Sunday, August 18, 2019

FALSAFA YA USTOA NA UTAJIRI.

Kwenye Falsafa ya Ustoa, vitu vimegawanyika katika makundi matatu;
Kundi la kwanza ni vitu vizuri kufanya au kuwa navyo (virtues), ambavyo ni vinne; hekima, ujasiri, haki na kiasi.
Kundi la pili ni vitu vibaya kufanya au kuwa navyo (vices), ambavyo ni kinyume na hivyo vizuri, yaani, upumbavu, woga, udhalimu na tamaa.
Kundi la tatu ni vitu ambavyo siyo vizuri na wala siyo vibaya (indifferent), ambavyo hakuna ubaya kuwa navyo, lakini pia hupaswi kujitesa ili kuwa navyo. Hapa vitu vingine vyote kwenye maisha vinaingia hapo, kuanzia afya, kazi, biashara, fedha na kadhalika.
Sasa kwa misingi ya ustoa, wengi hufikiri inawataka wawe masikini, watu wasiojali fedha wala utajiri. Lakini katika historia, moja ya wanafalsafa waliokuwa na maisha mazuri basi ni wastoa. Seneca alikuwa tajiri mkubwa enzi zake na mwanasiasa, Marcus Aurelius alikuwa mtawala wa Roma. Kwa kifupi wastoa walijihusisha na maisha ya kila siku na ya kawaida, wakifanya yale ambayo kila mtu anafanya.
Na hii ni sababu nyingine nzuri kwa nini tunapaswa kuwa wastoa, kwa sababu ni falsafa ambayo haipingi mtu kuwa na fedha, au kujihusisha na mambo mengine, kama tu hayavunji msingi wa wema.
Zipo baadhi ya dini na falsafa ambazo zinawafundisha wafuasi wake kuachana kabisa na mambo ya dunia, kutoa maisha yao kwa ajili ya falsafa au Mungu pekee. Lakini wote tunajua maisha yana mahitaji yake, hutaenda kulipa ada za watoto kwa falsafa, na wala hutaenda dukani kupata chakula kwa kusema wewe ni mwanafalsafa.
Hivyo kwa kuishi kwa falsafa ya ustoa, unakuwa huru kufanya upendacho, ila tu kiwe sahihi kwako na kwa wengine, na pia unakuwa huru kujikusanyia fedha utakavyo, ila tu ufanye hivyo kwa usahihi na kwa manufaa ya wengine pia.
Na kikubwa nilichojifunza ni kwamba ukiishi misingi ya falsafa ya ustoa, una nafasi kubwa ya kuwa tajiri, lakini pia utakuwa huru na utajiri huo. Kwa sababu kwanza utakuwa unafanya kilicho sahihi na kuachana na yasiyo sahihi, pia utaepuka kufanya mambo ambayo yatakupotezea fedha, kwa kudhibiti vizuri hisia zako. Lakini kilicho muhimu zaidi ni kwamba hutafungwa na utajiri wako, hata kama utapoteza kila kitu, bado utabaki imara na maisha yako yataendelea.
Naweza kuhitimisha kwa kusema, Ustoa ni falsafa ya watu wakuu na matajiri, najua unapenda kuwa mkuu, unapenda kuwa tajiri na kuwa huru na maisha yako, hivyo basi, ijue na kuiishi misingi ya ustoa.

KUHUSU KIFO NA KUJIUA.

Moja ya vitu ambavyo vimekuwa vinawasumbua watu wengi n kifo. Wote tunajua kuna siku tutakufa, lakini hatutaki kufikiria wala kupata picha ya kifo chetu. Kadhalika tunajua wale watu wa karibu kwetu, ambao tunawapenda sana kuna siku watakufa. Lakini huwa hatufikirii wala kupata picha ya vifo vyao. Kinachotokea ni tunakutana na vifo ghafla na vinatuumiza sana.
Wastoa wana maeneo matatu ya kuzingatia kuhusu kifo.
Kwanza ni kifo chako mwenyewe, ambapo wastoa wanasema hakuna sababu ya kukiogopa kifo, kwa sababu ni sehemu ya maisha yako na kinaweza kutokea muda wowote. Hivyo wakati wowote unapaswa kuwa tayari kukikabili kifo. Inapofanya jambo lolote, lifanye kama ndiyo mara ya mwisho kwako kulifanya, kama vile kifo kinakusubiri. Kwa njia hii hutaahirisha jambo lolote muhimu na utafanya mambo kwa usahihi. Wastoa wanasema kama unaogopa kifo, maana yake bado hujaanza kuishi. Lakini kama utachagua kuishi maisha yako, kifo hakitakusumbua, kwa sababu wakati wowote utakuwa tayari.
Mbili ni vifo vya watu wa karibu kwetu. Wazazi wetu, watoto wengu, wenzi wetu na ndugu wengine ni watu tunaowapenda na kuwajali sana. Inapotokea wamefariki dunia, huwa tunaumia, tunalia na kuhuzunika sana. Kwa wengine vifo vya watu wao wa karibu huwa vinawavuruga sana, vinaishia kuwapa magonjwa ya akili. Wastoa wanatuambia vifo vya watu wa karibu kwetu vinatuumiza kwa sababu vinatukuta hatujajiandaa. Wanatuambia kila unapoongea au kukutana na mtu wako wa karibu, jiambie kimoyomoyo kwamba hiyo ni mara ya mwisho kukutana naye. Epictetus anatuambia kila unapombusu mtoto wako, jiambie unambusu mtu ambaye anaweza kufa muda wowote. Kwa kuchukulia hivi, utajali sana, kwa sababu unajua mtu anaweza kupotea muda wowote, na hilo linapotokea utaumia, lakini halitakuvuruga, kwa sababu ni kitu ambacho ulijua kitatokea, a pia ulishatumia fursa ulizokuwa nazo kabla mtu huyo hajafariki.
Tatu ni kujiua. Wastoa wa zamani, wengi waliishia kujiua wenyewe au kupewa adhabu ya kifo. Hii ilitokana na tawala za kidhalimu zilizokuwepo enzi hizo na wastoa hawakuogopa kuzisema na kuzipinga. Hilo liliwafanya wawekwe vizuizini, kufukuzwa au kuhukumiwa kufa. Wastoa walikuwa wakipokea adhabu hizo bila ya kuruhusu ziharibu utulivu wao wa ndani. Mfano mstoa alipohukumiwa kifo, alikipokea kama sehemu ya maisha na kusimamia misingi yake. Lakini pia wapo wastoa ambao walipofika mwisho wa maisha yao, yaani uzee na kuona wameshakamilisha jukumu lao la maisha, basi walijiua. Hii ni dhana ambayo ilikuja kupotea, lakini zama hizi imeanza kurudi. Wapo watu ambao wanachagua kuyakatisha maisha yao kwa sababu mbalimbali. Hapa hatuzungumzii wale wanaojiua kukimbia majukumu au matatizo waliyosababisha, bali wale ambao wanaona imetosha sasa na wanataka kupumzika. Hilo pia ni zoezi la kistoa.

MATAWI MATATU YA FALSAFA YA USTOA.

Falsafa ya ustoa inafananishwa na mti ambao una vitu vitatu ili uweze kuwa mti. Mti una mizizi ambayo inaupa uimara na virutubisho, shina ambalo linahifadhi chakula na kutoa umbo na matawi ambayo yanatengeneza chakula na kuvuta hewa.
Falsafa ya ustoa ina matawi matatu;
Moja ni fizikia (physics), hili ni tawi linalojihusisha na sayansi ya asili, jinsi dunia ilivyo na inavyojiendesha. Hii ndiyo mizizi ya falsafa hii.
Mbili ni maadili (ethics), hili ni tawi ambalo linaipa falsafa hii msimamo, jinsi ya kuishi na kujihusisha na wengine. Hili ndiyo shina la falsafa hii.
Tatu ni mantiki (logic), hili ni tawi ambalo linahusika na kufikiri pamoja na kufanya maamuzi sahihi. Haya ndiyo matawi ya falsafa hii.
Ili maisha yetu yakamilike, lazima tuwe vizuri kwenye maeneo hayo matatu, kuijua dunia na hapa tunapaswa kuwa na ujasiri na kiasi, kuwa na maadili tunayoyaishi ambapo tunapaswa kuwa watu wa haki na mwisho kutumia akili zetu kufikiri, ambapo tutaweza kuwa na hekima.
Ukiona hapo, matawi matatu ya ustoa ambayo ni FIZIKIA, MAADILI NA MANTIKI, ndiyo yanazalisha misingi mikuu minne ya ustoa ambayo ni HEKIMA, UJASIRI, HAKI NA KIASI. Kwa kifupi, falsafa nzima ya Ustoa imejumuishwa kwenye sentensi hiyo.

FALSAFA YA USTOA

Falsafa ya Ustoa ilianza miaka 300 kabla ya Kristo ambapo Zeno, mwanzilishi wa falsafa ambaye kwa wakati huo alikuwa mfanya biashara alikuwa safarini na chombo chake kikaharibika akiwa Athens Ugiriki. Akiwa hapo Athens, alitembelea maktaba na kuperuzi maandiko yaliyokuwepo, alikutana na mafunzo ya Socrates na yakamvutia sana. Akamuuliza mhusika wa maktaba ile, ni wapi anaweza kuwapata watu ambapo atajifunza zaidi kuhusu falsafa, na hapo akaoneshwa mwanafalsafa Crates na akamfuata, hapo ndipo safari yake ya kujifunza na kuwa mwanafalsafa ilipoanzia.
Zeno alijifunza kupitia Crates ambaye alikuwa kwenye shule ya falsafa inayoitwa Cynics, ambao ni watu ambao hawakujali kuhusu chochote, waliishi maisha kwa wakati waliokuwa nao na walihoji na kutilia mashaka kila kitu.
Baada ya kujifunza kwenye falsafa hii kwa muda, Zeno aliona falsafa ya Cynics ilikuwa na mapungufu, kwa sababu huwezi kupuuza kila kitu kuhusu maisha na ukawa na maisha bora. Hivyo alianzisha shule yake ya falsafa, ambapo alikuwa akifundisha chini ya mti ulioitwa stoa. Na hapo ndipo jina la Ustoa (Stoicism) lilipoanzia.
Tangu kipindi cha Zeno, pamekuwepo wanafalsafa ambao wameiendeleza na kuikuza zaidi falsafa hii ya zeno. Wanafalsafa kama Cato, Musonius Rufus, Seneca, Epictetus na Marcus Aurelius kwa nyakati tofauti waliishi na kufundisha falsafa hii.

UNAHITAJI FALSAFA YA MAISHA.

Zamani za kale, wakati binadamu wanajifunza kuwa na makazi ya kudumu, watu walijenga nyumba zao bila ya misingi. Lakini walijifunza somo moja kubwa sana, kwamba kipindi cha dhoruba mbalimbali kama mvua, kimbunga na tetemeko, nyumba hizo zilibomoka haraka sana. Hivyo wakajifunza kwamba ili nyumba iwe imara na idumu, basi inapaswa kuanza kujengwa kwa msingi imara. Na mpaka sasa wahandisi wote wanajua kwamba nyumba imara inaanza na msingi imara. Na kadiri nyumba inavyopaswa kuwa kubwa, ndivyo msingi unavyopaswa kuwa imara zaidi. Mfano, msingi wa nyumba ya kawaida hauwezi kufanana na msingi wa nyumba ya ghorofa.
Hivi pia ndivyo ilivyo kwenye maisha yetu. Kwenye maisha tunakutana na dhoruba mbalimbali. Kuna kuugua, kuvunjika kwa mahusiano, kufukuzwa kazi, kufilisika kibiashara, kufa kwa watu wetu wa karibu na hata sisi wenyewe kufa. Dhoruba hizi huwa zina madhara tofauti kwa watu tofauti. Kuna watu wanapokutana na dhoruba za maisha zinawayumbisha sana na kuvuruga kabisa maisha yao. Lakini wapo wengine ambao wanakutana na dhoruba kali za maisha lakini maisha yao hayayumbi.
Kinachowatofautisha watu hao wa aina mbili ni msingi ambao wamejijengea. Kwenye nyumba tumeona msingi wa kuanza, kwenye maisha yetu, msingi muhimu sana ni falsafa ambayo mtu anakuwa nayo juu ya maisha. Falsafa unayokuwa nayo, ndiyo inapima kiasi gani dhoruba unazokutana nazo kwenye maisha. Kama huna falsafa unayoiishi na kuisimamia, dhoruba ndogo kama biashara kufilisika inatosha kukuvuruga kabisa. Lakini kama una falsafa unayoiishi, dhoruba kubwa kama kuhukumiwa kifo, inakufanya uwe imara na kuyafurahia maisha yako mpaka dakika ya mwisho.
Hii ni kukuambia wewe rafiki yangu kwamba unapaswa kuwa na falsafa ya maisha yako, falsafa ambayo unaitumia kama msingi wako wa kufanya maamuzi na kuendesha maisha yako. Falsafa ambayo itakuwezesha kukabiliana na dhoruba za maisha, ambazo kadiri siku zinavyokwenda zinazidi kuwa kali zaidi.
Dini zilipaswa kuwa msingi wetu kwenye changamoto hizi za maisha, lakini dini nyingi zimesahau jukumu hilo, na badala yake zimekuwa sehemu ya kuwapa watu hofu zaidi ya maisha kuliko matumaini. Dini zimekuwa zinaweka nguvu kubwa kwenye kuwaandaa watu kwa maisha yajayo (baada ya kifo) kuliko maisha waliyonayo sasa. Japokuwa unahitaji maandalizi ya maisha yajayo (kulingana na imani yako), lakini kitu muhimu sana unachohitaji ni maandalizi ya maisha unayoishi sasa, maana hayo ndiyo yanayokujenga au kukubomoa.
Kwa kuwa dini zimeshindwa kufanya kazi ambayo tulitegemea zifanye, kutujenga na kutuandaa kwa maisha ya sasa na kuweza kukabiliana na dhoruba tunazokutana nazo kwenye maisha yetu ya kila siku, basi linabaki kuwa jukumu la kila mmoja wetu kuwa na falsafa ya maisha, ambayo ataitumia kuendesha maisha yake.
Kukaa chini na kutengeneza falsafa yako mwenyewe ni kazi kubwa, inakuhitaji ujaribu na kukosea vitu vingi, kitu ambacho huna muda wala nguvu za kufanya, maana changamoto zinazokukabili ni nyingi.
Hivyo suluhisho ni wewe kujifunza falsafa zilizopo, na kisha kuchagua ile ambayo itakufaa wewe katika kuendesha maisha yako.
Zipo falsafa nyingi ambazo zinatokana na wanafalsafa mbalimbali kama Socrates, Plato, Aristotle, Epicurus, Zeno na wengineo.