Sunday, August 18, 2019

HAKUNA ANAYEKOSEA KWA MAKUSUDI.

Upo msingi wa ustoa ambao utakuwezesha kuishi maisha yako kwa utulivu bila ya kujali wengine wanasema au kufanya nini. Moja ya vitu ambavyo vinatusumbua sana zama hizi ni mambo ambayo wengine wanasema au wanafanya. Huwa tunayaruhusu yatuumize, tukiamini kwamba watu hao wanafanya mambo hayo kwa makusudi ili kutuumiza.
Lakini wastoa wanatuambia kwamba, watu wanaofanya mambo ambayo yanatuumiza, hawafanyi hivyo kwa makusudi, bali wanafanya hivyo kwa sababu hawajui kulicho sahihi kufanya. Hivyo hupaswi kuumia kwa sababu yao, badala yake unapaswa kuwaonea huruma na kuona kama kuna namna unaweza kumsaidia ili asiendelee kukosea.
Mfano mzuri ni pale mtoto mdogo anapokupiga kofi, je utarejesha kwa kumpiga kofi pia? Je utakasirika? Je utamnunia? Je utasema amekudharau? Majibu hapo ni hapana. Lakini vipi mtu mzima mwenzako akikupiga kofi? Hapo mambo yanabadilika, unaona amekudharau, utataka kulipiza, utakasirika na hata kumnunia. Lakini kama utachukulia mtu huyo amekupiga kofi kwa kutokujua au kwa bahati mbaya, hutapata hisia hizo.
Hivyo cha kujifunza hapa, tusikimbilie kuhukumu pale watu wanapofanya vitu kwamba ni vibaya au wamedhamiria kutuumiza. Badala yake tuchukulie kwamba watu hao hawajui wanachofanya au wamefanya kwa bahati mbaya, na hilo litatuzuia sisi kuumia.
Mfano mzuri ni kwenye wizi au utapeli, mtu akikuibia, badala ya kuumia, unapaswa kumwonea huruma, kwa sababu kwanza hajui njia sahihi ya kutengeneza kipato ambayo itampa maisha ya utulivu na pili, kwa tabia yake hiyo, ataishia jela au kaburini, maana ataiba akamatwe na wananchi wenye hasira kali hadi kufa, au apelekwe polisi na baadaye kufungwa. Unaona jinsi ambavyo unaondoka kwenye upande wa lawama na kuwa upande wa utulivu!

CHAGUA SHUJAA WA MAISHA YAKO.

Wastoa wamekuwa wanaelewa umuhimu wa kuwa na mashujaa, watu ambao tunayapima maisha yetu kupitia wao. Lakini hili ni eneo ambalo limekuwa na changamoto kubwa sana zama hizi, kwa sababu kumekuwa na mashujaa wengi feki. Siku hizi watu wanaoweza kutengeneza umaarufu rahisi kupitia mitandao ya kijamii, sanaa, michezo au siasa ndiyo wanaonekana mashujaa kwa wengi. Na wengi wanawafuata watu hao, lakini hakuna wanachojifunza kwa sababu mwisho wa siku umaarufu wa watu hao huanguka, kwa sababu haujajengwa kwenye misingi sahihi.
Ni muhimu uchague mashujaa sahihi wa maisha yako, kutokana na misingi wanayoiishi au waliyoiishi ambayo unaweza kujijengea kwenye maisha yako na ukaweza kupiga hatua pia. Kadiri unavyojifunza falsafa hii na kujifunza wengine walioiishi falsafa hii, utavutiwa na maisha ya baadhi ya wanafalsafa na kuwachagua kuwa mashujaa wako.

JINSI YA KUKABILIANA NA MABADILIKO MAKUBWA YA MAISHA KIAFYA.

Kuna wakati tunakutana na mabadiliko makubwa kimaisha kwenye afya zetu. mabadiliko haya yanaweza kutuyumbisha sana kama hatuna msingi sahihi tunaouishi. Mfano ni pale mtu anapopata ulemavu wa mwili ambao unaathiri maisha na hata kazi za mtu. Wengi huvurugwa sana na mabadiliko ya aina hii, kitu ambacho hupelekea maisha yao kudorora na hata kufa mapema.
Wastoa wanatupa njia sahihi ya kukabiliana na mabadiliko ya aina hii, kwa kutuambia tunapaswa kufikiria na kutumia kile tulichonacho na siyo kuangalia tumekosa nini. Kama umepata ulemavu wa miguu, kumbuka bado una mikono, macho, masikio, na viungo vingine, ambavyo kama utaweza kuvitumia vizuri maisha yako yatakuwa bora.
Mmoja wa wanafalsafa wa Ustoa, Epictetus, ambaye alikuwa mwalimu bora sana wa falsafa hii, alikuwa mtumwa. Katika maisha yake ya utumwa, aliumizwa na kupata ulemavu wa miguu. Hili lilimpa ulemavu wa maisha, lakini hakuruhusu ulemavu huo uathiri maisha yake, aliangalia mambo gani mengine anayoweza kufanya, kama kujifunza na kufundisha falsafa na siyo kuangalia alichokosa.
Somo muhimu la kuondoka nalo hapa ni usiweke nguvu zako kwenye yale uliyokosa au kupoteza, badala yake weka nguvu zako kwenye yale uliyonayo na jinsi unavyoweza kuyatumia kwa ubora zaidi.

FALSAFA YA USTOA NA UTAJIRI.

Kwenye Falsafa ya Ustoa, vitu vimegawanyika katika makundi matatu;
Kundi la kwanza ni vitu vizuri kufanya au kuwa navyo (virtues), ambavyo ni vinne; hekima, ujasiri, haki na kiasi.
Kundi la pili ni vitu vibaya kufanya au kuwa navyo (vices), ambavyo ni kinyume na hivyo vizuri, yaani, upumbavu, woga, udhalimu na tamaa.
Kundi la tatu ni vitu ambavyo siyo vizuri na wala siyo vibaya (indifferent), ambavyo hakuna ubaya kuwa navyo, lakini pia hupaswi kujitesa ili kuwa navyo. Hapa vitu vingine vyote kwenye maisha vinaingia hapo, kuanzia afya, kazi, biashara, fedha na kadhalika.
Sasa kwa misingi ya ustoa, wengi hufikiri inawataka wawe masikini, watu wasiojali fedha wala utajiri. Lakini katika historia, moja ya wanafalsafa waliokuwa na maisha mazuri basi ni wastoa. Seneca alikuwa tajiri mkubwa enzi zake na mwanasiasa, Marcus Aurelius alikuwa mtawala wa Roma. Kwa kifupi wastoa walijihusisha na maisha ya kila siku na ya kawaida, wakifanya yale ambayo kila mtu anafanya.
Na hii ni sababu nyingine nzuri kwa nini tunapaswa kuwa wastoa, kwa sababu ni falsafa ambayo haipingi mtu kuwa na fedha, au kujihusisha na mambo mengine, kama tu hayavunji msingi wa wema.
Zipo baadhi ya dini na falsafa ambazo zinawafundisha wafuasi wake kuachana kabisa na mambo ya dunia, kutoa maisha yao kwa ajili ya falsafa au Mungu pekee. Lakini wote tunajua maisha yana mahitaji yake, hutaenda kulipa ada za watoto kwa falsafa, na wala hutaenda dukani kupata chakula kwa kusema wewe ni mwanafalsafa.
Hivyo kwa kuishi kwa falsafa ya ustoa, unakuwa huru kufanya upendacho, ila tu kiwe sahihi kwako na kwa wengine, na pia unakuwa huru kujikusanyia fedha utakavyo, ila tu ufanye hivyo kwa usahihi na kwa manufaa ya wengine pia.
Na kikubwa nilichojifunza ni kwamba ukiishi misingi ya falsafa ya ustoa, una nafasi kubwa ya kuwa tajiri, lakini pia utakuwa huru na utajiri huo. Kwa sababu kwanza utakuwa unafanya kilicho sahihi na kuachana na yasiyo sahihi, pia utaepuka kufanya mambo ambayo yatakupotezea fedha, kwa kudhibiti vizuri hisia zako. Lakini kilicho muhimu zaidi ni kwamba hutafungwa na utajiri wako, hata kama utapoteza kila kitu, bado utabaki imara na maisha yako yataendelea.
Naweza kuhitimisha kwa kusema, Ustoa ni falsafa ya watu wakuu na matajiri, najua unapenda kuwa mkuu, unapenda kuwa tajiri na kuwa huru na maisha yako, hivyo basi, ijue na kuiishi misingi ya ustoa.

KUHUSU KIFO NA KUJIUA.

Moja ya vitu ambavyo vimekuwa vinawasumbua watu wengi n kifo. Wote tunajua kuna siku tutakufa, lakini hatutaki kufikiria wala kupata picha ya kifo chetu. Kadhalika tunajua wale watu wa karibu kwetu, ambao tunawapenda sana kuna siku watakufa. Lakini huwa hatufikirii wala kupata picha ya vifo vyao. Kinachotokea ni tunakutana na vifo ghafla na vinatuumiza sana.
Wastoa wana maeneo matatu ya kuzingatia kuhusu kifo.
Kwanza ni kifo chako mwenyewe, ambapo wastoa wanasema hakuna sababu ya kukiogopa kifo, kwa sababu ni sehemu ya maisha yako na kinaweza kutokea muda wowote. Hivyo wakati wowote unapaswa kuwa tayari kukikabili kifo. Inapofanya jambo lolote, lifanye kama ndiyo mara ya mwisho kwako kulifanya, kama vile kifo kinakusubiri. Kwa njia hii hutaahirisha jambo lolote muhimu na utafanya mambo kwa usahihi. Wastoa wanasema kama unaogopa kifo, maana yake bado hujaanza kuishi. Lakini kama utachagua kuishi maisha yako, kifo hakitakusumbua, kwa sababu wakati wowote utakuwa tayari.
Mbili ni vifo vya watu wa karibu kwetu. Wazazi wetu, watoto wengu, wenzi wetu na ndugu wengine ni watu tunaowapenda na kuwajali sana. Inapotokea wamefariki dunia, huwa tunaumia, tunalia na kuhuzunika sana. Kwa wengine vifo vya watu wao wa karibu huwa vinawavuruga sana, vinaishia kuwapa magonjwa ya akili. Wastoa wanatuambia vifo vya watu wa karibu kwetu vinatuumiza kwa sababu vinatukuta hatujajiandaa. Wanatuambia kila unapoongea au kukutana na mtu wako wa karibu, jiambie kimoyomoyo kwamba hiyo ni mara ya mwisho kukutana naye. Epictetus anatuambia kila unapombusu mtoto wako, jiambie unambusu mtu ambaye anaweza kufa muda wowote. Kwa kuchukulia hivi, utajali sana, kwa sababu unajua mtu anaweza kupotea muda wowote, na hilo linapotokea utaumia, lakini halitakuvuruga, kwa sababu ni kitu ambacho ulijua kitatokea, a pia ulishatumia fursa ulizokuwa nazo kabla mtu huyo hajafariki.
Tatu ni kujiua. Wastoa wa zamani, wengi waliishia kujiua wenyewe au kupewa adhabu ya kifo. Hii ilitokana na tawala za kidhalimu zilizokuwepo enzi hizo na wastoa hawakuogopa kuzisema na kuzipinga. Hilo liliwafanya wawekwe vizuizini, kufukuzwa au kuhukumiwa kufa. Wastoa walikuwa wakipokea adhabu hizo bila ya kuruhusu ziharibu utulivu wao wa ndani. Mfano mstoa alipohukumiwa kifo, alikipokea kama sehemu ya maisha na kusimamia misingi yake. Lakini pia wapo wastoa ambao walipofika mwisho wa maisha yao, yaani uzee na kuona wameshakamilisha jukumu lao la maisha, basi walijiua. Hii ni dhana ambayo ilikuja kupotea, lakini zama hizi imeanza kurudi. Wapo watu ambao wanachagua kuyakatisha maisha yao kwa sababu mbalimbali. Hapa hatuzungumzii wale wanaojiua kukimbia majukumu au matatizo waliyosababisha, bali wale ambao wanaona imetosha sasa na wanataka kupumzika. Hilo pia ni zoezi la kistoa.

MATAWI MATATU YA FALSAFA YA USTOA.

Falsafa ya ustoa inafananishwa na mti ambao una vitu vitatu ili uweze kuwa mti. Mti una mizizi ambayo inaupa uimara na virutubisho, shina ambalo linahifadhi chakula na kutoa umbo na matawi ambayo yanatengeneza chakula na kuvuta hewa.
Falsafa ya ustoa ina matawi matatu;
Moja ni fizikia (physics), hili ni tawi linalojihusisha na sayansi ya asili, jinsi dunia ilivyo na inavyojiendesha. Hii ndiyo mizizi ya falsafa hii.
Mbili ni maadili (ethics), hili ni tawi ambalo linaipa falsafa hii msimamo, jinsi ya kuishi na kujihusisha na wengine. Hili ndiyo shina la falsafa hii.
Tatu ni mantiki (logic), hili ni tawi ambalo linahusika na kufikiri pamoja na kufanya maamuzi sahihi. Haya ndiyo matawi ya falsafa hii.
Ili maisha yetu yakamilike, lazima tuwe vizuri kwenye maeneo hayo matatu, kuijua dunia na hapa tunapaswa kuwa na ujasiri na kiasi, kuwa na maadili tunayoyaishi ambapo tunapaswa kuwa watu wa haki na mwisho kutumia akili zetu kufikiri, ambapo tutaweza kuwa na hekima.
Ukiona hapo, matawi matatu ya ustoa ambayo ni FIZIKIA, MAADILI NA MANTIKI, ndiyo yanazalisha misingi mikuu minne ya ustoa ambayo ni HEKIMA, UJASIRI, HAKI NA KIASI. Kwa kifupi, falsafa nzima ya Ustoa imejumuishwa kwenye sentensi hiyo.