Monday, February 25, 2019

NGUVU YA KUFANYA KWA MALENGO.

Kinachowatofautisha wale wanaofikia ubobezi na wale wanaoishia kuwa kawaida siyo wanachofanya, bali namna wanavyofanya kile wanachofanya. Watu wawili wanaweza kuwa wanafanya kitu kimoja, lakini mmoja akabobea na mwingine asibobee.
Mwandishi anatuambia zipo aina tatu za ufanyaji ambazo zinawatofautisha wanaobobea na wanaokuwa kawaida.
Aina ya kwanza ni kufanya kwa kawaida, hapa mtu anafanya kile ambacho amezoea kufanya kila wakati, hakuna kipya anachofanya na hivyo hawezi kubobea. Hivi ndivyo wengi wanavyoendesha maisha yao, wanaonekana kufanya sana lakini hakuna hatua wanapiga. Hii ni kwa sababu wanafanya kwa mazoea.
Aina ya pili ni kufanya kwa malengo, hapa mtu anafanya kitu kwa malengo, na hivyo anakuwa na hatua anazopanga kupiga zinazomsukuma kufanya zaidi. Katika kufanya kwa malengo mtu anapiga hatua zaidi kwa sababu malengo anayojiwekea yanamsukuma zaidi. Kwenye kufanya kwa malengo mtu anakuwa na sifa nne; moja anakuwa na lengo la wapi anataka kufika, mbili anaweka umakini wake wote kwenye kile anachofanya. Tatu anakuwa na njia ya kujipima na kupata mrejesho wa hatua anazochukua na nne anajisukuma kutoka nje ya mazoea, kufanya vitu vipya ambavyo vinamwezesha kupiga hatua zaidi.
Aina ya tatu ni kufanya kwa makusudi, kama mwandishi anavyoita DELIRATE PRACTICE, hapa mtu anakuwa na kusudi kubwa linalomsukuma kufanya kitu. Hii ndiyo aina ya ufanyaji ambayo inazalisha watu wenye ubobezi wa hali ya juu. Kufanya kwa makusudi kuna sifa kama za kufanya kwa malengo, lakini ina sifa nyingine mbili za nyongeza. Ya kwanza ni eneo ambalo mtu anakuwa amechagua kubobea linapaswa kuwa na wabobezi ambao wanaweza kuangaliwa na mtu akajifunza kwao. Mtu anapoweza kuwaangalia wabobezi na kujifunza kile wanachofanya na namna wanavyofanya, inakuwa rahisi kwake naye kufanya. Sifa ya pili ni kuwa na mwalimu au kocha ambaye anamfundisha na kumsimamia mtu kwenye hatua anazochukua. Kwa kuwa na mtu wa nje anayetoa maelekezo au kupima hatua mtu anazochukua na kutoa mrejesho, kunamfanya mtu apige hatua kubwa zaidi.
Hizo ndizo aina tatu za ufanyaji na aina ya tatu ndiyo mwandishi ameijadili kwa kina sana kwenye kitabu cha PEAK.

SIYO KIPAJI NI JUHUDI.

Kwa  miaka mingi watu wamekuwa wakiamini kwamba kuna watu ambao wamezaliwa na vipaji ambavyo vimewawezesha kufikia kwenye ubobezi mkubwa ana katika maeneo waliyobobea.
Na mifano ipo mingi sana, kwenye utunzi wa nyimbo na upigaji wa vyombo, Morzat anaonekana kuwa mmoja wa watu wenye kipaji kikubwa. Kadhalika kwenye mchezo wa golf, Tiger Woods anaonekana kuwa mchezaji ambao ana kipaji kikubwa kwenye mchezo huo. Na hata michezo mingine na hata kwenye taaluma mbalimbali, wale ambao wamefanikiwa sana wanaonekana kuwa na kipaji kikubwa.
Lakini unapokwenda kuchimba ndani, na kuangalia kwa undani maisha ya wale wanaosemekana wana vipaji, huoni kipaji bali unaona juhudi kubwa na za muda mrefu. Katika mifano niliyotoa hapa, Morzat ambaye anaonena alikuwa na kipaji, alianza kufundishwa kupiga vyombo vya muziki akiwa na miaka minne, ana akawa anafanya hivyo kila siku. Huyu ni mtoto ambaye alikuwa akijua kufanya kitu kimoja tu, muziki. Je utamlinganisha na mtu mwingine anayekuja kujifunza muziki ukubwani?
Ukiangalia kwa Tiger Woods pia, wazazi wake wanakiri kumpa michezo ya kitoto inayoendana na mchezo wa golf tangu akiwa na miezi tisa, huyu ni mtu ambaye tangu anapata utambuzi wake, anajua kitu kimoja tu, golf, je utaweza kumshindanisha na mtu mwingine ambaye amejua mchezo huo baadaye?
Chagua mtu yeyote unayeamini ana kipaji, iwe ni mchezaji, mwanasayansi na hata kiongozi, na angalia maisha yake tangu utotoni, utagundua kuna mazingira ambayo yalimweka kwenye juhudi ambazo zilimwandaa kufikia ubobezi huo. Hata wachezaji wenye ubobezi mkubwa kama Christiano Ronaldo na Messi, ukiangalia utoto wao, wametumia sehemu kubwa kwenye kujifunza mchezo wa mpira. Angalia maisha ya wanasayansi kama Eistein, Newton na wengineo, wote waliweka muda na juhudi kubwa kabla hawajafikia ubobezi ambao wengi wanakuja kuamini ni vipaji vimewafikisha pale walipo.
Hivyo ujumbe kwako rafiki yangu ni huu, unaweza kubobea kwenye jambo lolote lile, kama tu utaweka juhudi ambazo zinapaswa kuwekwa ili kufikia ubobezi. Na kwenye kitabu cha juma hili cha PEAK, tunakwenda kujifunza juhudi sahihi unazopaswa kuweka ili kufikia ubobezi.
Usijiambie tena kwamba huwezi kufikia ubobezi kwa sababu huna kipaji au uwezo. Tafiti zote ambazo zimefanywa kwenye ubobezi zimekuja na jibu moja, wale wanaofikia ubobezi wana uwezo mkubwa sana, lakini ni uwezo ambao upo ndani ya kila mmoja wetu. Kinachotutofautisha sisi na wale waliobobea sana ni kiasi ambacho tumeendeleza uwezo ambao upo ndani yetu.
Uwezo tayari unao, unachohitaji ni juhudi ili kubobea, aina gani ya juhudi utakwenda kujifunza kwenye kitabu cha juma.

Friday, February 22, 2019

JE , WAFAHAMU KILA KIUMBE KINA NGUVU YA UKUAJI NDANI YAKE ? KWANINI USIITUMIE NGUVU ULIYONAYO TAYARI KWA AJILI YA MAFANIKIO YAKO ?

Kwa asili, kila kiumbe kinachozaliwa kina nguvu ya ukuaji ndani yake. Sisi hatuna cha kufanya kukiwezesha kitu hicho kikue, badala yake jukumu letu ni kuondoa vikwazo vya ukuaji.

KILA MTU ANA NGUVU YA MAFANIKIO MAKUBWA NDANI YAKE . ONDOA VIKWAZO VYA MAFANIKIO YAKO.

Kila mtu ana nguvu ya mafanikio ndani yake, kitu pekee anachopaswa kufanyia kazi ni kuondoa vikwazo vya mafanikio yetu. Vitu kama tabia zetu wenyewe, hisia zetu na mengine yanatuzuia tusifikie mafanikio ambayo tayari yapo ndani yetu.
Kwa kifupi, hakuna kikubwa tunachoweza kufanya kuyabadili mafanikio yaliyopo ndani yetu, ni makubwa sana, kinachotufanya tusiyafikie ni vikwazo tunavyotengeneza au kuruhusu viingie kwenye maisha yetu.
Kadhalika kwenye fedha na utajiri, kila mtu tayari ana utajiri ndani yake, kinachomzuia mtu kufikia utajiri wake ni vikwazo anavyokutana navyo au anavyotengeneza kwenye maisha yake.
Hivyo rafiki yangu, kila wakati jiulize swali hili, ni kikwazo gani nimeruhusu au kutengeneza kwenye maisha yangu ambacho kinanizuia kufikia mafanikio makubwa yaliyo ndani yangu?
Ukijiuliza swali hili na kujipa majibu sahihi, utaweza kuifanya safari yako ya mafanikio kuwa rahisi. Utaacha kujitesa na kujiumiza kwa vikwazo ulivyojiwekea au kuruhusu vikuzuie na utakuwa na mpango mzuri kwa mafanikio yako.
Tayari mafanikio unayo, unachohitaji ni kuondoa vikwazo vinavyoyazuia yasije kwako.
Moja ya njia za kuondoa vikwazo vya ukuaji kwako ni kujifunza kwa kujisomea vitabu.

Thursday, February 21, 2019

MUDA WA KUANGALIA TELEVISHENI , KUOGA, KULA TUNAO !! LAKINI LINAPOKUJA SUALA LA KAZI, BIASHARA , KUSOMA VITABU VISINGIZIO VINGI.

Kwenye maisha yetu ya kila siku, vitu vyote muhimu huwa hatuvifanyi mara moja na kuachana navyo, bali huwa tunavifanya kila siku. Na hakuna hata siku moja ambayo tunajiambia tumechoka na hivyo hatufanyi.


Fikiria yale tunayofanya kila siku ili maisha yetu yaende, unakula kila siku, unapumua kila siku, unasafisha mwili wako kila siku, na hata nyumba au nguo zako, unasafisha kila mara.


Lakini inapokuja kwenye kazi na biashara, huwa tunajipa kila aina ya sababu kwa nini tusifanye kwa baadhi ya siku. Huwa tunachukulia kazi na biashara zetu kama kitu cha ziada kwenye maisha yetu na siyo maisha yetu.


Kadhalika vitu kama kujifunza, mfano kusoma vitabu. Utasikia watu wakisema kabisa kwamba hawasomi vitabu kwa sababu hawana muda. Lakini hutawasikia watu hao wakisema wana siku mbili hawajala kwa sababu hawajapata muda.


Kwa kila kilicho muhimu kwenye maisha, huwa tunapata muda wa kukifanya, hata kama tumebanwa kiasi gani.


Hivyo ninachotaka uondoke nacho hapa rafiki yangu ni hiki, chagua vitu ambavyo lazima kila siku utavifanya na uvifanye kweli bila ya kusingizia muda au kuchoka. Na ukiacha vile ambavyo tayari unafanya ili uwe hai, kama kula na kadhalika, ongeza vitu kama kujifunza, kufanya majukumu yako na kukuza vipaji au kile unachopenda.


Kama wewe ni mwandishi basi hakikisha kila siku unaandika, usikubali siku ipite hujaandika. Na wengine kwa nafasi zao za kazi au biashara, hakikisha kila siku kuna kitu unakifanya cha kukufanya uwe bora zaidi.

Sunday, February 17, 2019

KULA MIMEA--NI SIRI YA KUISHI MIAKA ZAIDI YA 100.

Chakula chako kinapaswa kuwa mimea zaidi. Epuka kula nyama na vyakula vilivyosindikwa. Watu wengi walioishi miaka zaidi ya 100 sehemu kubwa ya chakula chao ni mimea. Nyama wanakula kwa kiwango kidogo sana na mara chache.
Ili kuongeza mimea zaidi kwenye vyakula vyako, zingatia mambo yafuatayo;
  1. Kula mbogamboga na matunda mara nne mpaka sita kwa siku. Kwa kila mlo wa siku, kuwa na matunda na matunda.
  2. Punguza ulaji wa nyama, kama unaweza acha kabisa, kama huwezi kula siyo zaidi ya mara mbili kwa wiki na kula kiasi kidogo cha nyama.
  3. Weka matunda sehemu ambayo ni rahisi kuyaona na kuyatumia unapokuwa unaendelea na shughuli zako. Hili litakusukuma kutumia matunda zaidi.
  4. Kula kunde zaidi. Vyakula vya jamii ya kunde vina virutubisho vya kutosha kwa mwili wako, fanya hivi kuwa sehemu kubwa ya chakula chako.
  5. Kula karanga kila siku, vyakula vya karanga na jamii yake, kama korosho na lozi vina mafuta mazuri kwa mwili wako na tafiti zinaonesha vinapunguza hatari ya magonjwa ya moyo.
  6. Kuwa karibu na karanga na vyakula vya jamii ya karanga ili iwe rahisi kwako kutumia mara kwa mara. Unaweza kuziweka kwenye chombo ambacho inakuwa rahisi kwako kutumia.

UWEKE MWILI WAKO KATIKA MWENDO---NI SIRI YA KUISHI ZAIDI YA MIAKA 100.

Mazoezi ya mwili ni siri ya kwanza ya kuishi miaka mingi. Katika utafiti wake, Dan aliweza kuona hili kwa kila aliyeishi miaka mingi. Watu hawa wamekuwa ni watu ambao kila siku miili yao iko kwenye mwendo. Siyo watu ambao wanakaa eneo moja kwa muda mrefu. Na licha ya kuwa na miaka zaidi ya 100, wengi bado walikuwa wanafanya majukumu yao wenyewe.
Na mazoezi ambayo yanakuwezesha kuishi miaka mingi siyo mazoezi magumu sana, bali mazoezi madogo madogo ambayo yanaufanya mwili utumie vyakula unavyokuwa umekula.
Katika kuiishi siri hii ya kuweka mwili kwenye mwenzo, zingatoa yafuatayo;
  1. Ondoa urahisi kwenye maisha yako. Hapa jisukume kutembea na kufanya kitu badala ya kutumia urahisi uliopo. Kwa mfano kama kuna ghorofa unapanda na kuna lifti na ngazi, wewe panda ngazi badala ya lifti. Kama unaangalia tv na uko mbali nayo, kama unataka kubadili chaneli au kuongeza sauti, badala ya kutumia rimoti amka na uende ukabadili mwenyewe. Mazoezi madogo madogo kama haya yanakusaidia sana.
  2. Fanya mazoezi kuwa kitu unachofurahia. Usifanye mazoezi magumu na ya kukuumiza, badala yake fanya mazoezi ambayo unayafurahia, kama kuna eneo la karibu unaloenda, badala ya kutumia gari basi tembea au nenda kwa baiskeli. Kadiri unavyopata nafasi kama hizi za kuupa mwili wako mazoezi, zitumie.
  3. Kuwa na muda wa matembezi kwenye siku yako. Kuwa na matembezi ya peke yako au pamoja na wengine kunaufanya mwili wako kuwa kwenye mwendo.
  4. Kuwa na mkutano wa kutembea. Kama kuna mtu ambaye unataka kuwa na mazungumzo naye, iwe ni ya kikazi, kibiashara au hata ya kindugu na kirafiki, unaweza kutumia mkutano huo kuwa sehemu ya mazoezi. Mnaweza kufanya mazungumzo yenu mkiwa mnatembea eneo tulivu na hii itakuwa msaada zaidi kwenu.
  5. Kuwa na bustani. Kwa kuwa na bustani ambayo unaihudumia kila siku ni zoezi tosha kwa mwili wako. Kupanda, kupalilia na hata kuvuna mazao kwenye bustani yako kunatosha kuupa mwili wako zoezi.
  6. Jiunge na darasa la yoga. Yoga ni mazoezi ya mwili yanayouwezesha mwili wako kuweza kuwa na usawa. Ukiweza kufanya zoezi hili la yoga angalau mara mbili kwa wiki inakusaidia sana.