Sunday, January 12, 2020

HATUA 04 ZA KUJIJENGEA TABIA YA KUJISOMEA VITABU VIZURI

Rafiki yangu mpendwa,

Huwa tunajenga tabia, halafu tabia zinatujenga, chochote ambacho unafanya sasa, ni tabia ambayo umejijengea siku za nyuma.

Mafanikio au kushindwa kwako ni matokeo ya tabia zako. Kama ukiwa na tabia bora utafanikiwa na ukiwa na tabia mbovu utashindwa.

Moja ya tabia muhimu unazopaswa kujijengea ili uweze kufanikiwa ni tabia ya kujisomea, ambayo itakupa maarifa bora na utakapoyatumia utaweza kupiga hatua zaidi.

Wengi wamekuwa wanasema wangependa sana kusoma vitabu, lakini hawana muda wa kufanya hivyo. Na mimi nimekuwa nawaambia siyo kweli kwamba hawapati muda, ila tu hawajaamua kusoma vitabu.

Hebu niambie unapataje muda wa kula milo mitatu kila siku, kuoga, kufuatilia habari na hata kulala? Ni kwa sababu vitu hivyo umevipa kipaumbele na vimeshakuwa tabia kwako.

Kadhalika kwenye usomaji, ukiupa kipaumbele na kujenga tabia, utakuwa msomaji mzuri sana.

Kwa upande wa kipaumbele hilo lifanye kwa kujiwekea ratiba nzuri, kila siku tenga muda wa kujisomea, unaweza kuanza na nusu saa au saa moja na pia unaweza kwenda mpaka masaa mawili na zaidi.

Kwa upande wa kuijenga tabia ya kujisomea, hapa tunakwenda kujifunza hatua nne za kutumia kujenga tabia hii. Karibu ujifunze na uchukue hatua na utaweza kuwa msomaji mzuri na kunufaika na maarifa unayoyapata.

( 1 ).TENGENEZA MWONEKANO.
Sisi binadamu huwa tunafanya kile ambacho tunakiona, kile tusichokiona huwa hatuhangaiki nacho, huwa hata hakipati nafasi kwenye fikra zetu.

Hivyo ili mipango ya kusoma ipate nafasi kwenye fikra zetu, lazima tutengeneze mwonekano wa yale yanayohusiana na kusoma.

Kitu cha kwanza kufanya ni kuwa na kitabu popote pale unapokuwepo, na usikiweke kwenye begi lako, bali kishike mkononi. Kwa kuwa umebeba kitabu, ni rahisi kukifungua na kusoma kurasa chache pale unapopata muda, kuliko ukiwa huna kitabu.

Unafikiri kwa nini unashika simu yako muda mwingi? Ni kwa sababu uko nayo. Ukikaa kwenye foleni kidogo tu unatoa simu na kuangalia, sasa badili hilo kwa kuwa na kitabu.

Najua kuna vitabu vya nakala tete, lakini katika kujijengea tabia ya kusoma, kuwa na nakala ngumu na tembea nayo popote.

Njia nyingine ya kutengeneza mwonekano ni kuwa na maktaba ndogo nyumbani kwako. Kama nyumbani kwako una tv, basi pia unapaswa kuwa na vitabu, na viweke pembeni ya tv yako. Kwa kuiona tv ambayo inakuvutia kuangalia, pembeni yake utaviona vitabu ambavyo vitakukumbusha lengo lako la kusoma zaidi.

Je umekuwa unatumia simu ukiwa kitandani? Kama jibu ni ndiyo, basi ni kwa sababu unaenda na simu hiyo kitandani. Hapa pia kuna fursa ya kutumia mwonekano kusoma zaidi. Badala ya kwenda kitandani na simu, wewe nenda na kitabu. Soma kurasa chache kabla ya kulala. Na hata wale ambao usingizi unawasumbua, ukienda na kitabu kitandani utapata usingizi haraka sana.

Tengeneza mwonekano ambao unakufanya ukione kitabu kila wakati na hilo litakusukuma kusoma zaidi.

( 2). TENGENEZA MVUTO.
Huwa tunafanya kile ambacho kinatuvutia kufanya, hivyo kwenye kujenga tabia ya kusoma vitabu, ufanye usomaji kuwa na mvuto kwako.

Zipo njia mbalimbali unazoweza kuzitumia kutengeneza mvuto kwenye usomaji.

Anza kwa kuweka kusoma kama kigezo cha wewe kufanya kile ambacho unapenda kufanya. Mfano kama unapenda sana kuangalia tv, basi weka lengo kwamba utaweza kuangalia tv kama tu utakuwa umesoma kurasa 5 za kitabu. Hili linafanya usomaji uwe na mvuto kwako, kwa sababu unakupeleka kufanya kile unachopenda kufanya.

Njia nyingine unayoweza kutumia kutengeneza mvuto kwenye usomaji ni kujiunga na watu ambao ni wasomaji. Unapowaona wengine wanasoma, na wewe unasukumwa kusoma pia. Unapoona wengine wameshirikisha vitabu walivyosoma, na wewe unapata mvuto wa kusoma ili ushirikishe pia.

Tumia kila fursa unayoipata kuufanya usomaji uwe na mvuto kwake, kiwe kitu ambacho unapendelea kukifanya kabla ya kufanya vitu vingine.

( 3 ). UFANYE USOMAJI KUWA RAHISI.
Kitu chochote ambacho kina mlolongo mrefu huwa hatukipendi, na hivyo hatukifanyi. Kitu chochote ambacho kinahitaji nguvu au kinaumiza huwa tunakwepa kukifanya.

Hivyo ili kujijengea tabia ya kusoma vitabu, rahisisha usomaji wako, ufanye usomaji kuwa rahisi, kwa kupunguza milolongo na kuondoa kazi au maumivu kwenye usomaji.

Punguza milolongo kwa kujiwekea masharti machache, kwamba ukipata muda ambao ni kuanzia dakika 5 na kuendelea, basi utafungua kitabu na kusoma, na hapo kitabu umekibeba muda wote. Usijiambie ni mpaka uwe umekaa, uwe na vitu gani ndiyo usome, wewe jiambie unapopata muda utafungua kitabu na kusoma, kisha fanya hivyo.

Ondoa ugumu kwenye usomaji kwa kuyafanya mazingira kuwa rahisi kusoma. Kama umetenga ratiba ya kusoma kwa umakini, basi hakikisha unakuwa kwenye mazingira ambayo yanachochea hilo. Kuwa eneo tulivu na simu yako iwe kwenye ukimya. Ukipata dakika 10 za kusoma eneo ambalo husumbuliwi, utajifunza mengi kuliko saa nzima ya kusoma eneo ambalo unasumbuliwa na kukatishwa mara kwa mara.

Tumia teknolojia kurahisisha usomaji wako. Kama unasoma nakala tete, unaweza kuboresha zaidi usomaji wako kupitia programu mbalimbali. Mfano kuweka lengo la kufikia kurasa fulani, kukumbushwa kuhusu mpango wako wa kusoma na hata kuchukua kumbukumbu kwa urahisi wakati wa kusoma.

Angalia ni vitu gani vinakupa ugumu kwenye kusoma sasa, kisha ondoa ugumu huo na utaweza kujijengea tabia nzuri ya usomaji.

SOMA; Kama Unataka Kufanikiwa 2020 Achana Na Malengo Na Kazana Na Kitu Hiki Kimoja.

( 4 ). PATA UFAHARI KUPITIA USOMAJI WAKO.
Sisi binadamu huwa tunafanya kile ambacho kinatupa raha, na kuepuka kile ambacho kinatupa maumivu. Hivyo ili uendelee kufanya kitu, lazima kiwe kinakupa raha.

Na hivyo ndivyo ilivyo kwenye usomaji, hakikisha usomaji wako unakupa raha na hapo utasukumwa kusoma zaidi. Zipo njia mbalimbali za kupata raha kupitia usomaji.

Washirikishe wengine kile ambacho umejifunza. Unaposoma kitabu, chagua mambo yasiyopungua kumi ambayo unaweza kuwaambia watu umejifunza kwenye kitabu hicho. Washirikishe kwenye maongezi, kwa maandishi na njia nyinginezo.

Weka orodha ya vitabu ulivyosoma na washirikishe wengine. Nafikiri utakuwa umeona jinsi ambavyo mwisho wa mwaka kila mtu anaorodhesha vitabu alivyosoma, na jinsi watu wanavyowasifia kwa kuweza kusoma vitabu hivyo vingi. Litumie hili kwa manufaa yako pia, na usisubiri mpaka mwaka uishe, wewe unaweza kufanya kila siku, kila wiki, kila mwezi na kadhalika. Cha kufanya, piga picha kitabu unachosoma kisha weka kwenye mitandao unayotumia na waambie watu unasoma kitabu hicho. Watajitokeza watu wa kukusifia na hilo litakufanya ujisikie vizuri. Pia kila wiki au mwezi unaweza kuorodhesha vitabu ulivyosoma na watu wanavyokusifia au kujadili kunakufanya ujisikie vizuri na uendelee kusoma zaidi.

Njia nyingine ya kujisikia vizuri kwenye usomaji ni kutoa nukuu na mifano kutoka kwenye vitabu unavyosoma wakati wa maongezi. Unapokuwa unaongea na wengine au kujadiliana mtandaoni na kwingineko, jenga hoja zako kwa mifano na nukuu kutoka kwenye kitabu ulichosoma. Hii itakufanya ujisikie vizuri kwa ubora wa hoja utakazokuwa umeshirikisha.

No comments:

Post a Comment