Tabia hizo kumi ni kama ifuatavyo;
(1).UNAENDA KILA SIKU.
Kila
siku ambayo ni ya kazi, unaenda kazini. Haijalishi kama unajisikia au
hujisikii, umechoka au hujachoka, ni siku ya kazi na unaenda kazini. Na
ili kuhakikisha unaenda, sehemu za kazi kuna daftari au mashine ya
kuweka sahihi, ili kuthibitisha kwamba kweli umefika kazini.
Unapojiajiri,
hakikisha kila siku ya kazi ambayo umejipangia kulingana na kile
unachofanya basi unaenda kwenye eneo lako la kazi. Japokuwa una uhuru wa
kwenda au kutokwenda, usiutumie kabisa uhuru huo, wewe nenda, iwe
unajisikia au hujisikii, iwe umechoka au la. Chukulia kuna bosi
anakusubiria pale, na hawezi kukuelewa kama hujaenda.
(2). CHANGAMOTO ZA MAISHA HAZIINGILII KAZI.
Usiku
umegombana na mke wako au mume wako, asubuhi unaamka na kujiandaa
kwenda kazini. Hukai nyumbani na kumwambia bosi leo huendi kwa sababu
kuna ugomvi nyumbani. Umeamka una mafua makali unajiandaa na kwenda
kazini, husemi mafua haya wacha nipone kwanza. Mwajiri wako hawezi
kukuelewa.
Peleka
tabia hiyo kwenye kujiajiri pia, usikubali sababu ndogo ndogo
zinazoendelea kwenye maisha yako kuingilia kazi zako. Endelea na kazi
kila siku, kama ambavyo ungeenda kwenye kazi ukiwa umeajiriwa.
(3). UNAKAA KAZINI MUDA WA KAZI.
Unaenda
kazini kila siku, na ukifika, unakaa mpaka muda wa kazi uishe ndiyo
unaondoka. Hata kama siku hiyo huna kazi za kufanya, utakaa hapo kazini
mpaka muda wa kutoka ufike. Hata kama siku hiyo hujisikii kufanya kazi,
utazurura zurura hapo ofisini mpaka muda wa kutoka ufike. Hutakatisha
siku yako ya kazi kwa sababu tu hujisikii, siku ya kazi inaisha muda wa
kazi unapoisha.
Hamishia
hili kwenye kujiajiri, kwenye muda uliopanga kufanya kazi yako, fanya
kazi na usiruhusu kuingiliwa na kitu kingine. Kama umepanga utaandika
kuanzia saa 2 asubuhi mpaka saa sita mchana, basi fanya hivyo.
Usiahirishe kwa sababu siku hiyo hujisikii kuandika. Kama umepanga
utafungua biashara yako saa moja asubuhi na kufunga saa moja jioni fanya
hivyo, isitokee siku unafunga saa 10 kwa sababu siku hiyo umechoka
zaidi. Jiulize kama ingekuwa kazi ya kuajiriwa je ungeacha, kama hapana,
fanya.
( 4 ).UNAFANYA KAZI KWA MIAKA MINGI.
Kazi
yoyote unayoifanya, utaifanya kwa miaka mingi. Kama ni mwalimu
utafundisha kwa miaka mingi, unaweza kuhama shule mbalimbali, lakini
utafundisha. Kama wewe ni daktari utatibu kwa miaka mingi, unaweza
kubadili vituo vya kazi, lakini utatibu. Utafanya kazi yako mpaka pale
utakapostaafu au kufikia uhuru wa kifedha. Na hufikirii kuifanya kwa
muda mchache na isipolipa unaacha, unaifanya kwa miaka mingi.
Peleka
tabia hiyo kwenye kujiajiri pia, kile unachochagua kufanya, jiandae
kukifanya kwa miaka mingi. Kama ni uandishi, jua utaandika kwa miaka
mingi, kama ni biashara pia, jipe muda mrefu wa kufanya. Acha kabisa
kujidanganya kwamba utafanya kwa siku chache na kama hailipi utaacha.
Jiandae kufanya kwa muda mrefu.
( 5 ). UNA MAHITAJI MAKUBWA.
Kinachokufanya
uendelee kuifanya kazi yako, hata kama ni ngumu au huipendi ni mahitaji
makubwa uliyonayo. Unahitaji fedha ya kuendesha maisha yako, kula,
kulala, kuvaa, kuendesha familia, kusomesha watoto na mengine. Una ndugu
wanaokutegemea ambapo kazi yako ndiyo inakuwezesha kuwasaidia. Mwajiri
akikuambia fanya tu kwa upendo hakuna haja ya malipo huwezi kumwelewa,
una mahitaji, unataka fedha, unafanya kazi ili ulipwe.
Chochote
unachofanya pale unapojiajiri, hakikisha unalipwa ili uweze kuendesha
maisha yako. Na hili ni muhimu sana kwenye kazi za sanaa, ni rahisi
kujiambia naandika kwa sababu napenda, siyo kwa sababu nataka kulipwa.
Andika ili ulipwe, una mahitaji ya maisha yako, unafikiri utayamudu vipi
kama unachofanya hakikulipi?
(6 ). UNAKUBALI MALIPO YA KAZI.
Unapoomba
kazi, cha kwanza unachouliza ni mshahara. Unapofanya kazi hiyo kwa muda
unamtaka mwajiri wako akuongeze mshahara. Unaenda kusoma au kuongeza
ujuzi ili upate mshahara zaidi. Unafanya kazi muda wa ziada ili upate
malipo zaidi.
Peleka
tabia hii kwenye kujiajiri pia, hakikisha unapata malipo na kila wakati
kazana kutoa thamani zaidi ili ulipwe zaidi. Weka juhudi kubwa ili
kupata malipo makubwa. Na asikusumbue mtu kwamba unataka sana kulipwa,
kama hayupo tayari kulipia achana naye. Hufanyi unachofanya kuuza sura,
ndiyo kinawasaidia watu, lakini asante haitaleta chakula mezani,
hakikisha unalipwa.
( 7 ). KAZI YAKO SIYO WEWE.
Kama
wewe ni mwalimu, unajua kabisa ualimu wako unaishia shuleni, hukutani
na watoto barabarani na ukaanza kuwafundisha hapo hapo. Kama ni daktari
udaktari wako unaishia hospitali, hupandi kwenye daladala na kuanza
kuwatibu watu. Kwa kifupi ni kwamba unapokuwa umeajiriwa, unajua
kuyatenganisha maisha yako binafsi na maisha ya kazi, huchanganyi hivyo
pamoja.
Hapa
ndipo wengi waliojiajiri huwa wanafeli, hawajitofautishi wao binafsi na
kazi zao. Kila wakati wanachanganya kazi na maisha, na ndiyo maana
hawapati muda wa kupumzika. Hivyo kwa kile ambacho umejiajiri kufanya,
tenga muda wa kukifanya na tenga muda wa maisha pia. Kushindwa kufanya
hivyo, utachoka haraka na kushindwa kuendelea.
(8). UNAJUA MBINU ZA KUFANYA KAZI.
Kama
wewe ni mwalimu, unajua mbinu za ualimu, njia za kufundisha watu mpaka
waelewe na pia unaendelea kujifunza. Kama wewe ni daktari, unajua jinsi
ya kudadisi dalili za mgonjwa, vipimo gani ufanye mpaka ujue mgonjwa
anaumwa nini na kisha umpe matibabu sahihi. Huamki siku moja na kujiita
daktari kisha ukaanza kutibu, unajifunza.
Peleka
tabia hii kwenye kile unachojiajiri kufanya, mwanzoni jua kabisa ni
muda wa kujifunza, kuzijua njia bora za kufanya kitu hicho na kila
wakati kazana kujua mbinu bora zaidi. Unafanya vizuri pale unapokuwa na
ujuzi wa kufanya. Hivyo jifunze ujuzi wa kile ulichojiajiri kufanya.
(9 ). UNA UCHESHI AU UTANI KWENYE KAZI.
Kwa
kila kazi, kuna utani fulani upo, ambao huwa haukuumizi. Utani huo
unaweza kuonekana kama ni kejeli, lakini haukusumbui. Mfano baina ya
madaktari, huwa wanataniana sana, mfano daktari wa upasuaji atamuita
daktari wa magonjwa ya ndani ni mtu wa kubahatisha, maana anatibu kitu
ambacho hakioni. Daktari wa magonjwa ya ndani atamuita daktari wa
upasuaji kama mtu wa buchani, kazi yake ni kukata vitu. Huu ni utani
ambao upo na madaktari hao hawapigani kwa sababu ya utani huo.
Tuhusu
utani au ucheshi kwenye kile ambacho umejiajiri kufanya. Kuna watu
watachukulia hiyo kama sehemu ya kukudhihaki au kukukejeli, lakini wewe
utachukulia ni kama utani tu na utaendelea kufanya. Mfano unaweza kuwa
mwandishi na watu wakakuambia unachoandika ni nadharia tu, hakiwezekani
kwa vitendo. Usichukulie kwa umakini sana hilo, ona kama ni utani na
endelea kuandika.
(10 ). UNAPOKEA SIFA NA LAWAMA KWA KAZI UNAYOFANYA.
Ukiwa
kwenye ajira, unaweza kufanya kazi yako vizuri na ukasifiwa sana,
wakati mwingine unakosolewa na kulaumiwa kupitia kazi yako. Unajua hiyo
ni sehemu ya kazi, hivyo huendi nyumbani na kukosa usingizi kwa sababu
bosi wako amekuambia ripoti uliyoadika siyo sahihi. Unajua kesho utaenda
kufanya marekebisho kama alivyokuambia, ni sehemu ya kazi.
Peleka
tabia hii kwenye kujiajiri pia. Kwa kila unachofanya, jua kuna wakati
itasifiwa na kuna wakati utapingwa, kukosolewa au kulaumiwa. Kuwa tayari
kupokea hayo na kuchukua hatua sahihi. Usiache kuandika kwa sababu mtu
amekuambia makala yako au kitabu chako ni cha hovyo, jua kipi hakipo
sahihi na boresha zaidi kwenye uandishi ujao.
Watu wengi waliopo kwenye ajira huwa wanatamani sana kuondoka kwenye ajira na kwenda kujiajiri wenyewe. Inaweza kuwa ni kupitia biashara au vipaji vya kisanii walivyonavyo kama uandishi, uchoraji, unenaji na kadhalika.
ReplyDeleteLakini wengi wa wanaotoka kwenye ajira na kwenda kuajiri, huwa wanashindwa kufanikiwa. Hii ni kwa sababu mazingira ya kujiajiri, ambapo mtu unajisimamia mwenyewe ni tofauti kabisa na mazingira ya kuajiriwa ambapo mtu unasimamiwa na wengine.
Kwa asili, sisi binadamu ni wavivu, huwa hatupendi kufanya kazi ngumu, hivyo inapokuwa chini ya uamuzi wetu wenyewe, huwa tunaahirisha kazi yoyote ambayo ni ngumu. Ndiyo maana hata kwenye ajira, majukumu mengi hufanywa pale mwisho wa kuyafanya unapokuwa umefika.
Ukipewa wiki moja ya kuandika ripoti, siku tatu za kwanza hutaigusa kabisa, siku ya nne na ya tano utapanga jinsi ya kuiandaa. Siku ya sita utaanza kuifanya lakini hutapiga hatua sana. Lakini inapofika siku ya saba, siku ambayo lazima ripoti ikamilike, hapo utafanya kazi kwa mfululizo bila kuruhusu usumbufu wowote, ikibidi utaongeza muda wa kufanya kazi.
Ripoti uliyokuwa na siku saba za kuifanya, umeifanya ndani ya siku moja. Je huo siyo muujiza? HAMISHIA TABIA HIZO UNAZOZIFANYA KATIKA AJIRA YAKO KWENDA KWENYE KUJIAJIRI----WENGI HUANGUKA HAPA ! BADILIKA SASA NA FANYA KAZI KWA BIDII
Asante sana nimejifunza kitu
ReplyDelete