Habari
nyingi ni hasi au zenye kuibua hisia kwa wafuatiliaji wake. Fungulia
chombo chochote cha habari au tembelea mtandao wowote unaotoa habari na
utaona habari gani zinapewa kipaumbele. Ni habari za kutisha au
kusisimua. Habari za mauaji, ajali, mapigano, wizi, utekaji, ukatili na
nyingine kama hizo.
Unapoianza
siku yako kwa habari za aina hii, unavuruga kabisa akili yako.
Unajikuta umepata hasira au kukata tamaa na kuona dunia haina maana.
Hata mambo ambayo ulipanga kuyafanya hutaweza kuyafanya kwa hamasa kubwa
pale ambapo umeshakutana na habari za kutisha au kukatisha tamaa.
Ndiyo
maana nakushauri usianze siku yako kwa habari, sijakuambia usifuatilie
kabisa habari (japo hilo ni jema ukiliweza), ila usianze nazo kwenye
siku yako. Anza siku yako kwa kusali/kutahajudi, kusoma vitabu,
kupangilia siku yako na kisha kuanza majukumu muhimu kwako kikazi au
kibiashara. Mwisho wa siku wakati umeshakamilisha yale muhimu, hapo sasa
unaweza kupitia habari ili ujue nini kinaendelea.
Ukifanya
hivi utajikuta unakuwa na siku tulivu, siku ambayo umeweka umakini wako
kwenye yale muhimu kwako kufanya na siyo kuvurugwa na habari za mambo
yanayoendelea, ambayo hayakuhusu moja kwa moja.
Wapo
wanaosema ni muhimu kuanza na habari kwa sababu kunaweza kuwa na kitu
muhimu unapaswa kujua kabla siku haijaanza, labda kuna daraja
limeharibika hivyo usipoanzana habari hutajua. Nasema hiyo siyo sababu
yenye mashiko ya kuruhusu siku yako ichafuliwe na habari nyingi hasi. Na
nikuambie kitu kimoja rafiki yangu, kama kuna habari muhimu kweli,
itakufikia hata kama hufuatilii habari. Tukienda na mfano huo wa daraja
kuharibika, hivi unafikiri unahitaji chombo cha habari kujua hilo? Kila
mtu atakuwa anazungumzia hilo na hivyo utajua tu.
Kadhalika
kwa habari nyingine ambazo ni muhimu, wale wanaokuzunguka watakuwa
wanazizungumzia, hivyo kama ni kitu chenye umuhimu utakijua tu.
Usikubali kuharibu siku yako kwa kuanza na habari, anza siku yako kwa mipango yako na kisha imalize kwa habari.
No comments:
Post a Comment