Ukiwachukua
watu 100 kutoka eneo lolote lile, kumi watakuwa na mafanikio makubwa
kuliko 90 na mmoja kati yao atakuwa na mafanikio makubwa kuliko wote.
Ni
namba hizi ndiyo zimekuwa zinawachanganya watu, wasielewe kwa nini
wachache sana ndiyo wafanikiwe huku wengi wanaopenda kufanikiwa wakiwa
hawafanikiwi.
Kiu ya kutaka kupata siri za mafanikio siyo ya zama hizi tunazoishi, imekuwepo tangu enzi na enzi.
Mwaka
1912 mwandishi Orison Swett Marden alikusanya pamoja ushuhuda wa wale
waliofanikiwa, kwa namna walivyoeleza wao wenyewe na kuja na kitabu
alichokiita; How They Succeeded: Life Stories of Successful Men Told by
Themselves. Kitabu hicho kimesheheni hadithi za watu waliokuwa na
mafanikio makubwa sana kipindi hicho, kwa namna ambavyo walieleza
wenyewe.
Ni
kitu kimoja kusoma hadithi ya mafanikio ya mtu inayoelezwa na wengine
na ni kitu kingine tofauti kabisa kusoma hadithi hiyo ikielezwa na mtu
mwenyewe.
Upekee wa kitabu hiki, unatufanya tuwasikie wenyewe wanasemaje kuhusu mafanikio yao.
Mmoja
wa watu waliofanikiwa ambaye hadithi yake inapatikana kwenye kitabu
hiki ni aliyekuwa mwandishi Amelia E. Barr (March 29, 1831–March 10,
1919). Ambaye pamoja na kupoteza mume wake pamoja na watoto wake watatu
kati ya sita aliokuwa nao, aliweza kufikia mafanikio makubwa sana kwenye
uandishi.
Kwenye insha yake iliyo kwenye kitabu hiki, ameshirikisha siri 9 za mafanikio kutokana na uzoefu wake binafsi.
Hapa
tunakwenda kujifunza siri hizo kama alivyoeleza mwenyewe, kisha
nitaongeza hatua ya wewe kuchukua ili kuweza kufanikiwa sana.
( 01). KUWA TAYARI KWA MAUMIVU
Amelia;
watu wanafanikiwa kwa sababu wako tayari kupokea maumivu wanayopitia
ili kufanikiwa. Juhudi na uvumilivu ni muhimu na wote waliofanikiwa
walifanya maamuzi na kung’ang’ana nayo. Wanajua kusudi lao na wanafanya
maamuzi ya kulifikia.
Somo;
jua hasa nini unachotaka kwenye maisha yako, amua kwamba utapata kitu
hicho na chukua hatua kukipata. Usikate tamaa hata kama unapitia maumivu
makali kiasi gani, hakuna aliyewahi kufanikiwa bila ya kupitia maumivu.
( 02 ). WEKA KAZI KILA SIKU.
Amelia;
mafanikio ni zawadi kwa wale ambao wanaweka kazi kila siku. Hii ndiyo
siri kuu ya mafanikio, kuweka juhudi kuliko wengine wanavyoweka. Kama
kuna kitu hujui, utajifunza kwa kufanya. Na hata pale unapopata matokeo
usiyotegemea, usiache kuweka juhudi mpaka umepata unachotaka.
(03 ). USISUMBUKE NA WANAOKUPINGA.
Amelia;
safari yako ya mafanikio haitakuwa rahisi, utakutana na vikwazo na moja
ya vikwazo hivyo ni watu watakaochagua kuwa maadui wako na kukupinga
kwenye kile unachofanya. Usiumizwe na upingaji wa wale wanaokupinga,
badala yake utumie kupiga hatua zaidi. Ukinzani una nguvu ya kukusukuma
zaidi.
Somo;
usitegemee kila mtu akubaliane na wewe, wengi watakupinga, kukukosoa na
kukukatisha tamaa. Lakini kumbuka kitu hiki kimoja, wote hao hawajui
nini unataka na uko tayari kujitoa kiasi gani kukipata. Hivyo usiumizwe
na ukosoaji wao, kama kuna kitu chenye manufaa wanakigusia kifanyie
kazi, kama hakuna wapuuze na endelea na safari yako.
(04 ). BAHATI INAUZWA.
Amelia;
kosa kubwa kwenye mafanikio ni kufikiria kwamba ni jambo la bahati,
kwamba wanaofanikiwa wanakuwa wamepata bahati. Dunia inaendeshwa na
sheria kali ambazo hazitoi nafasi kubwa kwa bahati kufanya kazi. Asili
huwa inauza vitu vyake, huwa haivitoi bure, hivyo hata bahati,
utainunua, hutapewa bure.
Somo;
ni kweli waliofanikiwa wanakutana na bahati fulani, lakini bahati hizo
huwa haziwafuati wakiwa wamelala kitandani, bali zinawakuta wakiwa
wanaweka kazi kwenye kile wanachotaka. Hivyo kama unataka kukutana na
bahati, lazima ulipe gharama ya kuwa tayari kuweka kazi. Kama ambavyo
tumekuwa tunajifunza, bahati ni pale maandalizi yanapokutana na fursa.
(05 ). PASHA CHUMA MOTO.
Amelia;
kwa miaka tumekuwa tunaambiwa tuziangalie fursa, kupiga wakati chuma ni
cha moto. Ni vizuri, lakini itakuwa bora kama tutakifanya chuma kuwa
cha moto kwa kupiga, badala ya kusubiri chuma kiwe cha moto ndiyo
tupige.
Somo;
usisubiri mpaka fursa ije ndiyo uanze kuchukua hatua, badala yake anza
kuchukua hatua na utakutana na fursa. Ukiwa kwenye kuchukua hatua
inakuwa rahisi kuziona na kuzitumia fursa kuliko ukiwa unasubiria mpaka
fursa ije huku hauchukui hatua. Usisubiri chuma kiwe cha moto ndiyo
upige, kipige chuma mpaka kiwe cha moto.
(06 ). UNAHITAJI MUDA.
Amelia;
kila kitu kizuri kinahitaji muda, usiwe na haraka kwenye kazi yako.
Weka muda na zama ndani kwenye kazi yako, kadiri unavyoweka muda zaidi
ndivyo inavyokulipa zaidi. Kazi za hovyo hufanywa kwa haraka, akili
kubwa ni kujipa muda wa kufanya vizuri kile ambacho wengine wanafanya
vibaya.
Somo;
hakuna njia ya mkato ya kufikia mafanikio makubwa, yeyote anayekuambia
njia hiyo ipo anataka kukutapeli. Jipe muda, kama ukiwahi sana jua
itakuchukua miaka 10, lakini mara nyingi ni zaidi ya hapo. Acha papara
za kutaka mafanikio ya haraka, hayapo. Jipe muda, weka muda wa kutosha
kwenye kazi yako, jua kwa kina kile unachokifanya na kazana kuwa bora,
kila unachoweka kitakulipa zaidi.
(07 ). KUWA NA MPANGILIO.
Amelia;
kazi inayofanywa bila mpangilio siyo kazi nzuri, ni uzembe au mtu
anayefanya ana matatizo ya akili. Siwezi kuamini kati ya mtu ambaye hana
mpangilio, kazi ambayo ni ya hovyo, duni na isiyoeleweka.
Somo;
kuwa na mpangilio kwenye kila eneo la maisha yako, tenga muda wako kwa
mambo sahihi na utumie hivyo, pangilia vizuri eneo lako la kazi na kila
eneo la maisha yako pia. Usiwe mtu wa kukurupuka na kufanya kila
kinachokuja mbele yako. Tenga muda wa kazi na fanya kazi, tenga muda wa
kupumzika na pumzika. Kazi yako ifanye kwa namna ambayo mtu akiona
anajua kweli umeweka juhudi kwenye kuifanya.
(08 ). HESHIMU KAZI YAKO.
Amelia;
usijione wewe ni bora kuliko kazi au biashara yako. Kuwa mnyenyekevu,
heshimu kile unachofanya na kipe heshima na umakini wa kutosha. Hata
kama kuna vitu vingine unafanya, usichukulie kitu hicho kama ni cha
pembeni. Kama ni mwandishi na pia ni daktari, usichukulie uandishi kama
kitu cha pembeni, bali kipe heshima kama kitu kikuu kwako.
Somo;
weka moyo wako wote, akili yako yote na umakini wako wote kwenye kile
unachokifanya. Kwa maana hiyo, unahitaji kuchagua vitu vichache ambavyo
utavifanya vizuri kwa kuweka kila kitu chako kwenye vitu hivyo na
kupuuza vitu vingine vyote. Acha kuhangaika na kila kitu, kutawanya
nguvu na umakini wako, maana hilo litakuzuia wewe kufanikiwa.
(09). USIWE NA HASIRA.
Amelia;
usiangukie kwenye hasira na hisia nyingine hasi pale unapokutana na
majaribu. Mara zote kuwa na furaha na moyo mkunjufu, ifanye kazi yako
kwa moyo mmoja na amua kuweka kila kikwazo pembeni. Na zaidi ya yote
kuwa na furaha huku ukijua utapata unachotaka kama hutakata tamaa.
Somo;
mambo hayatakwenda kama ulivyopanga, utakutana na vikwazo vya kila
aina, wakati mwingine watu watakuzuia au kukukwamisha kwa makusudi
kabisa. Hali hiyo itaibua hisia hasi ndani yako, hasira, chuki, kinyongo
na nyingine. Epuka kuruhusu hisia hizo kukutawala, badala yake ziondoe
na tawaliwa na hisia chanya ya furaha na matumaini. Endelea kuweka
juhudi huku ukijua kila kikwazo kitashindwa kama wewe hutakata tamaa.
Angalizo;
Amelia anatoa angalizo hili kuhusu siri hizi za mafanikio; kuna watu
unaweza kuwaona wamefanikiwa kwa kutumia njia ambazo siyo sahihi, lakini
jua hili, mafanikio yao hayatadumu kwa muda mrefu. Asili huwa haiibiwi,
huwa inalipa kila ambacho mtu anafanya. Anayepata mafanikio kwa njia
zisizo sahihi atalipa kwa kuyapotea. Na wewe unayetumia njia sahihi,
hata kama utachelewa, utafikia mafanikio makubwa kama unavyotaka.
Amelia
pia anashirikisha kwamba msingi wa mafanikio yake ulijengwa miaka mingi
kabla hajafanikiwa. Alianza kuyaona mafanikio baada ya miaka 45 ya kazi
bila ya kuchoka ndiyo alipata alichokitaka. Anasema mara nyingi akili
yake ilikwamisha, mikono yake ilimkwamisha, miguu yake ilimkwamisha,
lakini anashukuru roho yake haikuwahi kumwamisha.
Na
hicho ndiyo unachohitaji ili ufanikiwe, roho ambayo haitakukwamisha,
imani na matumaini kwamba licha ya kupitia magumu, bado utafanikiwa kama
tu hutakata tamaa.
No comments:
Post a Comment