Friday, November 2, 2018

TENGENEZA UHURU KAMILI KWENYE MAISHA YAKO UTAPATA FURAHA YA KWELI

Wapo watu ambao wameajiriwa na wanalipwa mshahara mkubwa sana, kipato chao kinawawezesha kupata chochote wanachotaka, kwa upande wa kipato, lakini bado wanakosa furaha kwenye maisha yao. Na sababu kubwa ni kukosa uhuru wa maisha yao. Kwa sababu kadiri mtu anavyolipwa, ndivyo anavyotumika zaidi. Kadiri kipato cha ajira kinavyokuwa kikubwa, ndivyo majukumu yanakuwa mengi na kutegemewa kuwa tayari na kazi wakati wowote. Mtu hawezi kuchagua afanye nini na maisha yake, ni mpaka aombe ruhusa kwanza.

Uhuru ni kiungo muhimu sana cha furaha, huwezi kuwa na furaha kama huna uhuru.
Na uhuru siyo kwenye eneo la fedha na kazi pekee, bali hata kwenye fikra za wengine. Kama una chuki na wengine haupo huru, hivyo huwezi kuwa na furaha. Kama unashindana na wengine huwezi kuwa huru, kwa sababu muda wote utakuwa unawaangalia wanafanya nini.
Ili kuwa na furaha ya kudumu kwenye maisha yako, lazima uwe na uhuru na maisha yako. Kadiri unavyokuwa huru, ndivyo unavyokuwa na furaha.

UFUNGUO  WA  FURAHA:Tengeneza uhuru kamili kwenye maisha yako, ondoa utegemezi wako kwa wengine au vitu fulani ndiyo maisha yako yakamilike. Hata kama huna kila unachotaka, kitendo cha kuwa huru na muda wako na maisha yako, kinakuwezesha kuwa na furaha ya kudumu kwenye maisha yako.

No comments:

Post a Comment