Friday, November 30, 2018

JIWEKEE MUDA WA UKOMO KWA CHOCHOTE UNACHOPANGA KUFANYA.

Mtu mmoja amewahi kusema kwamba jukumu huwa linachukua muda uliopangwa lifanyike. Akimaanisha kama kuna jukumu ambalo linapaswa kufanywa kwa masaa mawili, litakamilika ndani ya masaa mawili. Jukumu hilo hilo likipangwa kufanyika ndani ya masaa matano, litachukua masaa matano.
Huwa tunasukumwa kufanya zaidi pale ambapo muda unakuwa mdogo, na tunaahirisha mambo pale muda unapokuwa mwingi. Ndivyo maana wanafunzi ni vigumu sana kusoma siku za kawaida, lakini mtihani unapokaribia, hamasa ya kusoma inakuwa juu.
Jiwekee muda wa ukomo kwa chochote unachopanga kufanya, na muda huo uwe mfupi kuliko muda uliozoeleka. Kwa kuwa na muda huu na kuufuata, utaweza kujisukuma kufanya zaidi. Kadiri unavyokuwa na muda mfupi wa kutekeleza jambo, ndivyo mawazo ya kuahirisha yanavyopotea kwenye akili yako. Waahidi watu kwamba jukumu litakamilika mapema kuliko kawaida, na tekeleza hilo uliloahidi.

KUWA NA MAMBO YAKO MATANO KWA SIKU AMBAYO UTAYATEKELEZA.

Kila siku unayoianza, ainisha mambo matano muhimu ambayo ukiyafanya siku hiyo yatakusogeza karibu na mafanikio unayotaka kuyafikia. Mambo hayo matano unapaswa kuyafanyia kazi bila ya kujali mazingira yapoje. Inyeshe mvua au liwake jua, hayo matano ni muhimu kwa siku yako na unapaswa kuyafanyia kazi.
Kwa kuwa na tano za siku, unajiweka kwenye nafasi ya kutekeleza yale muhimu na kuepuka kupotezwa na kelele ambazo zimekuzunguka kila mahali.

TUMEZOEA KUSIMAMIWA : KUWA NA MTU WA KUKUSIMAMIA.

Sisi binadamu ni wabaya sana kwenye kujisimamia wenyewe, huwa tunajionea sana huruma na ni rahisi sana kujidanganya. Unaweza kuwa na orodha yako ya siku, umepanga mambo yako matano muhimu na hata kujiwekea ukomo. Lakini katikati ya siku yako ukawa hujisikii kuendelea na yale uliyopanga, ni rahisi kujihalalishia kwamba labda umechoka au ni kitu hakiwezekani.
Lakini unapokuwa na mtu wa pembeni, mtu ambaye jukumu lake ni kuhakikisha umekamilisha uliyopanga na hapokei sababu bali matokeo, utalazimika kufanya kile ulichopanga kufanya.
Tafuta mtu wa karibu kwako, ambaye hakuonei huruma kisha mtake akusimamie kwa karibu ili utimize unachotaka. Kama huwezi kupata mtu wa karibu basi kuwa na kocha au menta ambaye atakusimamia kwa karibu.

JIAMBIE HIVI " NAFANYA SASA , MUDA HUU ".

Kuna wakati unakuwa umeshapanga kabisa nini utafanya na kwa wakati gani. Lakini inapofika muda wa kufanya, mawazo ya kuahirisha yanaanza kukuingia. Unaanza kuona labda hujawa tayari au ni bora kusubiri.
Ni katika wakati kama  huu ndiyo unapaswa kujiambia kauli hii, NAFANYA SASA HIVI, rudia kauli hiyo mara nyingi uwezavyo na utajikuta umeanza kufanya. Kila unapofikiria kuahirisha kufanya kitu, jiambie kauli hiyo kwamba unafanya. Kila unapoanza kujiambia kwambe umechoka, anza kujiambia kauli hiyo.
Kwa kurudia rudia kujiambia kauli hiyo, unaanza kuiamini na kujiamini wewe mwenyewe na kuanza kufanya.

TUNA MIPANGO MINGI SANA NA MIZURI, TATIZO NI UTEKELEZAJI WAKE ???

Mipango ni rahisi sana, kila mtu anapanga na msimamishe mtu yeyote njiani na muulize mipango yake ni ipi, atakupa mipango mizuri sana.

Pamoja na kila mtu kuwa na mipango mizuri, ni wachache sana ambao wanaweza kufanyia kazi mipango hiyo na ikawa uhalisia kwenye maisha yao. Wengi wamekuwa wanabaki na mipango tu, lakini haiwi uhalisia.

Kinachowazuia wengi kutekeleza mipango waliyonayo ni tabia ya kuahirisha mambo. Hii ni tabia ambayo ni asili yetu sisi binadamu, huwa hatupendi kufanya chochote ambacho kinatuumiza au kinataka tuweke kazi.

Huwa tunapenda kutumia muda wetu kwa vitu visivyo na maana. Kwa muda ule ule na kwa nguvu zile zile, huwa tunaona ni bora kutumia kufanya vitu ambavyo vitatupa raha ya muda mfupi, kuliko kufanya vitu ambavyo havina raha ya muda mfupi lakini kwa muda mrefu vina maana.

Kinachowatofautisha wale wanaopata mafanikio makubwa kwenye maisha yao na wale wanaoshindwa siyo bahati wala akili wala fursa. Kinachowatofautisha ni namba wanavyoweza kuishinda tabia ya kuahirisha mambo. 

Wanaofanikiwa na wanaoshindwa wote wanakuwa kwenye mazingira sana, wanakutana na fursa sawa, lakini wale wanaoshindwa huwa wanasubiri wakati wanaofanikiwa wanachukua hatua.

FANYA BIASHARA HIZI UTAPIGA PESA SANA. UTAFANIKIWA SANA.

1. USAFIRI.
Moja ya biashara ambayo inaaminika hasa kwa bara la afrika ikiwa utaifanya kwa utulivu na ukafata misingi yake ni biashara ya usafiri. Hapa unaweza ukawa na kampuni yako ya kusafirishia abiria kutoka sehemu moja na kwenda nyingine.
Kwa sasa hitaji la usafiri bado ni kubwa, kama si mjini hata kijijini. Watu wanataka kusafiri kila siku na kwa bahati mbaya wengi hawana uwezo huo wa kumiliki vyombo vya usafiri. Hii ni mojawapo ya biashara ya kuifikiria kuifanya kama unaweza, kwani itakupa mafanikio sana.

2. AFYA.
Kama pia utajikita na kufanya biashara inayohususha mambo ya afya, basi upo uwezekano mkubwa zaidi wa wewe kufanikiwa sana. Huduma za afya katika maeneo mengi bado hazijafikiwa kisawasawa na zinahitajika kweli.
Hivyo kwa kufanya biashara hii, kama ukifungua hospitali au zahati au duka la dawa, utapata pesa na hapo pia utakuwa imeisaidia jamii. Kikubwa kubali kuzunguka kuangalia ni wapi ambapo ukifanya huduma au biashara hii wewe itakulipa.

3. CHAKULA.
Hakuna mtu asiyekula, hiyo ikiwa na maana ukianzisha biashara ya vyakula na ukaifanya kwa ufanisi mkubwa utafanikiwa. Hapa unaweza ukauza chakula, lakini si maanishi uje na picha ile ya mama ntilie ‘pasee.’
Ukiamua kuja na biashara ya kuuza chakula ifanye kwa ukisasa zaidi. Zipo sehemu bado nyingi zinazohitaji huduma hii ya chakula safi, mazingira safi, lakini hawaipati kwa uhakika kwahiyo unatakiwa ujue jinsi ya kuanza ili uanze kupiga pesa.

4. VIWANDA  VIDOGO  VIDOGO. 
Huwezi  kuendelelea sana kama utaendelea kuwa mlanguzi wa biashara za watu wengine. Changamsha akili na anza mchakato wa kuweka viwanda vidogo vidogo ambavyo vitasaidia wewe kuweza kukupa kipato kikubwa.
Uzuri wakuwa na kiwanda kidogo wewe ndio unakuwa mzalishaji wa kwanza kwa hiyo ni lazima utapata faida kubwa sana. Hapa unaweza ukatengeneza kiwanda chako cha kutengeneza juisi au unga wa sembe na lishe, uamuzi ni wako.

Thursday, November 22, 2018

KILA MTU NA HAMSINI ZAKE. HAKUNA ANAYEJALI SANA MAISHA YA WENGINE.

Maisha ya sasa hivi naweza kusema yamekuwa ni kama ya kuishi kisiwani, watu wamekuwa hawajali sana watu wengine kwa kiasi kikubwa, ukilinganisha na zamani. Kwa sasa ukipata changamoto kubwa wewe jua hiyo ni changamoto yako tu, inabidi ukomae nayo hadi utoke.
Kutokana na hili kuendelea kudumu kunafanya maisha yanazidi kuendelea kuwa magumu sana hadi watu wanakosa msaada ambao ungeweza kuwasaidia. Ubinafsi ambao wengi wanao imekuwa ni kichocheo kikubwa sana cha ugumu wa maisha.