Karibu rafiki yangu mpendwa kwenye makala yetu ya ushauri wa changamoto mbalimbali zinazokuwa kikwazo kwa mafanikio yetu.
Kwenye makala ya leo tunakwenda kushauriana kwenye msimamo muhimu mno unaouwezesha biashara kufanikiwa au kufa. Msimamo huo ni misingi ambayo biashara inafuata bila ya kuivunja.
Kila biashara inapaswa kuwa na misingi au miiko yake, ambayo walio ndani na nje ya biashara wanapaswa kuifuata bila ya kuivunja. Walio ndani ya biashara ni wamiliki na wafanyakazi na walio nje ni wateja na wadau mbalimbali wa biashara.
Pale mtu yeyote anapovunja misingi muhimu ambayo biashara hiyo imejengwa basi anapaswa kuondolewa kwenye biashara hiyo. Kwa sababu kama anayevunja misingi ataendelea kuachwa kwenye biashara, biashara hiyo itakuwa dhaifu na kufa.
Hapa ndipo changamoto za biashara nyingi zinapoanzia, watu wanavunja misingi na miiko ya biashara, lakini bado wanaachwa kwenye biashara. Wanaachwa kwa sababu mmiliki wa biashara anaona biashara yake haiwezi kwenda kama atawaondoa watu hao.
Na hapa ndipo ninapokupa kauli hii moja muhimu unayopaswa kuitafakari kila wakati; kama umeanzisha biashara yako binafsi na unashindwa kumfukuza mtu aliyendani (mfanyakazi au mbia) au nje (mteja au mdau) ya biashara basi funga biashara hiyo mara moja. Ifunge kwa sababu unachofanya ni kupoteza muda tu, kama biashara hiyo haina cha kusimamia itaangushwa na chochote.
Kama biashara haiwezi kwenda bila kuwategemea wasioheshimu misingi na miiko ya biashara hiyo, hapo huna biashara, ni swala la muda tu kabla haijafa kabisa.
Kwenye riwaya ya Fountainhead iliyoandikwa na Ayn Rand ambapo Howard Roark anapambana na wajamaa wanaotaka kutumia kipaji chake na kumdhibiti watakavyo, kuna kisa kimoja kinaeleza vyema hili ninaloshauri hapa. Gail Wynand mmoja kati ya wachache waliokuwa wanamuunga mkono Howard alikuwa anamiliki magazeti yenye ushawishi mkubwa. Ellsworth Toohey aliyekuwa anampinga sana Howard alikuwa mmoja wa waandishi na wahariri wa magazeti hayo. Toohey alipanga kuyatumia magazeti ya Wynand kumchafua Howard, kitu ambacho Wynand alikikataa.
Hivyo Toohey alitumia ujanja, wakati ambapo Wynand hayupo, aliajiri wafanyakazi wengi wanaokubaliana na wewe, akashawishi bodi ya wakurugenzi iwe upande wake na hapo akawa amepata udhibiti mkubwa wa magazeti hayo.
Baada ya kujihakikishia udhibiti wa magazeti, alianza kumchafua Howard kupitia magazeti hayo. Wynand aliporudi hakupendezwa na hilo, alimuita Toohey ofisini kwake na hapo Toohey akamwambia wazi kwamba kwa sasa yeye ndiye mwenye udhibiti wa magazeti hayo na hawezi kumfukuza. Wynand alimjibu kwa ufupi; siku ambayo nitashindwa kumfukuza mfanyakazi niliyemuajiri kwenye biashara yangu, ndiyo siku nitakayoifunga hiyo biashara kabisa. Na kweli ilimbidi Wynand kufunga magazeti yake maana Toohey alikuwa ameshakita mizizi.
Kuna mengi sana ya kujifunza kwenye kisa hicho na ushauri huu kwa ujumla. Lazima biashara iwe na misimamo na miiko na yeyote anayeivunja hapaswi kuachwa. Na kama kuondolewa kwake hakuwezekani, basi bora biashara ifungwe.
Kingine muhimu cha kujifunza ni umuhimu wa biashara kuendeshwa kwa mfumo ambapo hakuna mtu mmoja ambaye asipokuwepo basi biashara inakuwa imekufa. Hata wewe mmiliki wa biashara, lazima biashara iweze kwenda bila uwepo wako, la sivyo huna biashara.
Hatua
za kuchukua hapa ni kujenga mfumo imara wa biashara yako ambao una
misingi, miiko na miongozo ya jinsi ya kuendesha biashara hiyo. Kila
anayehusika kwenye biashara anapaswa kuuelewa vizuri mfumo huo na
kuufuata. Na pale inapotokea mtu anakwenda kinyume na mfumo basi
anapaswa kuondolewa mara moja. Na kama unaona huwezi kumwondoa kwa kuwa
biashara haiwezi kwenda, basi bora ufunge biashara moja kwa moja.
JIUNGE leo DARASA ONLINE " ili uweze KUJIFUNZA MISINGI NA MIIKO YA BIASHARA kujenga biashara imara na isiyotikiswa na kitu chochote. Wasiliana NAMI KOCHA MWL. JAPHET MASATU ( WhatsApp + 255 716924136 ) NIKUUNGE LEO.
Makala hii imeandikwa na Kocha Mwl Japhet Masatu ambaye ni MWALIMU KITAALUMA, kocha wa mafanikio, mwandiashi na mjasiriamali.