Zifuatazo ni hatua za kuchukua ili kukabiliana na ushindani wa bei pale unapofanya biashara kwa mtaji mdogo.
(01 ). CHEZA MCHEZO WAKO MWENYEWE.
Kama
unataka kupata ushindi kwenye eneo lolote la maisha yako, basi unapaswa
kucheza mchezo wako mwenyewe. Hii ina maana kwamba unapaswa kutengeneza
mchezo wako, kujiwekea sheria zako mwenyewe, kisha kucheza mchezo huo.
Ukiingia kucheza mchezo wa wengine, ambao wameutengeneza wao na kuweka
sheria zao, huwezi kushinda, maana wao ndiyo wanaoujua mchezo huo kuliko
wewe.
Hivyo
pia ndivyo ilivyo kwenye biashara, haijalishi unafanya biashara gani,
unapaswa kucheza mchezo wako mwenyewe. Hapa unapaswa kupanga ni aina
gani ya biashara unaifanya na utaifanya kwa njia zipi. Tengeneza njia
zako mwenyewe, ambazo zinatumia uwezo ulio ndani yako na aina ya wateja
unaowalenga, kwa kile unachouza. Jiwekee sheria zako mwenyewe na kisha
endesha biashara yako kwa sheria hizo.
Chagua
kufanya biashara ya tofauti, ambapo sheria yako kuu kwenye ushindani
siyo bei, bali utofauti. Usishindane kwa kupunguza bei, bali shindana
kwa kutoa kitu ambacho biashara nyingine hazitoi. Kwa maneno mengine,
usikazane kuwa bora zaidi ya wengine, bali kazana kuwa tofauti na
wengine.
Hakikisha
kuna kitu ambacho wateja wanakipata kwenye biashara yako, ambacho
hawawezi kukipata kwenye biashara nyingine yoyote. Inaweza kuwa aina ya
bidhaa unazouza, inaweza kuwa aina ya huduma wanayoipata. Ni lazima uwe
na kitu ambacho wateja wanakipata kwako tu na hawawezi kukipata kwa
wafanyabiashara wengine.
Kama
kwenye biashara unayoifanya huwezi kutengeneza kitu cha aina hiyo,
ushindani wa bei hauwezi kukuacha salama. Usitegemee utoe kile ambacho
kinaweza kupatikana kwa wengine, halafu wateja waje kununua kwako kwa
bei juu wakati wanaweza kupata kwingine kwa bei ya chini.
Kumbuka
ubinafsi ni asili yetu binadamu, huwa tunaangalia maslahi yetu kwanza
kabla ya kitu kingine. Hivyo hakikisha kwenye biashara yako kuna kitu
unachowapa wateja wako, kinachowanufaisha na hawawezi kukipata sehemu
nyingine. Kwa kuwa na kitu hicho, watakuwa tayari kuja kununua kwako kwa
bei ya juu kuliko kwenda kwa wengine wanaouza kwa bei ya chini.
( 02 ). ANZA NA WATEJA SAHIHI.
Kuna
wateja ambao wanachoangalia ni bei tu, na wapo wateja ambao
wanachoangalia ni thamani wanayoipata. Ni vigumu sana kumshawishi mteja
anayeangalia bei rahisi kuona thamani.
Hivyo
kabla hujaweka nguvu zako kwenye ushawishi au mengine yoyote, anza na
wateja sahihi. Jua kwanza kinachomsukuma mteja kununua ni bei au
thamani.
Kama
kinachomsukuma mteja kununua ni bei peke yake, usipoteze hata muda
wako, kwa sababu atakwenda kule ambapo anapata kwa bei ya chini. Lakini
unapokutana na mteja ambaye anaangalia thamani anayoipata, hapo una
nafasi ya kumshawishi kulipa zaidi ili apate thamani zaidi.
Wateja
wa thamani siyo wengi, lakini wale wachache unaowapata watakufanya
ufurahie kuifanya biashara yako, maana huwa ni waelewa na hawakusumbui
sana.
Wateja
wa bei rahisi huwa ni wengi, lakini pia ni wasumbufu. Unaweza
kuwapunguzia bei na bado wakaona umenufaika zaidi na hivyo kutaka zaidi
kutoka kwako.
Kwa
biashara unayofanya, chagua aina ya wateja unaotaka kwenda nao, kisha
tafuta aina hiyo ya wateja. Wanapokuja wateja wanaoangalia bei tu,
waeleze thamani unayotoa na kama bado wanasisitiza kwenye bei, unaweza
kuwaelekeza wapi pa kupata kwa bei wanayotaka wao, lakini pia waoneshe
nini watakosa kwa kuangalia bei pekee.
( 03 ). KUWA KARIBU ZAIDI NA WATEJA WAKO.
Biashara
ndogo huwa zinazishinda biashara kubwa kwenye eneo hili, uwezo wa kuwa
karibu na wateja. Biashara kubwa zinahudumia watu wengi, hivyo huwa
hazihangaiki na mteja mmoja mmoja, hivyo mteja hawezi kupata upekee
kwenye biashara kubwa.
Ila
kwenye biashara ndogo, kwa sababu wateja ni wachache, ni rahisi kumpa
kila mteja upekee anaostahili. Ni rahisi kumjua kila mteja na matakwa
yake, hivyo wajibu ni kumtimizia mteja yale anayotaka kwa namna yake
mwenyewe.
Kosa
kubwa ambali wafanyabiashara wengi wadogo huwa wanafanya ni kufanya
biashara zao ndogo kama vile ni biashara kubwa, kitu ambacho
kinawagharimu sana.
Kuwa
karibu zaidi na wateja wako, wasiliana nao mara kwa mara, jua matukio
mbalimbali kwenye maisha yao, mfano siku zao za kuzaliwa, watu wao wa
karibu na kadhalika. Kisha watumie salamu au jumbe mbalimbali katika
siku zao hizo muhimu.
Tumia
kila fursa kuwapa wateja wako upekee, uwafanye wajisikie vizuri
wanapokuja kwenye biashara yako ambapo wanalipa zaidi kuliko
wanavyojisikia wanapokwenda kwenye biashara kubwa ambapo wanalipa
kidogo.
( 04 ). WAFUATE WATEJA KULE WALIPO.
Njia
nyingine ya kuongeza thamani kwa wateja wako ili wawe tayari kulipa
zaidi kwako ni kuwafuata kule walipo. Sasa hivi watu hawana muda, hivyo
wanapenda sana pale biashara inapowafuata wao kule walipo. Lakini pia
uaminifu umekuwa mdogo, hivyo watu wengi huhofia kuagiza vitu ambavyo
hawajaviona.
Wewe
kwa kuwa na biashara ndogo, una nafasi ya kujenga uaminifu na wateja
wako na kisha kuwafanya waweze kuagiza kile unachouza popote walipo na
wakapelekewa. Hii inawafanya wateja wawe tayari kulipa zaidi, kwa sababu
imewapunguzia usumbufu na upotevu wa muda kutoka walipo na kwenda
kutafuta wanachotaka.
Biashara ndogo inaweza kuwafikia wateja kule walipo kwa ufanisi zaidi kuliko biashara kubwa, hivyo tumia vizuri nafasi hiyo.
( 05 ) WEKEZA ZAIDI KWENYE BIASHARA YAKO.
Unapomtaka
mteja alipie zaidi kile anachonunua kwako, ambacho anaweza kukipata kwa
bei ya chini sehemu nyingine, lazima utengeneze mazingira ambayo
yatamfanya mteja aone anastahili kulipa zaidi. Mfano ukinunua soda ya
cocacola kwenye duka la mtaani utalipa shilingi mia tano, lakini soda
hiyo hiyo ukiinunua hotelini utalipa shilingi elfu mbili. Ukiwa hotelini
hutalalamika kwa nini uuziwe soda ya mia tano kwa shilingi elfu mbili,
kwa sababu kuna mazingira yanayokufanya uone kulipa elfu mbili ni
halali. Unakuwa umekaa eneo zuri na tulivu, unahudumiwa na watu
wanaokujali na kadhalika.
Hivyo
pia ndivyo unavyopaswa kufanya kwenye biashara yako, fanya uwekezaji
unaoipa biashara yako thamani zaidi kuliko washindani wako. Kuna kitu
kidogo sana unaweza kukifanya kwenye eneo lako la biashara na
likawafanya watu waipe thamani kubwa. Kitu hicho ni mwonekano wa eneo la
biashara, linapaswa kuwa safi na lililopangiliwa vizuri. Mtu akifika
kwenye eneo hilo anaona utofauti mkubwa, na ndani yake anakuwa tayari
kulipa zaidi.
Wewe
mwenyewe ni shahidi, huenda umewahi kufika kwenye eneo la biashara, na
kwa jinsi lilivyo na mwonekano mzuri, ukajua utatozwa gharama kubwa,
lakini ulipotozwa gharama za kawaida ukashangaa. Hiyo ndiyo hali
unayopaswa kuileta kwenye biashara yako pia, kufanya uwekezaji
unaowaandaa wateja kuwa tayari kulipa zaidi.
Mwonekano
na mpangilio wa eneo la biashara, vifaa unavyotumia na huduma unayowapa
wateja wako vinapaswa kuwa vya viwango vya juu sana kiasi cha mteja
kuona kama anakuibia pale unapomtajia bei. Na kumbuka hapa utakuwa
unawalenga wateja sahihi na siyo wale wanaoangalia bei ya chini pekee.
Rafiki,
hizo ndizo hatua tano za kuchukua ili kuweza kukabiliana na ushindani
wa bei pale unapofanya biashara kwa mtaji kidogo. Kama ulivyoona, kuna
mengi ya kufanya kuliko kuingia kwenye ushindani wa moja kwa moja kwenye
bei, ambao utakuumiza sana.
Nimalizie
kwa kukuambia hili rafiki yangu, kama upo kwenye biashara ambayo kitu
pekee unachoweza kujitofautisha nacho ni kupunguza bei, basi upo kwenye
biashara ambayo siyo sahihi. Kwa sababu kuna wengine wapo tayari
kupunguza bei zaidi yako, na wakiwa na mtaji mkubwa kuliko wewe,
watapata faida kwa kuuza kwa wengi zaidi kuliko wewe unayeuza kwa
wachache.
Hivyo
fanyia kazi haya matano uliyojifunza, na mengine yanayoendana na hayo,
lakini siyo kupunguza bei. Na kama biashara haina namna nyingine bali
bei basi achana nayo na nenda kwenye biashara sahihi, ambapo unaweza
kutengeneza mchezo wako mwenyewe na kuucheza vizuri.
JIUNGE NA DARASA ONLINE KWA KULIPIA ADA YA MWEZI , MWAKA---UJIFUNZE KWA UNDANI NA MAPANA--ELIMU YA BIASHARA & UJASIRIAMALI--- NA UCHUKUE HATUA --UTAFANIKIWA
SEE YOU AT THE TOP
Ndimi rafiki yako KOCHA / MWL. JAPHET MASATU , BLOGGER
Kwa maelekezo zaidi tuwasiliane kwa ;--
SIMU / MESEJI / ( WhatsApp + 255 716 924136 ) / +255 755 400128 / + 255 688 361 539 / + 255 629 748 937
JIUNGE NA DARASA ONLINE KWA KULIPIA ADA YA MWEZI , MWAKA---UJIFUNZE KWA UNDANI NA MAPANA--ELIMU YA BIASHARA & UJASIRIAMALI--- NA UCHUKUE HATUA --UTAFANIKIWA
SEE YOU AT THE TOP
Ndimi rafiki yako KOCHA / MWL. JAPHET MASATU , BLOGGER
Kwa maelekezo zaidi tuwasiliane kwa ;--
SIMU / MESEJI / ( WhatsApp + 255 716 924136 ) / +255 755 400128 / + 255 688 361 539 / + 255 629 748 937
Tumia kila fursa kuwapa wateja wako upekee, uwafanye wajisikie vizuri wanapokuja kwenye biashara yako ambapo wanalipa zaidi kuliko wanavyojisikia wanapokwenda kwenye biashara kubwa ambapo wanalipa kidogo.
ReplyDeleteChagua kufanya biashara ya tofauti, ambapo sheria yako kuu kwenye ushindani siyo bei, bali utofauti. Usishindane kwa kupunguza bei, bali shindana kwa kutoa kitu ambacho biashara nyingine hazitoi. Kwa maneno mengine, usikazane kuwa bora zaidi ya wengine, bali kazana kuwa tofauti na wengine.
ReplyDelete