Wanasema
unaweza kulalamika huna viatu, ila ni mpaka siku utakayokutana na mtu
asiye na miguu ndiyo utakumbuka kushukuru kwamba angalau wewe una miguu
na hivyo viatu haviwi tatizo tena kwako.Ni
kawaida kwetu binadamu kuzoea vitu tulivyonavyo na kuvichukulia
kawaida, kwa sababu tumekuwa tunaviona kila siku. Lakini vitu hivyo
hivyo tunavyovichukulia pia, kuna wengine wanavitamani kweli ila
hawawezi kuvipata.
Moja
ya vitu hivyo ni hizi siku tunazokuwa nazo kila siku, tangu umezaliwa
mpaka hapo ulipofika sasa, umekua unaanza na kumaliza siku zako na hivyo
umeshazoea, asubuhi unaamka, unaenda na shughuli zako na siku inaisha,
unalala na kuamka tena siku inayofuata.
Kwa
kuwa umeshazoea sana siku zako, umekuwa unajiaminisha kabisa kwamba
kesho ipo na huchelewi kuacha kufanya kitu leo kwa kujiambia utafanya
kesho. Ni kitu gani kinakupa uhakika kiasi hicho?
Unapopata
habari za misiba ya watu wa karibu, wale ambao uliwajua na walikuwa na
mipango mikubwa ila wamefariki ghafla, huwa unapata mshtuko, unaona
kweli maisha ni mafupi. Lakini haikuchukui siku nyingi unarudi kwenye
mazoea yako, unazichukulia siku zako poa na kuahirisha mambo.
Tunawezaje kuondokana na hali hii ili tuweze kuzipa siku zetu uzito unaostahili na kuishi kwa ukamilifu?
Mwanafalsafa
Seneca ana mengi ya kutueleza kwenye hili. Kwenye moja ya barua
alizoandika kwa rafiki yake Lucilius akimweleza kuhusu wengi
wanavyokihofia kifo, aligusia hili la kuishi kila siku kwa mazoea.
Seneca
anasema wengi wamekuwa wakijiuliza maisha yao yataenda hivyo mpaka
lini, kila siku kulala na kuamka, kuwa na njaa na kushiba, majira ya
masika na kiangazi. Kwa kuyatazama maisha hivyo unaona kama ni mzunguko,
hakuna kipya, kila kitu kinajirudia.
We
slip into this condition, while philosophy itself pushes us on, and we
say; "How long must I endure the same things? Shall I continue to wake
and sleep, be hungry and be cloyed, shiver and perspire? There is an
end to nothing; all things are connected in a sort of circle; they flee
and they are pursued. – Seneca
Seneca
anatutahadharisha kwamba tukiyaangalia maisha kwa mtazamo huo,
tutayaona maisha ni maumivu yasiyo na mwisho, unaimaliza leo ukijua
kesho inakwenda kuanza na kuisha kama leo. Majira ya masika yanaisha
ukijua kiangazi kinakuja. Una njaa na kutafuta chakula kizuri kula, ila
ukishashiba unajua kuna njaa itakuja tena. Kwa namna hii, maisha
yanakuwa kama gereza la mateso, kusukuma siku usubiri kufa.
Lakini
ipo namna nyingine ya kuyaangalia maisha kwa namna ambayo
yatatunufaisha, mtazamo wa tofauti unaotusukuma kuyaishi maisha yetu kwa
ukamilifu. Mtazamo huo ni kuyaona maisha kama zawadi, kila siku mpya
unayoipata inakuwa kama nyongoza na hivyo unaitumia vizuri zaidi.
There are many who think that living is not painful, but superfluous. – Seneca.
Unapoiona
siku mpya unayoianza kama nyongeza, unaitumia vizuri kwa sababu unajua
huna uhakika kama utaiona siku nyingine kama hiyo. Huangalii jana
ulifanya nini maana imeshapita, na wala huangalii kesho itakuwaje maana
haipo, unachoangalia ni zawadi iliyo mbele yako.
Tukiweza
kuziishi siku zetu kwa mtazamo huu, tutaacha kuona marudio
yanayotuumiza na tutaanza kuona vitu vizuri vya kufanyia kazi.
Mahali pengine Seneca amewahi kutuasa jinsi ya kuziishi siku zetu kwa ukamilifu, mfano ni nukuu hizi;
“Anza kuishi mara moja na ichukulie kila siku mpya kama maisha tofauti.”
“Nitaendelea kuyaangalia maisha yangu na muhimu zaidi nitaitathmini kila siku yangu kwa kufunga vitabu vya maisha kila siku.”
Kama
kauli za Seneca zinavyosisitiza, usichukulie poa hii siku uliyonayo
leo, kuna wengine wangetamani sana kuwa nayo lakini haijawezekana. Iishi
kwa upekee wake, ipangilie vizuri na fanya mambo ambayo mwisho wa siku
ukiyaangalia unajiambia kweli umeiishi siku hii.
Kila
unapoimaliza siku yako, jifanyie tathmini, pitia kila ulichofanya tangu
kuamka mpaka unaporudi kulala na kisha jiulize maswali haya matatu;
Moja; Ni yapi mazuri nimefanya leo na ambayo nitaendelea kuyafanya nikipata zawadi ya siku nyingine?
Mbili; Ni yapi mabaya nimefanya leo ambayo sitarudia tena kufanya kama nitazawadiwa siku nyingine?
Tatu; Yapi ambayo sijayafanya kwa ubora unaostahili na ambayo nitayaboresha zaidi nitakapopata zawadi ya siku nyingine?
Ukijiuliza
maswali hayo matatu kila siku na kujipa majibu sahihi, kisha kuyafanyia
kazi, maisha yako yatakuwa bora, hutazichoka siku zako, hutaahirisha
chochote na utayazuia matatizo mengi kabla hayajawa makubwa.
Wenye hekima wanajua, maisha siyo mateso bali zawadi, ichukulie hivyo na utakuwa na maisha bora na tulivu.