Kupata uhuru kamili kwenye maisha ni mtego ambao wengi wamekuwa wananasa.
Chukua
mfano huu, mtu aliyeajiriwa anafanya kazi kwa juhudi, ili atoe thamani
zaidi na hilo lipelekee yeye kulipwa zaidi. Kwa juhudi anazoweka,
mwajiri wake anaona anastahili kulipwa zaidi, hivyo anampandisha cheo na
kumwongezea mshahara. Lakini cheo anachopandishwa kinakuja na majukumu
zaidi, hivyo licha ya kipato kuongezeka, mtu huyo anazidi kukosa muda na
hivyo anakosa uhuru na maisha yake.
Kadhalika
kwenye biashara, mtu anaanza biashara ndogo, ambayo inampa muda mwingi
wa kufanya mambo yake, biashara inakua, wateja wanaongezeka na faida
inaongezeka pia, lakini hilo linamtaka atumie muda zaidi kwenye
biashara. Wingi wa wateja unakuja na changamoto nyingi za wateja hao
ambazo zinampa kazi zaidi. Hivyo licha ya biashara kukua na kipato
kuongezeka, uhuru unazidi kupungua kwa sababu muda wa kufanya mambo
mengine kwenye maisha yake unakuwa haupo.
Tusipokuwa
makini, tutakuwa tunakimbiza uhuru kama kipepeo ambacho kinakimbilia
maua mazuri, kila wakati utaona nikipiga hatua hii nitakuwa huru na
unaishia kukosa uhuru zaidi.
Ili
kuweza kupata uhuru kamili wa maisha yetu, ambao unajumuisha uhuru wa
muda, uhuru wa fedha na uhuru a eneo, kuna hatua nne za kuchukua.
Hatua hizi nne tumeshirikishwa na Tim Ferriss kwenye kitabu chake cha THE 4-HOUR WORK WEEK.
Hapa
nakwenda kukushirikisha hatua hizo nne kwa ufupi,
Karibu kwenye hatua nne za kuchukua ili kupata uhuru kamili wa maisha yako.
HATUA YA KWANZA NI D (DEFINITION)
Hapa
unabadili sheria na kanuni zote za mchezo wa kazi au biashara na
kujiwekea utaratibu wako mpya ambao utautumia kuendesha maisha ya
tofauti kwako kwenye eneo la kazi.
Baadhi
ya mambo ya kubadili ni kutokusubiri mpaka uzeeke ndiyo upate mapumziko
kupitia kustaafu, badala yake tengeneza mapumziko mafupi kwenye maisha
yako ya sasa.
Pia
jua maana halisi ya mafanikio kwako, unajipimaje kwamba umefanikiwa, na
siyo kujilinganisha na wengine au kuiga yale ambayo wengine wanafanya.
Kwa kifupi, jua hasa kile unachokitaka na jinsi ambavyo utakipata kwa namna ambayo ni bora kwako.
HATUA YA PILI NI E (ELIMINATION)
Hapa
unakwenda kufuta mambo yote yasiyo muhimu na ambayo yanachukua muda
wakoi mwingi, hivyo kubaki na machache muhimu ambayo yanachukua muda
wako mchache. Hapa ndipo unapokwenda kupunguza sana muda wako wa kazi na
kupata uhuru wa kwanza ambao ni MUDA.
Kuna sheria mbili ambazo Tim ametushirikisha kwenye hatua hii;
Sheria
ya kwanza ni ya Pareto (80/20) ambayo inasema asilimia 80 ya matokeo
inatokana na asilimia 20 ya juhudi, hivyo kuna mambo machache yanayoleta
matokeo makubwa na tunapaswa kufanya hayo tu.
Sheria
ya pili ni ya Parkinson, ambayo inasema jukumu huwa linameza muda ambao
limepangiwa, hivyo tunapaswa kujiwekea muda mdogo wa kukamilisha
majukumu yetu ili tuache kupoteza muda.
Kwenye uchambuzi wa kitabu hili utajifunza vizuri jinsi ya kutumia sheria hizi kwa pamoja ili ziwe na manufaa kwako.
HATUA YA TATU NI A (AUTOMATION)
Hapa
unatengeneza mpango wa kulipwa hata kama wewe haupo, unajenga misingi
ya kuiwezesha biashara au kazi yako kujiendesha yenyewe hata kama wewe
haupo na wewe kupokea fedha. Kupitia hatua hii, unapata uhuru wa pili
ambao ni FEDHA.
Kikwazo
cha kwanza kwenye uhuru wako ni wewe mwenyewe. Umeshajiweka sana kwenye
kile unachofanya kiasi kwamba hakiwezi kwenda bila ya wewe kuwepo na
ndiyo maana kila hatua unayopiga unazidi kupoteza uhuru wako.
Unapaswa kuweka mfumo unaoiwezesha kazi au biashara yako kujiendesha yenyewe hata kama wewe haupo.
HATUA YA NNE NI L (LIBERATION)
Hapa
unapata uhuru kamili wa maisha yako, kwa kuweza kuwa eneo lolote
duniani huku kazi au biashara yako ikiendelea kujiendesha yenyewe na
fedha zikiingia. Hapa unapata uhuru wa tatu ambao ni wa ENEO.
Baada
ya kuamua mafanikio yana maana gani kwako, kuachana na yasiyo muhimu na
kutengeneza mfumo wa biashara yako kwenda hata kama haupo, sasa unakuwa
huru na maisha yako, na unaweza kuchagua kuwa eneo lolote kwa wakati
wowote unaotaka wewe. Na huu ndiyo uhuru kamili ambao wengi hawapati
nafasi ya kuufikia kwenye maisha yao. Lakini wewe unaweza kuufikia kama
utafanyia kazi maarifa haya uliyoyapata.
Kwa
pamoja, hatua hizi nne zinatupa neno DEAL, ambapo ni kutengeneza mpango
mpya, kufuta yasiyo muhimu, kuiwezesha kazi kwenda bila wewe kuwepo na
kuwa huru kusafiri kwenda popote.
Katika
utekelezaji wa hatua hizi nne, Tim anashauri waliojiajiri kutumia
mtiririko huo wa DEAL, lakini walioajiriwa kutumia mtiririko wa DELA,
yaani kwa waajiriwa, kabla hajaweza kutengeneza njia ya kazi yake kwenda
bila ya yeye kuwepo, anapaswa kutengeneza kwanza uhuru wa kutokuwepo
kwenye kazi.
No comments:
Post a Comment