Kila
mmoja wetu ana sauti iliyopo ndani yake, hisia fulani unazozipata
ambazo huwezi kuzielezea, ambazo zinakuashiria kama kitu ni kibaya au
kizuri, kama ni sahihi au siyo sahihi. Mara nyingi huwa tunapuuza sauti
hii na matokeo yake tunafanya makosa makubwa. Kuna wakati ndani yako
unapata msukumo wa kufanya au kutokufanya kitu, lakini ushawishi wa nje
unakufanya uende kinyume na sauti hiyo na unakuja kugundua
ungejisikiliza ungekuwa sahihi zaidi.
Jifunze
kuamini sauti yako ya ndani, hata kama inaendana na uhalisia wa nje.
Kuna kitu kwa nje kinaweza kuonekana ni sahihi, lakini sauti yako ya
ndani ikakuambia siyo sahihi, au kitu kwa nje kikaonekana siyo sahihi,
lakini sauti yako ya ndani ikakuambia ni sahihi. Jifunze kusikiliza
sauti yako ya ndani, inajua zaidi kuliko wewe na itakuongoza kwa usahihi
mara zote.
Watu
wote ambao wamefikia utajiri na mafanikio makubwa, kuna hatua ambazo
wamewahi kuzichukua, ambazo watu wa nje waliwaambia wanakosea, lakini
wao walifanya, kwa sababu sauti ya ndani iliwaambia ndiyo kitu sahihi
kufanya.
Unapojikuta
njia panda na hujui hatua ipi sahihi kuchukua, isikilize sauti yako ya
ndani, inajua njia sahihi na utaweza kufanya kilicho sahihi.
No comments:
Post a Comment