Umasikini
siyo tu ni mzigo na kikwazo kwa mtu kuwa na maisha bora na yenye uhuru,
bali pia ni laana ambayo inamfanya anase kwenye maisha ambayo hawezi
kujinasua.
Utafiti ambao umewahi kufanywa nchini Marekani na India unaonesha kwamba umasikini huwa unaharibu akili ya mtu.
Utafiti
huo ulionesha kwamba wale wanaoishi kwa umasikini, wana upungufu wa
alama 13 za kipimo cha akili (IQ) ukilinganisha na wale ambao hawaishi
kwenye umasikini.
Kwa lugha rahisi na ya kueleweka vizuri ni kwamba umasikini unawafanya watu kuzidi kuwa wajinga.
Swali unaloweza kujiuliza ni kwa namna gani umasikini unaharibu akili za watu na kuwafanya kuwa wajinga?
Jibu
liko wazi, masikini anakuwa ametingwa zaidi na mawazo ya hali ngumu
anayokuwa anapitia, hivyo akili yake inakuwa imechoka muda wote.
Inapokuja kwenye uhitaji wa kufikiri mambo makubwa na magumu, masikini
hawezi kufikiri kwa usahihi, kwa kuwa akili yake tayari imeshachoka.
Chukua
mfano wa watu wawili, wana elimu sana na wanafanya kazi ya aina moja.
Mtu A ni tajiri na B ni masikini. Mtu A ameamka asubuhi, kapata kifungua
kinywa kizuri, kaingia kwenye gari yake binafsi na kwenda kazini. Mtu B
ameamka hana hata kifungua kinywa, anaenda kazini kwa kutumia usafiri
wa umma ambao ni wa shida na hajui siku hiyo atakula nini, wakati huo
huo kuna watu wanamdai na wanamtafuta sana. Watu hao wawili wanapewa
jukumu moja la kukamilisha, ambalo linahitaji utulivu wa akili ili
kulikamilisha, unafikiri yupi atalikamilisha kwa umakini?
Unajionea mwenyewe hapo, jinsi ambavyo umasikini unakuwa mzigo ambao unaharibu akili ya mtu na kumfanya awe mjinga.
Umasikini
unapunguza uwezo wa mtu kufikiri na kufanya maamuzi kwa sababu muda
mwingi akili yake inakuwa imetingwa na fikra na hofu mbalimbali.
Mbaya
zaidi sasa, na hapa ndipo ilipo laana ya umasikini, ni pale uwezo mdogo
wa kufikiri unapomfanya mtu afanye maamuzi mabovu zaidi na yanayomfanya
abaki kwenye umasikini.
Tuendelee
na mfano wa mtu B, ambaye anafikiria siku yake inaishaje, maana
mshahara umeshaisha na mwezi ndiyo kwanza uko katikati. Anasikia kuna
mtu anatoa mkopo wa haraka ila una riba kubwa. Kwa sababu anachohofia
zaidi ni fedha na hawezi kufikiri kwa usahihi, anajikuta anachukua mkopo
huo. Anakuja kulipa mkopo kwa riba kubwa, kitu kinachopunguza kipato
chake zaidi.
Maamuzi
mengi ambayo mtu anasukumwa kuyafanya akiwa masikini huishia kuwa
maamuzi ya kumuumiza zaidi na kumfanya abaki kwenye umasikini.
Unaondokaje kwenye mtego na laana hii ya umasikini?
Umejionea hapo jinsi umasikini unavyoharibu akili na kumnasa mtu kwenye umasikini zaidi.
Kama
bado hujafikia uhuru wa kifedha, kama bado unategemea kipato
unacholipwa kwa kufanya kazi au biashara ndiyo uendeshe maisha yako,
haijalishi kipato hicho ni kikubwa kiasi gani, upo kwenye hii hatari.
Hivyo
hatua muhimu kwako kuchukua ni kujijengea uhuru wa kifedha. Na hapa
kuna maeneo sita muhimu ya kufanyia kazi ili kuondoka kwenye mtego na
laana ya umasikini.
Eneo
la kwanza ni kuongeza kipato chako. Kipato chochote unachoingiza sasa
hakiwezi kukutosha, gharama za maisha zinachukua sehemu kubwa ya kipato
chako. Hivyo pambana kuongeza kipato chako. Kama umeajiriwa anzisha
biashara ya pembeni. Kama upo kwenye biashara ongeza huduma na bidhaa
zaidi na wafikie wateja wengi zaidi. Kwa kipato chochote unachoingiza
sasa, pambana kukikuza zaidi.
Eneo
la pili ni kudhibiti matumizi yako. Matumizi huwa yana tabia ya kukua
kadiri kipato kinavyokua. Usipoyadhibiti, ongezeko la kipato
ulilopambana nalo halitaleta tofauti kwenye maisha yako, badala yake
litakuwa limekuchimbia kwenye umasikini zaidi. Dhibiti matumizi yako kwa
kuhangaika na yale ya msingi pekee, hasa kama unaanzia kwenye umasikini
wa chini kabisa.
Eneo
la tatu ni kuwa na akiba ya dharura ya miezi 6 mpaka 12. Kama unaishi
maisha ya mkono kwenda kinywani, yaani unafanya kazi, unaingiza kipato
na unakitumia chote, basi upo kwenye hatari ya umasikini kuharibu akili
yako zaidi. ukipata dharura yoyote ile, iwe ni kazi kusimama au biashara
kuyumba, utaanguka vibaya mno. Hakikisha unakuwa na akiba ya
kukuwezesha kuendesha maisha yako kwa miezi sita mpaka 12 hata kama
hutakuwa na kipato kabisa. Unapokuwa na akiba ya aina hii, unapata
utulivu mkubwa ndani yako na kuweza kufanya maamuzi sahihi kwako. Mfano
kama umefukuzwa kazi na huna akiba, utalazimika kufanya kazi yoyote hata
kama haikulipi, kwa sababu unataka kipato cha kuendesha maisha. Lakini
kama umefukuzwa kazi na una akiba ya miezi 12 ya kuendesha maisha,
unaweza kusubiri kwa muda mpaka upate kazi nzuri, maana akiba ya
kuendesha maisha ipo.
Eneo
la nne ni uwekezaji. Huwezi kufanya kazi muda wote na kila muda ambao
hufanyi kazi hunufaiki. Unapaswa kuwa na njia ya kuingiza kipato hata
kama hufanyi kazi moja kwa moja. Na njia ya kufanya hivyo ni kuwa na
uwekezaji ambao unazalisha faida na kukua thamani kadiri muda
unavyokwenda. Unapokuwa na uwekezaji unaozalisha faida kubwa ya
kukuwezesha kuendesha maisha yako hata kama hufanyi kazi moja kwa moja,
unakuwa umefikia uhuru wa kifedha.
Eneo
la tano ni kulipa madeni ambayo unayo. Kama umekopa, pambana kulipa
madeni yako kwa kutumia ongezeko la kipato ulilofanyia kazi.
Eneo
la sita ni kuacha kukopa. Usikope tena, rahisisha maisha yako, punguza
yasiyo muhimu na kama kitu huwezi kukimudu jipe muda. Vitu vingi
unavyoingia kwenye madeni ili kuwa navyo ni vitu ambavyo siyo muhimu
sana kwako. Ukiacha kuiga maisha ya wengine na kuchagua kuishi maisha
yako, hutahangaika na mikopo inayokusumbua.
Zingatia maeneo hayo sita ili kuweza kuondokana na mtego na laana ya umasikini.
Ndimi KOCHA MWL. JAPHET MASATU , DAR ES SALAAM
( WhatsApp + 255 716 924 136 ) / + 255 755400128 / + 255 688361539
EMAIL : japhetmasatu@gmail.com