwa tuumie au tupandwe na hasira la hasha ila kutusaidia kuwa na utulivu pale tunapopitia hali ya kuudhiwa na watu wanaotuzunguka. Marcus Aurelius kaziweka kama hatua 09 za kufuata ili kwa lolote litakalojitokeza la kutuudhi basi tusipoteze utulivu wetu wa ndani.
Hatua hizi 09 zimegawanyika katika makundi mawili. Mosi ni hatua 04 za awali ambazo ni maswali 04 ya kujiuliza unapopitia hali ya kuudhiwa na pili ni hatua 05 za mwisho ambazo ni makumbusho/ tafakari kuhusu hali unayopitia ya kuudhiwa na mtu au matukio maishani.
Jiulize haya; [ Haya ni maswali ambayo Marcus Aurelius anatupa mwongozo wa kujiuliza pale ambapo tunakuwa kati kati ya hali za kuudhiwa au dakika chache ya tendo la kuudhiwa limejitokeza ]
1. Usizidishe ukali wa tatizo- Je ni mahusiano gani ninayo na huyu mtu?
mfano mtu aliyekukosea ni ndugu yako wa karibu, mfanyakazi wako, mke au mume wako. Ukiondoa upande wa kosa ambalo limejitokeza la kukufanya uudhike ila upande mwingine mzuri huyo mtu ni ndugu yako, mfanyakazi wako, mke au mume wako. Unaporuhusu kuona mahusiano ya mtu aliyekutendea kosa unakuwa katika nafasi ya kupunguza ukubwa wa tatizo au tukio lilojitokeza.
2. Jitahidi kufahamu nini msukumo wa mtu kufanya hivyo;
Mtu anapotenda kitu usifanye haraka kutoa hukumu maana unazibwa na kutokujua kwa kina, je nini ni msukumo wa jambo alotenda. Ukiangalia kwa kina unaweza kuona msukumo wa kutenda jambo hilo. Huenda ni msukumo wa chuki, ujinga, wivu au wakati mwingine kutokukusudia.
3. Itafakari hali ilojitokeza
Usiwe na haraka ya kilichotokea kukipa tafsiri. Vuta ukimya na kuwa tayari kuona hali ilojitokeza imechangiwa na nini. Utaona pengine kuna nafasi ya ujinga kuwepo ndo maana tukio hilo limejitokeza. Usitoe mwitikio haraka tukio linapojitokeza.
4. Hebu jiangalie hujawahi watendea wengine ulofanyiwa ?
Ni rahisi sana kuona watu wanaotuudhi wanamakosa zaidi na tukasahau hata sisi kuna watu wengi tunawaudhi kwa mambo yetu. Mimi na Wewe ni bado wanadamu na tuna mapungufu mengi kama wengine. Wanapokosea wengine tuwe waelewa kama ambavyo nasi tunavyotaka watu wengine watuelewe.
Jikumbushe haya; [Haya ni mambo ya kujikumbusha ambayo Marcus Aurelius anatupa mwongozo wa kujikumbusha pale ambapo tunakuwa kati kati ya hali za kuudhiwa au dakika chache ya tendo la kuudhiwa limejitokeza]
5. Jua kuwa huna picha kamili ya jambo lilivyo
Wakati mwingine tunaona vitu kwa picha ndogo kuliko uhalisia ulivyo. Huwezi jua mtu aliyekukosea kwa wakati huo ni mambo gani anayoyapitia, au ni mambo yepi yalochangia yeye kufanya hivyo. Utaona mambo mengi ya watu walokosea ukichimba kwa kina kuna baadhi ya taarifa hatukuweza kuzijua kwanini hilo limejitokeza. Kila tukio linapotokea jua kuwa huna picha kamili ya mambo yalivyo. Usifanye haraka kutoa hukumu.
6. Kumbuka Maisha ni mafupi
Miaka 200 toka sasa na kuifikiria ijayo hatutakuwepo; hii ikiwa ina maana wewe unayesoma hii makala miaka 200 ijayo sote hatutakuwepo. Hili linadhihirisha maisha yalivyo mafupi na hatupaswi kuhifadhi hasira au chuki na mtu yeyote yule. Kwa kujua hili unakazana kuishi katika kuchagua furaha kuliko kitu kingine chochote.
7. Jua maoni ya mtu mwingine hayana nguvu dhidi yako endapo utapuuza au kuzuia kuyapa tafsiri
Kinachotuumiza sana siku zote kwa watu wanaotuudhi, wanaotutukana ni juu ya kuyapa tafsiri yale ambayo wamesema. Kuyapa tafsiri ni kuruhusu waloyasema yawe na nguvu dhidi yetu. Kwa kuona hilo Marcus anatushauri kutoyapa tafsiri au tukiweza tuyapuuze.
8. Jua hasira ukiijenga itakuumiza zaidi ndani yako
Hasira inaunguza kama mtu aliye na kaa la moto katika kiganja. Ukiudhiwa na ukajenga hasira ndani yako, hasira inaanza kukuumiza wewe na pengine aliyekuudhi hana mpango wowote wa kukuwazia wewe. Hasira isiruhusiwe idumu ndani yako.
9. Ukiweza tabasamu
Hakuna kitu kinachomfanya mtu aliyekuudhi au kukutukana pale unapotabasamu na wakati mwingine kucheka kwa kile alichokifanya. Inaonesha kwako kuwa alichokifanya hujakipa nguvu na pengine kukidharau. Lengo la mtu wakati mwingine kukutusi ni kutegemea kuona umekasirika, sasa unapokuwa unacheka unampa aumie zaidi kuona alichotegemea hakijafanikiwa.
Hizi hatua 09 ni mwongozo mzuri unaoweza kuutumia kila inapoitwa leo unapoendelea kukutana na watu mbalimbali. Maisha ya kila siku hatutaacha kukutana na watu ambao kwa namna moja wataleta adha dhidi yetu. Tutumie huu msingi kulinda utulivu wetu wa ndani maana tukumbushe maisha yetu ni mafupi.
KILA SIKU NI YA PEKEE SANA , ISHI KAMA LEO NA USIIPOTEZE.
Ni kawaida kwetu binadamu kuzoea vitu tulivyonavyo na kuvichukulia kawaida, kwa sababu tumekuwa tunaviona kila siku. Lakini vitu hivyo hivyo tunavyovichukulia pia, kuna wengine wanavitamani kweli ila hawawezi kuvipata.
Moja ya vitu hivyo ni hizi siku tunazokuwa nazo kila siku, tangu umezaliwa mpaka hapo ulipofika sasa, umekua unaanza na kumaliza siku zako na hivyo umeshazoea, asubuhi unaamka, unaenda na shughuli zako na siku inaisha, unalala na kuamka tena siku inayofuata.
Kwa kuwa umeshazoea sana siku zako, umekuwa unajiaminisha kabisa kwamba kesho ipo na huchelewi kuacha kufanya kitu leo kwa kujiambia utafanya kesho. Ni kitu gani kinakupa uhakika kiasi hicho?
Unapopata habari za misiba ya watu wa karibu, wale ambao uliwajua na walikuwa na mipango mikubwa ila wamefariki ghafla, huwa unapata mshtuko, unaona kweli maisha ni mafupi. Lakini haikuchukui siku nyingi unarudi kwenye mazoea yako, unazichukulia siku zako poa na kuahirisha mambo.
Tunawezaje kuondokana na hali hii ili tuweze kuzipa siku zetu uzito unaostahili na kuishi kwa ukamilifu?
Mwanafalsafa Seneca ana mengi ya kutueleza kwenye hili. Kwenye moja ya barua alizoandika kwa rafiki yake Lucilius akimweleza kuhusu wengi wanavyokihofia kifo, aligusia hili la kuishi kila siku kwa mazoea.
Seneca anasema wengi wamekuwa wakijiuliza maisha yao yataenda hivyo mpaka lini, kila siku kulala na kuamka, kuwa na njaa na kushiba, majira ya masika na kiangazi. Kwa kuyatazama maisha hivyo unaona kama ni mzunguko, hakuna kipya, kila kitu kinajirudia.
We slip into this condition, while philosophy itself pushes us on, and we say; "How long must I endure the same things? Shall I continue to wake and sleep, be hungry and be cloyed, shiver and perspire? There is an end to nothing; all things are connected in a sort of circle; they flee and they are pursued. – Seneca
Seneca anatutahadharisha kwamba tukiyaangalia maisha kwa mtazamo huo, tutayaona maisha ni maumivu yasiyo na mwisho, unaimaliza leo ukijua kesho inakwenda kuanza na kuisha kama leo. Majira ya masika yanaisha ukijua kiangazi kinakuja. Una njaa na kutafuta chakula kizuri kula, ila ukishashiba unajua kuna njaa itakuja tena. Kwa namna hii, maisha yanakuwa kama gereza la mateso, kusukuma siku usubiri kufa.
Lakini ipo namna nyingine ya kuyaangalia maisha kwa namna ambayo yatatunufaisha, mtazamo wa tofauti unaotusukuma kuyaishi maisha yetu kwa ukamilifu. Mtazamo huo ni kuyaona maisha kama zawadi, kila siku mpya unayoipata inakuwa kama nyongoza na hivyo unaitumia vizuri zaidi.
There are many who think that living is not painful, but superfluous. – Seneca.
Unapoiona siku mpya unayoianza kama nyongeza, unaitumia vizuri kwa sababu unajua huna uhakika kama utaiona siku nyingine kama hiyo. Huangalii jana ulifanya nini maana imeshapita, na wala huangalii kesho itakuwaje maana haipo, unachoangalia ni zawadi iliyo mbele yako.
Tukiweza kuziishi siku zetu kwa mtazamo huu, tutaacha kuona marudio yanayotuumiza na tutaanza kuona vitu vizuri vya kufanyia kazi.
Mahali pengine Seneca amewahi kutuasa jinsi ya kuziishi siku zetu kwa ukamilifu, mfano ni nukuu hizi;
“Anza kuishi mara moja na ichukulie kila siku mpya kama maisha tofauti.”
“Nitaendelea kuyaangalia maisha yangu na muhimu zaidi nitaitathmini kila siku yangu kwa kufunga vitabu vya maisha kila siku.”
Kama kauli za Seneca zinavyosisitiza, usichukulie poa hii siku uliyonayo leo, kuna wengine wangetamani sana kuwa nayo lakini haijawezekana. Iishi kwa upekee wake, ipangilie vizuri na fanya mambo ambayo mwisho wa siku ukiyaangalia unajiambia kweli umeiishi siku hii.
Kila unapoimaliza siku yako, jifanyie tathmini, pitia kila ulichofanya tangu kuamka mpaka unaporudi kulala na kisha jiulize maswali haya matatu;
Moja; Ni yapi mazuri nimefanya leo na ambayo nitaendelea kuyafanya nikipata zawadi ya siku nyingine?
Mbili; Ni yapi mabaya nimefanya leo ambayo sitarudia tena kufanya kama nitazawadiwa siku nyingine?
Tatu; Yapi ambayo sijayafanya kwa ubora unaostahili na ambayo nitayaboresha zaidi nitakapopata zawadi ya siku nyingine?
Ukijiuliza maswali hayo matatu kila siku na kujipa majibu sahihi, kisha kuyafanyia kazi, maisha yako yatakuwa bora, hutazichoka siku zako, hutaahirisha chochote na utayazuia matatizo mengi kabla hayajawa makubwa.
Wenye hekima wanajua, maisha siyo mateso bali zawadi, ichukulie hivyo na utakuwa na maisha bora na tulivu.