Friday, September 3, 2021

MITIHANI YA MAISHA HAINA MWISHO , UKISHINDA MTIHANI HUU UNAKUJA ULE.

Bila maandalizi maishani ni kukubali kushindwa au kufeli. Maandalizi hutusaidia kupunguza mawezekano ya kushindwa, kushangazwa au hata kuumia. Wanasema wakati wa vita sio wakati sahihi wa kufanya maandalizi isipokuwa kabla ya vita ndo ulikuwa wakati sahihi wa kujiandaa. Si hilo tu hata maisha ya kila siku bila maandalizi ya mapema ni mtu kujiandaa kushindwa au kuumia zaidi.

Imekuwa ni kawaida yetu sisi binadamu kutoweka uzito katika maandalizi ya mambo mengi maishani na hili linajitokeza kutokea kwa mambo yakitukuta hatukuwa na maandalizi yoyote yale. Inawezekana ni suala la kiuchumi, mahusiano au hata masuala ya kiafya huwa hatujiandai mpaka pale mambo yamejitokeza na kutuzindua kuwa tulipaswa kujiandaa mapema kabisa.

Maisha yamejaa mitihani na majaribu katika kila kona ya kuishi kwetu ikiwa ni kutufungua na kutukumbusha ilivyo haja kubwa ya kuwa na maandalizi mapema ya mambo hayo. Mambo mengi yanayojitokeza na tukayaona ni kama yametokea ghafla kama ajali ni kuwa hatukuwa na maandalizi nayo. Kila mtego ambao mtu anaweza kukutwa amenaswa ni kuwa hakugundua mapema kuwa ilibidi kujua ishara za awali na kujiandaa ili asijekushindwa katika mtihani huo. Wengi tumejikuta tunaanguka katika mambo mengi maishani sababu ya kuondoa nafasi ya maandalizi ambayo ilipaswa kuwepo kila siku.

Maisha hayaachi kutufundisha uhalisia wake kuwa kuna nyakati ngumu na nyepesi, furaha na huzuni, giza na nuru, kushuka na kupanda, kufaulu na kufeli na kuishi na kufa. Safari zote hizi hujitokeza na zinakuja wakati wowote ule ambao mtu anaweza asitegemee ingekuwa hivyo. Bila maandalizi ya kujua hilo ndo kunakozalisha kuyaona maisha yana sura moja tu ya kuwa ni magumu na yasoruhusu watu kuwa na furaha. Yote hujitokeza sababu ya mtu kukosa kujiandaa na kujua ukweli huu wa maisha kuwa wakati wowote ni safari ya maandalizi kwa kuwa mitihani haikosi kuwepo maishani.

Tunapaswa kujiandaa kukutana na kila aina ya watu ambao wanaweza kutufundisha vitu au kutuachia maumivu, wanaweza kutusaidia kukua au kutudumaza kabisa, watu wanaoweza kutuunga mkono au kutukatisha kabisa tamaa, watu ambao watafurahia hatua zetu au kutozifurahia. Aina ya watu hawa tunaweza kukutana nao katika safari ya maisha yetu ya kila siku. Tunapokosa kuwa tayari kujiandaa kwa hilo tunakubali kuumia na kushangazwa na mambo yatakapojitokeza.

Jiandae kwa kila hatua yako hasa pale ambapo upo karibu na watu wanaokuzunguka. Watu wanaotuzunguka wana uwezo mkubwa wa kutufanya tujikute tunaumizwa nao kwa vitu ambavyo wanaweza kuvifanya na tukabaki kushangaa kwa sababu huwa hatujiandai kuwa hata wanaotuzunguka ni watu wenye madhaifu na wanaweza kutuumiza pia. Mitihani ya maisha inaweza kuja kutoka eneo lolote na mtu anapokosa kujua hili tu ni kujiandaa kuumia na kushangazwa na mambo hayo.

Jiandae kwa kuyaweka mambo katika makundi mawili. Kundi la kwanza ni lile lile la kuangalia mambo yaliyo katika uwezo wako ushughulike nayo na kundi la pili ni yale mambo yaso katika uwezo wako uyaache kama yalivyo au kuwa tayari kuishi nayo. Ni falsafa ngumu kuifuatilia ila inampa nguvu mtu katika kujiandaa na kukabiliana na mitihani maishani na majaribu mengi ambayo hujitokeza kutupima na kufungua uhitaji wa kujiandaa zaidi kila siku. 

JIUNGE  DARASA--ONLINE  "  UJIFUNZE   MENGI USIYOYAJUA  TUWASILIANE  SASA  NIKUUNGE KWA   DARASA. "

NA KOCHA   MWL. JAPHET  MASATU , DAR  ES  SALAAM , TANZANIA

WhatsApp + 255 716924136  /    + 255  755 400128

 

Thursday, September 2, 2021

KUWA NA VIPAUMBELE KATIKA MAISHA NA VIFANYIE KAZI



Tunaingia katika taabu maishani sababu ya kukosa msingi wa kujipa msimamo dhidi ya mambo fulani fulani katika maisha. Mtu anaporuhusu kila kitu kiwe sehemu ya maisha yake ni kuruhusu kuyaweka maisha hatarini. Mtu anayekosa msimamo ni rahisi kuyumbishwa na hali zozote zile zitakazojitokeza katika safari ya maisha. Na watu wengi wapo katika hatari hii ya kutoyapa maisha msimamo au msingi fulani unaowaongoza kutoyumbishwa na mambo maishani.

Msimamo hauendi pekee katika maisha bali hata uendeshaji wa kazi unahitaji mtu ajiwekee msimamo fulani ili kutoyumba kwa kazi zake. Mfano kama kazi ya utabibu mtu akikosa msimamo fulani alojiwekea wa kazi ni rahisi kuyakubali mambo mengine ambayo ni nje na maadili ya kazi yake.

Msimamo huu wa maisha ni kuchagua mambo ambayo hutakuwa tayari kuyavunja iwe kwa namna yoyote ile mtu atashawishiwa. Msimamo huu ni katika kuweka ugumu wa kutovunja ahadi ambayo mtu amejiwekea mwenyewe dhidi ya misingi fulani maishani. Hili humsaidia mtu kuwa na maisha yasoyumbishwa.

Ni hatua ngumu ambayo si watu wote wanaweza kuiendea katika maisha. Kuwa maisha yao yataongozwa na misimamo fulani fulani ambayo itawafanya waonekane ni watu wenye misimamo mikali dhidi ya wengine, au watu wasojali hisia za watu wengine. Ila hakuna matokeo mazuri maishani yanaweza kujitokeza isipokuwa kwa mtu kuweka mambo yake katika msimamo asokubali kuvunja kwa namna iwayo yoyote ile.

Weka msimamo katika kazi unayofanya, weka msimamo katika namna unavyohusiana na watu na weka msimamo katika mambo yote unayojua bila kuwa na msimamo thabiti basi mambo mengi yanaweza kuharibika. Hili litakusaidia kuwa na maisha yenye uimara na utulivu wakati wote. Kuna faida kubwa katika kujenga msimamo maishani ili lolote linalokuja kwako linakukuta ukiwa imara na hutayumbishwa na kitu chochote kile. 

 

NA  KOCHA  MWL.  JAPHET  MASATU , DAR  ES  SALAAM , TANZANIA.

WhatsApp + 255 716 924 136 / + 255 755 400128 / + 255 68 361  539

 

MAGUMU , MATATIZO NI SEHEMU UKUAJI KATIKA SAFARI YA MAISHA , USIJILAUMU NA KULALAMIKA

Kujilaumu ni kitendo cha kujiona mwenye hatia dhidi ya jambo fulani unaloona kwa namna moja umelisababisha litokee na linakuumiza sana ukilitafakari. Hali hii ni mbaya tena iso na usaidizi wowote ule mbali na kuongeza ugumu na taabu ya jambo apitialo mtu. Mtu anaweza kuendelea kuumia juu ya jambo alofanya iwe ni siku za karibuni au miaka mingi imepita. Haisaidii kujilaumu au kulaumu mtu juu ya matukio mbalimbali yanayotokea maishani.

Jamii zetu nyingi tumejengewa hali za kulaumu watu pale mambo yanapoenda tofauti na vile ambavyo tumepanga. Hivyo watu wengi kulaumu wengine inakuwa inaonekana ni kisingizio cha kujiondoa dhidi ya jukumu hilo na kuona wengine walipaswa kuadabishwa kwa hilo. Wakati wote kulaumu au kujilaumu hakujawahi kusaidia kutatua majukumu ya maisha mtu anapoishi. Ni kujisahaulisha tu kuwa tatizo halipo ingali tatizo lipo.

Eneo mojawapo ambalo watu wengi huanza kujilaumu ni pale ambapo vipindi vya hali ngumu maishani vinapobisha hodi, watu hujilaumu huenda wao si watu wenye bahati maishani, wao ni watu wanaonewa, wao hawastahili kupitia hayo na wengine ni kuona ni mikosi tu wao kutokoma kupitia hayo magumu. Magumu ni tafsiri yetu tunayoiweka katika yale yanapotokea maishani. Inaweza kuwa ni matukio yenye kuumiza yamekuja kwa mkupuo kama misiba, hali zisizoleta dalili za afueni iwe ni mahusiano au uchumi, hali za kiugonjwa na kadhalika.

Magumu hutukuza misuli ya akili, hutukuza kuwaza kiutu uzima. Hili ndilo linalowasaidia watu wengi katika umri mdogo kuwa na uwezo mkubwa wa kukabiliana na maisha ambapo kumetokana na wao kupitia magumu na magumu hayo hayakuwadumaza bali yaliwasaidia kukua zaidi. Si rahisi mtu aliyepitia magumu na yakamsaidia kukomaa kushangazwa na hali ngumu za maisha zikitokea maana tayari anajua na uzoefu wa kupitia magumu ya awali. Watu imara hawatengenezeki kwa njia rahisi isipokuwa kwa darasa la kushinda changamoto na kukabiliana na kila gumu njiani.

Mtoto ambaye anaepushwa asipitie magumu au kujua uhalisia wa maisha mapema ni kumwandaa kutokuwa imara siku za baadaye. Atakapokuja kuishi na kukutana na magumu kwa mara ya kwanza lazima itampa wakati mgumu sana kukabiliana na hilo. Huenda wazazi wengi wanaogopa kuwaambia watoto wao juu ya ugumu katika kuyakabili maisha kwa kuona watakuwa wakiwaonea ila si kweli bali wanawapa wakati mgumu baadaye watakapopita katika magumu hayo. Magumu humfanya mtu akutane na ukweli wa maisha kuwa maisha ili ukue kiuzoefu lazima upite magumu mbalimbali yanayomjenga mtu kuwa imara na kuyaendesha maisha.

Uhalisia wa maisha ni kuwa mtu atapitia magumu katika siku za kuishi kwetu. Magumu yapo na yataendelea kuja kwa namna tofauti tofauti. Si kuyalaumu pale yanapokuwa zamu yake kujitokeza. Magumu hutuimarisha na kutukuza kuyaona mambo

NA  KOCHA  MWL.  JAPHET   MASATU , DAR  ES  SALAAAM , TANZANIA

WhatsApp + 255 716 924136 / + 255 755 400128  /   +  255 688  361 539


 

KUPOTEZA " TUMAINI " NI KITU KIBAYA SANA KATIKA MAISHA

Maisha yanaweza kukupitisha katika nyakati ngumu ambazo mbele yako huoni kama utatoka au kuna nafuu yoyote. Nyakati hizi ndizo zinazofanya wengine wasiamini kama lipo tumaini au njia ya kuvuka. Ni lugha ngumu mtu kukuelewa pale anapopitia magumu na unamwambia kuwa hayo magumu utashinda tu huku akiangalia hakuna dalili zozote za suluhisho. Kibinadamu si hali rahisi kushawishiwa kuwa mambo yatakaa sawa na yatapita. Hili ndilo ambalo watu wengine huamua kukatisha maisha yao kwa kuona hawaoni msaada unaoweza kuwatoa walipo.

Hali ya kukosa tumaini inaweza kumkuta mtu yeyote yule katika zama tuishizo. Mambo yanapobadilika ghafla na matarajio mbalimbali kupotea ni hali inayosababisha mtu ashuke hamasa ya kufanya vitu, changamoto zinapokuwa hazikomi, hali ngumu za kiuchumi, migogoro katika kazi au mahusiano, nyakati ngumu za masoko na biashara vinapokuja kwa pamoja kwa mtu mmoja si jambo jepesi la kuvumilika. Ni wengi utakuta wanapata hali ya kukosa hamasa, wanashuka ari ya kufanya kazi na mzigo unapowazidia basi tumaini la nafuu ya hali wapitiazo hufifia au hata kuzima kabisa. Inahitaji ustahimilivu, faraja na nguvu ya kutia moyo na watu wengine kipindi cha hali ngumu.

Mtu anapoanza kupoteza matumaini ni dalili za hatari ambapo asiposaidiwa ni rahisi kufanya maamuzi mabaya ya kimaisha. Hali ya kukosa tumaini huanza pale ambapo mtu huanza kukata tamaa kwa yale anayoyapitia. Huenda ni katika kila jaribio mtu anaona kushindwa na kuanguka. Kukata tamaa kunamsababisha mtu afadhaike na kupata hali ya kupata hatia, kuona hamasa haipo tena na kujawa na hali ya kukata tamaa kabisa ya kimaisha. Hali hizi huwatokea watu wengi wanaopitia hali za sonona katika maisha ambapo kutokana na hali mbalimbali walizoshindwa kuzikabili basi wakajikuta wanazidiwa na kupoteza tumaini.

Magumu katika maisha hayakosekani na si kuwa watu hawapitii magumu. Ikiwa kila mmoja atahadithia simulizi ya yale aloyapitia utakuja kuona unayoyapitia huenda ni madogo. Kinachotia moyo ni kuwa wapo ambao maisha yao ukiyatazama unaona la kwako unalopitia ni dogo na wakati mwingine maisha yao yanaweza kukutia moyo kuwa hupaswi kumbe kukata tamaa. Kila wasaa unapoona tumaini linafifia jipe wasaa wa kuona watu wengine wenye magumu zaidi wasivyokata tamaa wala mioyo yao kuinama.

Unaweza kupoteza kila kitu maishani na ukarejea tena katika kuyaishi maisha endapo hutapoteza “tumaini”. Watu wengi ambao wamepitia magumu, taabu na shida na wakainuka tena hawakupoteza tumaini. Waliweka tumaini kuwa licha magumu yote ambayo yamejitokeza bado wanaona ipo njia, hali zitabadilika na mbele kuna njia ya kutoka. Maisha huwa mapya pale ambapo kila unapopitia magumu hupotezi tumaini kwa kile unachokifanya, tumaini la kuishi na tumaini la kuona kila kitu kitakuwa sawa kadri muda unavyoenda.

Kuna nyakati ambazo nilipitia ngumu sana, niliona siwezi kuinuka tena, niliona ndo mwisho wa kile nilichokuwa nakitegemea ila ninashukuru kuwa nilibakiwa na hali ya kuwa na tumaini kuwa hali nayoipitia itapita. Hili limekuwa likinisaidia hata sasa kuwa kwa kila hali ambayo itatokea iwe ngumu, yenye misusuko mingi nachotakiwa kukitunza ni kuwa na tumaini kuwa mambo yataenda tu. Tumaini ni ukombozi mkubwa katika maisha tuishiyo duniani.

NA  KOCHA   MWL.  JAPHET  MASATU , DAR  ES    SALAAM

WhatsApp + 255 716924136 /   + 255 755 400128

 

Wednesday, July 21, 2021

BIASHARA YA GENGE : JINSI YA KUIENDESAHA NA KUFANIKIWA.

Rafiki yangu mpendwa,
Nimekuwa naamini na kusema hili mara kwa mara na nilirudie tena hapa, kukosa mtaji siyo sababu ya kushindwa kuingia kwenye biashara. Ni kisingizio tu.

Sasa visingizio vyote huwa ni vya uongo, kwa sababu vinaficha kile ambacho mtu hataki kukikabili.

Wengi wanaotumia kisingizio cha mtaji, hawapo tayari kuukabili ukweli kwamba ni wavivu, wazembe, wasio tayari kujitoa na wanaopenda mazoea. Ni vigumu sana mtu kukiri una tabia hizo, hivyo kisingizio cha mtaji au muda kinakuwa rahisi.

Kwa zama tunazoishi sasa, hakuna kinachoweza kumzuia mtu aliyejitoa kweli kuingia kwenye biashara. Siyo wazo, siyo mtaji na wala siyo muda.
Kinachomzuia mtu hakitoki nje, bali kipo ndani yake.
Na yule ambaye hana kizuizi cha ndani, anaweza kuyafanya makubwa mno.




Chukua mfano wa biashara ya genge la mahitaji muhimu ya kila siku kwenye familia.
Ni biashara yenye uhitaji, kwa sababu watu kila siku wanakula.
Ni biashara unayoweza kuanza kwa mtaji kidogo.
Ni biashara ambayo huhitaji kuwa na eneo la gharama kubwa kuifanyia.
Na ni biashara ambayo haina vitu vingi, hivyo unaweza kuisimamia vizuri.

Hii ni biashara ambayo mtu ambaye hana shughuli nyingine ya kufanya anaweza kuianzisha, akaiendesha vizuri na ikawa sehemu ya yeye kupiga hatua na kuelekea kwenye biashara kubwa zaidi.

Unapochagua kufanya biashara kama hii, unapaswa kuifanya kwa tofauti, ili ikue na kuweza kuzalisha biashara nyingine kubwa zaidi.

Huenda unawajua wauza genge ambao miaka yote unawaona wakiwa pale pale. Siyo kwamba biashara hailipi, ila wanaifanya kwa viwango vya chini.

Kwenye makala hii unakwenda kujifunza jinsi ya kuifanya biashara ya genge kwa viwango vya juu sana na ikawa na manufaa makubwa kwako.

Kabla hatujaingia kwenye ushauri, tusome aliyotuandikia msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili.

“Nahitaji kufungua genge la matunda na mboga mboga napenda kuelimishwa namna ya kuboresha iliniweze kukuza biashara yangu na wateja wavutiwe na huduma yangu.” – Hussein B. M.

I. MAONO MAKUBWA.
Anza kidogo lakini fikiri kwa ukubwa. Japo unafanya biashara ya genge, kwenye fikra zako usione genge, bali ona biashara kubwa kabisa.
Ona ukiwa na maduka mengi ya kuuza mahitaji hayo ya msingi na ona ukifanya kwa kiwango kikubwa zaidi.
Ni maono makubwa unayokuwa nayo ndiyo yanakusukuma kupiga hatua kubwa pia.
Tunapata kile tunachoona, hivyo kuwa na maono makubwa na jisukume kuyafikia.

II. BIDHAA BORA.
Kwenye biashara ya genge wateja wanaangalia vitu vikuu viwili, bidhaa bora na kwa bei nafuu. Pambana kuwapatia wateja vitu hivyo viwili na watakuwa wako kwa muda mrefu.
Chagua bidhaa zilizo bora kabisa ndiyo uweke kwenye biashara yako.
Jua maeneo unayoweza kupata bidhaa hiyo bora kwa bei nafuu ili pia uweze kuwauzia wateja wako kwa bei nzuri.
Jiwekee viwango vya ubora wa bidhaa utakazouza ili wateja waweze kujenga imani kwako na kwa biashara yako.

III. ENEO ZURI.
Biashara yako inapaswa kuwa eneo ambalo ni rahisi kuwafikia wateja wako na hata wateja kuifikia pia.
Kwa kuwa unachouza ni mahitaji muhimu ya maisha ya kila siku, biashara itafanya vizuri pale inapokuwa eneo lenye watu wengi.
Lakini pia mazingira ya eneo lako la biashara yanapaswa kuwa safi na mazuri, yamfanye mteja aiamini na kuithamini biashara yako.
Wengi wanaofanya biashara ya genge hawaweki maeneo yao ya biashara kwenye mwonekano mzuri, ukifanyia kazi hilo unajitofautisha kabisa na wengine.

IV. HUDUMA BORA KWA WATEJA.
Wahudumie vizuri saba wateja wako ili waweze kurudi tena na tena. Wasikilize kwa umakini na wajali pia. Jua mahitaji yao na uwatimizie.
Usiuze tu na kuishia hapo, jenga mahusiano mazuri na wateja wako na hayo yataiwezesha biashara kukua zaidi.
Pale wateja wanapopata huduma nzuri, wanaendelea kuja na wanawaleta wengine pia.

V. KUWEKA MAFUNGU.
Unayajua mahitaji ya wateja wako, unaweza kutengeneza mafungu ya vitu vinavyonunuliwa kwa pamoja na kisha kumshawishi mteja anunue kama fungu badala ya kununua kimoja kimoja.
Kumsukuma kuchukua hatua, hakikisha bei ya fungu inakuwa na unafuu kuliko mteja akinunua kimoja kimoja.
Njia hii itakuwezesha kuuza zaidi kwa wateja ambao tayari unao, ambao ni wateja wazuri tayari.

VI. KUWAFIKIA WATEJA.
Usisubiri tu wateja waje, badala yake watuate kule walipo. Watu sasa wametingwa na mambo mengi wanaweza kusahau kabisa hata uwepo wako.
Hivyo watembelee wateja wako maeneo walipo na kuwashawishi kuja kununua.
Hapa pia unaweza kutoa huduma ya mteja kuagiza na kupelekewa bidhaa zake.
Na kama umeziweka bidhaa kwa mafungu na bidhaa zako ni bora, mteja anaagiza na kupelekewa, akijua anapata anachotaka na ambacho ni bora pia.

VII. KUWASILIANA NA WATEJA.
Omba mawasiliano ya wateja wako na wasiliana nao mara kwa mara.
Unajua wateja wa genge wanapanga mahitaji yao ya siku asubuhi. Unaweza kuwatumia ujumbe asubuhi kuwasalimia na kuwaomba oda pia. Mteja anapopata ujumbe wako, anakufikiria kwa muda mrefu na hilo linamshawishi kuja kununua kwako.
Tumia kila sababu na ushawishi kupata mawasiliano ya wateja wako na wasiliana nao kwa njia ambayo siyo ya usumbufu kwako.

VIII. KUWEKA AKIBA.
Kwa lengo lako la kufika kwenye mafanikio makubwa kibiashara, unapaswa kuweka akiba kwenye kila faida unayoingiza kwenye biashara yako.
Wakati biashara inafanya vizuri, usibweteke na kuona mambo yataenda hivyo wakati wote.
Weka akiba ambayo itakusaidia wakati biashara haiendi vizuri.
Akiba hiyo ndiyo itakusaidia kwenye ukuaji wa biashara yako.

IX. KUKUZA BIASHARA.
Kwa kuwa una maono makubwa ya biashara yako, kila wakati angalia fursa za ukuaji zaidi.
Kila wakati piga hatua kuikuza biashara yako zaidi.

X. KUJIFUNZA KILA SIKU.
Kujifunza kila siku ni hitaji muhimu la ukuaji wa biashara yako.
Kila siku hakikisha unajifunza kitu kwenye kuikuza biashara yako.
Biashara inahitaji ubobezi maeneo mbalimbali kama masoko, mauzo, fedha, ushawishi na uongozi.
Soma vitabu mbalimbali vya biashara yako na  unayojifunza yafanyie kazi.

Saturday, July 10, 2021

MITANDAO YA KIJAMII INAELEKEA KUWAGAWA WATU KATIKA MAKUNDI HAYA.

Umakini wako ndiyo utajiri wako, kama utaweza kuweka umakini wako wote kwenye kile unachofanya, kwa hakika utaweza kuongeza kipato chako maradufu.

Mtaalam Mmoja Aliwahi Kusema Hivii.Siku zijazo, kutakuwa na makundi makuu mawili ya watu duniani.

Kundi la kwanza litakuwa la wale ambao wanaruhusu umakini wao kudhibitiwa na watu wengine, ambao wanaruhusu kila aina ya usumbufu kuwaingia. Kundi hili litakuwa na watu wengi sana, na mara zote watakuwa wamevurugwa na wasiweze kufanya makubwa kwenye maisha yao.

Kundi la pili litakuwa la wale ambao wanadhibiti umakini wao na kutoruhusu usumbufu wa aina yoyote ile kuwavuruga. Kundi hili litakuwa na watu wachache sana, na hawa ndiyo watakaoweza kufanya makubwa na kufanikiwa sana.”

Swali kwako, je kwa hali inavyokwenda sasa kwenye maisha yako, unajiona ukielekea kwenye kundi lipi kati ya hayo mawili?

Na je ungependa kuwa kwenye kundi lipi? Kama ungependa kuwa kwenye kundi la kwanza huna cha kufanya, endelea kufuata mkumbo na kila aina ya kelele.

Lakini kama ungependa kuwa kwenye kundi la pili, basi yale yote ambayo umejifunza kwenye kitabu cha juma hili yafanyie kazi.

Jua usumbufu wako wa ndani na wa nje na tenga muda wa kufanya yale muhimu na kuepukana na usumbufu.

Maarifa tayari unayo, kama hutachukua hatua huna wa kumlaumu, utakuwa umechagua wewe mwenyewe.

Tuko kwenye vita, adui mkuu anajua yuko vitani ila wanaolengwa hawajui.

Hivyo unapaswa kuwa na maandalizi mazuri ya kupambana na vita hii ili uweze kutoka salama na siyo kuwa mfungwa.


KAMA UNATAKA MAFANIKIO MAKUBWA , USIWE " FAIR " KWENYE MAENEO HAYA KUMI ( 10 ).

Rafiki yangu mpendwa,
Kuna vitu waliofanikiwa sana wanavijua, lakini huwa hawaviweki wazi.

Wanafanya hivyo kwa sababu jamii huwa haielewi vitu vingi kuhusu mafanikio, na hivyo huishia kuwashambulia waliofanikiwa pale wanapojaribu kuwa wakweli.

Mara ngapi umesikia masikini wakiwasema matajiri kwamba ni freemason au wamepata utajiri wao kwa njia za giza?
Umewahi kumwona tajiri akibishana na masikini juu ya hilo?

Jibu ni hapana, tajiri anajua masikini hawezi kuelewa na hata kuamini mengi yaliyomsaidia yeye, hivyo anamuacha aamini anachochagua kuamini.

Leo nakupa siri kubwa, nakupa ukweli mchungu ambao ukiweza kuupokea na kuuishi, utaweza kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako.

Ukweli huo ni kama unataka mafanikio makubwa, basi usiwe ‘fair’.
Neno fair yaani usawa limekuwa linatumika sana.
Wengi wamekuwa wanalalamika kwamba maisha hayapo fair, pamoja na juhudi wanazoweka bado hawapati wanachotaka.

Leo nakwenda kukushirikisha maeneo 10 ambayo upaswi kuwa ‘fair’ kama unayataka mafanikio makubwa.
Kwenye maeneo hayo, unapaswa kuwa tofauti kabisa na wengine walivyo ili uweze kupata matokeo ya tofauti.




Kama unataka mafanikio makubwa, usiwe fair kwenye maeneo haya 10.

(1). USIWE  "FAIR"   KWENYE  KAZI.
Watu wengi wanafanya kazi kwa mazoea na kwa viwango vya chini sana. Wewe nenda kinyume nao, fanya kazi kwa juhudi kubwa na kwa viwango vya juu sana.
Anza kwa kufanya kazi muda mrefu kuliko wengine.
Kama wanaanza kazi saa mbili asubuhi na kumaliza saa 10 jioni, wewe anza saa moja asubuhi na kumaliza saa 12 jioni.
Kila siku weka masaa 2 mpaka 4 ya ziada kwenye kazi unayofanya.
Na unapofanya kazi  weka umakini wako wote kwenye kile unachofanya na usiruhusu usumbufu wowote ukuvuruge.

( 2 ). USIWE  "FAIR"  KWENYE  MUDA.
Watu wengi huwa wanachezea muda kama vile ni kitu ambacho hakina ukomo.
Lakini muda una ukomo, kuna masaa 24 tu kwenye siku, ukishayatumia huwezi kupata tena mengine.
Kuwa bahili sana wa muda wako, usikubali upotee hovyo kwa mambo yasiyo na tija.
Kila siku unayoianza pangilia muda wako, weka vipaumbele vyako vya siku na vifuate hivyo.
Kuwa na orodha ya mambo utakayoyafanya kwenye siku yako na ifuate hiyo.
Usiruhusu usumbufu au mahitaji ya wengine yaingilie ratiba yako muhimu ya siku.

( 3 ). USIWE  "FAIR"  KWENYE  FEDHA.
Watu wengi wakipata fedha huwa wanakimbilia kuzitumia mpaka ziishe na hata zikiisha hawaishii hapo, badala yake wanakopa ili waendelee kutumia zaidi.
Wewe usiwe hivyo, unapopata fedha yoyote ile, tenga kwanza akiba kabla hujatumia. Usitumue kisha inayobaki ndiyo uweke akiba, fedha huwa haibaki. Badala yake weka akiba kwanza kisha inayobaki ndiyo utumie.
Na akiba unayoweka, iwekeze mahali inapozalisha na kukua zaidi. Hiyo ndiyo njia ya uhakika ya kuondoka kwenye umasikini na kwenda kwenye utajiri.

(4). USIWE  " FAIR "  KWENYE  KUSUDI.
Watu wengi wanaishi maisha ya bendera kufuata upepo, hawalijui kusudi la maisha yao na hivyo ni rahisi kushawishiwa na chochote kinachopita mbele yao.
Wewe usiwe na maisha ya aina hii, pambana ulijua kusudi la maisha yako na kuliishi kila siku.
Jua kwa nini uko hapa duniani, maisha yako yanapaswa kuacha alama gani na jipe wajibu mkubwa unaokusukuma kuchukua hatua kila siku.
Ukiwa na kusudi unakuwa na msimamo.

( 5 ). USIWE " FAIR " KWENYE   NDOTO.
Watu wengi hawana ndoto kubwa, wanaishi maisha ya mazoea, wanafanya shughuli zao, wanapata pesa ya kula na wanaridhika na hayo.
Wewe usiwe mtu wa kuridhika na mambo madogo unayopata sasa.
Kuwa na ndoto kubwa sana, ndoto ambazo wengine wakizisikia wanaona kama umechanganyikiwa na wanakuambia haiwezekani.
Ni ndoto kubwa unazoziamini bila ya shaka zinazokusukuma kufanya makubwa zaidi kwenye maisha yako.

( 6 ). USIWE " FAIR "  KWENYE  KUJIFUNZA.
Watu wengi wakishahitimu shule, hawajifunzi tena vitu vipya wala kusoma vitabu. Watu hawasomi kabisa vitabu, wakiamini hakuna kipya wanachoweza kujifunza, tayari wanajua kila kitu.
Wewr usiwe hivyo, kuwa mtu wa kujifunza vitu vipya kila siku. Kuwa mtu wa kusoma vitabu kila siku.
Hakikisha kila mwezi unasoma angalau kitabu kimoja na kwa kila kitabu unachosoma chukua hatua za kuyabadili maisha yako.
Hilo pekee linatosha kukupa fursa nyingi na kukuwezesha kupiga hatua kuliko wengine.

(7).USIWE  " FAIR "  KWENYE  MAHUSIANO.
Walio wengi wanazungukwa na watu hasi, watu waliokata tamaa na wanaowakatisha tamaa pia. Mahusiano yao mengi yanakuwa kikwazo kwao kupiga hatua.
Wewe kuwa makini sana na mahusiano yote uliyonayo, hakikisha yanakuwa mahusiano bora na yanayokusukuma uwe bora zaidi.
Waepuke watu hasi na waliokata tamaa kama ukomo, usijenge ukaribu na watu wa aina hiyo, kwani watakuambukiza waliyonayo.
Ulivyo ni wastani wa watu watano wanaokuzunguka, chagua watano bora ambao watakusukuma upige hatua zaidi.

( 8). USIWE " FAIR "  KWENYE  KUJIAMINI.
Watu wengi hawajiamini, wanaweza kuwa na ndoto kubwa ila wanapowaambia wengine na wakawakatisha tamaa, wanawasikiliza na kukubaliana nao.
Ndiyo maana kundi kubwa la watu kwenye jamii hawawi na maisha wanayoyataka, maana hawajiamini kiasi cha kuwashinda wale wanaowakatisha tamaa.
Wewe jiamini kupitiliza, amini ndoto kubwa ulizonazo utaweza kuzifikia bila ya kujali unaanzia wapi sasa.
Hata kama wengine wanakuambia haiwezekani, hata kama wanakuonesha na mifano kabisa, usiwaamini zaidi ya unavyojiamini wewe. Jifunze yote muhimu na endelea kusimama kwenye ndoto zako kubwa.

( 9 ). USIWE  " FAIR " KWENYE  UNG"ANG"ANIZI.
Ili ufanikiwe lazima uwe king’ang’anizi sana, ujitoe kweli kweli na ukomae mpaka upate kile unachotaka.
Utakutana na magumu, vikwazo na kushindwa, lakini usiruhush hayo kuwa mwisho wa safari yako.
Jipe kiapo kwamba utapata kile unachotaka au utakufa ukiwa unakipambania, hakuna mbadala wa hilo.

( 10 ). USIWE " FAIR " KWENYE  KUTOA  KAFARA.
Ili upate kile ambacho hujawahi kupata, lazima uwe tayari kupoteza kile ambacho tayari unacho sasa. Kuna vitu vizuri unavyo sasa lakini ni kikwazo kwako kupata mafanikio makubwa unayotaka.
Wengi wanataka mafanikio lakini hawapo tayari kutoa kafara, kuachana na vile vizuri walivyonavyo sasa ili kupata vilivyo bora zaidi.
Ukiweza kuvuka hilo, utaweza kupata makubwa.

Ukiondoa usawa kwenye maeneo haya 10 muhimu, utakuwa na maisha ya tofauti kabisa na utaweza kufanya makubwa sana.
Lakini utakapokua na maisha ya tofauti wengi watakushambulia, hivyo utakuwa kama mpweke katikati ya kundi kubwa la watu.

Nakukaribisha ujiunge kwenye " DARASA  ONLINE " UJIFUNZE  MENGI  USIYOYAJUA.

Usikubali tena kuendelea kuwa fair kwenye mambo yanayokurudisha nyuma.
Chagua kushika hatamu ya maisha yako ili uweze kufanya makubwa.

Ndimi  rafiki yako  mpendwa,
KOCHA  MWL.  JAPHET   MASATU , DAR  ES SALAAM, TANZANIAW

 

WASILIANA  NAMI   SASA  KWA

 

 ( WhatsApp + 255 716 924136    )  + 255 755 400 128