Monday, August 31, 2020

KUJIJENGEA NIDHAMU NA UDHIBITI WA MUDA.

Tambua muda ndiyo rasilimali yenye uhaba, ambayo ukishapoteza hairudi tena. Katika kujijengea nidhamu na udhibiti wa muda, fanya yafuatayo;

1. Chukua kalamu na karatasi, gawa karatasi yako katika pande mbili, A na B.

2. Upande A orodhesha mambo yote ambayo umefanya kwenye wiki moja iliyopita, kila ulichofanya kiorodheshe, uliingia mtandaoni, orodhesha, uliangalia mpira, weka, ulibishana na watu weka.

3. Upande B orodhesha malengo na mipango uliyonayo, kile unachotaka kufikia ndani ya mwaka mmoja, miaka 5, 10 na mpaka 20 ijayo.

4. Linganisha orodha A na B, piga mstari kile ulichofanya upande A ambacho kinakusaidia kufikia upande B.

5. Baada ya hapo, chukua yale ya upande A ambayo yana mchango kwenye upande B na hayo tu ndiyo utakayoanza kuyafanya kuanzia sasa. Yale mengine uliyokuwa unafanya na hayana mchango kwenye kufikia malengo na mipango yako, achana nayo mara moja.

Yaani jiambie tu kuanzia leo sifanyi tena haya, na acha mara moja. Vitu kama kufuatilia habari, kubishana, mitandao ya kijamii na mengine utapaswa kuachana nayo mara moja.

Manufaa ya zoezi hili ni wewe kupata muda mwingi zaidi wa kufanya yale ambayo ni muhimu zaidi kwako. Na hapo hutakuwa tena na tatizo la muda.


 

Sunday, August 30, 2020

JINSI YA KUJIJENGEA NIDHAMU NA UDHIBITI WA FEDHA.

Kila pesa inayopita kwenye mikono yako ni mbegu, ambayo ukiitumia vizuri itakuwa na manufaa kwako. Lakini wengi wamekuwa hawana nidhamu na udhibiti mzuri wa fedha zao. Hapa kuna hatua za kuchukua kwenye kujijengea nidhamu na udhibiti wa fedha zako.

1. Nenda kwenye benki unayotumia sasa na fungua akaunti maalumu ambayo unaweza kuweka fedha lakini kutoa siyo rahisi au kuna ukomo. Karibu kila benki ina akaunti ya aina hii.

2. Omba huduma ya fedha kuhamishwa kwenye akaunti yako ya sasa ambayo ndiyo inaingiza kipato chako kikuu, iwe ni mshahara au fedha unazoweka akiba. Kwamba kila mwezi kuna kiasi watakikata kwenye akaunti yako ya akiba kwenda kwenye akaunti yako maalumu.

3. Weka akiba kwenye akaunti hiyo maalumu kila mwezi, bila kuigusa kwa angalau mwaka mmoja. Jiwekee kiwango cha kipato chako ambacho kitaenda kwenye akaunti yako, unaweza kuanza na asilimia 10 au nyingine itakayokufaa wewe.

4. Hakikisha kipato chako kinakatwa kabla ya matumizi, kama unafanya shughuli zako binafsi basi unapolipwa, kabla hujaanza kutumia weka kwanza pembeni kiasi cha akiba na kiweke kwenye akaunti hiyo.

5. Pesa iliyo kwenye akaunti hiyo maalumu isahau kabisa, chukulia kama ulinunua kitu fulani na hivyo usiiweke kwenye mahesabu. Ni mpaka mwaka uishe ndiyo utarudi kwenye fedha hiyo na kuchagua ufanye nayo kitu gani cha kuzalisha zaidi.

Zoezi hili linakulazimisha kujiwekea akiba na baadaye kuiwekeza, kitu ambacho kitakuweka vizuri kwenye eneo la fedha.



 

Saturday, August 22, 2020

KWANINI UNAPITIA CHANGAMOTO NYINGI ? JIFUNZE SABABU TANO ( 05 ) NA JINSI YA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO HIZO.

Kitu pekee tunachojifunza kwenye historia ni kwamba hakuna tunachojifunza kwenye historia, hiyo ni kauli aliyowahi kuitoa mwanafalsafa Hegel.

Ni kauli nzito na inayopaswa kutufundisha mengi, lakini kama Hegel alivyoeleza, haitufundishi chochote.

Iko hivi rafiki, hakuna kitu kipya kinachotokea hapa duniani kwa sasa. Kila kinachotokea sasa kimewahi kutokea huko nyuma, kwa sasa kimetokea tu kwa namna tofauti, labda kutokana na teknolojia kuwa ya juu.

Kuanzia matatizo yanayoikumba dunia, nchi na hata mtu mmoja mmoja, yote yamewahi kutokea tena huko nyuma. Maisha tunayoishi sasa ni marudio tu.


Lakini cha kushangaza, tunarudia makosa yale yale ambayo waliotutangulia waliyafanya walipokuwa wanapitia hali kama tunazopitia sasa. Kama tungechukua muda kujifunza kupitia waliotutangulia, tungepunguza makosa ambayo tunafanya.


Lakini hatufanyi hivyo, kwa sababu ambazo nakwenda kukushirikisha hapa. Kwa kila sababu nitakushirikisha hatua ya kuchukua ili maisha yako yaweze kuwa bora na uweza kukabiliana na kila changamoto unayopitia sasa.

( 01 ). WATU   KUACHA  KUSOMA  VITABU.

Uandishi ndiyo uvumbuzi mkubwa kuwahi kutokea duniani, alinukuliwa Abraham Lincolin. Hebu fikiria, leo hii unaweza kusoma vitabu vilivyoandikwa zaidi ya miaka elfu 2 iliyopita. Ni kwa sababu uandishi umeruhusu maarifa hayo kuweza kutunzwa na kurithishwa vizazi na vizazi.


Uzuri ni kwamba, kila unachopitia sasa, kuna mtu alishapitia miaka mingi iliyopita na akaandika kitabu kuhusu uzoefu wake kwenye hilo alilopitia. Kama mtu alipambana na kitu kwa miaka kumi na kukiandika kitabu, unaweza kukisoma kwa siku chache na ukaokoa kupoteza miaka 10 kwa kurudia makosa waliyofanya wengine.


Lakini cha kusikitisha ni kwamba watu wameamua kuacha kusoma vitabu. Wana kila sababu kwa nini hawasomi vitabu, lakini hakuna sababu yenye mashiko. Ni sawa na kukutana na mtu ambaye yuko mbio na unajaribu kumsimamisha anakuambia anachelewa. Ukimuuliza kwani unawahi wapi, hajui, lakini yuko kasi.

Ondoka mara moja kwenye tabia hiyo ya kutokusoma vitabu, chagua eneo unalotaka kubobea, amua wapi unataka kufika, kisha tafuta vitabu bora kwenye hayo na visome.


Ukitenga saa moja kila siku ya kusoma, au ukaweka utaratibu wa kusoma kurasa 10 za kitabu kila siku, kila mwezi utamaliza angalau kitabu kimoja na kwa mwaka angalau vitabu kumi.


Kama utatafakari yale uliyojifunza kwa kina, kisha ukachukua hatua kwenye maisha yako, huwezi kubaki pale ulipo sasa. Lazima utapiga hatua kubwa, utaepuka kurudia makosa ya wengine na kujifunza njia bora zaidi za kufanya unachofanya. 

( 02 ). WATU  KUPENDA    KUSOMA   VITU  VIFUPI.

Vitabu ni njia moja ya kujifunza, lakini pia zipo njia nyingine za kujifunza, kama kupitia makala, tafiti, ripoti mbalimbali na hata insha.


Uzuri ni kwamba, tunaishi kwenye zama ambazo mtandao wa intaneti unarahisisha kusoma maarifa hayo mbalimbali, tena bure kabisa.


Lakini cha kushangaza, watu hawapendi kusoma vitu virefu. Makala kama hii, wengi walioanza kusoma wameishia aya ya tatu, na wengine wanapita wakiangalia vichwa au maneno yaliyokolezwa tu.

Watu hawana tena umakini na utulivu wa kuweza kutenda dakika kumi za kusoma kitu kwa kina na kuondoka na maarifa ya kwenda kufanya kazi.

Usumbufu ni mwingi, kila mtu anapitia vitu juu juu, kinachotokea ni maarifa mazuri yanaelea huko mtandaoni huku wanaoyahitaji wakiteseka. Ni sawa na mtu ambaye anaogelea kwenye ziwa, lakini anakufa kwa kiu.

Kuondokana na hili, kwenye siku yako tenga muda ambao utasoma vitu kwa kina, ni bora usome vitu vichache kwa kina kuliko usome vitu vingi kwa juu juu. Kwa kila unachosoma, usikiache mpaka umeorodhesha nini umejifunza na namna gani unaenda kuboresha maisha yako.

Chagua mitandao au waandishi ambao utakuwa unajifunza kwao na weka umakini wako wakati unasoma kitu chochote kile. Usiwe na haraka wala kukimbilia popote, hakuna mashindano wala tuzo za aliyesoma vitu vingi zaidi. Tuzo pekee ni maisha yako kuwa bora, hivyo kazana na hilo.

( 03 ).  WATU  KUTUMIA   MUDA  MWINGI  KWENYE   MITANDAO  YA  KIJAMII.

Mitandao ya kijamii imepata umaarufu mkubwa na karibu kila mtu anaitumia kwa sasa. Mitandao hii imetuhadaa kwamba inatupa nafasi ya kuwasiliana na wengine na kutengeneza marafiki wengi.

Lakini ukweli wa mitandao huu umekuwa unafichwa. Mitandao hii imetengeneza mabilioni ya pesa, kwa kukuuza wewe. Angalia, hii mitandao haina bidhaa yoyote inayouza, na wewe unaitumia bure. Unajua inapataje pesa? Kwa kuuza umakini wako kwa watu wanaotaka kutangaza biashara zao mbalimbali.

Mitandao hii pia imechangia watu kukosa muda na umakini wa kusoma vitabu na mafunzo mengine mazuri.


Mtandao wa instagram umepata umaarufu mkubwa kwa sababu huhitaji kufikiria chochote, wewe piga picha yako na weka, halafu subiri wa kukusifia na kukupa likes.

Mtandao wa twitter umepata umaarufu mkubwa kwa sababu ukomo wa unayoweza kuandika, ambao ni herufi 280 tu, huwezi kuandika zaidi ya hapo. Hivyo ni vitu vifupi vifupi tu vinaandikwa huko, na kwa sababu watu hawataki vitu virefu, wanafurahia sana mtandao huo.

Rafiki, kama hutumii mitandao hiyo ya kijamii kibiashara, yaani kama huingizi fedha moja kwa moja kutoka kwenye mitandao hiyo, basi acha kuitumia mara moja. Hakuna manufaa yoyote unayoyapata kwenye mitandao hiyo, zaidi ya usumbufu, msongo na kupunguza umakini wako.

Jitoe kabisa kwenye mitandao yote ya kijamii, na ghafla utaona jinsi ulivyo na muda mwingi wa kufanya yale muhimu kwako. Nilichukua hatua hii mwaka 2018 baada ya kukaa kwenye mitandao hiyo kwa miaka 9 na sijawahi kujutia maamuzi hayo.

(04 ). WATU  KUISHI  KWA   MAZOEA  NA  KUFUATA  MKUMBO.

Hivi umewahi kukaa chini na kujiuliza kwa nini unafanya kila unalofanya? Umefanya kazi au biashara uliyonayo sasa kwa muda, lakini je unajua kwa nini uliingia kwenye kazi au biashara hiyo? Unajua wapi unapotaka kufika?


Hata mengine unayofanya kwenye maisha, labda umechukua mkopo, umejenga nyumba, umeoa au kuolewa, umewahi kujiuliza kwa nini ulifanya maamuzi hayo?


Kwa bahati mbaya sana, maamuzi mengi ambayo watu wanafanya ni kwa mazoea au kufuata mkumbo. Mtu anaambiwa wenzako wameshaoa au kuolewa, na yeye anafanya hivyo. Mtu anaona wenzake wanachukua mkopo na yeye anachukua. 

Maisha ya aina hii yamekuwa hayakosi changamoto, kwa sababu mtu anahangaika na mengi lakini hayana maana kwake. Hivyo mwisho wa siku anayaona maisha yake yakiwa tupu, anaweza kuwa na kila anachoambiwa anapaswa kuwa nacho, lakini hana furaha.

Huwezi kuwa na furaha kwenye maisha kama hujayaishi maisha yako, kama hujajijua wewe mwenyewe na kuishi kwa uhalisia wako. Unaweza kupata kila ambacho wengine wanacho, tena wengine wakakuonea wivu kwa nafasi uliyonayo, lakini ndani yako ukajiona ni mtupu.

Acha sasa kuishi maisha ya mazoea au kufuata mkumbo, kwa kila jambo unalofanya, jua kwa nini unafanya. Kwanza kabisa jitambue wewe mwenyewe, jua uimara na udhaifu wako, jua wapi unataka kufika na maisha yako. Kisha hoji kila unalotaka kufanya linaendanaje na wewe na linakufikishaje kule unakotaka kufika.


Usiogope kufanya kitu peke yako, usiogope kupingwa, kukosolewa na kuchukiwa na wengine. Wewe pekee ndiye unayejijua kuliko wengine wanavyokujua, chagua kuyaishi maisha yako na siyo kuwafurahisha wengine.


( 05 ). KUTEGEMEA  FURAHA  KUTOKA  KWNEYE  VITU  VYA   NJE.

Kama unajiambia ukishafika hatua fulani au kuwa na kitu fulani ndiyo utakuwa na furaha basi jua unatembea na laana. Hiyo ni kwa sababu hakuna furaha ya kudumu utakayoipata kwa kitu chochote cha nje yako. Unaweza kupata raha ya muda mfupi, lakini siyo furaha ya kudumu.

Kutegemea furaha kutoka kwenye vitu vya nje imekuwa ndiyo chanzo cha matatizo ambayo wengi wanakutana nayo kwenye maisha. Ulevi ambao wengi wanaangukia ni kutafuta furaha za nje na za haraka, kitu ambacho kimekuwa hakidumu.

Tambua kwamba furaha ya kweli na idumuyo inaanzia ndani yako, inaanza na wewe mwenyewe na haitegemei chochote cha nje. Kama huna furaha kabla hujapata unachotaka, hata ukikipata huwezi kuwa na furaha.

Mafanikio hayaleti furaha, bali furaha ndiyo inaleta mafanikio. Hivyo anza na furaha, jitambue, jua wapi unakwenda, jipende, penda unachofanya na kila siku piga hatua kuwa bora zaidi. Kwa njia hizi, utakuwa na furaha bila kujali uko kwenye ngazi ipi.

Rafiki yangu mpendwa, hizo ndizo sababu kubwa tano za changamoto nyingi tunazopitia kwenye maisha ya zama hizi. Tukiweza kutatua hizi kwa kuzingatia yale tuliyojifunza, hakuna kitakachokukwamisha, utakuwa na maisha tulivu, yenye furaha na mafanikio makubwa.

 

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri 

ENDELEA  KUSOMA   HAPA " MAISHA   NA  MAFANIKIO( LIFE  AND  YOU )  BLOG  " KARIBU   PIA    UJIUNGE  KATIKA   " DARASA  LETU--ONLINE  " KWA   KUWA   MWANACHAMA.

Makala Hii Imeandikwa Na MWL.  JAPHET   MASATU , Ambaye Ni MWALIMU   KITAALUMA , KOCHA   WA  MAISHA   NA   MAFANIKIO , MSHAURI , MWANDISHI NA MJASIRIAMALI,  PUBLIC  SPEAKER


Tuwasiliane  kwa  WhatsApp + 255 716924136   /    + 255 755  400128  / + 255 688361539

 

Wednesday, August 19, 2020

WATEJA WA ZAMANI NI LULU ?? WEKA KUMBUKUMBU ZAO . !!!

 Nguzo muhimu katika biashara yoyote duniani ni wateja. Ninaweza kusema kwamba biashara inafanikishwa na watu wawili; yaani mfanyabiashara ambaye ndiye anauza bidhaa au huduma na wa pili ni mteja ambaye ananunua bidhaa. Kama unafanya biashara ambayo wateja wapo, tunasema biashara hiyo inalipa lakini kama wateja hawapo tunasema biashara yako hailipi. Kwahiyo, kuendelea kwa biashara yako ni
wateja. Kwenye biashara kuna aina mbili za wateja, ambao ni wateja wa zamani na wateja wapya. 

Kwa jinsi hali ilivyo huku mitaani kwetu, ni kwamba wafanyabiashara wengi wanajali zaidi wateja mpya. 

Mteja mpya anaonyeshwa kila aina ya upendo kiasi cha kumkatishatamaa mteja wa zamani endapo ikitokea wote wawili wakawepo pamoja eneo la biashara. 

Hali hii ya kutengwa kama mteja wa zamani imenitokea mara nyingi na kunifanya niamini kwamba kadiri unavyozidi kununua bidhaa mara nyingi kutoka kwa mfanyabiashara fulani ndivyo anavyoacha kukujali. 

Kiashiria mojawapo ni wakati mwingine mteja wa zamani anapouziwa vitu kwa bei tofauti na Yule mteja mpya. Yaani ni ajabu wateja wapya wanapunguziwa wakati wale wa zamani wanaonunua vitu mara kwa mara wanapandishiwa bei. 

Wakati mwingine baadhi ya wafanyabiashara wanakupunja wewe mteja wao wa zamani kupitia vipimo hasa kwa bidhaa kama sukari, nyama, mchele n.k. 

Ukweli ni kwamba, mteja wa zamani ni LULU. Unapashwa kumtengenezea mazingira rafiki kwa kuhakikisha unampatia unafuu kadiri mtakavyozidi kukaa pamoja kibiashara. Ikiwa utazidi kumjali na yeye atazidi kuwa na sababu ya kuendelea kuwa mteja wako daima. 

Kwanini mteja wa zamani? 

Ukizidi kuwajali wateja wa zamani inakusaidia wewe kupata wateja wapya kwa gharama kidogo sana; kuliko ambavyo ungewatafuta wewe mwenyewe moja kwa moja. 

Mteja wa zamani ni mtaji mkubwa” endapo utakaanaye vizuri, na hii nikutokana na ukweli kwamba, anaouwezo wa kukuletea wateja wapya kila mara. 

Mteja wa zamani ni rahisi kumtunza kuliko kupata mteja mpya. 

Sisi wataalamu wa masuala ya masoko tunasema kuwa gharama za kumpata mteja mpya ni mara saba zaidi ya gharama za kukaa na mteja wako wa zamani. 

Mteja wa zamani tayari anakufahamu kwahiyo, akiambiwa juu ya mali mpya hana mud sana wa kuhoji kwasababu tayari anakuamini na hivyo ataweza kuitikia haraka. 

Uzoefu wangu unaonyesha kuwa inachukua muda na nguvu nyingi kumshawishi mteja mpya kukubali bidhaa yako kuliko wa mteja zamani. 

Tayari wewe unafahamu vizuri tabia na mahitaji ya wateja wako wa zamani, kwahiyo inakuwa rahisi kujua namna nzuri ya kutengeneza mkakati wa kuongeza mauzo yako bila kusahau kuwapa kilicho bora. 

Nifanye nini kukuza uhusiano na wateja wangu wa zamani? 
Unachotakiwa kufanya ni kujifunza jinsi ya kujenga na kuimalisha mahusiano na watu hasa wale wanaokuja kununua bidhaa na huduma mbalimbali kutoka kwako. 

Ni muhimu sana kujenga mahusiano ya karibu na kila mteja mpya wakiwemo wale walioletwa na mteja wako wa zamani, lakini jenga uhusiano na kila mmoja peke yake siyo kama kikundi. 

Katika mchakato wa kujenga uhusiano na wateja fanya yafuatayo; 

Badili tabia yako juu ya mahusiano: Tabia yako ya mahusiano na watu wengine ni muhimu sana. Usidhani suala zima la kujali watu litatokea tu siku moja, lazima uzame ndani kwenye tabia yako kwanza. 

Andaa orodha ya majina na namba za simu: Jiwekee utaratibu wa kuwa na orodha ya majina pamoja na namba zao za simu. Ukiwa na orodha ya majina ni rahisi kuwa na kumbukumbu ya nani kanunua nini na kiasi gani mwaka mwezi au mwaka huu. 

Inapofika sikukuu maalum kama Krismas hawa ndio wa kuwapa kipaumbele unapotuma salam za pongezi. Sijui wewe kama uliwahi kumtumia mtu heri ya krismas kwasababu tu ni mteja wako mzuri..kama hujafanya hivyo basi jitafakari na uchukue hatua. 

Toa elimu juu ya bidhaa/huduma: Hakikisha wateja wako wanapata elimu bora juu ya matumizi sahihi ya bidhaa zako, ili waweze siyo tu kununua bali kueneza habari njema kwa wateja wengine. Kadiri utakavyozidi kuwaelimisha ndivyo utakavyozidi kuzalisha wateja wengi ambao ni waaminifu. 

Shirikiana nao shughuli za kijamii: Jaribu kuwa nao karibu kwenye shughuli za kijamii; kama ni kuchangia harusi fanya hivyo, hawa ndio unatakiwa kuwachangia, kama ni misiba hawa unalazimika kuwatembelea na kuwafariji. 

Kwahiyo, kupitia mahusiano yako na wateja, unajikuta umejenga kundi kubwa la marafiki na ndugu mlioshibana. 

Bahati mbaya sana wengi tunashiriki zaidi shughuli za kijamii kwa watu ambao hawana uhusiano wowote na biashara zetu. 

Unahitaji kuwaongeza kwenye orodha wateja wako, ili linapofika suala zima la kushirikiana katika shughuli za kijamii, nao wawe ni sehemu ya watu unaowakumbuka. 

Toa tuzo kwa wateja: Kama unachukua kumbukumbu za wateja vizuri ni rahisi kwako kuona nani amechukua pesa zake kwa wingi kwa katika kipindi cha mwezi, robo, nusu mwaka au mwaka mzima. 

Hapa utakuwa na nafasi ya kujua ni nani umpe tuzo. Tuzo hiyo siyo lazima uwambie, unaweza ukatafuta utaratibu wa kumpongeza au kumpa tuzo. 

Mafano; kutoa mwaliko wa chakula cha jioni au kinywaji nyumbani au hoterini; unaweza kutuma salam za pongezi mfano kupata mtoto, kumaliza shule kwa watoto n.k. 

Wewe uliye na biashara yoyote tambua kuwa unahitaji kuendelea kujifunza mpaka ufike sehemu uone kwamba wateja ndio ndugu namba moja. 
 
KWA   KUJIFUNZA   KWA  MAPANA  NA   MAREFU    JIUNGE  NA   "  DARASA   ONLINE "   KWA  KUWA  MWANACHAMA.
Tuwasiliane  kwa  WhatsApp  + 255 716924136  /   + 255 755  400128  + 255  688  361  539

Ndimi  RAFIKI   NA   KOCHA   MWL.  JAPHET  MASATU , 
DAR  ES  SALAAM , TANZANIA.

 

MAMBO 03 UNAYOHITAJI ILI UNUFAIKE NA USOMAJI WA VITABU

 



Wengi wa wanaosoma vitabu wanapoteza tu muda wao, wanakazana kusoma ili waweze kuwaambia wengine wamesoma vitabu vingapi, huku maisha yao yakiwa hayabadiliki kwa namna yoyote ile.

Huu siyo tu upotevu wa muda, bali pia kuchafua akili, maana kama ambavyo Alexander Pope amewahi kusema, “Maarifa kidogo ni kitu hatari, unapaswa kunywa kwa kina au usionje kabisa maji ya chemchem ya maarifa. Maarifa ya juu juu ni sumu kwa akili.”

Hili tumekuwa tunaliona wazi, mtu anapata maarifa kidogo ambayo hata hajayaelewa kwa kina na kuanza kuona anajua kila kitu, kuanza kuwadharau wengine ambao hawana maarifa hayo, lakini cha kushangaza, maisha yao yanabaki vile vile.




Mtu anaweza kusoma kitabu kimoja au vichache na kujifunza juu juu kwamba elimu rasmi ni upotevu wa muda na ajira ni utumwa. Akatoka hapo na moto wa kwenda kuacha shule au kuacha kazi, lakini anakuwa hajaiva kwenye nini aende kufanya, kinachotokea ni majuto baadaye.

Wapo wanaokuja kukiri wazi kwamba waliponzwa na vitabu na wapo ambao hawataki kuona kosa ni lao, bali hutafuta wengine wa kuwalaumu. Na siku hizi limepatikana kundi rahisi la kulaumu kwenye kupotezwa na maarifa ambalo ni la wahamasishaji au kama wanavyojulikana ‘motivational speakers’.

Mtu anapata maarifa ya juu juu, anatoka akiwa amejaa upepo na kwenda kuchukua hatua, ambazo zinamwangusha vibaya. Badala ya kuangalia tatizo liko wapi, ambalo ni yeye, anatupa lawama kwa mwingine.

Leo tunakwenda kujifunza vitu vitatu unavyohitaji ili uweze kunufaika na usomaji wa vitabu. Ukizingatia vitu hivi vitatu, hutakuja kulaumu usomaji wa vitabu, maana utakuwa na manufaa makubwa kwako.

Kwenye kitabu cha Fahrenheit 451, mhusika mkuu, Guy Montag ni mzima moto (Fireman), ambaye kwenye jamii yao kazi yao siyo tena kuzima moto, bali kuchoma vitabu moto. Ni jamii ya watu ambao wameacha kusoma vitabu na kuendekeza starehe na burudani mbalimbali kama kuangalia tv na michezo mingine.

Guy amefanya kazi hiyo kwa miaka kumi, lakini hajawahi kupata nafasi ya kutafakari kama kazi hiyo ina maana kwake au inampa furaha. Kwa udadisi, amekuwa akiiba vitabu kwenye nyumba wanazokwenda kuchoma, ila hajawahi kuvisoma, amekuwa anavificha ndani.

Siku moja Guy anakutana na binti ambaye anamhoji maswali yanayomfanya aanze kuyatafakari maisha yake na hapo anagundua kwamba maisha anayoishi siyo sahihi.

Anaamua aanze kusoma vitabu, lakini tatizo linakuja kwamba haelewi chochote anachosoma. Siku nzima anakazana kufungua vitabu na kusoma, lakini haelewi chochote.

Anakumbuka aliwahi kukutana na mzee mmoja ambaye alikuwa profesa aliyepoteza kazi yake baada ya watu kuacha kusoma. Anamtafuta ili amsaidie jinsi anavyoweza kusoma vitabu na kuelewa.

Profesa huyo anampa vitu vitatu anavyopaswa kuzingatia ili aweze kusoma vitabu, kuvielewa na maisha yake yabadilike. Hapa nakwenda kukushirikisha vitu hivyo vitatu ili na wewe uweze kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako kupitia usomaji wa vitabu.

Kitu cha kwanza; jua jinsi ya kuchagua vitabu vyenye maarifa bora.

Vitabu havifanani, ubora wa maarifa unaopatikana kwenye vitabu haulingani. Kuna vitabu ambavyo ni bora, vyenye maarifa mazuri na unayoweza kutumia kupiga hatua.

Halafu kuna vitabu ambavyo ni vya hivyo, vyenye maarifa ambayo hayana manufaa kwako.

Kitu cha kwanza kuzingatia ni ubora wa maarifa yaliyo kwenye kitabu. Unapaswa kujua jinsi ya kuchagua vitabu bora kwako kusoma ili uweze kupata maarifa ambayo ni bora.

Kwa zama tunazoishi sasa, mitandaoni kunapatikana kila aina ya vitabu, na vingi sana ni vya hovyo. Ikiwa unataka kuanza kusoma vitabu kwa sasa, utajikuta njia panda usijue ni vitabu gani vya kuanza navyo.

Njia rahisi kwako kujua vitabu vya kuanza navyo, ni kuchagua watu ambao wamepiga hatua kwenye eneo unalotaka kupiga hatua, kisha waulize ni vitabu gani wamesoma.

Kama kuna mtu amefanikiwa zaidi yako, kwenye eneo lolote la maisha, kuna vitu anajua ambavyo wewe hujui. Badala ya kumwonea wivu au kumwogopa, mwombe akushirikishe ni aina gani ya vitabu anasoma, hapo utapata vya kuanzia.

Uzuri wa zama hizi ni mitandaoni kuna orodha za vitabu ambavyo wale waliofanikiwa wamekuwa wanashauri watu wavisome.

Hicho ni kitu cha kwanza, kuweza kuchagua vitabu ambavyo ni bora kwa maarifa yaliyo ndani yake.

Kitu cha pili; muda wa kutafakari yale uliyoyasoma.

Kusoma pekee, hata kama ni kitabu chenye maarifa bora kabisa hakutakuwa na manufaa kwako. Kwanza kabisa hutaweza kukumbuka kila ulichosoma na pili siyo kila maarifa yaliyo kwenye kitabu yatakuwa na manufaa kwako.

Hivyo unapaswa kupata muda wa kutafakari kile ulichosoma. Na hapa ndipo wengi wanapofeli na kuja kulaumu wengine. Wanasoma au kusikia kitu na kukimbilia kuchukua hatua kabla hawajatafakari kwa kina.

Kila maarifa unayoyapata, yatafakari kwa kina. Angalia maisha yako yalipotoka, yalipo sasa na kule yanakokwenda. Angalia ni jinsi gani maarifa uliyoyapata unaweza kuyaingiza kwenye maisha yako.

Kwa bahati mbaya sana, kutafakari ni kitu unachopaswa kukifanya mwenyewe, kwa sababu ni wewe pekee unayeyajua maisha yako kwa undani. Watu wawili mnaweza kusoma kitabu kimoja na wote mkakielewa, lakini hatua za kuchukua zikawa tofauti, kwa sababu maisha yenu ni tofauti.

Ambacho nimekuwa nashauri watu kwenye usomaji wa vitabu ni hiki, anza kwa kujua unataka nini kwenye maisha yako, kisha kila kitabu unachosoma jiulize kinakusaidiaje kupata au kufika pale unapotaka kufika.

Ikiwa hujafanya maamuzi unataka nini, kwenye kila kitabu unachosoma utakuja na vitu vipya. Utasoma kitabu cha kilimo cha tikiti na kuona ndiyo kitu bora, unaenda kufanya, unasoma kitabu cha ufugaji wa kuku unaona huo ndiyo wenyewe, unaenda kufuga. Unasoma kitabu cha forex na kusema siwezi kupitwa na hii, unaenda kufanya. Mwisho unajikuta umejaribu mengi lakini hakuna hatua uliyopiga.

Anza na unachotaka, kisha kwa kila kitabu unachosoma, tafakari kinakusaidiaje kufika kule unakotaka kufika.

Kitu cha tatu; kuchukua hatua kwenye yale uliyojifunza na kutafakari.

Kusoma maarifa ambayo ni bora na kuyatafakari jinsi unavyoweza kuyatumia kwenye maisha yako ili kupata unachotaka ni asilimia 10 ya manufaa ya kitabu.

Asilimia 90 inapatikana kwenye kuchukua hatua. Usikubali usome kitabu halafu maisha yako yabaki kama yalivyokuwa kabla hujasoma kitabu hicho. Chukua hatua, hata kama ni ndogo kabisa, kuhakikisha unakuwa bora kuliko ulivyokuwa kabla ya kusoma kitabu hicho.

Hivyo kwa tafakari unayoifanya, weka hatua utakazochukua na anza kuzichukua mara moja. Hazihitaji kuwa hatua kubwa sana, bali zinapaswa kuwa hatua zenye tija kwako, kiasi kwamba ukijiangalia unaona kitabu ulichosoma kimekuwa na manufaa kwako.

Siyo maarifa yote unayoyapata kwenye kitabu utaweza kuyatumia kwa mara moja, kuna mengine utayahifadhi kwa ajili ya baadaye. Lakini hupaswi kusoma kitabu na ukamaliza kisha ukarudi kwenye maisha yako ya awali kama yalivyokuwa. Badili kitu kwenye maisha yako, hata kama ni mtazamo wako au jinsi unavyotumia muda wako na kuendesha siku zako.

Kuna mengi ya kufanya pale unapopata maarifa bora na kuyatafakari yanakufaaje kwenye maisha yako.

Soma vitabu kwa tija na viwe na manufaa kwenye maisha yako, chagua vitabu vilivyo bora, pata muda wa kutafakari ulichojifunza na chukua hatua kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi. Ukizingatia hayo matatu, usomaji wa vitabu utayafanya maisha yako kuwa bora zaidi.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri , JIUNGE  NA   DARASA  ONLINE---NA  ENDELEA   KUSOMA  KILA   SIKU  HAPA   "MAISHA  NA   MAFANIKIO   BLOG "  LIFE   AND   YOU  

Tuwasiliane  kwa  + 255 716 924136 /   + 255  755 400128 /  + 255 688 361 539  

Ndimi  KOCHA   MWL    JAPHET   MASATU


Monday, August 17, 2020

NI WAKATI GANI WA KUCHUKUA MKOPO WA BIASHARA ILI UWE NA MANAUFAA ?


WAKATI    SAHIHI  WA  KUCHUKUA   MKOPO    KWA  AJILI  YA    BIASHARA .



Kwenye makala hii nitakwenda kushauri mambo matatu ambayo kila mfanyabiashara anapaswa kuyafanyia kazi ili biashara yake iweze kukua.

JAMBO LA KWANZA; WAKATI SAHIHI WA KUCHUKUA MKOPO.

Usichukue mkopo kwenye biashara kwa sababu umeambiwa unakopesheka,

Usichukue mkopo kwa sababu wewe ni mfanyakazi hivyo unaweza kukopa kwa kutumia mshahara wako.

Na usichukue mkopo kwenye biashara kwa sababu umesikia watu wanasema biashara haiwezi kufanikiwa bila mkopo.

Zote hizo ni sababu mbovu za kuchukua mkopo kwenye biashara, ambazo zimewapoteza wengi.

Kabla hujachukua mkopo kwenye biashara, hakikisha imetimiza vigezo hivi vikubwa vitatu;

Kigezo cha kwanza ni biashara inajiendesha kwa faida, yaani tayari biashara inaingiza faida, hivyo unapochukua mkopo unakwenda kukuza faida hiyo zaidi.

Kigezo cha pili ni biashara ina mfumo mzuri wa uendeshaji ambapo kuna vitengo mbalimbali na kila kitengo kina majukumu yake ya kutekeleza. Hata kama uko mwenyewe kwenye biashara, unapaswa kuwa na vitengo hivyo.

Kigezo cha tatu ni matumizi ya fedha za biashara na matumizi yako binafsi hayaingiliani. Yaani fedha ya biashara inakaa kwenye biashara na huitumii kwa namna yoyote ile, una akaunti ya biashara benki ambapo fedha zinaenda huko. Hata kama huna pesa ya kula, hutoi tu kwenye biashara kiholela.

Kama biashara yako haijafikisha vigezo hivyo vitatu, ukichukua mkopo unaiwahisha kufa.

JAMBO LA PILI; MAMBO YA KUZINGATIA PALE UNAPOCHUKUA MKOPO.

Baada ya kuhakikisha kwamba biashara yako imefikia vigezo vya kuchukua mkopo, kwa maana kwamba inajiendesha kwa faida, ina mfumo mzuri na fedha za biashara haziingiliani na matumizi yako binafsi, basi unaweza kuchukua mkopo.

Lakini pamoja na kukidhi vigezo hivyo, mkopo unaweza kuwa hatari kwa biashara kama hutazingatia mambo muhimu katika kuuchukua na kuutumia. Yafuatayo ni mambo matano muhimu ya kuzingatia pale unapochukua mkopo wa biashara.

Moja ni kupanga matumizi ya mkopo huo kabla hujauchukua. Usichukue mkopo kisha ndiyo upangilie unautumiaje. Badala yake iangalie biashara yako kwanza, angalia ni bidhaa au huduma zipi zinazotoka haraka, zina uhitaji na faida yake ni nzuri, hivyo unapochukua mkopo unaenda kuweka kwenye bidhaa au huduma hiyo. Mfano kwenye hardware kama umegundua cement ndiyo inatoka sana na yenye faida na kwa mtaji wako huwezi kununua kwa wingi, unapochukua mkopo basi unawekeza kwenye eneo hilo.

Mbili ni kutokutumia mkopo wote uliouchukua, tumia robo tatu na robo iache kama akiba. Mipango yako ya mwanzo inaweza kuwa siyo sahihi, sasa kama mkopo wote umeshautumia, utajikuta umekwama. Acha kiasi fulani cha mkopo kama fedha taslimu, ili kama ulivyopanga awali mambo hayajaenda hivyo, unakuwa na kiasi cha kukuwezesha kufanya mpango mwingine wa kuokoa hali unayokuwa umeingia.

Tatu ni usitumie mkopo kufanya mambo yasiyozalisha faida, mfano kufanya marekebisho eneo la biashara, kununua samani na mengineyo. Mkopo unarudi kwa riba, hivyo unapaswa kuzalisha faida ambayo ni kubwa kuliko riba unayolipa. Kama mkopo hauzalishi faida, maana yake riba unayoilipa inatoka kwenye mtaji wako, ndiyo maana utamaliza kulipa mkopo na biashara kufa.

Nne ni kuweka nguvu na kujisukuma zaidi, ulipokuwa huna mkopo, hukuwa na gharama kubwa za kuendesha biashara, ukishachukua mkopo, gharama zimeongezeka. Hivyo pia lazima ujisukume sana, pambana kuongeza wateja na kuwashawishi wateja wako kununua zaidi. Usiendelee kuendesha biashara yako kwa mazoea kama wakati huna mkopo.

Tano ni kufuatilia kwa karibu mwenendo wa biashara na marejesho ya mkopo. Usirejeshe tu bila kuangalia biashara inaendaje, kama unafika wakati unakuta marejesho unayofanya ni makubwa kuliko faida unayoingiza, jua mapema kabisa kwamba unamega mtaji wa biashara. Hivyo anza kuchukua hatua mapema na siyo kusubiri mpaka umemaliza kurejesha mkopo huku biashara imekufa. Ukishagundua marejesho ni makubwa kuliko faida una mengi ya kufanya, kwa upande wako ni kukazana kuongeza mauzo, kwa upande wa mkopo unaweza kwenda kuongea nao wapunguze kiwango cha marejesho unachofanya.

Ukizingatia haya matano pale unapochukua mkopo, utainufaisha biashara yako na kuiwezesha kukua zaidi.

JAMBO LA TATU; UFANYE NINI PALE UNAPOKUWA HUNA VIGEZO VYA KUCHUKUA MKOPO.

Wafanyabiashara wengi wadogo na wa kati wamekaririshwa na kuamini kwamba njia pekee ya kupata mtaji wa kuanza na kukuza biashara ni kuchukua mkopo. Ndiyo maana utasikia kilio cha wengi kwamba hawakopesheki au hawana dhamana ya kupata mkopo.

Usikimbilie kuchukua mkopo kama bado hujakidhi vigezo vya kuchukua mkopo ambavyo tumejadili hapo juu.

Swali ni je ufanyeje ili kukuza biashara yako wakati huwezi kuchukua mkopo? Kuna mengi ya kufanya, hapa kuna matatu ya kuzingatia.

Moja ni kuanza biashara kwa akiba zako wewe mwenyewe. Kwenye njia nyingine ulizonazo za kuingiza kipato, basi weka akiba kwenye kila kipato na akiba hiyo iwekeze kwenye biashara, anza kidogo na endelea kukua. Kila mwezi jiwekee kiango ambacho utawekeza kwenye biashara yako kutoka kwenye njia zako nyingine za kuingiza kipato.

Mbili ni kutokuondoa fedha kwenye biashara kabisa, acha biashara ijiendeshe yenyewe kwa kutokuingilia na kutoa fedha kwa matumizi yako binafsi. Unapaswa kuwa na nidhamu kubwa sana ya kutenganisha matumizi yako binafsi ya fedha na fedha za biashara. Zione fedha za biashara kama za mtu mwingine kabisa na usiwe na mazoea ya kutumia biashara kutatua shida zako.

Tatu ni kuanza na biashara nyingine ili kutengeneza mtaji wa kwenda kuanza biashara ya ndoto yako. Kama biashara unayotaka kuanzisha inahitaji mtaji mkubwa ambao huna, anza na biashara nyingine unayoweza kuanza kwa mtaji kidogo kisha tumia biashara hiyo kutengeneza mtaji wa kuingia kwenye biashara ambayo ndiyo unataka kufanya. Hili ni jibu kwa wale watakaokuwa wamesoma namba moja hapo na kusema sina ajira nitatengenezaje mtaji au kuendesha maisha bila kutegemea biashara. Fanya chochote unachoweza kuhakikisha kwanza unaingiza kipato, omba hata kuwa wakala wa mauzo kwenye biashara za wengine ambapo watakulipa kamisheni, pambana kuuza na tengeneza mtaji wako ili baadaye uwe na biashara yako.

Kuanzisha na kukuza biashara ili ikupe mafanikio kunahitaji kazi, msimamo na uvumilivu. Hakuna njia ya mkato inayoweza kuondoa mahitaji hayo matatu. Wengi wamekuwa wanakimbilia kuchukua mkopo wakifikiri ni njia ya mkato na kinachotokea ni kuua kabisa biashara zao.

Zingatia haya uliyojifunza kwenye ushauri huu, yafanyie kazi na biashara yako itapata manufaa makubwa.

Sunday, August 2, 2020

UFUKARA UNAONDOA FURAHA.

Kwenye moja ya tafiti ambazo Daniel ametumia kwenye kitabu chake, inaonesha kwamba wale ambao wako kwenye umasikini mkubwa, ambao wanaishi chini ya kiwango cha kawaida cha maisha, wanakuwa na wakati mwingi wa kukosa furaha kuliko ambao hawapo kwenye ufukara.
Mfano kitendo tu cha kuumwa na kichwa, kinawapelekea walio kwenye ufukara kupatwa na wasiwasi zaidi kuliko ambao hawapo kwenye ufukara.
Katika changamoto za kawaida za maisha, kama kuumwa, kufukuzwa kazi, biashara kufa, kutengana na mwenza, zinawaumiza zaidi walio kwenye umasikini kuliko wale ambao hawapo kwenye umasikini.
Na kikubwa zaidi ambacho Daniel ametushirikisha kwenye hili ni kwamba kwa walio masikini, maamuzi yoyote anayofanya ni ya kupoteza.
Iko hivi, sisi binadamu huwa tunaepuka hali ya kupoteza na kupenda hali ya kupata. Hivyo hatua yoyote ya kupoteza tunayochukua, huwa tunajisikia vibaya na hilo linachangia kukosa furaha.
Kwa kuwa masikini ana uhaba wa fedha, kila fedha aliyonayo haimtoshi, hivyo akitumia fedha hiyo kupata kitu fulani, anakuwa amechagua kukosa kitu kingine. Una elfu 5 mfukoni, unataka kwenda kujiburudisha mahali, ungependa kununua chakula na kinywaji, lakini fedha hiyo haitoshi, hivyo utaishia kupata chakula tu, au kinywaji tu.
Haijalishi chakula utakachopata au kinywaji utakachokunywa kitakuwa kizuri kiasi gani, akili yako haitaangalia kile ulichopata, bali itafikiria kile ulichokosa. Hilo ndiyo linachangia hali ya kukosa furaha kwa walio masikini.
Maumivu ya kukosa ni makubwa kuliko raha ya kupata. Ukipoteza elfu 10, utaumia kuliko raha utakayoipata kwa kuokota kiasi hicho hicho cha fedha.