Zamani
za kale, wakati binadamu wanajifunza kuwa na makazi ya kudumu, watu
walijenga nyumba zao bila ya misingi. Lakini walijifunza somo moja kubwa
sana, kwamba kipindi cha dhoruba mbalimbali kama mvua, kimbunga na
tetemeko, nyumba hizo zilibomoka haraka sana. Hivyo wakajifunza kwamba
ili nyumba iwe imara na idumu, basi inapaswa kuanza kujengwa kwa msingi
imara. Na mpaka sasa wahandisi wote wanajua kwamba nyumba imara inaanza
na msingi imara. Na kadiri nyumba inavyopaswa kuwa kubwa, ndivyo msingi
unavyopaswa kuwa imara zaidi. Mfano, msingi wa nyumba ya kawaida hauwezi
kufanana na msingi wa nyumba ya ghorofa.
Hivi
pia ndivyo ilivyo kwenye maisha yetu. Kwenye maisha tunakutana na
dhoruba mbalimbali. Kuna kuugua, kuvunjika kwa mahusiano, kufukuzwa
kazi, kufilisika kibiashara, kufa kwa watu wetu wa karibu na hata sisi
wenyewe kufa. Dhoruba hizi huwa zina madhara tofauti kwa watu tofauti.
Kuna watu wanapokutana na dhoruba za maisha zinawayumbisha sana na
kuvuruga kabisa maisha yao. Lakini wapo wengine ambao wanakutana na
dhoruba kali za maisha lakini maisha yao hayayumbi.
Kinachowatofautisha
watu hao wa aina mbili ni msingi ambao wamejijengea. Kwenye nyumba
tumeona msingi wa kuanza, kwenye maisha yetu, msingi muhimu sana ni
falsafa ambayo mtu anakuwa nayo juu ya maisha. Falsafa unayokuwa nayo,
ndiyo inapima kiasi gani dhoruba unazokutana nazo kwenye maisha. Kama
huna falsafa unayoiishi na kuisimamia, dhoruba ndogo kama biashara
kufilisika inatosha kukuvuruga kabisa. Lakini kama una falsafa
unayoiishi, dhoruba kubwa kama kuhukumiwa kifo, inakufanya uwe imara na
kuyafurahia maisha yako mpaka dakika ya mwisho.
Hii
ni kukuambia wewe rafiki yangu kwamba unapaswa kuwa na falsafa ya
maisha yako, falsafa ambayo unaitumia kama msingi wako wa kufanya
maamuzi na kuendesha maisha yako. Falsafa ambayo itakuwezesha
kukabiliana na dhoruba za maisha, ambazo kadiri siku zinavyokwenda
zinazidi kuwa kali zaidi.
Dini
zilipaswa kuwa msingi wetu kwenye changamoto hizi za maisha, lakini
dini nyingi zimesahau jukumu hilo, na badala yake zimekuwa sehemu ya
kuwapa watu hofu zaidi ya maisha kuliko matumaini. Dini zimekuwa
zinaweka nguvu kubwa kwenye kuwaandaa watu kwa maisha yajayo (baada ya
kifo) kuliko maisha waliyonayo sasa. Japokuwa unahitaji maandalizi ya
maisha yajayo (kulingana na imani yako), lakini kitu muhimu sana
unachohitaji ni maandalizi ya maisha unayoishi sasa, maana hayo ndiyo
yanayokujenga au kukubomoa.
Kwa
kuwa dini zimeshindwa kufanya kazi ambayo tulitegemea zifanye,
kutujenga na kutuandaa kwa maisha ya sasa na kuweza kukabiliana na
dhoruba tunazokutana nazo kwenye maisha yetu ya kila siku, basi linabaki
kuwa jukumu la kila mmoja wetu kuwa na falsafa ya maisha, ambayo
ataitumia kuendesha maisha yake.
Kukaa
chini na kutengeneza falsafa yako mwenyewe ni kazi kubwa, inakuhitaji
ujaribu na kukosea vitu vingi, kitu ambacho huna muda wala nguvu za
kufanya, maana changamoto zinazokukabili ni nyingi.
Hivyo suluhisho ni wewe kujifunza falsafa zilizopo, na kisha kuchagua ile ambayo itakufaa wewe katika kuendesha maisha yako.
Zipo falsafa nyingi ambazo zinatokana na wanafalsafa mbalimbali kama Socrates, Plato, Aristotle, Epicurus, Zeno na wengineo.