Monday, May 27, 2019

UONGO TUNAOJIAMBIA KUHUSU MAFANIKIO NA KWA NINI HATUPENDI KUBADILIKA.

 Mwandishi anasema yapo mambo ambayo tumekuwa tunajidanganya sana kwenye mafanikio, na haya ndiyo yamekuwa yanachochea matatizo mengi tunayokutana nayo kwenye maisha. Baadhi ya mambo tunayojidanganya kwenye mafanikio ni haya; Tunajikadiria zaidi kwenye mchango wetu kwa mafanikio ya kile tunachofanya. Tunafikiri bila sisi mafanikio yasingepatikana, huku ni kujidanganya. Tunachukua sifa ambazo hatustahili kuchukua, kazi wamefanya wengine lakini wewe kama kiongozi ndiye unayetaka upewe sifa. Huwa tunajiona tuna ujuzi wa juu kuliko wale wanaotuzunguka. Huwa tunapuuza muda na gharama ambazo tumeshapoteza kwenye miradi ambayo haizalishi. Kukuza matarajio ya mafanikio ya mradi, kuwa na mategemeo makubwa kuliko uhalisia. Uongo huu ambao tumekuwa tunajiambia, hasa tunapokuwa viongozi kwenye kazi au biashara, unaathiri mahusiano yetu na wale walio chini yetu. Uongo huu unakuwa umetokana na mafanikio ambayo tunakuwa tumeyapata huko nyuma. Tunapopata mafanikio kidogo, huwa tunajiamini zaidi ya uhalisia. Kujiamini huku kulikopitiliza ndiyo kunawaingiza wengi kwenye matatizo na kuwazuia kufanikiwa zaidi.

Friday, May 24, 2019

FURSA 10 ZA KUTENGENEZA PESA FACEBOOK ------ " Fursa Afrika Mashariki Blog "

SHAUKU NI NGUVU ITAKAYOKUWEZESHA KUPATA CHOCHOTE KATIKA MAISHA YAKO.


Shauku ndiyo nguvu ya kwanza ya kukuwezesha kupata kile ambacho unataka kwenye maisha yako. Shauku ni ule msukumo wa ndani wa kukutaka upate kile unachotaka. Msukumo ambao hauondoki wala kupungua. Shauku ina nguvu kubwa ya kukusukuma kufanya mambo ambayo wengine wanaogopa, lakini kwako yanaonekana kawaida.

Watu wengi wamekuwa wanategemea hamasa iwafikishe kwenye mafanikio makubwa, lakini tatizo la hamasa ni huwa haidumu, mara kwa mara inabidi uchochee upya hamasa yako. Lakini shauku huwa haipungui wala kuhitaji kuchochewa, shauku unakuwa nayo muda wote na hii ndiyo inakusukuma wewe kupiga hatua zaidi.
 
Shauku inatokana na ile sababu kubwa inayokusukuma kupata unachotaka, ile KWA NINI inayokufanya wewe upambane kupata unachotaka. Kwa nini zinatofautiana kwa watu, wapo ambao wanafanya kwa sababu wamejitoa kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi, wapo ambao wanafanya ili kuwaonesha wengine wanaweza na kadhalika.
 
Hakikisha una msukumo mkubwa ndani yako wa kukupeleka kwenye kile unachotaka, kwa sababu bila ya msukumo huu, hakuna nguvu nyingine itakayoweza kukusaidia kupata unachotaka.

UNAHITAJI KUWA NA KOCHA , MENTA AU MSHAURI ILI UWEZE KUPATA CHOCHOTE UNACHOHITAJI KATIKA MAISHA YAKO

Ili kupata unachotaka, unahitaji kupata mwongozo kutoka kwa mtu mwingine. Mtu huyo anaweza kuwa kocha, menta au mshauri ambaye anakusimamia ufike kule unakotaka kufika.
 
Iko hivi rafiki, sisi binadamu ni wavivu na hatupendi kujitesa. Tunaweza kuweka mipango mikubwa na mizuri sana, lakini tunapokutana na ugumu ni rahisi kuacha na kujiambia haiwezekani au hatuwezi.
 
Lakini unapokuwa na mtu wa pembeni ambaye anakuangalia na kukusimamia, kwanza hutataka kumwangusha, hivyo utajisukuma zaidi na pili yeye mwenyewe hatakubaliana na wewe kirahisi, hivyo itakubidi ujaribu tena na tena na tena kabla hujasema haiwezekani.
 
Watu wengi wamekuwa wanajiwekea malengo peke yao, na asilimia 99 wamekuwa hawayafikii. Ila wale wanaoweka malengo na kuwa na mtu wa kuwasimamia kwenye malengo yao, zaidi ya asilimia 90 wanayafikia.
 
Hii ndiyo nguvu kubwa iliyopo kwa kuwa na mwongozo. Kwa sababu pia mtu anayekuongoza anaweza kukushauri vizuri pale ambapo unakuwa umekwama. Ni rahisi kuona makosa ya mchezaji aliyepo uwanjani ukiwa nje ya uwanja, lakini yule aliyepo uwanjani anaweza asione kwa urahisi. Kuna makosa unaweza kuwa unafanya kwenye maisha yako lakini huyaoni, ila unapokuwa na mtu anayekusimamia, atakuonesha makosa hayo kwa urahisi na utaweza kupiga hatua sana.
 
Unahitaji kuwa na mtu wa kukusimamia kwenye malengo na mipango uliyonayo ambaye atakusukuma kuyafikia.

WATU WANAOKUZUNGUKA WANA MCHANGO MKUBWA SANA KATIKA KUPATA CHOCHOTE UNACHOTAKA


Watu wanaokuzunguka wana nguvu kubwa sana kwako, hata kama hujui. Watu hao, hasa wale wa karibu, wana ushawishi mkubwa kwako. Kama wanaokuzunguka wana mtazamo hasi wa kuona mambo hayawezekani, na wewe pia utajikuta umebeba mtazamo huo, hata kama utakuwa unapingana nao kiasi gani.
 
Na kama watu wanaokuzunguka wana mtazamo chanya wa inawezekana, na wewe pia utabeba mtazamo huo. Nguvu hii ya wanaokuzunguka ni nguvu kubwa sana unayopaswa kuwa nayo makini. Wengi wamekuwa wanapuuza nguvu hii, wakiamini wanaweza kuzungukwa na watu wa aina yoyote lakini wakafanikiwa. Hicho kitu hakipo kabisa, kama haujazungukwa na watu sahihi, huwezi kufanikiwa. Ni asili ya binadamu, hatuwezi kwenda juu zaidi ya wale ambao wanatuzunguka.
 
Hivyo ili kupata kile unachotaka kwenye maisha, tafuta watu wanapiga hatua kwenye maisha yao na uwe nao karibu. Watu ambao wanaamini kwenye ndoto kubwa na wasiokata tamaa. Watu hawa watakupa nguvu ya kuendelea hata pale unapokutana na magumu na changamoto.

UNAPOSHIKWA NA HASIRA , JIPE MUDA WA KUTAFAKARI.

 Ukishagundua kwamba upo kwenye hasira, basi kaa kimya, jipe muda wakutafakari na kutulia na utajiepusha na makosa makubwa unayoweza kufanya ukiwa na hasira.
 
Hasira ni moja ya hisia zenye nguvu sana, na hisia zinapokuwa juu uwezo wetu wa kufikiri unakuwa chini. Hivyo unapokuwa na hasira, unakuwa umetawaliwa na hisia na siyo fikra. Na ni wakati mbaya sana wa kufanya chochote, kwa sababu unaposukumwa na hisia, hujui kipi sahihi kufanya, kwa kuwa hufikiri sawasawa.
 
Hivyo rafiki, unapogundua kwamba una hasira, usifanye chochote.
 
Kama kuna mtu amekukosea na umepatwa na hasira usimjibu wakati una hasira hizo.
 
Kama kuna mtoto wake amekosea usimwadhibu ukiwa na hasira.
 
Ukiwa na hasira usifanye chochote, jipe muda wa kukaa mbali na kile kinachokupa hasira na akili zako zitarudi.