WAKATI SAHIHI WA KUCHUKUA MKOPO KWA AJILI YA BIASHARA . |
Kwenye makala hii nitakwenda kushauri mambo matatu ambayo kila mfanyabiashara anapaswa kuyafanyia kazi ili biashara yake iweze kukua.
JAMBO LA KWANZA; WAKATI SAHIHI WA KUCHUKUA MKOPO.
Usichukue mkopo kwenye biashara kwa sababu umeambiwa unakopesheka,
Usichukue mkopo kwa sababu wewe ni mfanyakazi hivyo unaweza kukopa kwa kutumia mshahara wako.
Na usichukue mkopo kwenye biashara kwa sababu umesikia watu wanasema biashara haiwezi kufanikiwa bila mkopo.
Zote hizo ni sababu mbovu za kuchukua mkopo kwenye biashara, ambazo zimewapoteza wengi.
Kabla hujachukua mkopo kwenye biashara, hakikisha imetimiza vigezo hivi vikubwa vitatu;
Kigezo cha kwanza ni biashara inajiendesha kwa faida, yaani tayari biashara inaingiza faida, hivyo unapochukua mkopo unakwenda kukuza faida hiyo zaidi.
Kigezo cha pili ni biashara ina mfumo mzuri wa uendeshaji ambapo kuna vitengo mbalimbali na kila kitengo kina majukumu yake ya kutekeleza. Hata kama uko mwenyewe kwenye biashara, unapaswa kuwa na vitengo hivyo.
Kigezo cha tatu ni matumizi ya fedha za biashara na matumizi yako binafsi hayaingiliani. Yaani fedha ya biashara inakaa kwenye biashara na huitumii kwa namna yoyote ile, una akaunti ya biashara benki ambapo fedha zinaenda huko. Hata kama huna pesa ya kula, hutoi tu kwenye biashara kiholela.
Kama biashara yako haijafikisha vigezo hivyo vitatu, ukichukua mkopo unaiwahisha kufa.
JAMBO LA PILI; MAMBO YA KUZINGATIA PALE UNAPOCHUKUA MKOPO.
Baada ya kuhakikisha kwamba biashara yako imefikia vigezo vya kuchukua mkopo, kwa maana kwamba inajiendesha kwa faida, ina mfumo mzuri na fedha za biashara haziingiliani na matumizi yako binafsi, basi unaweza kuchukua mkopo.
Lakini pamoja na kukidhi vigezo hivyo, mkopo unaweza kuwa hatari kwa biashara kama hutazingatia mambo muhimu katika kuuchukua na kuutumia. Yafuatayo ni mambo matano muhimu ya kuzingatia pale unapochukua mkopo wa biashara.
Moja ni kupanga matumizi ya mkopo huo kabla hujauchukua. Usichukue mkopo kisha ndiyo upangilie unautumiaje. Badala yake iangalie biashara yako kwanza, angalia ni bidhaa au huduma zipi zinazotoka haraka, zina uhitaji na faida yake ni nzuri, hivyo unapochukua mkopo unaenda kuweka kwenye bidhaa au huduma hiyo. Mfano kwenye hardware kama umegundua cement ndiyo inatoka sana na yenye faida na kwa mtaji wako huwezi kununua kwa wingi, unapochukua mkopo basi unawekeza kwenye eneo hilo.
Mbili ni kutokutumia mkopo wote uliouchukua, tumia robo tatu na robo iache kama akiba. Mipango yako ya mwanzo inaweza kuwa siyo sahihi, sasa kama mkopo wote umeshautumia, utajikuta umekwama. Acha kiasi fulani cha mkopo kama fedha taslimu, ili kama ulivyopanga awali mambo hayajaenda hivyo, unakuwa na kiasi cha kukuwezesha kufanya mpango mwingine wa kuokoa hali unayokuwa umeingia.
Tatu ni usitumie mkopo kufanya mambo yasiyozalisha faida, mfano kufanya marekebisho eneo la biashara, kununua samani na mengineyo. Mkopo unarudi kwa riba, hivyo unapaswa kuzalisha faida ambayo ni kubwa kuliko riba unayolipa. Kama mkopo hauzalishi faida, maana yake riba unayoilipa inatoka kwenye mtaji wako, ndiyo maana utamaliza kulipa mkopo na biashara kufa.
Nne ni kuweka nguvu na kujisukuma zaidi, ulipokuwa huna mkopo, hukuwa na gharama kubwa za kuendesha biashara, ukishachukua mkopo, gharama zimeongezeka. Hivyo pia lazima ujisukume sana, pambana kuongeza wateja na kuwashawishi wateja wako kununua zaidi. Usiendelee kuendesha biashara yako kwa mazoea kama wakati huna mkopo.
Tano ni kufuatilia kwa karibu mwenendo wa biashara na marejesho ya mkopo. Usirejeshe tu bila kuangalia biashara inaendaje, kama unafika wakati unakuta marejesho unayofanya ni makubwa kuliko faida unayoingiza, jua mapema kabisa kwamba unamega mtaji wa biashara. Hivyo anza kuchukua hatua mapema na siyo kusubiri mpaka umemaliza kurejesha mkopo huku biashara imekufa. Ukishagundua marejesho ni makubwa kuliko faida una mengi ya kufanya, kwa upande wako ni kukazana kuongeza mauzo, kwa upande wa mkopo unaweza kwenda kuongea nao wapunguze kiwango cha marejesho unachofanya.
Ukizingatia haya matano pale unapochukua mkopo, utainufaisha biashara yako na kuiwezesha kukua zaidi.
JAMBO LA TATU; UFANYE NINI PALE UNAPOKUWA HUNA VIGEZO VYA KUCHUKUA MKOPO.
Wafanyabiashara wengi wadogo na wa kati wamekaririshwa na kuamini kwamba njia pekee ya kupata mtaji wa kuanza na kukuza biashara ni kuchukua mkopo. Ndiyo maana utasikia kilio cha wengi kwamba hawakopesheki au hawana dhamana ya kupata mkopo.
Usikimbilie kuchukua mkopo kama bado hujakidhi vigezo vya kuchukua mkopo ambavyo tumejadili hapo juu.
Swali ni je ufanyeje ili kukuza biashara yako wakati huwezi kuchukua mkopo? Kuna mengi ya kufanya, hapa kuna matatu ya kuzingatia.
Moja ni kuanza biashara kwa akiba zako wewe mwenyewe. Kwenye njia nyingine ulizonazo za kuingiza kipato, basi weka akiba kwenye kila kipato na akiba hiyo iwekeze kwenye biashara, anza kidogo na endelea kukua. Kila mwezi jiwekee kiango ambacho utawekeza kwenye biashara yako kutoka kwenye njia zako nyingine za kuingiza kipato.
Mbili ni kutokuondoa fedha kwenye biashara kabisa, acha biashara ijiendeshe yenyewe kwa kutokuingilia na kutoa fedha kwa matumizi yako binafsi. Unapaswa kuwa na nidhamu kubwa sana ya kutenganisha matumizi yako binafsi ya fedha na fedha za biashara. Zione fedha za biashara kama za mtu mwingine kabisa na usiwe na mazoea ya kutumia biashara kutatua shida zako.
Tatu ni kuanza na biashara nyingine ili kutengeneza mtaji wa kwenda kuanza biashara ya ndoto yako. Kama biashara unayotaka kuanzisha inahitaji mtaji mkubwa ambao huna, anza na biashara nyingine unayoweza kuanza kwa mtaji kidogo kisha tumia biashara hiyo kutengeneza mtaji wa kuingia kwenye biashara ambayo ndiyo unataka kufanya. Hili ni jibu kwa wale watakaokuwa wamesoma namba moja hapo na kusema sina ajira nitatengenezaje mtaji au kuendesha maisha bila kutegemea biashara. Fanya chochote unachoweza kuhakikisha kwanza unaingiza kipato, omba hata kuwa wakala wa mauzo kwenye biashara za wengine ambapo watakulipa kamisheni, pambana kuuza na tengeneza mtaji wako ili baadaye uwe na biashara yako.
Kuanzisha na kukuza biashara ili ikupe mafanikio kunahitaji kazi, msimamo na uvumilivu. Hakuna njia ya mkato inayoweza kuondoa mahitaji hayo matatu. Wengi wamekuwa wanakimbilia kuchukua mkopo wakifikiri ni njia ya mkato na kinachotokea ni kuua kabisa biashara zao.
Zingatia haya uliyojifunza kwenye ushauri huu, yafanyie kazi na biashara yako itapata manufaa makubwa.