1. Andika kile ambacho kinatoka ndani ya moyo wako, kile ambacho unasukumwa kukiandika, na siyo kuandika kuwafurahisha watu.
2.
Tengeneza sauti yako ya uandishi, unaweza kuwa na waandishi au
mwandishi unayemkubali au kujifunza kwake, ukajikuta unaandika kama
yeye, huwezi kufika mbali kiuandishi, tafuta mtindo wako mwenyewe wa
uandishi, ambao utakutofautisha.
3.
Kazi ya uandishi kuna wakati ina upweke mkubwa, inakuhitaji uwe na muda
mwingi peke yako kuliko kazi wanazofanya wengine, lazima uwe tayari
kwenye hilo.
4. Unastahili na unapaswa kulipwa kupitia uandishi wako, usiache kuwataka watu walipie pale wanapotaka zaidi kutoka kwako.
5.
Chagua hadhira utakayoiandikia na cha kutaka kila mtu awe msomaji wako,
kama unalenga kila mtu huna unayemlenga. Jua kabisa unamwandikia mtu wa
aina gani, na hapo uandishi wako utagusa maisha ya mtu.
6.
Unaweza kuandika makala 100 nzuri kabisa, na watu wachache mno
wakakushukuru au kukupa moyo kwa unachofanya. Lakini ukaandika makala au
kutuma ujumbe mmoja ambapo umekosea na utashangaa kila mtu anakukosoa
na kukupinga. Hata watu ambao hawajawahi kukupa moyo kwa makala nzuri
100 ulizoandika, watakuwa wa kwanza kukuhukumu kwa makala moja mbaya
uliyoandika. Elewa hilo na usikubali likuumize.
7.
Sehemu kubwa ya wale wanaokukosoa kwenye uandishi ni wivu tu.
Wanatamani wangeandika, ila hawawezi kukaa chini na kuandika, wakiona
wewe unaandika wanatafuta makosa ya kuonesha kwamba wewe siyo bora
kuliko wao.
8.
Epuka sana kujisifia kila wakati kupitia uandishi wako, watu wana wivu,
kadiri unavyojisifia ndivyo wanavyotafuta makosa ya kukurudisha nyuma.
9.
Usisubiri ukamilifu, andika na toa, iwe ni makala au kitabu au
chochote, una nafasi ya kuboresha zaidi baadaye, kwa kutoa toleo la pili
na mengine mengi.
10.
Fanya uandishi kuwa kitu cha kwanza kwenye siku yako, andika kabla
hujaendelea na ratiba nyingine za siku yako. Ukishindwa kutenga muda wa
asubuhi na kuandika, ni vigumu sana kupata muda siku yako ikishaanza, na
pia siku inavyoenda unachoka, na akili ikishachoka, utajipa kila sababu
kwa nini usiandike.
Makala hii imeandikwa na KOCHA MWL JAPHET MASATU ambaye ni mwalimu kitaaluma ( B.Ed ( AE ) , Kocha wa MAISHA NA MAFANIKIO , MWANDISHI na MJASIRIAMALI , BLOGGER
WhatsApp + 255 716 924 136 / + 255 755 400128 / + 255 688 361 539
No comments:
Post a Comment