Saturday, September 22, 2018

KILA MTU APAMBANE NA HALI YAKE,USINUNUE MATATAIZO YA WATU.

Chukua mfano una ndugu wa karibu au mtoto ambaye bado hajaweza kutengeneza maisha yake vizuri, lakini wewe maisha yako yameshakaa vizuri. Yeye hana kazi na ni mlevi. Hivyo unaamua kumsaidia awe na kipato, kwa sababu maisha yake siyo mazuri. Unampa mtaji wa kuanzisha biashara, anatumia vibaya na biashara inakufa. Unaona kwa kuwa una uwezo, basi unaweza kuwa unampa fedha ya kujikimu, lakini ukimpa fedha anaenda kulewa. Unakwama, usipompa fedha maisha yake yanakuwa magumu na unaonekana umemtenga ndugu yako, ukimpa anaenda kulewa na kuzitumia vibaya.

Wawezeshe watu kutatua matatizo yao wenyewe, na usisukumwe kufanya vitu kwa sababu unataka kuonekana una roho nzuri. Wale utakaowawezesha kutatua matatizo yao, utawasaidia hata wakati wewe haupo. Ila wale unaobeba matatizo yao, utawaandaa kuanguka vibaya pale ambapo wewe hutakuwepo. Na nikukumbushe tu, haijalishi unampenda mtu kiasi gani, hutakuwa naye kwa maisha yako yote, hivyo mpende kwa kumfanya aweze kutatua matatizo yake mwenyewe.

Katika kukazana kwetu kuwasaidia wengine, hasa wale wa karibu kwetu, watoto, wenza, ndugu tuliozaliwa nao, tumekuwa tunakazana kuwaibia matatizo yao. Tunayachukua kabisa matatizo yao na kuyafanyia kazi na wao wanabaki hawana cha kufanya.



Hii ni njia mbovu sana ya kutaka kumsaidia mtu, kwa sababu unakuwa humsaidii, badala yake unamsababishia matatizo zaidi. Kwa sababu unapomchukulia matatizo yake, anabaki hana cha kufanya, hivyo anaenda kutengeneza matatizo zaidi.

Kwa sababu ukikimbilia kuyabeba ili uonekane una roho nzuri, utaishia kumharibu zaidi yule mwenye matatizo. Kwa sababu maisha yetu yanatoa maana kwenye matatizo na changamoto tunazokutana nazo mara kwa mara na kuzitatua.

Na  Mwl  Japhet  Masatu , Dar  es  salaam , Tanzania,  Afrika Ya  Mashariki ---Mwl  wa  Maisha Na  Mafanikio, Mshauri, Public Speaker(MC), Mwandishi, Mjasiriamali /
Tuwasiliane kwa :+ 255 755 400 128 / + 255 716 924136(WhatsApp ).  EMAIL: japhetmasatu@gmail.com

Friday, September 21, 2018

JE, WAIJUA AKAUNTI YA FEDHA YA SAIKOLOJIA ?

Unahitaji kujizoesha kifikra na kisaikolojia kuwa na fedha nyingi, hata kama bado hujazishika kwenye mikono yako au kuwa nazo kwenye akaunti yako ya benki. Na unaweza kuanza kwa kufikiria mara kumi ya kipato unachopata sasa, kisha kufikiria kipato hicho mara kwa mara, kukiwekea mipango na kuweka lengo lako la kipato liwe ni kukua kufikia mara kumi ya kipato chako cha sasa. Kwa njia hii utaongeza kiwango chako cha fedha kisaikolojia.

 Watu wengi wanajua aina moja ya akaunti ya kifedha, ambayo ni akaunti ya benki, au akiba na uwekezaji ambao wamekuwa wamefanya. Hivyo ukitaka kuangalia utajiri wa mtu, unaangalia ni kiasi gani cha fedha anacho kwenye akaunti zake za benki na uwekezaji kiasi gani amefanya.

 Aina ya pili ya akaunti ya kifedha, ukiacha akaunti ya benki, ni akaunti ya fedha ya kisaikolojia. Kila mmoja wetu, ana kiwango chake cha kifedha kwenye fikra zake, ambacho ndiyo ameshajiambia anapaswa kupata kiwango hicho. Yaani kila mmoja wetu, kuna kiwango chake cha fedha, ambacho ameshakiweka kwenye fikra na mawazo yake, na akishapata kiwango hicho basi akili yake inatulia na hakazani tena kupata fedha zaidi.

Waangalie watu wote ambao wamepata fedha nyingi kwa mkupuo, kiasi kikubwa cha fedha ambacho hawajawahi kukishika kwenye maisha yao. Waangalie watu ambao wameshinda bahati nasibu, waangalie watu ambao wamerithi mali, waangalie watu ambao wamepokea mafao. Wengi haiwachukui muda wanakuwa wameshapoteza fedha nyingi walizopata na kurudi kwenye maisha yao ya kawaida.
Wanakuwa wamepata fedha nyingi kwenye akaunti ya benki, lakini akaunti yao ya kisaikolojia inasoma kiwango cha chini. Hivyo wanaacha kufikiria kabisa kuhusu fedha, wanaanza kupoteza fedha, mpaka zinapofika kwenye kile kiwango chao cha kisaikolojia ndiyo wanastuka na kuanza kufikiria kuhusu fedha.

 Pia unaweza kufikiria mara 100, mara 1000 na hata zaidi ya kipato unachopata sasa. Fikra zote hizo zitaiandaa akili yako kupokea fedha zaidi na kuweza kutulia na fedha zaidi unazopata. Unapofikiria mara elfu moja ya kipato unachopata sasa, ongezeko kidogo halitakusumbua kama linavyokusumbua sasa.


Na  Mwl  Japhet  Masatu , Dar  es  salaam , Tanzania,  Afrika Ya  Mashariki ---Mwl  wa  Maisha Na  Mafanikio, Mshauri, Public Speaker(MC), Mwandishi, Mjasiriamali /
Tuwasiliane kwa :+ 255 755 400 128 / + 255 716 924136(WhatsApp ).  EMAIL: japhetmasatu@gmail.com

Sunday, September 16, 2018

JE, WAJUA NJIA ZA KUONGEZA THAMANI YA MAISHA YA WATEJA WAKO ?? JIFUNZE HAPA .

Wateja wako wanapokaa na wewe kwa muda mrefu ndivyo unavyonufaika zaidi. Hivyo unahitaji kuweka juhudi kuhakikisha wateja wanabaki na wewe kwa muda mrefu. Yafuatayo ni mambo muhimu ya kuzingatia ili wateja wakae na wewe kwa muda mrefu.

  1. Toa huduma bora sana kwa wateja wako, ambazo hawawezi kuzipata sehemu nyingine yoyote ila kwako tu.
  2. Kutengeneza mahusiano mazuri na wateja wako, wafanye wateja kuwa rafiki kwako na kwa biashara yako, waone siyo tu wanakuja kununua, bali wanakuja kwa rafiki yao, anayewajali na kuwapa kile kilicho sahihi kwao.
  3. Weka mbele maslahi ya wateja wako na siyo faida unayotaka kupata.
  4. Waelimishe wateja wako, washauri vizuri, hata kama utapoteza mauzo, lakini hilo litawajengea imani zaidi na hivyo kuendelea kununua zaidi.
  5. Wafanye wateja wako kuwa mashabiki wa biashara yako.
Zipo hatua saba ambazo wateja wanapitia mpaka kufikia ngazi ya ushabiki.

Hatua ya kwanza ni wapitaji tu, wanaisikia au kiona biashara yako lakini hawajawahi kuuliza chochote.

Hatua ya pili ni wateja tarajiwa, wamesikia na wamefuatilia kutaka kujua zaidi kuhusu biashara yako.

Hatua ya tatu ni wanunuaji, hapa wamejua, wakafuatilia na wakajaribu kununua kile unachouza.

Hatua ya nne ni wateja, hapa mtu amejaribu kununua kwa mara ya kwanza, na amerudi tena kununua. Mtu kununua mara moja haimfanyi kuwa mteja, na wala haikufanyi wewe kuwa mjanja. Ni mpaka mtu atakaporudi tena kununua ndiyo utajua umefanya kazi nzuri.

Hatua ya tano ni mwanachama, hapa mteja anakuwa mnunuaji wa mara kwa mara na unaweza kumpa manufaa ya kadiri anavyonunua. Labda akifika kiwango fulani anapata zawadi, au akinunua mara tano, ya sita anapata bure. Hapa mwanachama anakuwa na kielelezo cha kuonesha idadi ya manunuzi yake.

Hatua ya sita ni mtetezi wa biashara yako, hapa mteja anakuwa tayari kuwaambia watu wengine kuhusu biashara yako, anatoa shuhuda kwa wengine na hasiti kuwaalika wengi waje kununua.
Hatua ya saba ni shabiki kindakindaki, hawa ni wale wateja ambao hawaambiwi chochote kuhusu biashara yako, yaani wao wameshachukulia biashara yako kama sehemu ya maisha yako. Hawa ni wateja ambao wanaiongelea biashara yako muda wote, na wakikutana na mtu ambaye hanunui kwako wanaona anakosa kitu kikubwa sana.
Katika kuboresha thamani ya maisha ya wateja wako, kazana kuwapandisha wateja wako ngazi mpaka wafikie kiwango cha watetezi na mashabiki wa biashara yako.
 
Na  Mwl  Japhet  Masatu , Dar  es  salaam , Tanzania,  Afrika Ya  Mashariki ---Mwl  wa  Maisha Na  Mafanikio, Mshauri, Public Speaker(MC), Mwandishi, Mjasiriamali /
Tuwasiliane kwa :+ 255 755 400 128 / + 255 716 924136(WhatsApp ).  EMAIL: japhetmasatu@gmail.com

JE, WAJUA AINA ZA GHARAMA ZA KUWAPATA WATEJA WA BIASHARA YAKO ?? JIFUNZE HAPA.

Kuna aina mbili za gharama ya kupata wateja wa biashara yako.

Aina ya kwanza ni GHARAMA ZINAZORUHUSIWA za kupata mteja. Hapa unatumia gharama ambazo mteja akinunua mara moja basi gharama ile inarudi. Chukua mfano umetengeneza tangazo ambalo limekugharimu tsh 100,000/= na tangazo hilo limewafikia watu 1000. Katika hao 1000 ndiyo wamenunua. Na kwa kila unayenunua unapata faida ya shilingi elfu moja. Inamaana kwa watu 100, faida unayopata ni tsh 100,000/= sawa sawa na gharama ulizoingia kutoa tangazo. Hivyo hiyo ni gharama inayoruhusiwa ya kupata mteja. Kama utaandaa tangazo kwa gharama kubwa kuliko faida unayopata, hiyo sasa siyo GHARAMA INAYORUHUSIWA kupata wateja.

Aina ya pili ni GHARAMA UWEKEZAJI KWA WATEJA. Hapa unatumia gharama kubwa, ambayo inakuletea wateja, lakini manunuzi ya mwanzo ya mteja hayalipi gharama hiyo. Lakini kwa kuwa mteja ataendelea kununua, basi huko mbeleni ile gharama inarudi. Hivyo hapa unakuwa umewekeza kwa mteja, ukijua kwamba atafanya biashara na wewe kwa muda mrefu na gharama zako zitarudi.
Kwa biashara ndogo, ni vyema kutumia gharama zinazoruhusiwa, kwa biashara kubwa, ambazo zina rasilimali nyingi, zinaweza kuwekeza kwa wateja na baadaye zikanufaika zaidi. Usikimbilie kununua wateja kabla hujajua ni gharama kiasi gani unaingia na kama zinalipwa na idadi ya wateja watakaonunua.

Na  Mwl  Japhet  Masatu , Dar  es  salaam , Tanzania,  Afrika Ya  Mashariki ---Mwl  wa  Maisha Na  Mafanikio, Mshauri, Public Speaker(MC), Mwandishi, Mjasiriamali /
Tuwasiliane kwa :+ 255 755 400 128 / + 255 716 924136(WhatsApp ).  EMAIL: japhetmasatu@gmail.com

JE, WAJUA JINSI YA KUNUNUA WATEJA WA BIASHARA YAKO ??? JIFUNZE HAPA !!

Kazi kubwa ya kila biashara ni kununua wateja wa biashara hiyo. Sasa ili biashara iweze kufanikiwa, lazima iweze kununua wateja bora kwa gharama ambazo siyo kubwa. Kitu ambacho wafanyabiashara wengi siyo tu hawakifanyii kazi, ila hata hawakijui.
Inawezekana upo kwenye biashara, lakini hujui kama biashara yako inanunua wateja. Sasa nikuambie tu, kila biashara huwa inatumia fedha kununua wateja, na biashara yako pia inatumia fedha kununua wateja.
Labda nikuulize swali, biashara yako inatumia gharama kiasi gani kununua wateja? Na je gharama ambazo biashara yako inatumia kununua wateja zinarudi? Najua maswali haya yanaweza kukuacha ukiwa umeduwaa kwa sababu hujawahi kufikiria kuhusu kununua wateja.
Sasa kwenye kitabu nilichosoma ; BUYING CUSTOMERS, kilichoandikwa na kocha wa biashara Bradley Sugars, mwandishi ametushirikisha njia sahihi za kununua wateja bora wa biashara zetu na kwa gharama nafuu ambazo biashara inaweza kumudu.
Kwa kuanza, kila biashara huwa inanunua wateja. Kila hatua unayotumia kuwafanya wateja wajue kuhusu uwepo wa biashara yako, ni kununua wateja. Kama umewahi kutangaza biashara yako, umewahi kuandaa vipeperushi, kama umetengeneza bango, au kuuza vitu kwa pamoja kwa bei ya punguzo, kama umewahi kupunguza bei ili mteja anunue, au kutoa zawadi kwa mteja anayenunua. Kama umewahi kutoa usafiri kwa mteja, au kumpelekea alichonunua, au kumwomba mteja wako akuletee wateja zaidi. Zote hizo ni harakati za kununua wateja unazotumia kwenye biashara yako.
Sasa kuna ambazo zinakuletea wateja bora, nyingine hazikuletei wateja wazuri. Nyingine ni za gharama kubwa kwako, nyingine ni za gharama ndogo.
Kupitia kitabu cha BUYING CUSTOMERS, tunakwenda kujifunza jinsi ya kununua wateja bora kwa gharama nafuu kwenye biashara zetu.

 Na  Mwl  Japhet  Masatu , Dar  es  salaam , Tanzania,  Afrika Ya  Mashariki ---Mwl  wa  Maisha Na  Mafanikio, Mshauri, Public Speaker(MC), Mwandishi, Mjasiriamali /
Tuwasiliane kwa :+ 255 755 400 128 / + 255 716 924136(WhatsApp ).  EMAIL: japhetmasatu@gmail.com

JE, WAJUA NJIA ZA KUTENGEHEZA FAIDA KATIKA BIASHARA YAKO ? JIFUNZE HAPA ,

 Njia hizi zinategemeana na zinaenda kama ngazi, hivyo ili kunufaika lazima uzifanyie kazi kwa pamoja.

Njia ya kwanza ni kuongeza idadi ya watu wanaoijua biashara yako. Na hapa ndipo zoezi zima la kununua wateja linapofanya kazi. Kadiri watu wengi wanavyojua kuhusu biashara yako, ndivyo inakuwa rahisi kwako kuwageuza watu hao kuwa wateja. Kama watu 1000 ndiyo wanaojua kuhusu uwepo wako, ukiongeza watu 100 unakuwa umeenda mbele zaidi.

Njia ya pili ni kuwageuza wanaojua kuhusu biashara yako kuwa wateja halisi. Mtu kujua biashara yako haimaanishi ndiyo mteja wa biashara hiyo. Mteja ni yule ambaye ametoa fedha na kununua kitu kwenye biashara yako. ili kuongeza wateja wa biashara yako, unahitaji kuwashawishi wale wanaojua kuhusu biashara yako wanunue kile unachouza.

Njia ya tatu ni kuwafanya wateja warudi kununua tena na tena. Kama umetumia gharama kumfikisha mteja kwenye biashara yako, jua kabisa akinunua mara moja ni hasara kwako. Unapata faida pale mteja anaponunua tena na tena na tena. Na unachopaswa kujua ni kwamba, ni rahisi kumuuzia mteja ambaye alishanunua kwako kuliko kumuuzia mteja mpya kabisa. Hivyo weka juhudi katika kuwafanya wateja waendelee kununua kwako zaidi na zaidi.

Njia ya nne; kuongeza kiwango cha manunuzi. Kama mteja akija kwako ananunua kitu kimoja, unahitaji kumshawishi anunue kitu kingine ambacho kinaendana na kile alichonunua. Hapo unaongeza mauzo na kuongeza faida pia. Kwa mfano kama unauza vifaa vya ujenzi, akaja mteja kununua rangi, unahitaji kumshawishi anunue na brashi za kupakia rangi na vitu vingine vinavyoendana na hili. Kadhalika kwenye mavazi na hata vifaa vya kielektroniki, mpe mteja wigo wa kununua vitu vinavyoendana na kile anachotaka.

Njia ya tano ni kuongeza bei, hii ndiyo wengi huwa wanaikimbilia, lakini ukitumia hizo nne na hii kwa pamoja, utanufaika sana. kwenye njia ya tano, unaongeza bei ya kitu ili upate faida zaidi. Kama utafanyia kazi hatua hizi tano kwa pamoja, ongezeko dogo, kama la asilimia 10 kwenye kila hatua, litaleta ongezeko la asilimia 61 kwenye faida. KAZI  KWAKO  NDUGU .

 Na  Mwl  Japhet  Masatu , Dar  es  salaam , Tanzania,  Afrika Ya  Mashariki ---Mwl  wa  Maisha Na  Mafanikio, Mshauri, Public Speaker(MC), Mwandishi, Mjasiriamali /
Tuwasiliane kwa :+ 255 755 400 128 / + 255 716 924136(WhatsApp ).  EMAIL: japhetmasatu@gmail.com

WEKA MKAZO KATIKA THAMANI YA MAISHA YA MTEJA , GHARAMA YA KUMPATA MTEJA NA KIWANGO CHA WATEJA WANAOPATIKANA KWENYE BIASHARA YAKO UTAFANIKWA SANA.

Ili biashara yako ifanikiwe, inahitaji kuweka mkazo kwenye maeneo haya matatu muhimu sana.

(1). THAMANI YA MAISHA YA MTEJA. Wafanyabiashara wengi huwa wanamwangalia mteja kwa wakati ule anaokuja kununua tu. Huwa hawaangalii thamani yake ya maisha. Kwa mfano kama mteja akija kununua kwako mara moja, unapata faida ya shilingi elfu moja, ni rahisi kuona elfu moja inakuja. Lakini chukua mfano kwamba mteja huyo ananunua kila wiki, na anaweza kununua kwako kwa miaka mitano ijayo. Hii ina maana kwa mwaka, anakuingizia faida ya 1000 x 52(idadi ya wiki za mwaka) ambayo ni tsh 52,000/= na kwa miaka mitano; 5 x 52,000/= ambayo ni sawa na 260,000/=. Thamani ya maisha ya mteja wako huyo ni shilingi laki mbili na elfu sitini, na siyo ile elfu moja unayoiona anapokuja. Je kwa kujua hilo hutaongeza umakini zaidi kwa mteja huyu ili aendelee kuwa na wewe kwa miaka hiyo mitano na hata zaidi?

(2).GHARAMA YA KUMPATA MTEJA. Hapa ndipo gharama za kununua wateja wa biashara yako zinapoingia. Kabla hujachukua hatua yoyote ya kuongeza wateja zaidi kwenye biashara yako, lazima ujiulize gharama unayotumia inaleta wateja wangapi na kama gharama hizo zinarudi kupitia mauzo. Upo usemi kwenye utangazaji wa biashara kwamba nusu ya bajeti ya matangazo huwa inapotea, ila mtu hawezi kujua ni nusu ipi. Hii ina maana kwamba, gharama nyingi watu wanazotumia kutangaza biashara zao zinapotea, hazirudi kabisa kwenye biashara. Lazima ujue gharama zako na zinarudije.

(3). KIWANGO CHA WATEJA WAPYA WANAOPATIKANA. Unapotangaza biashara yako, watu wengi wanajua kuhusu uwepo wako. Lakini watu kujua kuhusu biashara yako hakukunufaishi chochote. Ni mpaka pale watu hao watakapochukua hatua ya kununua ndiyo biashara inanufaika, kama gharama zimepigwa vizuri. Hivyo eneo la kuweka mkazo ni kuongeza kiwango cha wanaojua biashara kuwa wateja wa biashara hiyo. kadiri watu wengi wanaofikiwa na tangazo wanakua wateja, ndivyo gharama za kupata wateja zinakuwa ndogo na faida inakuwa kubwa baadaye.


 Na  Mwl  Japhet  Masatu , Dar  es  salaam , Tanzania,  Afrika Ya  Mashariki ---Mwl  wa  Maisha Na  Mafanikio, Mshauri, Public Speaker(MC), Mwandishi, Mjasiriamali /
Tuwasiliane kwa :+ 255 755 400 128 / + 255 716 924136(WhatsApp ).  EMAIL: japhetmasatu@gmail.com