Sunday, September 16, 2018

MAARIFA SAHIHI + KUCHUKUA HATUA KUBWA = MAFANIKIO MAKUBWA.

JIFUNZE KUJITHIBITI, KUWA HALISIA , KUJITAMBUA ,KUJIENDELEZA UTAFANIKIWA SANA KIMAISHA.

(1).  KUJIDHIBITI
Eneo la kwanza kabisa unalohitaji kulifanyia kazi kila siku ili kuwa na maisha bora ni kwenye udhibiti. Unahitaji kujidhibiti wewe mwenyewe, la sivyo utawapa wengine nafasi ya kukudhibiti wewe. Unahitaji kujipangia nini utafanya na kipi hutafanya na kufuata mpango huo.
Muda ulionao kila siku ni mfupi sana, ni muda ambao kama ukiweza kujidhibiti utaweza kufanya makubwa. Lakini ukishindwa kujidhibiti, utashangaa muda unaisha na hakuna ulichofanya. Lazima uweze kujiambia HAPANA wewe mwenyewe, pale unapojiona unakosa udhibiti. Pia lazima uweze kujiadhibu wewe mwenyewe pale unapokwenda kinyume na mipango uliyojiwekea wewe mwenyewe.
Jidhibiti wewe mwenyewe na kila siku yako itakuwa siku ya ushindi, kwa sababu utafanya yale ambayo ni muhimu zaidi kwako.

(2). KUWA  HALISIA / ACHA MAIGIZO
Kitu kimoja ambacho dunia inakazana sana kufanya kwako ni wewe uwe kama wengine. Kwa sababu dunia inajua ukiwa wewe, utakuwa msumbufu, hutafaa kutawaliwa na hivyo inakazana sana uwe kama wengine, uwe ndani ya kundi ili uweze kutawaliwa na kutumiwa vizuri na wengine.
Hivyo eneo la pili la kufanyia kazi kila siku ili kuwa na maisha bora ni uhalisi. Unapaswa kukazana kuwa halisi kila siku, kuishi maisha yako kwa uhalisia, kuacha kuigiza na kuacha kufanya vitu ili kuwaridhisha wengine au uonekane na wewe unafanya.
Hutaweza kufanikiwa kama huishi maisha halisi kwako, hata kama utapata vitu vingi kiasi gani, kama maisha unayoishi siyo halisi kwako, kila mara utasikia sauti inakuambia wewe bado sana. Na hapa ndipo wengi husema wamefanikiwa lakini hawana furaha.
Shida yao ni moja tu, maisha wanayoishi siyo halisi kwao, ni maisha feki na hivyo mafanikio yoyote wanayopata yanakuwa yanaonekana na wengine lakini siyo ndani yao binafsi.
Kuwa halisi kwako, jua uimara wako, jua madhaifu yako, jua yapi yenye maana kwako na jua kusudi la maisha yako ni lipi. Kisha tumia kila dakika ya siku yako kuishi maisha ambayo ni halisi kwako. Utafanikiwa kariri unavyoishi maisha halisi kwako.

(4). JITAMBUE.
Kujitambua ni eneo muhimu sana la kufanyia kazi, na linatangulia uhalisia. Kwa sababu bila ya kujitambua, hutaweza kuishi uhalisia wako. Na changamoto ya kujitambua ni kwamba ni zoezi endelevu.
Watu wengi wamekuwa wakifikiri wakishajua wanataka nini kwenye maisha yao, wakishaweka malengo makubwa basi wamemaliza. Hiyo siyo sahihi, unachojua leo kuhusu wewe, kinaweza kuwa tofauti kabisa na utakachotambua kesho kuhusu wewe.
Kubadili mazingira, kukutana na changamoto, kote huko kutakufunulia kwa undani kuhusu wewe. Mara nyingi huwezi kujua una uwezo wa kufanya makubwa kiasi gani mpaka pale unapokutana na changamoto kubwa kwenye maisha yako.
Hivyo zoezi la kujitambua ni endelevu, kila siku, kwa kila unachopitia, jiulize ni kipi kipya umejua kuhusu wewe. Na wakati mzuri wa kujipima ni pale unapopitia mambo magumu. Utaweza kupima uwezo wako wa kudhibiti hasira pale unapokasirishwa hasa. Unaweza kujua unaweza kuvumilia ugumu kiasi gani pale unapokutana na ugumu zaidi.
Kila siku mpya ya maisha yako ni siku ya kujitambua zaidi, ishi kila siku kwa kutaka kujitambua na maisha yako yatakuwa bora sana.


(4).KUJIENDELEZA.
Eneo la nne ambalo unapaswa kulifanyia kazi kila siku ni kujiendeleza wewe binafsi. Kila siku lazima ukazane kuwa bora zaidi kuliko siku iliyopita. Kila siku unapaswa kujifunza kitu kipya. Usikubali siku iishe ukiwa kama siku ya jana ilivyoisha.
Weka kipaumbele kwenye kujifunza. Jifunze kupitia kusoma, kusikiliza, kuangalia na hata kufanya. Soma vitabu, sikiliza mafundisho mbalimbali, waangalie wengine kwa namna wanavyofanya na jaribu vitu vipya kwa ajili ya kujifunza kwa kufanya.
Jinsi unavyojifunza kila siku, unazidi kuwa bora na kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.
Rafiki yangu mpendwa, maeneo haya manne ni muhimu sana kwako kuyafanyia kazi kila siku. Ninaposema kila siku, namaanisha kila siku ya maisha yako. Na usiache hata siku moja, mpaka siku unaondoka hapa duniani.
Kama unajiambia huwezi kila siku, kama unajiambia utajisahau au kupitiwa na maisha mengine, ninayo nafasi ya kukumbusha hili kila siku, na kukushirikisha fursa za kujifunza na kujitambua kila siku. Karibu kwenye KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utapata nafasi ya kuingia kwenye kundi la wasap, na kila siku utajifunza kwenye maeneo hayo manne na mengine mengi.


 Na  Mwl  Japhet  Masatu , Dar  es  salaam , Tanzania,  Afrika Ya  Mashariki ---Mwl  wa  Maisha Na  Mafanikio, Mshauri, Public Speaker(MC), Mwandishi, Mjasiriamali /
Tuwasiliane kwa :+ 255 755 400 128 / + 255 716 924136(WhatsApp ).  EMAIL: japhetmasatu@gmail.com

Saturday, September 15, 2018

UKIFANYA KWA MSUKUMO WA NDANI , UTAPATA PESA SANA.

Kwa chochote ambacho unafanya kwenye maisha yako, kuna misukumo au hamasa za aina mbili.
(2):-
         Aina ya kwanza ni msukumo au hamasa inayotoka ndani yako. Hapa ni pale unapofanya kitu kwa sababu umechagua kufanya, kwa sababu unajua ni kitu muhimu kwako kufanya na kwa sababu unajua kuna thamani unaongeza kwenye maisha ya wengine.

        Aina ya pili ni msukumo au hamasa inayotoka nje. Hapa ni pale unapofanya kitu ili kuonekana unafanya, au kwa sababu wengine wanafanya, au kwa sababu watu wanakutegemea ufanye hivyo. Pia unaweza kuwa unafanya ili upate kitu fulani unachotaka.(BENDERA  FUATA  UPEPO ).

(1) .MSUKUMO  AU   HAMASA KUTOKA  NDANI

Msukumo wa ndani yako ndiyo wenye nguvu sana, kwa sababu utafanya licha ya kinachoendelea nje yako. Lakini msukumo wa nje hauna nguvu kubwa, kwa sababu mazingira ya nje yakibadilika, basi na msukumo unabadilika.
Sasa kama unataka kupata fedha zaidi, tafiti zinaonesha kwa kutumia msukumo wa ndani unaweza kutengeneza fedha mara tatu zaidi ya unavyotumia msukumo wa nje.
Pale unapofanya kitu kwa sababu umechagua kufanya, kwa sababu unataka kuwasaidia wenye uhitaji au unataka kutoa mchango wako, utatengeneza kipato kikubwa kuliko pale unapofanya ili tu upate fedha ya kulipa gharama za maisha yako.
 
Unapofanya kitu kwa sababu tu unataka fedha, unapata fedha kidogo, kuliko kama utafanya kitu hicho hicho kwa msukumo kutoka ndani yako.
Na pale unapofanya kitu kwa msukumo wa ndani, haimaanishi kwamba hujali fedha, unajali sana, ila msukumo wa wewe kufanya ni mkubwa kuliko fedha, hivyo unakuwa umejiweka juu ya fedha, kitu ambacho kinakuwezesha kupata fedha kama unavyotaka.



(2).MSUKUMO  AU   HAMASA  KUTOKA  NJE

Lakini unapofanya kwa ajili ya fedha pekee, utapata fedha, lakini utakuwa umeweka fedha juu yako, hivyo unakuwa umejiwekea ukomo wewe mwenyewe, ukishafika kiwango fulani cha fedha utaacha kufanya kwa sababu hamasa yako ilikuwa fedha pekee.

Kuwa na msukumo wa ndani kwenye kila unachofanya, penda fedha na ihitaji, lakini isiwe msukumo pekee wa wewe kufanya kitu. Fanya unachofanya kwa msukumo wa ndani na utaweza kupata fedha kadiri utakavyo, na hutakuwa na ukomo wowote kwenye kipato unachoweza kutengeneza.


 Na  Mwl  Japhet  Masatu , Dar  es  salaam , Tanzania,  Afrika Ya  Mashariki ---Mwl  wa  Maisha Na  Mafanikio, Mshauri, Public Speaker, MC,Mwandishi, Mjasiriamali /
Tuwasiliane kwa :+ 255 755 400 128 / + 255 716 924136(WhatsApp ).  EMAIL: japhetmasatu@gmail.com


Sunday, September 2, 2018

JINSI YA KUDHIBITI TABIA YA KUNUNUA VITU OVYO ! KWA KUTUMIA SHERIA YA SIKU 30 KWENYE FEDHA.

Moja ya tatizo kubwa ambalo watu wanalo kwenye fedha ni kushindwa kudhibiti matumizi. Watu wanapokuwa na fedha, na wakakutana na kitu kizuri, wanajikuta wameshanunua.
Ndiyo maana watu wanaishia kuwa na nguo ambazo hawazivai, vitu ambavyo hawavitumii, lakini wamenunua. Ukiwauliza kwa nini walinunua hata hawawezi kukupa jibu la wazi. Wengine watakuambia ilikuwa rahisi na wasingeweza kupata kwa bei rahisi vile. Wengine watakuambia wanajua watakuja kuhitaji kitu hicho siku moja.
Haijalishi unajifariji kwa maneno gani, kama umenunua kitu ambacho hukitumii sana, umepoteza fedha. Au kama umenunua kitu, lakini inakulazimu ukitumie ili usijione umepoteza fedha, jua umeshapoteza fedha.
Sasa, ipo sheria inayoweza kukusaidia usirudie tena makosa uliyofanya huko nyuma ya kununua kitu ambacho hukitumii. Sheria hiyo ni sheria ya siku 30.
Sheria hii inasema kwamba, kama umekutana na kitu na ukajishawishi unahitaji kukinunua, usikinunue hapo hapo. Badala yake andika mahali kwamba unataka kununua kitu hicho, kisha subiri kwa siku 30 kabla hujakinunua. Sasa kama siku 30 zitaisha na bado ukawa unauhitaji mkubwa wa kitu hicho, au hata siku 30 hazijaisha uhitaji unakuwa mkubwa mno la sivyo maisha hayawezi kwenda, nunua kitu hicho.
Rafiki, kwa sheria hii, usijidanganye kwamba hii ni bei rahisi na hutapata tena, au kitu hicho ni cha mwisho na hakitapatikana tena. Sheria ni moja, subiri siku 30 zipite na utanunua.
Kitu ambacho utanufaika nacho kwenye sheria hii ni kwamba baada ya siku tatu kupita, wala hata hutakumbuka kama ulipanga kununua kitu hicho.

 Na  Mwl  Japhet  Masatu , Dar  es  salaam , Tanzania,  Afrika Ya  Mashariki  /+ 255 755 400 128 / + 255 716 924136(WhatsApp ).  EMAIL: japhetmasatu@gmail.com

USIOGOPE KUACHA KITU KAMA HAKINA TIJA.


Usiogope kuacha kitu pale unapoona hakikupi matokeo uliyotaka. Watu wengi huwa wanafikiria kuacha ni kushindwa. Siyo sahihi, unaweza kuacha kitu ambacho hakifanyi vizuri na kufanya kingine ambacho kitakuwezesha kufanikiwa zaidi.


Na  Mwl  Japhet  Masatu , Dar  es  salaam , Tanzania,  Afrika Ya  Mashariki  /+ 255 755 400 128 / + 255 716 924136(WhatsApp ).  EMAIL: japhetmasatu@gmail.com

FANYA MAAMUZI KWA WAKATI.

Fanya maamuzi wakati unapokutana na hitaji la kufanya maamuzi. Usijiambie wacha nifikiri nitaamua baadaye. Kama kitu ni muhimu fanya maamuzi sasa, au hutayafanya kabisa. Maamuzi yanayosogezwa mbele ni maamuzi ambayo yamekuwa hayafanywi.

Usiogope kukosea pale unapochagua kufanya maamuzi. Ni bora ufanye maamuzi ukosee, kwa sababu utarekebisha makosa yako, kuliko kutokufanya maamuzi kabisa.


Na  Mwl  Japhet  Masatu , Dar  es  salaam , Tanzania,  Afrika Ya  Mashariki  /+ 255 755 400 128 / + 255 716 924136(WhatsApp ).  EMAIL: japhetmasatu@gmail.com

USIKIMBIZANE NA VITU VYA KUPITA . WEWE KAZANA NA AMBAVYO SIYO VYA KUPITA.

Weka nguvu zako kwenye vitu ambavyo havitabadilika. Watu wengi huwa wanakazana kukimbizana na vitu vinavyopita, fursa mpya, fasheni na habari mpya ya mjini. Wewe kazana na vile ambavyo siyo vya kupita, na biashara yako itakuwa imara. Achana na vitu ambavyo watu wanataka sasa, kazana na vitu ambavyo watu wataendelea kuhitaji miaka kumi ijayo.



Na  Mwl  Japhet  Masatu , Dar  es  salaam , Tanzania,  Afrika Ya  Mashariki  /+ 255 755 400 128 / + 255 716 924136(WhatsApp ).  EMAIL: japhetmasatu@gmail.com