Monday, January 14, 2019

SIFA YA WASHINDI KATIKA MAISHA.

“Victory belongs to the most persevering.” - Napoleon Bonaparte
Ushindi unaenda kwa wale ambao ni ving’ang’anizi na wavumilivu.
Huwa tunawaangalia wale waliofanikiwa na kupenda sana kufika walipofika. Lakini sisi wenyewe kuna vitu vingi ambavyo tulishawahi kuanza kwenye maisha yetu, lakini havikutufikisha mbali, kwa sababu tulikosa ung’ang’anizi na uvumilivu.
Sasa chagua kitu kimoja au vichache unavyotaka kwenye maisha yako, kisha weka juhudi zako zote na usikate tamaa mpaka umekipata, na ninakuhakikishia utakipata. Maana washindi wote wameng’ang’ana na kupata walichotaka.

Tuesday, January 8, 2019

HEKIMA.

Bila ya hekima, fedha na afya tunazopigania kuwa nazo, zitatupoteza kabisa. Hekima ndiyo inayotuongoza vizuri kwenye maisha yetu, ndiyo inayotuwezesha kufanya maamuzi sahihi kwetu ambayo yanafanya maisha yetu yawe bora zaidi.
KUSOMA; kila siku ya maisha yako, soma angalau kwa dakika 30, na soma vitabu vinavyoongeza maarifa na uelewa wako kwenye kile unachofanya na hata maisha kwa ujumla. Tenga na linda sana muda huu wa kujisomea, ndiyo utakaokutoa hapo ulipo sasa na kukufikisha mbali zaidi.
UZOEFU WA WENGINE; chagua watu ambao utajifunza kupitia wao, hawa tunawaita menta. Unapaswa kuwa na mtu ambaye unataka kufikia hatua ambazo amefikia yeye, kisha kujifunza kila kitu kuhusu yeye. Kama yupo hai na yupo karibu unaweza kutafuta nafasi ya kuonana naye. Na kama yupo mbali huwezi kumfikia au alishafariki basi jifunze kupitia maandiko yake na hata maandiko yaliyoandikwa kuhusu wewe. Mazuri aliyofanya na pia jifunze makosa aliyoyafanya ili uweze kuyaepuka.
KUTAFAKARI; Unapaswa kuwa na muda wako mwenyewe, muda wa kutafakari, kuyatafakari maisha yako na kutafakari kila unachofanya, kuanzia ulikotoka, ulipo sasa na kule unakokwenda. Kila mwisho wa siku yako tafakari kila hatua uliyochukua kwenye siku hiyo na angalia wapi umefanya vizuri, wapi umekosea na wapi unahitaji kurekebisha na kuboresha zaidi. Majibu ya maswali mengi uliyonayo kuhusu maisha tayari unayo, ni wewe kutafakari na kujisikiliza na utapata majibu mengi sana.

UTAJIRI.

Fedha ni sehemu muhimu sana ya maisha yetu, ukiondoa pumzi ambayo kila mtu anaipata bure, kila kitu kinahitaji fedha. Na hata hiyo pumzi unapoumwa inaacha kuwa bura na unaanza kuilipia. Fedha ni hitaji muhimu sana kwenye maisha yetu, kwa sababu ndiyo inatuwezesha kupata kila tunachotaka.
KIPATO; ongeza kipato chako kwa kutoa thamani zaidi, kujituma zaidi na kuwafikia wengi zaidi. Kama umeajiriwa tekeleza majukumu mengi zaidi na magumu zaidi. Kama unafanya biashara wafikie wateja wapya na wengi zaidi. Fanya zaidi ya ulivyozoea kufanya huko nyuma na kipato chako kitaongezeka.
MATUMIZI; Dhibiti sana matumizi yako, peleka fedha zako kwenye yale mambo ambayo ni muhimu pekee kwenye maisha yako, kama kitu siyo muhimu, achana nacho. Matumizi huwa yana tabia ya kukua kadiri kipato kinavyokua, usipoyadhibiti yatakurudisha nyuma.
UWEKEZAJI; Hutakuwa na nguvu za kufanya kazi kama unavyofanya sasa  miaka yako yote. Hivyo unahitaji kuifanya fedha yako ikufanyie kazi na kukiingizia kipato. Na hapa ndipo uwekezaji unapokuwa muhimu. Weka akiba na wekeza akiba hiyo kwenye maeneo ambayo yanazalisha zaidi kwa baadaye.

AFYA

Afya ndiyo mtaji wa kwanza na muhimu sana kwenye maisha yetu, bila ya afya bora na imara huwezi kufanya chochote kikubwa kwenye maisha yako. Afya unaweza kuichukulia kirahisi sana unapokuwa nayo, lakini ukishaipoteza gharama zake ni kubwa sana.

KULA VYAKULA vya kiafya kwa kuepuka sukari, kupunguza wanga na kuongeza zaidi mbogamboga, matunda, mafuta na protini. Sumu namba moja kwenye afya zetu ni wanga na sukari, ukiweza kudhibiti hili utakuwa na afya bora.
KUFANYA MAZOEZI, kila siku fanya mazoezi ya kukimbia kwa angalau nusu saa. Mazoezi ya kukimbia ni mazoezi bora kabisa na yasiyo na gharama kwako. Hakikisha unafanya haya kila siku.
KUPUMZIKA, pata muda wa kutosha wa kulala kulingana na uhitaji wa mwili wako. Kwa wastani binadamu tunahitaji masaa 6 mpaka 8 ya kulala kwa siku. Jua mwili wako unahitaji kiasi gani na kila siku upe muda huo. Hili litakufanya uwe imara na kuweza kuweka juhudi kwenye shughuli zako.

Sunday, January 6, 2019

JINSI UTAJIRI UNAVYOKUJA KWAKO.

 Utajiri unakuja kwako kwa njia ya thamani. Unapaswa kutoa thamani kubwa zaidi ya matumizi kuliko thamani ya fedha ambayo mtu anakupa. Ili kupata zaidi lazima uwe tayari kutoa zaidi.
 
Usiwalangue watu, wala usitumie mbinu kuwashawishi wanunue kitu ambacho hakitawasaidia. Wape watu kitu ambacho kitakuwa na msaada kwenye maisha yao na wewe utaweza kupata kile unachotaka.

USIWE MTU WA KULALAMIKA AU KUKOSA SHUKRANI.

Tumeona kwamba kuna mfumo wa fikra ambao unatupa kila ambacho tunakifikiri kwa muda mrefu. Njia pekee ya kushirikiana na mfumo huu ni kuwa na shukrani.
 
Kwa kushukuru, mfumo huu wa fikra unajua kwamba upo tayari kupokea zaidi na hivyo kukuwezesha kupata zaidi.
 
Usiwe mtu wa kulalamika au kukosa shukrani, mara zote shukuru na utaweza kupata zaidi. Shukuru kwa kidogo na utafungua milango ya kupata kikubwa zaidi.

NAMNA FULANI YA KUFIKIRI ILI KUVUTIA UTAJIRI.

 Hatua muhimu ya kupata kile unachotaka ni kujua kwa hakika nini hasa unachotaka. Huwezi kupata kile usichokijua, hivyo lazima ujue kwa undani kile unachotaka na kukifikiria kwa ukamilifu wake ndiyo uweze kukipata.

Unapaswa kutengeneza picha kwenye fikra yako ya kile unachotaka, kwa namna unavyokitaka kisha weka picha hii kwenye fikra zako mara nyingi. Kila unapokuwa na muda ambao huna kazi, tumia muda huo kufikiria picha hiyo na kujiona tayari umeshapata kile unachotaka.
Unapoifikiria picha ya kile unachotaka, unapaswa kuwa na imani kwamba tayari umeshakipata kwa namna unavyokitaka. Ona kama tayari unacho. Kwa njia hii, mfumo wa fikra unaoongoza dunia utakuwezesha kupata kile unachotaka.