Iko
hivi rafiki, biashara huwa hazitofautiani sana, bali tamaa za watu
ndiyo zinatofautiana. Hakuna biashara ambayo ni nzuri zaidi ya nyingine,
bali uzuri wa biashara unategemea ni nani anayeifanya.
Msingi
wa kwanza wa kufanikiwa kwenye biashara yoyote ile, ni kuwa tayari
kujituma zaidi kwenye biashara hiyo zaidi ya wengine, kuijua kwa undani
kuliko wengine. Na hili linakuwa rahisi kama mtu ataipenda biashara
ambayo anaifanya, hapo atajituma zaidi na atapenda kuifuatilia kwa
karibu na hivyo kuijua zaidi.
Ili kuachana na umalaya wa fursa mpya, zingatia haya yafuatayo;
( 1 ). Anza na kusudi kuu la maisha yako.
Kabla
hujaamua ni biashara au kazi gani ufanye, jua lipi kusudi la maisha
yako. Unapaswa kujua ni kitu gani uko hapa duniani kukifanya. Na hili
utalijua kupitia vitu unavyopenda kufanya au vitu unavyovijali sana.
Hata vipaji ulivyonavyo vinaashiria kusudi lako.
Kwa
kulijua kusudi la maisha yako, hapo unaweza kuangalia ni biashara au
kazi gani inayoendana na kusudi hilo, na hivyo ukiifanya, utakuwa kwenye
nafasi nzuri ya kufanikiwa kuliko ukifanya kitu kingine.
( 2 ). Jiwekee maono makubwa.
Baada
ya kujua kusudi, unapaswa kujiwekea maono, kwamba miaka kadhaa ijayo
unajiona uko wapi. Jiwekee maono makubwa ya maisha yao, kwamba unajiona
ukiwa wapi, ili maisha yako yawe na maana, unajiona ukifanya nini kila
siku, maisha yako yakiwaje.
Ukishakuwa
na maono, ni rahisi kuchagua biashara zipi zinazokufikisha kwenye maono
hayo. Hutakimbilia kujaribu kila aina ya biashara, kwa sababu tayari
unajua wapi unapotaka kufika.
( 3 ). Weka malengo ya kufikia maono yako.
Maono
ni picha ya mbali, kitakachokufikisha kwenye picha hiyo ni malengo na
mipango ambayo unakuwa umejiwekea. Hivyo unapaswa kuweka malengo ya
kukufikisha kwenye maono uliyonayo.
Malengo
yanapaswa kuwa ya muda mfupi, miezi, mwaka, mpaka miaka 2 na ya muda
mrefu, miaka mitano, 10, 20 na kuendelea. Unapoweka malengo, unachagua
kwa uhakika unatakaje kufika kwenye maono uliyonayo. Hivyo hata biashara
utakazochagua, utaanza na malengo uliyojiwekea.
( 4 ). Komaa na malengo yako na mchakato wa kuyafikia.
Ukishakuwa
na malengo, sasa hiyo ndiyo ramani yako, usihangaike na kitu kingine
chochote. Wewe komaa na malengo uliyojiwekea na mchakato wa kuyafikia.
Unapokutana na fursa mpya jiulize je hii ipo kwenye malengo yangu, kama
haipo achana nayo na rudi kwenye malengo yako.
Malengo
yanakupa wewe nidhamu ya kusimamia kitu kimoja mpaka kitimie, kwa
sababu kuna muda uliojiwekea. Unahangaika na fursa mpya kila siku kwa
sababu hakuna malengo unayofanyia kazi, hivyo chochote kipya kinachokuja
huwezi kukikataa.
( 5 ). Acha tamaa na kutaka mafanikio ya haraka.
Rafiki,
nina habari ambazo siyo njema sana kwako, hakuna mafanikio rahisi, ya
haraka na yasiyohitaji kazi. Huo ni uongo ambao umewanasa wengi wenye
tamaa na kuishia kutapeliwa. Jua kabisa kwamba kila biashara inahitaji
kazi, muda, ujuzi na uvumilivu mkubwa. Haijalishi watu wanakuambia
inalipa kiasi gani, usidanganyike, jua hakuna mafanikio bila ya
uwekezaji mkubwa wa kazi, nguvu, muda na maumivu.
Hivyo
mtu anapokuja kwako na fursa mpya, akikuambia hii inalipa sana, muulize
ni gharama gani unapaswa kulipa kwa upande wa kazi, muda, ujuzi, nguvu
na hata maumivu. Kama atakuambia hii ni rahisi, huhitaji hata kufanya
kazi, kimbia haraka, unaingizwa kwenye utapeli.
( 6 ).Usisikilize maneno, angalia matokeo.
Mtu
anapokuja kwako na kukuambia fursa fulani inalipa sana na unapaswa
kuifanya, mwambie akuoneshe jinsi ambavyo yeye inamlipa. Kama ni fedha
akuoneshe hizo fedha alizonazo ambazo amepata kwenye fursa hiyo mpya.
Kadhalika kama ni mali pia akuoneshe.
Wengi
wanaotangaza fursa mpya na wanazosema zinalipa, wao wenyewe zinakuwa
hazijawalipa, ila wanakushawishi wewe uingie ili wanufaike kupitia wewe.
Mfano mtu anayekuambia kware ni fursa inayolipa, unakuta yeye ndiye
anayekuuzia mayai au kware wenyewe, hivyo ananufaika kupitia wewe
kuhamasika na fursa.
Chunga sana, unapoambiwa kuna fursa mpya, mara nyingi wewe ndiye unayekuwa fursa yenyewe.
( 7 ). Rudi kwenye msingi mkuu wa biashara ambao ni thamani.
Rafiki, msingi mkuu wa biashara ni huu; mabadilishano ya fedha kwa thamani.
Yaani kuna mtu mmoja ana fedha na ana uhitaji, halafu kuna mtu mwingine
anaweza kutimiza uhitaji wake na anahitaji fedha, hapo sasa ndipo
biashara inapofanyika. Kama hakuna thamani ambayo mtu anaihitaji, hakuna
biashara.
Hivyo
kwa kila fursa mpya unayokutana nayo, jiulize ni thamani gani ambayo
utatoa kwa watu wenye uhitaji na kisha wewe ukapata fedha. Ukianza na
biashara ya Forex ambayo imeulizwa hapa, jiulize kwa watu unaowafahamu
wewe, forex inaongeza thamani gani kwao kiasi kwamba watakuwa tayari
kukulipa wewe fedha. Utapata jibu ni hakuna.
Kadhalika
kwenye vitu unavyoambiwa ni fursa kama ufugaji wa kware au sungura,
jiulize wewe mwenyewe na wale wanaokuzunguka, ni lini umewahi kutafuta
sana nyama ya sungura kwa sababu unaipenda sana? Jibu ni hakuna, lakini
anakuja mtu anakuambia hii ni dili, na wewe unakubali!
Kama
unaambiwa kitu ni fursa, lakini wewe mwenyewe hujawahi kuwa na uhitaji
nacho, na hata wale wanaokuzunguka hawana uhitaji nacho, jua wewe ndiye
fursa rafiki yangu, na kaa mbali.
Rudi
kwenye msingi mkuu wa biashara, angalia kile ambacho tayari kina
uhitaji. Badala ya kukimbizana na kware au sungura, fanya ufugaji wa
kuku, kuku amekuwa kitoweo kwa kila mtu tangu enzi na enzi, huhitaji
kumfundisha mtu faida za kula kuku au mayai ndiyo akuelewe na kununua.
Ukiwa na kuku au mayai mazuri, kwa bei ambayo watu wanaweza kuimudu, una
biashara.
Rafiki,
watu wengi wanayumbishwa na fursa mpya kwa sababu hawana msimamo kwenye
maisha yao, hawajui wanataka nini na hawajajipanga ni kwa namna gani
watakipata, ndiyo maana kila kipya kinachokuja wanaona ndiyo tumaini
lao. Ondoka kwenye hali hiyo sasa na jua nini hasa unataka kwenye maisha
yako, jinsi gani utakipata na kisha kuwa na msimamo katika kuchukua
hatua. Kila la kheri.
Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako
Mwl Japhet Masatu
No comments:
Post a Comment