Tuesday, April 23, 2019

JIAMINI WEWE MWENYEWE.

Kama hujiamini wewe mwenyewe, hakuna yeyote anayeweza kukuamini na hutaweza kufanikiwa kwenye jambo lolote maishani mwako.
Unapaswa kujiamini wewe mwenyewe, unapaswa kuamini kwamba una uwezo mkubwa ndani yako wa kukuwezesha kupata chochote unachotaka, unapaswa kuamini hakuna kinachoweza kukuzuia kupata kile unachotaka. Tunaambiwa imani inaweza kuihamisha milima, na hii ndiyo imani unayopaswa kuwa nayo ili kufanikiwa na kufikia utajiri.
Katika safari yako ya kusaka utajiri utakutana na vikwazo vya kila aina, utapatwa na hofu nyingi, wapo watakaokukatisha tamaa kwa kukupa mifano ya wengi walioshindwa. Kitu pekee kinachoweza kukuvusha kwenye hali hizo ni kujiamini wewe mwenyewe.
Pia hakuna utakachopanga na kikaenda kama ulivyopanga, utashindwa kwenye mambo mengi licha ya kufanya kila unachopaswa kufanya. Kujiamini ndiyo kutakupa nguvu ya kuamka kila unapoanguka ili uweze kuendelea na safari ya mafanikio.
Jiamini wewe mwenyewe na hakuna kitakachoweza kukuzuia kufanikiwa.

AMINI SAUTI YAKO YA NDANI.

Kila mmoja wetu ana sauti iliyopo ndani yake, hisia fulani unazozipata ambazo huwezi kuzielezea, ambazo zinakuashiria kama kitu ni kibaya au kizuri, kama ni sahihi au siyo sahihi. Mara nyingi huwa tunapuuza sauti hii na matokeo yake tunafanya makosa makubwa. Kuna wakati ndani yako unapata msukumo wa kufanya au kutokufanya kitu, lakini ushawishi wa nje unakufanya uende kinyume na sauti hiyo na unakuja kugundua ungejisikiliza ungekuwa sahihi zaidi.
Jifunze kuamini sauti yako ya ndani, hata kama inaendana na uhalisia wa nje. Kuna kitu kwa nje kinaweza kuonekana ni sahihi, lakini sauti yako ya ndani ikakuambia siyo sahihi, au kitu kwa nje kikaonekana siyo sahihi, lakini sauti yako ya ndani ikakuambia ni sahihi. Jifunze kusikiliza sauti yako ya ndani, inajua zaidi kuliko wewe na itakuongoza kwa usahihi mara zote.
Watu wote ambao wamefikia utajiri na mafanikio makubwa, kuna hatua ambazo wamewahi kuzichukua, ambazo watu wa nje waliwaambia wanakosea, lakini wao walifanya, kwa sababu sauti ya ndani iliwaambia ndiyo kitu sahihi kufanya.
Unapojikuta njia panda na hujui hatua ipi sahihi kuchukua, isikilize sauti yako ya ndani, inajua njia sahihi na utaweza kufanya kilicho sahihi.

SIKILIZA NA JIFUNZE.

Kusikiliza ndiyo silaha yenye nguvu sana katika safari ya mafanikio. Ukiwa msikilizaji mzuri, utajifunza mambo mengi sana kwa watu wengine. Kuanzia wale unaofanya nao kazi na hata wale ambao inabidi upatane nao kwenye makubaliano mbalimbali.
Kusikiliza ni kugumu sana, na wengi hawawezi kusikiliza kwa umakini ndiyo maana hawajifunzi, hawajui watu wanataka nini na kuweza kuwapatia. Ukiwa mtu wa kusikiliza kwa umakini, kwa lengo la kuelewa na kujifunza, utajua mengi na pia utazijua tabia za watu, ambazo utaweza kuzitumia kwa mafanikio zaidi.
Ukiwasikiliza wateja wako utayajua mahitaji yao hata kama hawajakuambia wazi na kuweza kuwatimizia. Ukiwasikiliza wafanyakazi wako utajua kinachowahamasisha na ukiwapatia watajituma zaidi. Ukiwasikiliza unaotaka kufikia nao makubaliano, utajia udhaifu wao uko wapi na kuweza kuutumia.
Katika safari ya mafanikio na utajiri, kusikiliza na kujifunza ni hitaji muhimu sana. Hata watu wanawaheshimu sana wale ambao wanachukua muda na kusikiliza. Tumia nguvu hii kwa manufaa yako na ya wengine pia.

KUWA NA VYANZO VINGI VYA KIPATO.

Chanzo kimoja cha kipato ni utumwa, iwe ni kazi au biashara, huwezi kutajirika kwa kutegemea chanzo kimoja pekee. Angalia matajiri wote wakubwa, hakuna hata mmoja ambaye anategemea chanzo kimoja pekee cha kipato.
Kila biashara huwa ina changamoto zake, hakuna biashara ambayo inafanya vizuri wakati wote, kila biashara kuna kipindi inafanya vizuri na kipindi kingine inafanya vibaya. Unapotegemea biashara moja pekee, kila wakati utakuwa kwenye kupanda au kushuka.
Dawa ya kuondoa hali hiyo ya kupanda na kushuka ni kuwa na vyanzo vingi vya kipato, na ambavyo havitegemeani. Hivyo unapokuwa na changamoto eneo moja, eneo jingine linakuwa linaenda vizuri.
Kanuni hii haiwahusu wale wanaoanza, unapokuwa unaanza, anza na kitu kimoja na kiwekee msingi imara wa kuweza kujiendesha chenyewe. Baada ya kuhakikisha kitu cha kwanza kimekuwa imara, hapo sasa unaweza kuanzisha kitu kingine. Kuanza vitu vingi kwa wakati mmoja ni njia ya uhakika ya kushindwa.

UKWELI KUHUSU UTAJIRI.

Wengi wanapoingia kwenye safari hii ya utajiri, huwa wanaona mambo mazuri tu mbele, kwamba wakishapata utajiri maisha yatakuwa mazuri na watakuwa na furaha.
Felix anatupa ukweli kuhusu utajiri, kupitia maisha yake binafsi, ili tuelewe ni kitu gani tunakwenda kukutana nacho mbele, na tujiandae vizuri.
Kwanza kabisa anasema utajiri haujawahi kumletea yeye furaha, zaidi umemletea matatizo makubwa ya kiafya baada ya kujihusisha na ulevi, madawa ya kulevya na uzinzi.
Pili anasema utajiri unakufanya uwe chambo ambapo kila mtu atatumia kila njia kupata fedha zako. Wapo watakaotumia njia za kuomba, wengine kuiba na hata wengine kukushitaki kwa kitu ambacho hujafanya.
Tatu utajiri utaharibu mahusiano mengi uliyonayo. Mahusiano ya ndoa, kwa wengi yanaathirika sana. mahusiano ya kifamilia na kindugu nayo yanaathiriwa sana na safari yako ya utajiri na hata baada ya kufikia utajiri.
Kwa kifupi kadiri unavyokuwa tajiri siyo kwamba matatizo uliyonayo yanaondoka, bali yanakuwa makubwa zaidi. Hivyo jiandae kukabiliana nayo, na kazana kujijengea busara zaidi kadiri unavyoendelea kutajirika. Kwa sababu utajiri bila busara utakuwa ni kujichimbia kaburi lako mapema.

JE, NI KWELI WALIOFANIKIWA WANA BAHATI ?


Felix Dennis katika kitabu chake anatuambia ni kweli kwamba watu waliofanikiwa wana bahati kuliko wale ambao hawajafanikiwa. Lakini kitu tunachopaswa kujua ni hiki, bahati hazikuwafuata vitandani kwao wakiwa wamelala. Bali walikutana na bahati katika mapambano yao.

Hivyo ili ufanikiwe unahitaji kupata bahati, lakini bahati hiyo haitakutafuta wewe, itabidi uitafute wewe. Lazima uweke kazi, lazima ujitume sana, na katika kujituma kwako ndiyo utakutana na fursa ambazo wengine hawawezi kuzitumia kwa sababu hawana maandalizi kama uliyonayo wewe.

Hivyo tunajumuisha kwa kusema, bahati ni pale maandalizi yanapokutana na fikra. Kama unataka bahati zaidi, hakikisha unakuwa na maandalizi bora zaidi.

Wednesday, April 17, 2019

KWA KUFANYA MACHAGUO HAYA TUTAWEZA KUDHIBITI MAISHA YETU.


1. Kuwa wewe, usiwe wao.
 
2. Fanya zaidi, tarajia kidogo.
 
3. Kuwa chanya, usiwe hasi.
 
4. Kuwa suluhisho, usiwe tatizo.
 
5. Kuwa mwanzilishi, usiwe mkwamishaji.
 
6. Hoji zaidi, amini kidogo.
 
7. Kuwa mtu fulani, usiwe mtu yeyote.
 
8. Penda zaidi, chukia kidogo.
 
9. Toa zaidi, pokea kidogo.
 
10. Ona zaidi, angalia kidogo.
 
11. Weka akiba zaidi, kuwa na matumizi kidogo.
 
12. Sikiliza zaidi, ongea kidogo.
 
13. Tembea zaidi, kaa kidogo.
 
14. Soma zaidi, angalia kidogo.
 
15. Jenga zaidi, bomoa kidogo.
 
16. Sifia zaidi, kosoa kidogo.
 
17. Safisha zaidi, chafua kidogo.
 
18. Ishi zaidi, usiwe upo upo tu.
 
19. Kuwa majibu, usiwe maswali.
 
20. Kuwa mpenzi, usiwe adui.
 
21. Kuwa mtuliza maumivu, usiwe mtoa maumivu.
 
22. Fikiri zaidi, itikia kidogo.
 
23. Kuwa wa tofauti, usiwe wa kawaida.