Njia ya kuondokana na msongo na kuwa na utulivu kwenye maisha yako ni kubadili mpangilio wa vipaumbele vyako kulingana na mazingira unayojikuta upo. Kila mmoja wetu ana mpangilio wake wa vipaumbele, na tunapenda mpangilio huo uende hivyo bila ya kubadilika. Inapotokea hali inayobadili mpangilio huo tunapatwa msongo na kuona hatuna udhibiti wa maisha yetu.
Hatua bora za kuchukua hapa ni kubadili mpangilio wa vipaumbele vyako. Mfano inawezekana familia kwako ni kipaumbele cha kwanza, kazi au biashara ni kipaumbele cha pili. Sasa unajikuta kwenye kazi au biashara ambayo inataka muda wako mwingi na kukunyima muda wa kukaa na familia, ambayo ndiyo kipaumbele cha kwanza. Hali hii inaweza kukuletea msongo mkubwa na kukosa utulivu, kwa sababu vipaumbele vyako vinavurugwa. Lakini unaweza kuchukua hatua ya kubadili mpangilio wa vipaumbele vyako kulingana na hali uliyonayo. Kwa kipindi fulani kuweka kipaumbele cha kwanza kuwa kazi au biashara kabla ya familia, na baada ya kujijengea msingi mzuri ukarudi kwenye vipaumbele vyako vya awali.
Hilo pia linakwenda kwa vipaumbele vingine kwenye maisha, mfano kama umekuwa unapendelea kufanya kazi mwenyewe, lakini ukajikuta kwenye kazi inayokutaka ushirikiano na wengine, kama hutabadili kipaumbele kuwa kufanya kazi na wengine utakuwa na msongo kipindi chote cha kazi. Kadhalika kwenye mahusiano na maeneo mengine ya maisha, pale mazingira yanapobadilika au unapokutana na uhitaji tofauti, kuwa tayari kubadili vipaumbele vyako.
Unapobadili vipaumbele kulingana na mazingira au hali inapobadilika, unakuwa tayari kutumia kila hali unayokutana nayo badala ya kupambana nayo.