Monday, December 30, 2019

VITABU VIZURI VYA KUSOMA----HITS THE BOOKS

  1. THE SCIENCE OF GETTING RICH Kilichoandikwa Na Wallace D. Wattles; Kila mtu anaweza kuwa tajiri bila ya kujali mazingira, kipato, kipaji au hata shughuli anayofanya. Ipo namna ya kufikiria na kufanya ambayo kila mtu anaweza kuitumia na akapata utajiri mkubwa kwenye maisha yake.
  2. THE MASTER KEY SYSTEM Kilichoandikwa Na Charles Haanel. Hiki ni kitabu ambacho kinatufundisha jinsi ya kutumia nguvu kubwa iliyopo ndani yetu kuweza kupata chochote tunachotaka kwenye maisha yetu. Nguvu hii kubwa iliyopo ndani yetu, ni fikra zetu.
  3. THE 5 AM CLUB; Own Your Morning, Elevate Your Life kilichoandikwa na Robin Sharma ambaye anatushirikisha umuhimu wa kuianza siku yako asubuhi na mapema, wakati watu wengine bado wamelala. Anasema kwa kuimiliki asubuhi yako, utaweza kuyainua zaidi maisha yako.
  4. MILLIONAIRE SUCCESS HABITS: The Gateway To Wealth & Prosperity Ambacho Kimeandikwa Na Milionea Dean Graziosi. Kitu pekee kinachokuzia wewe usipate yale matokeo ambayo wengine wanayapata, ni tabia ambazo unaziishi sasa. Kama ukijua tabia za waliofanikiwa na ukaziishi, basi utaweza kupata matokeo ambayo wanayapata.
  5. HABITS OF A HAPPY BRAIN: Retrain Your Brain to Boost Your Serotonin, Dopamine, Oxytocin, & Endorphin Levels ambacho kimeandikwa na Loretta Graziano Breuning. Ubongo unazalisha kemikali nne ambazo ndizo zinaleta furaha kwenye maisha yetu. Kemikali hizi zinatofautiana kwa ufanyaji wake wa kazi, lakini mwisho wa siku zote zinaishia kuleta furaha. Kemikali hizo ni dopamini, serotonini, oksitosini na endofini.
  6. THE BLUE ZONES; Lessons For Living Longer From The People Who’ve Lived The Longest ambacho kimeandikwa na Dan Buettner. Kupitia utafiti wa mwandishi wa kitabu cha THE BLUE ZONES, yapo maeneo manne duniani ambayo yameonesha kuwa na watu wanaoishi miaka mingi kuliko maeneo mengine. Maeneo hayo ni Sardinia nchini Italy, Okinawa nchini Japan, Loma Linda Calfornia nchini Marekani na Nicoya nchini Costa Rica. Mwandishi ameshirikisha masomo ambayo ameondoka nayo kwenye kila eneo na jinsi ya kuyatumia kwenye maisha yetu ili tuweze kuishi miaka mingi.
  7. FLOW: The Psychology of Optimal Experience kilichoandikwa na Mihaly Csikszentmihalyi. Kitabu hichi kinatufundisha jinsi ambavyo tunaweza kufikia ufanisi mkubwa na furaha kwenye chochote ambacho tunafanya, iwe kikubwa au kidogo, tunakipenda au hatukipendi.
  8. PEAK; Secrets from the New Science of Expertise kilichoandikwa na Anders Ericsson. Kitabu hiki kinatupa siri za kisayansi za kuweza kufikia ubobezi mkubwa kwenye kitu chochote tunachochagua kufanya kwenye maisha yetu. Kitabu hiki kimetokana na tafiti mbalimbali ambazo zimefanywa kwenye eneo la ubobezi na hivyo kimekuja na majibu sahihi ya hatua unazopaswa kuchukua ili kufikia ubobezi.
  9. 21 LESSONS FOR THE 21ST CENTURY ambacho kimeandikwa na mwanahistoria Yuval Noah Harari. Kwenye kitabu hiki, Yuval amezichambua changamoto kubwa 21 zinazotukabili kwenye karne hii ya 21 na kupendekeza hatua tunazopaswa kuchukua ili tusiachwe nyuma na mabadiliko yanayotokea kwa kasi kubwa.
  10. BECOMING SUPERNATURAL: How Common People Are Doing the Uncommon kilichoandikwa na Dr. Joe Dispenza. Hiki ni kitabu ambacho kinatufundisha namna ya kutumia nguvu kubwa iliyopo ndani ya kila mmoja wetu kufanya makubwa na miujiza kwenye maisha yetu.
  11. STEALING FIRE: How Silicon Valley, the Navy SEALs, and Maverick Scientists Are Revolutionizing the Way We Live and Work kilichoandikwa na waandishi Steven Kotler na Jamie Wheal. Hiki ni kitabu kinachotuonesha mapinduzi makubwa ya kiutambuzi yanayoendelea duniani, ambayo wachache wanaoyaelewa wanayatumia kufanya makubwa sana kwenye kazi zao na hata maisha yao kwa ujumla.
  12. THE CODE OF THE EXTRAORDINARY MIND: 10 Unconventional Laws to Redefine Your Life and Succeed On Your Own Terms ambacho kimeandikwa na Vishen Lakhiani. Hiki ni kitabu ambacho kinatupa mtazamo wa tofauti kabisa wa namna tunavyoyachukulia maisha yetu. Katika kitabu hiki tunajifunza kwa nini sheria na kanuni nyingi tunazoziishi siyo sahihi au zimepitwa na wakati. Na muhimu zaidi, kitabu kinatufundisha jinsi ya kuwa na maisha yasiyo ya kawaida, yaani kuwa na maisha ya kipekee kwetu, kwa namna tunavyotaka sisi wenyewe.
  13. CAN’T HURT ME: Master Your Mind and Defy the Odds ambacho kimeandikwa na Mwanajeshi mstaafu David Goggins. Kupitia historia na magumu aliyopitia kwenye maisha yake mpaka kufikia ukomando, Goggins anatushirikisha jinsi ya kutangaza vita na maisha yetu wenyewe ili kufanikiwa. Kwenye kitabu hiki tunajifunza jinsi ya kwenda kwenye vita dhidi yetu wenyewe, yaani tunakwenda kupambana na sisi wenyewe, ili tuache kujihujumu na kujirudisha nyuma, tufungue uwezo wetu mkubwa na kuutumia kufanikiwa zaidi.
  14. SEEKING WISDOM; From Darwin to Munger kilichoandikwa na Peter Bevelin. Mwandishi amefanya kazi kubwa ya kukusanya hekima za watu mbalimbali walioweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yao na kwenda kinyume na mazoea. Kuanzia mwanabaiolojia Charles Darwin ambaye alileta mapinduzi makubwa kwenye baiolojia kwa kufikiri tofauti, mpaka kwa mwanafalsafa mwekezaji Charles Munger ambaye pamoja na mshirika wake Warren Buffett wameweza kupata mafanikio makubwa sana kwenye uwekezaji, kuliko wawekezaji wengine wote.
  15. THE LAWS OF HUMAN NATURE ambacho kimeandikwa na Robert Greene. Kwenye kitabu hiki, Green ametupa sheria 18 za kuijua asili ya binadamu, akitupa mifano halisi iliyowahi kutokea kwa watu waliozingatia sheria hizi na wakafanikiwa au walizipuuza na kushindwa.
  16. HOW TO GET RICH: One of the World’s Greatest Entrepreneurs Shares His Secrets ambacho kimeandikwa na Felix Dennis. Felix Dennis alikuwa mjasiriamali mwenye mafanikio makubwa sana katika sekta ya uchapishaji wa majarida. Felix alianzia chini kabisa, bila ya elimu kubwa wala mtaji, lakini aliweza kuingia kwenye biashara ya uchapishaji wa majarida na kuweza kuwa tajiri mkubwa sana nchini Uingereza. Katika kitabu hiki, Felix anatushirikisha safari ya mafanikio yake, makosa aliyofanya, bahati alizopata na ushauri muhimu kwa wote ambao wanataka kupata utajiri kwenye maisha yao.
  17. YOUR BRAIN AT WORK: Strategies for Overcoming Distraction, Regaining Focus, and Working Smarter All Day Long ambacho kimeandikwa na David Rock. Kwenye kitabu hiki, David ametushirikisha yale muhimu unayopaswa kujua kuhusu ubongo wako, jinsi unavyofanya kazi na njia bora ya kuutumia ili kuondokana na usumbufu, kuongeza umakini na kufanya kazi zako vizuri pamoja na kuwa na utulivu siku nzima.
  18. TRACTION; Get A Grip On Your Business kilichoandikwa na Gino Wickman. Kwenye kitabu hiki, Gino anatuambia kama tutazingatia maeneo sita muhimu ya biashara ambayo ameyafundisha, biashara zetu zitakua na kuwa huru, kiasi kwamba hazitegemei uwepo wetu wa moja kwa moja ndiyo ziweze kwenda.
  19. THE BULLETPROOF DIET: Lose Up to a Pound a Day, Reclaim Energy and Focus, Upgrade Your Life, Kilichoandikwa na Dave Asprey. Kwenye kitabu hiki, Dave siyo tu anatupa dayati ya kufuata, bali anatusaidia kujenga mfumo mpya wa maisha kwenye ulaji. Huu ni mfumo ambao mtu ukiufuata, unapunguza uzito wa mwili bila ya shida, unakuwa na nguvu muda wote na afya yako inakuwa bora. Mpangilio wa ulaji aliouweka kwenye kitabu hiki unaupatia mwili virutubisho sahihi unavyohitaji na kuzuia mwili kwenda kwenye hali ya uhitaji mkubwa ambao unawasukuma wengi kula zaidi na kuongeza uzito.
  20. THE E-MYTH REVISITED: Why Most Small Businesses Don’t Work and What to Do About It, mwandishi Michael E. Gerber anatupa maarifa sahihi ya kutuwezesha kuanzisha na kuendesha biashara zetu kwa mfumo ambao zinafanya vizuri na kutupa uhuru mkubwa. Michael anasema uhuru kwenye biashara upo kwenye mfumo. Kama unaendesha biashara na huna mfumo, huna biashara, bali una kazi, na hiyo ni kazi mbaya kuliko zote.
  21. WHAT GOT YOU HERE WON’T GET YOU THERE: How Successful People Become Even More Successful mwandishi Marshall Goldsmith anatuonesha jinsi ambavyo tabia zetu zinatuzuia kufanikiwa zaidi. Anaanza kwa kutuonesha jinsi ambavyo tabia zetu zinakuwa kikwazo kwetu, kisha anatupa hatua saba za kujenga tabia bora kwa mafanikio yetu.
  22. DIGITAL MINIMALISM: Choosing a Focused Life in a Noisy World ambacho kimeandikwa na Cal Newport. Mwandishi Cal Newport baada ya kuona changamoto kubwa ya simu janja na mitandao ya kijamii kwa wengi, amekuja na falsafa bora ya matumizi mazuri ya mitandao hii, ambayo itakuwa na manufaa kwetu na kuondokana na madhara ya mitandao hii. Falsafa hii haibadili kitu kimoja kwenye matumizi yetu ya simu janja na mitandao ya kijamii, bali inabadili mfumo wetu mzima wa maisha na jinsi tunavyoichukulia na kuitumia mitandao hii. Falsafa hii anaiitwa DIGITAL MINIMALISM na ameieleza kwenye kitabu hiki.
  23. THE URBAN MONK: Eastern Wisdom and Modern Hacks to Stop Time and Find Success, Happiness, and Peace  ambacho kimeandikwa na Pedram Shojai. Pedram amekuwa mtawa wa falsafa ya Taoism na pia daktari wa tiba za mashariki. Kupitia uzoefu wake wa utawa na kutibu watu, amegundua kuna changamoto kubwa kumi ambacho tunazipitia binadamu kwa zama tunazoishi. Changamoto hizo ni msongo, muda, nguvu, usingizi, mtindo wa maisha wa kukaa, ulaji, kutengana na asili, upweke, fedha na kukosa kusudi la maisha. Kupitia kitabu chake, Pedream amejadili kila changamoto na kutupa hekima za kuzikabili changamoto hizo kutoka kwenye falsafa za mashariki.
  24. HIGH PERFORMANCE HABITS: How Extraordinary People Become That Way ambacho kimeandikwa na kocha wa mafanikio Brendon Burchard. Kwenye kitabu hiki, Brendon ametushirikisha hatua sita za kujijengea kama tunataka kufanikiwa zaidi. Pia ametutahadharisha na tabia tatu zinazoharibu kabisa mafanikio yetu na tabia moja kuu inayobeba tabia zote za mafanikio.
  25. BUILT TO SELL: Creating a Business That Can Thrive Without You ambacho kimeandikwa na mwandishi John Warrillow. Kupitia kitabu hiki, John ametushirikisha hatua nane za kutengeneza biashara inayoweza kujiendesha bila ya uwepo wako na pia unayoweza kuiuza na kupata fedha zaidi.
  26. THE CHECKLIST MANIFESTO: How to Get Things Right ambacho kimeandikwa na Daktari bingwa wa upasuaji Atul Gawande. Kwenye kitabu hiki, Atul ametuonesha jinsi ambavyo sisi binadamu tunafanya makosa kwenye kazi zetu za kila siku, na njia rahisi ya kupunguza makosa hayo ambayo ni kutumia orodha (checklist).
  27. 101 CRUCIAL LESSONS THEY DON’T TEACH YOU IN BUSINESS SCHOOL kilichoandikwa na Chris Haroun. Kwenye kitabu hiki tumejifunza siri 101 za mafanikio kwenye biashara na maisha kwa ujumla ambazo hazifundishwi kwenye shule ya biashara.
  28. JUST RUN IT!: Running an Exceptional Business is Easier Than You Think kilichoandikwa na Dick Cross. Kupitia kitabu hiki tunajifunza mfumo rahisi wa kuendesha biashara yenye mafanikio makubwa huku ukiwa na uhuru.
  29. THE MIRACLE MORNING: The Not-So-Obvious Secret Guaranteed to Transform Your Life: Before 8AM, ambacho kimeandikwa na Hal Elrod. Kupitia kitabu hiki, Hal anatuonesha kwamba nguvu ya kuyabadili maisha yetu, kutoka umasikini na ukawaida mpaka kufika utajiri na mafanikio ipo ndani yetu. Na kwa kuwa kila mtu analalamika kwamba hana muda, Hal ametuonesha jinsi ambavyo kwa kutenga saa moja tu kila siku na kufanya vitu sita muhimu sana, maisha yako yanaweza kubadilika.
  30. STAND OUT: How to Find Your Breakthrough Idea and Build a Following Around It ambacho kimeandikwa na Dorie Clark. Kwenye kitabu hiki mwandishi anatushirikisha jinsi ambavyo tunaweza kujitofautisha na wengine kwa kile tunachofanya. Mwandishi anatufundisha njia ya kubobea sana kwenye kile tunachofanya kwa namna ambayo tutakuwa viongozi ambao wengine wanatuangalia na kujifunza kutoka kwetu (thought leader).
  31. GETTING EVERYTHING YOU CAN OUT OF ALL YOU’VE GOT: 21 Ways You Can Out-Think, Out-Perform, and Out-Earn the Competition ambacho kimeandikwa na kocha wa biashara Jay Abraham. Kwenye kitabu hiki, Jay ametushirikisha njia 21 za kuweza kufikiri, kufanya na kutengeneza kipato zaidi kuliko wengine kupitia kazi au biashara tunazofanya.
  32. THE ART OF PUBLIC SPEAKING ambacho kimeandikwa na waandishi Dale Carnegie na J. Berg Esenwein. Kwenye kitabu hiki, waandishi wametushirikisha maarifa na mbinu sahihi za kuweza kuongea mbele ya wengine kwa kujiamini na kwa ushawishi ili tuweze kupata kile tunachotaka na hata kuwanufaisha wengine pia.
  33. HOW TO WRITE COPY THAT SELLS; The Step-By-Step System For More Sales, to More Customers, More Often kilichoandikwa na Ray Edwards. Mwandishi Ray ni mmoja wa waandishi mashuhuri wa matangazo na nakala za mauzo. Kupitia kitabu hiki anatushirikisha siri na mbinu muhimu ambazo tukizielewa na kuzitumia tutaweza kuandika nakala bora kabisa za kuuza chochote tunachouza.
  34. TO SELL IS HUMAN: The Surprising Truth About Moving Others kilichoandikwa na Daniel H. Pink. Kwenye kitabu hiki, mwandishi anatuonesha kwamba kila mtu sasa yupo kwenye mauzo na kwamba mauzo kwa sasa yamebadilika sana. Anatushirikisha misingi mipya ya kufanikiwa kwenye uuzaji pamoja na mbinu sahihi za kupata ushawishi kwa wengine.
  35. HOW TO BE A STOIC: Using Ancient Philosophy to Live a Modern Life kilichoandikwa na mmoja wa wastoa wa zama zetu Massimo Pigliucci. Ustoa ni Falsafa ambayo imekuwepo kwa zaidi ya miaka elfu mbili sasa, ambayo lengo lake kubwa limekuwa kuwafanya watu kuwa na maisha bora, kwa kuishi kwa misingi sahihi. Hii ni falsafa ambayo kila mtu akiweza kuielewa na kuiishi basi lazima atakuwa na maisha bora.
  36. RICH DAD’S BEFORE YOU QUIT YOUR JOB: 10 Real-Life Lessons Every Entrepreneur Should Know About Building a Multimillion-Dollar Business ambacho kimeandikwa na Robert Kiyosaki. Kwenye kitabu hiki, Kiyosaki ametushirikisha mambo 10 ambayo mtu anapaswa kuwa na maandalizi nayo kabla hajatoka kwenye ajira na kwenda kujiajiri. Wapo watu wengi ambao wapo kwenye ajira, wanatamani sana kutoka na kwenda kujiajiri, lakini wakiwaangalia wale waliowahi kutoka kwenye ajira na kwenda kujiajiri, wanapatwa na hofu kubwa. Kwa sababu wengi wanakuwa hawajapiga hatua kubwa. Sasa iwe upo kwenye ajira na unataka kwenda kujiajiri au tayari umeshajiajiri, masomo haya kumi tunayokwenda kujifunza hapa yatakusaidia sana kuanzisha na kukuza biashara yako.
  37. FREELANCE TO FREEDOM: The Roadmap for Creating a Side Business to Achieve Financial, Time and Life Freedom kilichoandikwa na mpiga picha aliyeweza kutoka kwenye ajira mpaka kujiajiri mwenyewe na kufikia mafanikio makubwa. Mpiga picha huyo ni  Vincent Pugliese akishirikiana na mke wake Elizabeth katika safari ya kutoka kwenye utumwa wa ajira pamoja na madeni mpaka kufikia uhuru wa kifedha, muda na hata maisha kwa ujumla. Kwenye hiki, Vicent anatushirikisha safari nzima ya maisha yake ya kutoka kwenye utumwa mpaka kwenye uhuru.
  38. RANGE: Why Generalists Triumph In A Specialized World kilichoandikwa na David Epstein. Kwenye kitabu hiki, David ametuonesha jinsi ambavyo hadithi ya kubobea haraka ambayo imekuwa inatumiwa na wengi kama mfano wa mafanikio isivyo sahihi. Ametushirikisha kwa kina jinsi ambavyo kutokubobea kwenye jambo moja kuna manufaa makubwa kwa mtu, hasa kwa maisha na mafanikio ya baadaye.
  39. STREET SMARTS: An All-Purpose Tool Kit for Entrepreneurs kilichoandikwa na waandishi na wafanyabiashara wawili ambao ni Norm Brodsky na Bo Burlingham. Norm na Bo wana uzoefu wa muda mrefu katika kuanzisha na kukuza biashara, na kupitia kitabu hiki wametushirikisha uzoefu wao katika biashara, wametupa mafunzo muhimu ambayo tukiweza kuyatumia tutapiga hatua sana kwenye biashara zetu. Kitabu hiki kina sura 17 na mwisho wa kila sura kuna mambo manne muhimu ya kuondoka nayo na kwenda kuyafanyia kazi.
  40. PROFIT FIRST: A Simple System To Transform Any Business From A Cash-Eating Monster To A Money-Making Machine kilichoandikwa na Mike Michalowicz. Mike anatuambia biashara nyingi zimekuwa zinaendeshwa bila ya kutengeneza faida, kitu kinachopelekea biashara hizo zife. Hivyo anatuambia njia pekee ya kuendesha biashara yenye mafanikio, ni kwa kuanza kupata faida kwanza kabla ya mengine yote. Mike anasema, faida kwenye biashara inapaswa kuanza kupatikana siku ya kwanza unapoanza biashara, na siyo kusubiri mpaka siku zijazo.
  41. SMALL GIANTS: Companies That Choose to Be Great Instead of Big ambacho kimeandikwa na Bo Burlingham. Kitabu hiki kimeandikwa kupitia utafiti uliofanyika kwa biashara ambazo zimechagua kuwa bora badala ya kuwa kubwa. Hizi ni biashara ambazo zilikuwa na nafasi ya kukua zaidi lakini wamiliki wa biashara hizo kuchagua kuzifanya zibaki kuwa biashara ndogo ambazo ni bora zaidi. Kwenye kitabu hiki utajifunza jinsi ambavyo tunaweza kuendesha biashara yako kwa ubora hata kama ni ndogo.
  42. FINANCIAL INTELLIGENCE; A Manager’s Guide to Knowing What the Numbers Really Mean kilichoandikwa na waandishi na washauri wa biashara Karen Berman, Joe Knight na John Case. Kupitia kitabu hiki tunajifunza kwa kina kuhusu namba za biashara na taarifa za kifedha unazopaswa kuzijua na kuzielewa. Haijalishi kama umeajiriwa, unafanya biashara au umejiajiri mwenyewe, bila ya kuzijua namba za biashara kwenye kile unachofanya, huna tofauti na mtu anayetembea gizani huku amefungwa kitambaa machoni.
  43. THIS IS MARKETING: You Can’t Be Seen Until You Learn To See kilichoandokwa na Seth Godin. Seth Godin anasifika kama mmoja wa wabobezi wa masoko katika zama tunazoishi sasa. Seth amekuwa akihubiri aina ya tofauti ya masoko, ambayo haimlengi kila mtu, bali inachagua kulenga watu wachache. Kwenye kitabu hiki, tunajifunza namna bora ya kufanya masoko yenye tija kwenye biashara zetu na maisha kwa ujumla, kwa sababu kila kitu kwenye maisha yetu kinahusu masoko.
  44. TRILLION DOLLAR COACH: The Leadership Playbook of Silicon Valley's Bill Campbell, kitabu hiki kimeandikwa na Alan Eagle, Eric Schmidt, na Jonathan Rosenberg. Hawa ni wakurugenzi wa makampuni ya teknolojia ambao waliwahi kufanya kazi na Kocha Bill Campbell ambaye ana mchango mkubwa sana kwenye ukuaji wa makampuni makubwa ya teknolojia duniani ambayo ni Google, Apple, Amazon, Facebook, Intuit na mengine mengi. Kitabu hiki kimeeleza maisha ya Bill pamoja na misingi yake ya ukocha wa mafanikio.
  45. THE INTELLIGENT ENTREPRENEUR: How Three Harvard Business School Graduates Learned the 10 Rules of Successful Entrepreneurship kilichoandikwa na Bill Murphy Jr. Kitabu hiki ni tofauti kabisa na vitabu vingine vya ujasiriamali, kwani kimetushirikisha sheria kumi za kufanikiwa kwenye ujasiriamali, kupitia hadithi za wajasiriamali watatu waliofuatiliwa kwa kipindi cha miaka kumi. Wajasiriamali hao walikuwa wahitimu wa shahada ya uzamili ya biashara (MBA) kutoka shule ya biashara ya chuo kikuu cha Havard (Havard Business School).
  46. START SMALL FINISH BIG: 15 Key Lessons to Start and Run Your Own Successful Business. Kitabu hiki kinaelezea hadithi ya aliyekuwa mwanzilishi wa migahawa inayoitwa SubWay ambayo ni migahawa maarufu duniani kwa vyakula vya haraka. Mwanzilishi huyo ambaye alikuwa ni Fred DeLuca aliweza kuanzisha biashara hiyo akiwa na umri wa miaka 17 pekee, kwa mtaji mdogo wa dola elfu moja (mwaka 1965) ambao alikopeshwa na rafiki yake.
  47. IT STARTS WITH PASSION: Do What You Love and Love What You Do ambacho kimeandikwa na Keith Abraham. Kupitia kitabu hiki Keith anatufundisha kwamba, hatuwezi kufanikiwa kwenye maisha kama hatupendi kile ambacho tunakifanya. Kama ndani yetu hakuna msukumo mkubwa unaoanza na upendo, hatuwezi kuhimili mikiki mikiki na changamoto tutakazokutana nazo kwenye safari ya mafanikio. Hivyo tunapaswa kujua kile ambacho tunakipenda na kukifanya na kama hatujui tunachopenda, basi chochote ambacho tunakifanya, tukipende sana.
  48. INDISTRACTABLE: How To Control Your Attention And Choose Your Life, ambacho kimeandikwa na Nir wa Eyal. Nir ni mtaalamu teknolojia na mwanasaikolojia pia, mtu ambaye amesoma tafiti nyingi zinazohusisha jinsi saikolojia wa mwanadamu inavyoweza kutekwa na kuwa tegemezi wa teknolojia. Kwenye kitabu chake cha INDISTRACTABLE, Nir anatuonesha jinsi ambavyo tunaweza kuondokana na mitego ya kisaikolojia iliyowekwa na makampuni ya teknolojia na kuweza kunasa umakini wetu na kuleta usumbufu kwetu.
  49. STILLNESS IS THE KEY ambacho kimeandikwa na Ryan Holiday. Ryan amekuwa akiandika vitabu vyake kutoka kwenye msingi wa falsafa ya ustoa na kuiweka kwa namna ambayo tunaweza kuiishi na kunufaika nayo kwenye zama tunazoishi sasa. Kwenye kitabu cha STILLNESS IS THE KEY, Ryan ametuonesha nguvu kubwa iliyopo kwenye utulivu, ambayo tukiijua na kuweza kuitumia basi itakuwa ufunguo wa mambo mengi kwenye maisha yetu. Tangu enzi na enzi, ukiangalia kila aina ya falsafa au dini, utulivu umekuwa unasisitizwa sana. Ni kupitia utulivu ndiyo tunaweza kufikiri sawasawa, kuiona picha kubwa na kujua hatua sahihi za kuchukua.
  50. THE SUBTLE ART OF NOT GIVING A F*CK: A Counterintuitive Approach to Living a Good Life ambacho kimeandikwa na Mark Manson. Kama jina lilivyo, mwandishi anatufundisha jinsi ya kuacha kujali yale yasiyotuhusu. Anachotuambia ni kwamba, maisha yetu yanakuwa magumu kwa sababu tunahangaika na mambo yasiyotuhusu au yaliyo nje ya uwezo wetu. Pia ameeleza jinsi ambavyo ushauri wa wahamasishaji wengi unavyowafanya watu wengi kuwa watumwa na kushindwa kuwa na maisha bora.
  51. SAPIENS: A Brief History of Humankind kilichoandikwa na mwanahistoria Yuval Noah Harari. Yuval amefanya kazi kubwa ya kuchimba historia kamili ya binadamu tangu miaka 70,000 iliyopita ambapo ndipo historia ya binadamu imeanza kuhesabiwa wakati mapinduzi ya kifikra yalipotokea. Miaka 12,000 iliyopita ndipo mapinduzi ya kilimo yalipotokea na miaka 500 iliyopita, mapinduzi ya sayansi yalianza, ambayo ndiyo tunayaishi mpaka sasa. Kwenye kila mapinduzi ambayo tumepitia, Yuval ameonesha mafanikio na changamoto mbalimbali.
  52. FOOLED BY RANDOMNESS: The Hidden Role of Chance in Life and in the Markets kilichoandikwa na mwanahisabati, mwanafalsafa na mwekezaji Nassim Nicholas Taleb. Taleb ameandika kitabu hiki kwa kushirikisha uzoefu wake kwenye uwekezaji kwenye soko la hisa, ambapo wachache wanaochukuliwa wamefanikiwa sana siyo kwa sababu ya ujanja wao au juhudi zao, bali ni kwa bahati tu. Taleb anakwenda mbali zaidi na kuonesha kwamba katika kila eneo la maisha, kuna bahati ambazo watu wanakutana nazo na zinawasaidia kupiga hatua. Lakini wakishapiga hatua wanasahau bahati hizo na kuona ni juhudi zao wenyewe. Kwa sisi kujua mchango wa bahati kwenye maisha yetu, tunaweza kujiweka kwenye upande mzuri wa bahati kuwa na manufaa kwetu.
  53. ATOMIC HABITS: An Easy & Proven Way to Build Good Habits & Break Bad Ones kilichoandikwa na James Clear. Mwandishi James Clear baada ya kupitia tafiti mbalimbali za kisayansi, kisaikolojia na kijamii, ameweza kuja na mfumo bora sana wa kujenga au kuvunja tabia yoyote ile. Mfumo huo una hatua nne ambazo mtu ukiweza kuzifuata, hakuna tabia itakayokushinda. Mfumo huo unapatikana kwenye kitabu hiki cha ATOMIC HABITS.
  54. HOOKED: How to Build Habit-Forming Products, kilichoandikwa na Nir Eyal ambaye anatuonesha jinsi ambavyo makampuni makubwa yanatumia saikolojia yetu sisi binadamu kutengeneza bidhaa na huduma ambazo tunasukumwa kuzitumia muda wote.Kupitia kitabu hiki unajifunza vitu viwili kwa wakati mmoja; kutengeneza bidhaa au huduma ambayo watu watasukumwa kuitumia muda wote na kuepuka kuwa mtumwa wa bidhaa na huduma ambazo zimetengenezwa kwa lengo la kukusukuma wewe kuzitumia, hasa pale zinapokuwa hazina manufaa kwako.

USIJISUMBUE KUWABADILISHA WATU , WATU HUWA HAWABADILISHWI

Watu huwa hawapendi kubadilishwa, na wakigundua mtu anataka kuwabadilisha basi wanaleta upinzani mkubwa kuhakikisha hilo halitokei.
Watu huwa wanaweza kubadilika kama watachagua kubadilika wao wenyewe, lakini siyo kulazimishwa kubadilika, hivyo ndivyo saikolojia ya binadamu ilivyo.
Hivyo usijisumbue kumbadili mtu yeyote yule, hutaweza, utaishia kuibua tu migogoro isiyo na manufaa.
Kama unataka mtu mwenye sifa fulani, mtafute mtu mwenye sifa hizo na siyo kumchukua yeyote na kujiambia utambadilisha, unajidanganya.
Kwenye mahusiano, iwe ni ya mapenzi au ndoa, chagua mtu ambaye sifa alizonazo sasa unaweza kwenda nazo na siyo kujiambia utambadilisha.
Kwenye ushirikiano wa biashara au kazi, chagua kushirikiana na mtu ambaye sifa unazoziona sasa kwake unaweza kwenda nazo.
Na hata unapoajiri, angalia sifa ambazo mtu anazo na kama unaweza kwenda nazo.
Usijidanganye kwamba sifa fulani ambayo mtu anayo unaweza kuibadili, unatafuta matatizo wewe mwenyewe.
Mtu mmoja amewahi kuulizwa anawezaje kuwafanya wafanyakazi wake kuwa na tabia nzuri, alijibu kwa kusema; “siwaambii wafanyakazi wawe na tabia nzuri, bali naajiri watu ambao tayari wana tabia nzuri”.

USITOE USHAURI KWA MTU AMBAYE HAJAKUOMBA , USICHUKUE USHAURI KWA AMBAYE HUJAMWOMBA.

Ushauri ni kitu ambacho unapaswa kuwa nacho makini sana wakati wa kutoa na hata kutokea.

Tuanze na kutoa, kamwe usitoe ushauri kwa mtu ambaye hajakuomba umshauri, unaweza kuona unamsaidia mtu huyo, lakini utakuwa unapoteza muda wako bure. Watu huwa hawafanyii kazi ushauri ambao hawajautafuta wenyewe. Unaweza kumwona mtu yupo kwenye hali fulani na kufikiri ushauri wako utamsaidia, ukamshauri vizuri na ukashangaa hafanyii kazi yale uliyomshauri. Hii ni kwa sababu mtu huyo hajawa na maumivu ya kutosha kumsukuma kutaka kutoka pale alipo sasa na ushauri wako ni kelele tu kwake. Mtu anayekuja kwako na kukuomba ushauri, ni mtu ambaye ameshaumia vya kutosha na anataka njia ya kuondoka kwenye maumivu, huyu ukimshauri anazingatia. Hivyo kama mtu hajakuomba ushauri, usijisumbue kutoa ushauri wako.

Tukienda kwenye kupokea ushauri, usichukue ushauri wa mtu ambaye hujamwomba akushauri. Hii ni kwa sababu mtu anaweza kuona jambo fulani kwa nje na akajumuisha kwamba tatizo lako ni hili na hatua za kuchukua ni hizi. Lakini mtu huyo anakuwa hajajua kwa undani unapitia nini hivyo ushauri huo unakuwa siyo sahihi. Kama unataka ushauri, mtafute mtu ambaye unamwamini, mweleze kile unachopitia bila ya kuficha chochote, kisha yeye awe na taarifa sahihi na kukushauri kwa usahihi. Lakini siyo ule ushauri wa juu juu ambao watu wanatoa kwa kuona mambo ya nje bila kujua yale ya ndani.
Huwa nasema ushauri wa bure utaona gharama yake pale unapoanza kuufanyia kazi. Huwa siyo ushauri sahihi. Hivyo chukua ushauri kwa watu ambao ni sahihi, watu wenye uzoefu au ujuzi na ambao wanaielewa hali yako. Na siyo kuchukua ushauri kwa kila anayekuambia ungefanya hivi au ungefanya vile. Kadhalika usikimbilie kutoa ushauri kwa mtu ambaye hajakuomba, kwa sababu unakuwa hujaelewa kwa undani anapitia nini na utakachomshauri hatofanyia kazi.
Wapo wanaosema mbona mimi natoa ushauri kupitia makala hizi wakati sijaombwa. Ukweli ni kwamba mimi sijakuletea maarifa haya nyumbani kwako, au kukulazimisha usome, bali wewe umeyatafuta au kukutana nayo na kuona yanakufaa, hivyo ukasoma. Kuna wengi wanakutana na maarifa haya, lakini wanayapita, kwa sababu hayana maana au umuhimu kwao. Lakini wewe umeyapokea, kwa sababu kuna kitu unatafuta na hivyo unayathamini. Hivyo wajibu wangu ni kushirikisha maarifa sahihi ambayo mtu akiyatumia anaweza kupiga hatua kwenye maisha yake, lakini siwezi kumlazimisha mtu asome au kuchukua hatua.

USIANZE SIKU YAKO KWA KUFUATILIA HABARI.

Habari nyingi ni hasi au zenye kuibua hisia kwa wafuatiliaji wake. Fungulia chombo chochote cha habari au tembelea mtandao wowote unaotoa habari na utaona habari gani zinapewa kipaumbele. Ni habari za kutisha au kusisimua. Habari za mauaji, ajali, mapigano, wizi, utekaji, ukatili na nyingine kama hizo.
Unapoianza siku yako kwa habari za aina hii, unavuruga kabisa akili yako. Unajikuta umepata hasira au kukata tamaa na kuona dunia haina maana. Hata mambo ambayo ulipanga kuyafanya hutaweza kuyafanya kwa hamasa kubwa pale ambapo umeshakutana na habari za kutisha au kukatisha tamaa.
Ndiyo maana nakushauri usianze siku yako kwa habari, sijakuambia usifuatilie kabisa habari (japo hilo ni jema ukiliweza), ila usianze nazo kwenye siku yako. Anza siku yako kwa kusali/kutahajudi, kusoma vitabu, kupangilia siku yako na kisha kuanza majukumu muhimu kwako kikazi au kibiashara. Mwisho wa siku wakati umeshakamilisha yale muhimu, hapo sasa unaweza kupitia habari ili ujue nini kinaendelea.
Ukifanya hivi utajikuta unakuwa na siku tulivu, siku ambayo umeweka umakini wako kwenye yale muhimu kwako kufanya na siyo kuvurugwa na habari za mambo yanayoendelea, ambayo hayakuhusu moja kwa moja.
Wapo wanaosema ni muhimu kuanza na habari kwa sababu kunaweza kuwa na kitu muhimu unapaswa kujua kabla siku haijaanza, labda kuna daraja limeharibika hivyo usipoanzana habari hutajua. Nasema hiyo siyo sababu yenye mashiko ya kuruhusu siku yako ichafuliwe na habari nyingi hasi. Na nikuambie kitu kimoja rafiki yangu, kama kuna habari muhimu kweli, itakufikia hata kama hufuatilii habari. Tukienda na mfano huo wa daraja kuharibika, hivi unafikiri unahitaji chombo cha habari kujua hilo? Kila mtu atakuwa anazungumzia hilo na hivyo utajua tu.
Kadhalika kwa habari nyingine ambazo ni muhimu, wale wanaokuzunguka watakuwa wanazizungumzia, hivyo kama ni kitu chenye umuhimu utakijua tu.
Usikubali kuharibu siku yako kwa kuanza na habari, anza siku yako kwa mipango yako na kisha imalize kwa habari.

PUNGUZA SANA AU ACHA KABISA KUTUMIA MITANDAO YA KIJAMII KAMA HAIKUINGIZII KIPATO

Mitandao ya kijamii imekuwa chanzo cha wengi kupoteza muda mwingi wa maisha yao. Pia imekuwa chanzo cha wengi kupata msongo na sonona kutokana na kufuatilia maisha ya wengine na kujilinganisha nao, kitu ambacho siyo sahihi kwa sababu wengi huigiza kwenye mitandao hiyo.
Hivyo ili kuepuka kupoteza MUDA  na  UTULIVU wako, na ili kupata AMANI ya moyo na kuepukana na msongo na sonona, acha kabisa kutumia mitandao ya kijamii. Jaribu hili , ile mitandao ambayo inachukua muda wako mwingi na kila ukiingia unatoka ukiwa unawaonea wengine wivu kwa mambo mazuri yanayoendelea kwenye maisha yao, acha kuitumia mara moja.
Ukiacha kutumia mitandao hii utajikuta ukiwa na muda mwingi wa kufanya kazi zako, kujifunza kupitia kusoma vitabu na hata muda wa kukaa na wale watu wa karibu na muhimu kwako.
Tumia mitandao hii ya kijamii kama tu inakuingizia KIPATO, kama unafanya biashara na unatangaza kupitia mitandao hii na inakuletea wateja, basi endelea kutumia kwa madhumuni ya biashara. Tofauti na hapo achana nayo.
Mitandao ya kijamii inaingiza fedha kupitia wewe, wewe ndiyo bidhaa inayouzwa na mitandao hii kwa wale wanaotangaza biashara zao. Hivyo kama na wewe huingizi fedha kupitia mitandao hii, achana nayo, usikubali kuuzwa kwa wengine.
Wapo wanaosema kama siyo mitandao ya kijamii hawawezi kukutana na maarifa mazuri kama haya. Hilo siyo kweli, maarifa mazuri yanapatikana pale unapoyatafuta, na mitandao ya kijamii siyo sehemu nzuri kwako kujifunza.
Hivyo acha kutumia mitandao ya kijamii 2020, labda kwa lengo la kibiashara pekee.

TOFAUTI KATI YA TAJIRI NA MASIKINI KATIKA KUJIFUNZA NA KUKUA...

MATAJIRI huwa wanajifunza kila siku na kuendelea kukua zaidi. Wanajisomea vitabu na kutafuta maarifa mbalimbali yanayowawezesha kupiga hatua. Wanaamini kuna mengi hawajui hivyo kujifunza zaidi, na hilo linawafanya wafanikiwe.
 
MASIKINI wao hawana muda wa kujifunza, wanaamini tayari wanajua kila kitu. Hawasomi vitabu ila habari za udaku na mitandao ya kijamii ndivyo wanapenda kufuatilia. Kwa njia hii wamekuwa hawajifunzi na hivyo kubaki kwenye umasikini wao.

Wednesday, December 25, 2019

TOFAUTI YA TAJIRI NA MASKINI KATIKA KUDHIBITI FEDHA.


MATAJIRI  wana uwezo wa kudhibiti fedha zao na hivyo kuweza kupiga hatua zaidi. Hawana ulimbukeni kwenye fedha, hawabadili maisha yao kwa sababu wamepata fedha zaidi. Na pale wanapopata fedha zaidi, wanaiwekeza. 

MASKINI  hawawezi kudhibiti fedha zao, wana ulimbukeni mkubwa kwenye fedha. Wakipata fedha zaidi wanabadilika, wanaanza kununua vitu visivyo muhimu mpaka fedha hiyo iishe. Kwa namna hii, wanashindwa kupiga hatua na kila wanapopata fedha zaidi, ndiyo wanapotea zaidi.
Acha ulimbukeni kwenye fedha, jifunze jinsi ya kudhibiti fedha zinazokuja kwako ili uweze kuzitumia kupiga hatua zaidi.

Friday, December 20, 2019

KUWA MKWELI KWAKO ------- ???

Dunia inatupa kila fursa ya kukata kona, kuchukua njia za mkato kwenye kila ambacho tunafanya. Ni rahisi kufanya hivyo kwa sababu kila mtu anafanya hivyo. Lakini pale unapofanya kitu kisichokuwa sahihi, ni wewe ambaye utabeba matokeo yake na hilo litakusumbua kwa muda mrefu. Kuepuka usumbufu unaotokana na yale uliyofanya, ni muhimu kuwa mkweli kwako binafsi.


Thursday, December 19, 2019

NENDA HATUA KWA HATAUA !! ----COACH MWL. JAPHET MASATU

USIDHANIE UNAJUA SANA , JIFUNZE KWA WENGINE !! -----COACH MWL. JAPHET MASATU

ULIZA WATAALAMU ----COACH MWL. JAPHET MASATU

HABARI ZA PEMBE------Na SHEIKH YAHYA HUSSEIN

TOFAUTI KATI YA TAJIRI NA MASKINI KATIKA KIPIMO CHA MALIPO

 MATAJIRI huwa wanachagua kulipwa kwa matokeo ambayo wanazalisha na hilo linawapelekea kulipwa zaidi kadiri wanavyozalisha zaidi.
MASKINI huwa wanachagua kulipwa kwa muda wanaofanya kazi, na hilo linawapa ukomo kwenye kulipwa kwao kwa sababu muda una ukomo.
Acha sasa kutaka kulipwa kwa muda na anza kuchagua kulipwa kwa matokeo unayozalisha. Muda una ukomo, lakini matokeo hayana ukomo.
Ajira ni moja ya maeneo ambao unalipwa kwa muda, ndiyo maana unapaswa kuwa na biashara ya pembeni.

WENGI TUNAISHI KIMAZOEA---------- ?????

Moja ya vitu vinavyowazuia watu wengi kupiga hatua kwenye maisha ni kukosa kipimo sahihi cha kujipima na kujifanyia tathmini kwenye maisha yao. Wengi wanaishi kwa mazoea, leo wakifanya kile walichofanya jana, na kesho kwenda kufanya kile walichofanya leo. Halafu wanaweza kulalamika kwa nini wanajituma sana lakini hawafanikiwi

Sunday, December 1, 2019

ACHA KUKIMBIZANA NA KILA AINA YA FURSA

Kuna fursa mpya imekuja, umeshawishiwa kwamba ni nzuri na ukafanya maamuzi ya kuingia kwenye fursa hiyo. (fuga kware)
 
Umeamua kuingia, wakati unaanza kufanya unakutana na ugumu fulani, kabla hujaanza kutatua ugumu uliokutana nao, unasikia kuna fursa nyingine bora zaidi ya hiyo ya kwanza. Hii ya sasa ni ya uhakika zaidi inalipa zaidi na haisumbui. (fuga sungura, ndiyo habari ya mjini).
 
Unaingia kwenye fursa ya pili nayo unaianza, ukiwa na matumaini makubwa, lakini pia unakutana na baadhi ya changamoto kwenye fursa hiyo, ambazo awali hukuambiwa. Wakati unaanza kufanyia kazi changamoto hizo, unasikia kuna fursa nyingine kabambe, hiyo siyo ya kukosa, ni nzuri, na haikuhitaji wewe ufanye kazi kabisa, ni kukaa kwenye mtandao tu kwa dakika chache na kuingiza fedha. Oh, tena huhitaji kufanya, wewe unaweka tu hela na wataalamu wanakusaidia kufanya unasubiri kupokea tu faida (fanya forex au cryptocurrency).
 
Kama mpaka sasa hujaelewa kinachoendelea hapo, una tatizo, na nipo hapa kutatua tatizo hilo.
 
Iko hivi rafiki, kila fursa ni nzuri na ina changamoto zake, kila fursa ina ugumu ambao lazima ukutane nao, uuvuke na ndiyo uweze kufanikiwa.
 
Sasa unapokutana na ugumu kwenye fursa moja, usikimbilie kwenye fursa nyingine, badala yake tatua ugumu huo na kuendelea na fursa hiyo mpaka ufanikiwe.
 
Ninachokuambia leo ni hiki; ACHA kukimbizana na kila aina ya fursa mpya inayokuja. Hutafanikiwa kwa kujaribu kila fikra, bali utafanikiwa kwa kuchagua fursa moja na kuifanyia kazi kweli mpaka kufanikiwa, na hapo utakutana na magumu na changamoto nyingi, katika kuyavuka magumu hayo ndiyo utafanikiwa.
 
Bilionea Richard Branson amewahi kusema fursa ni kama daladala, ukikosa moja jua kuna nyingine inakuja. Hivyo ACHA kabisa kukimbizana na kila aina ya fursa, chagua kitu kimoja na kifanye, weka kazi, weka muda na kuwa na subira na ung’ang’anizi mpaka upate kile unachotaka.
 
Na kwa kumalizia, ukiona unakaribishwa kwenye fursa ambayo unaahidiwa kupata fedha bila ya kufanya kazi yoyote ile, yaani wewe unaweka tu fedha halafu kwa namna fulani zinazaliana na unavuna faida kubwa na kwa haraka, basi jua hili; WEWE NDIYO FURSA YENYEWE.
 
ACHA kukimbizana na kila aina ya fursa, chagua kitu kimoja au vichache utakavyofanya mpaka ufanikiwe.