Ushauri ni kitu ambacho unapaswa kuwa nacho makini sana wakati wa kutoa na hata kutokea.
Tuanze
na kutoa, kamwe usitoe ushauri kwa mtu ambaye hajakuomba umshauri,
unaweza kuona unamsaidia mtu huyo, lakini utakuwa unapoteza muda wako
bure. Watu huwa hawafanyii kazi ushauri ambao hawajautafuta wenyewe.
Unaweza kumwona mtu yupo kwenye hali fulani na kufikiri ushauri wako
utamsaidia, ukamshauri vizuri na ukashangaa hafanyii kazi yale
uliyomshauri. Hii ni kwa sababu mtu huyo hajawa na maumivu ya kutosha
kumsukuma kutaka kutoka pale alipo sasa na ushauri wako ni kelele tu
kwake. Mtu anayekuja kwako na kukuomba ushauri, ni mtu ambaye ameshaumia
vya kutosha na anataka njia ya kuondoka kwenye maumivu, huyu ukimshauri
anazingatia. Hivyo kama mtu hajakuomba ushauri, usijisumbue kutoa
ushauri wako.
Tukienda
kwenye kupokea ushauri, usichukue ushauri wa mtu ambaye hujamwomba
akushauri. Hii ni kwa sababu mtu anaweza kuona jambo fulani kwa nje na
akajumuisha kwamba tatizo lako ni hili na hatua za kuchukua ni hizi.
Lakini mtu huyo anakuwa hajajua kwa undani unapitia nini hivyo ushauri
huo unakuwa siyo sahihi. Kama unataka ushauri, mtafute mtu ambaye
unamwamini, mweleze kile unachopitia bila ya kuficha chochote, kisha
yeye awe na taarifa sahihi na kukushauri kwa usahihi. Lakini siyo ule
ushauri wa juu juu ambao watu wanatoa kwa kuona mambo ya nje bila kujua
yale ya ndani.
Huwa
nasema ushauri wa bure utaona gharama yake pale unapoanza kuufanyia
kazi. Huwa siyo ushauri sahihi. Hivyo chukua ushauri kwa watu ambao ni
sahihi, watu wenye uzoefu au ujuzi na ambao wanaielewa hali yako. Na
siyo kuchukua ushauri kwa kila anayekuambia ungefanya hivi au ungefanya
vile. Kadhalika usikimbilie kutoa ushauri kwa mtu ambaye hajakuomba, kwa
sababu unakuwa hujaelewa kwa undani anapitia nini na utakachomshauri
hatofanyia kazi.
Wapo
wanaosema mbona mimi natoa ushauri kupitia makala hizi wakati
sijaombwa. Ukweli ni kwamba mimi sijakuletea maarifa haya nyumbani
kwako, au kukulazimisha usome, bali wewe umeyatafuta au kukutana nayo na
kuona yanakufaa, hivyo ukasoma. Kuna wengi wanakutana na maarifa haya,
lakini wanayapita, kwa sababu hayana maana au umuhimu kwao. Lakini wewe
umeyapokea, kwa sababu kuna kitu unatafuta na hivyo unayathamini. Hivyo
wajibu wangu ni kushirikisha maarifa sahihi ambayo mtu akiyatumia
anaweza kupiga hatua kwenye maisha yake, lakini siwezi kumlazimisha mtu
asome au kuchukua hatua.
No comments:
Post a Comment