Thursday, September 2, 2021

KUPOTEZA " TUMAINI " NI KITU KIBAYA SANA KATIKA MAISHA

Maisha yanaweza kukupitisha katika nyakati ngumu ambazo mbele yako huoni kama utatoka au kuna nafuu yoyote. Nyakati hizi ndizo zinazofanya wengine wasiamini kama lipo tumaini au njia ya kuvuka. Ni lugha ngumu mtu kukuelewa pale anapopitia magumu na unamwambia kuwa hayo magumu utashinda tu huku akiangalia hakuna dalili zozote za suluhisho. Kibinadamu si hali rahisi kushawishiwa kuwa mambo yatakaa sawa na yatapita. Hili ndilo ambalo watu wengine huamua kukatisha maisha yao kwa kuona hawaoni msaada unaoweza kuwatoa walipo.

Hali ya kukosa tumaini inaweza kumkuta mtu yeyote yule katika zama tuishizo. Mambo yanapobadilika ghafla na matarajio mbalimbali kupotea ni hali inayosababisha mtu ashuke hamasa ya kufanya vitu, changamoto zinapokuwa hazikomi, hali ngumu za kiuchumi, migogoro katika kazi au mahusiano, nyakati ngumu za masoko na biashara vinapokuja kwa pamoja kwa mtu mmoja si jambo jepesi la kuvumilika. Ni wengi utakuta wanapata hali ya kukosa hamasa, wanashuka ari ya kufanya kazi na mzigo unapowazidia basi tumaini la nafuu ya hali wapitiazo hufifia au hata kuzima kabisa. Inahitaji ustahimilivu, faraja na nguvu ya kutia moyo na watu wengine kipindi cha hali ngumu.

Mtu anapoanza kupoteza matumaini ni dalili za hatari ambapo asiposaidiwa ni rahisi kufanya maamuzi mabaya ya kimaisha. Hali ya kukosa tumaini huanza pale ambapo mtu huanza kukata tamaa kwa yale anayoyapitia. Huenda ni katika kila jaribio mtu anaona kushindwa na kuanguka. Kukata tamaa kunamsababisha mtu afadhaike na kupata hali ya kupata hatia, kuona hamasa haipo tena na kujawa na hali ya kukata tamaa kabisa ya kimaisha. Hali hizi huwatokea watu wengi wanaopitia hali za sonona katika maisha ambapo kutokana na hali mbalimbali walizoshindwa kuzikabili basi wakajikuta wanazidiwa na kupoteza tumaini.

Magumu katika maisha hayakosekani na si kuwa watu hawapitii magumu. Ikiwa kila mmoja atahadithia simulizi ya yale aloyapitia utakuja kuona unayoyapitia huenda ni madogo. Kinachotia moyo ni kuwa wapo ambao maisha yao ukiyatazama unaona la kwako unalopitia ni dogo na wakati mwingine maisha yao yanaweza kukutia moyo kuwa hupaswi kumbe kukata tamaa. Kila wasaa unapoona tumaini linafifia jipe wasaa wa kuona watu wengine wenye magumu zaidi wasivyokata tamaa wala mioyo yao kuinama.

Unaweza kupoteza kila kitu maishani na ukarejea tena katika kuyaishi maisha endapo hutapoteza “tumaini”. Watu wengi ambao wamepitia magumu, taabu na shida na wakainuka tena hawakupoteza tumaini. Waliweka tumaini kuwa licha magumu yote ambayo yamejitokeza bado wanaona ipo njia, hali zitabadilika na mbele kuna njia ya kutoka. Maisha huwa mapya pale ambapo kila unapopitia magumu hupotezi tumaini kwa kile unachokifanya, tumaini la kuishi na tumaini la kuona kila kitu kitakuwa sawa kadri muda unavyoenda.

Kuna nyakati ambazo nilipitia ngumu sana, niliona siwezi kuinuka tena, niliona ndo mwisho wa kile nilichokuwa nakitegemea ila ninashukuru kuwa nilibakiwa na hali ya kuwa na tumaini kuwa hali nayoipitia itapita. Hili limekuwa likinisaidia hata sasa kuwa kwa kila hali ambayo itatokea iwe ngumu, yenye misusuko mingi nachotakiwa kukitunza ni kuwa na tumaini kuwa mambo yataenda tu. Tumaini ni ukombozi mkubwa katika maisha tuishiyo duniani.

NA  KOCHA   MWL.  JAPHET  MASATU , DAR  ES    SALAAM

WhatsApp + 255 716924136 /   + 255 755 400128

 

Wednesday, July 21, 2021

BIASHARA YA GENGE : JINSI YA KUIENDESAHA NA KUFANIKIWA.

Rafiki yangu mpendwa,
Nimekuwa naamini na kusema hili mara kwa mara na nilirudie tena hapa, kukosa mtaji siyo sababu ya kushindwa kuingia kwenye biashara. Ni kisingizio tu.

Sasa visingizio vyote huwa ni vya uongo, kwa sababu vinaficha kile ambacho mtu hataki kukikabili.

Wengi wanaotumia kisingizio cha mtaji, hawapo tayari kuukabili ukweli kwamba ni wavivu, wazembe, wasio tayari kujitoa na wanaopenda mazoea. Ni vigumu sana mtu kukiri una tabia hizo, hivyo kisingizio cha mtaji au muda kinakuwa rahisi.

Kwa zama tunazoishi sasa, hakuna kinachoweza kumzuia mtu aliyejitoa kweli kuingia kwenye biashara. Siyo wazo, siyo mtaji na wala siyo muda.
Kinachomzuia mtu hakitoki nje, bali kipo ndani yake.
Na yule ambaye hana kizuizi cha ndani, anaweza kuyafanya makubwa mno.




Chukua mfano wa biashara ya genge la mahitaji muhimu ya kila siku kwenye familia.
Ni biashara yenye uhitaji, kwa sababu watu kila siku wanakula.
Ni biashara unayoweza kuanza kwa mtaji kidogo.
Ni biashara ambayo huhitaji kuwa na eneo la gharama kubwa kuifanyia.
Na ni biashara ambayo haina vitu vingi, hivyo unaweza kuisimamia vizuri.

Hii ni biashara ambayo mtu ambaye hana shughuli nyingine ya kufanya anaweza kuianzisha, akaiendesha vizuri na ikawa sehemu ya yeye kupiga hatua na kuelekea kwenye biashara kubwa zaidi.

Unapochagua kufanya biashara kama hii, unapaswa kuifanya kwa tofauti, ili ikue na kuweza kuzalisha biashara nyingine kubwa zaidi.

Huenda unawajua wauza genge ambao miaka yote unawaona wakiwa pale pale. Siyo kwamba biashara hailipi, ila wanaifanya kwa viwango vya chini.

Kwenye makala hii unakwenda kujifunza jinsi ya kuifanya biashara ya genge kwa viwango vya juu sana na ikawa na manufaa makubwa kwako.

Kabla hatujaingia kwenye ushauri, tusome aliyotuandikia msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili.

“Nahitaji kufungua genge la matunda na mboga mboga napenda kuelimishwa namna ya kuboresha iliniweze kukuza biashara yangu na wateja wavutiwe na huduma yangu.” – Hussein B. M.

I. MAONO MAKUBWA.
Anza kidogo lakini fikiri kwa ukubwa. Japo unafanya biashara ya genge, kwenye fikra zako usione genge, bali ona biashara kubwa kabisa.
Ona ukiwa na maduka mengi ya kuuza mahitaji hayo ya msingi na ona ukifanya kwa kiwango kikubwa zaidi.
Ni maono makubwa unayokuwa nayo ndiyo yanakusukuma kupiga hatua kubwa pia.
Tunapata kile tunachoona, hivyo kuwa na maono makubwa na jisukume kuyafikia.

II. BIDHAA BORA.
Kwenye biashara ya genge wateja wanaangalia vitu vikuu viwili, bidhaa bora na kwa bei nafuu. Pambana kuwapatia wateja vitu hivyo viwili na watakuwa wako kwa muda mrefu.
Chagua bidhaa zilizo bora kabisa ndiyo uweke kwenye biashara yako.
Jua maeneo unayoweza kupata bidhaa hiyo bora kwa bei nafuu ili pia uweze kuwauzia wateja wako kwa bei nzuri.
Jiwekee viwango vya ubora wa bidhaa utakazouza ili wateja waweze kujenga imani kwako na kwa biashara yako.

III. ENEO ZURI.
Biashara yako inapaswa kuwa eneo ambalo ni rahisi kuwafikia wateja wako na hata wateja kuifikia pia.
Kwa kuwa unachouza ni mahitaji muhimu ya maisha ya kila siku, biashara itafanya vizuri pale inapokuwa eneo lenye watu wengi.
Lakini pia mazingira ya eneo lako la biashara yanapaswa kuwa safi na mazuri, yamfanye mteja aiamini na kuithamini biashara yako.
Wengi wanaofanya biashara ya genge hawaweki maeneo yao ya biashara kwenye mwonekano mzuri, ukifanyia kazi hilo unajitofautisha kabisa na wengine.

IV. HUDUMA BORA KWA WATEJA.
Wahudumie vizuri saba wateja wako ili waweze kurudi tena na tena. Wasikilize kwa umakini na wajali pia. Jua mahitaji yao na uwatimizie.
Usiuze tu na kuishia hapo, jenga mahusiano mazuri na wateja wako na hayo yataiwezesha biashara kukua zaidi.
Pale wateja wanapopata huduma nzuri, wanaendelea kuja na wanawaleta wengine pia.

V. KUWEKA MAFUNGU.
Unayajua mahitaji ya wateja wako, unaweza kutengeneza mafungu ya vitu vinavyonunuliwa kwa pamoja na kisha kumshawishi mteja anunue kama fungu badala ya kununua kimoja kimoja.
Kumsukuma kuchukua hatua, hakikisha bei ya fungu inakuwa na unafuu kuliko mteja akinunua kimoja kimoja.
Njia hii itakuwezesha kuuza zaidi kwa wateja ambao tayari unao, ambao ni wateja wazuri tayari.

VI. KUWAFIKIA WATEJA.
Usisubiri tu wateja waje, badala yake watuate kule walipo. Watu sasa wametingwa na mambo mengi wanaweza kusahau kabisa hata uwepo wako.
Hivyo watembelee wateja wako maeneo walipo na kuwashawishi kuja kununua.
Hapa pia unaweza kutoa huduma ya mteja kuagiza na kupelekewa bidhaa zake.
Na kama umeziweka bidhaa kwa mafungu na bidhaa zako ni bora, mteja anaagiza na kupelekewa, akijua anapata anachotaka na ambacho ni bora pia.

VII. KUWASILIANA NA WATEJA.
Omba mawasiliano ya wateja wako na wasiliana nao mara kwa mara.
Unajua wateja wa genge wanapanga mahitaji yao ya siku asubuhi. Unaweza kuwatumia ujumbe asubuhi kuwasalimia na kuwaomba oda pia. Mteja anapopata ujumbe wako, anakufikiria kwa muda mrefu na hilo linamshawishi kuja kununua kwako.
Tumia kila sababu na ushawishi kupata mawasiliano ya wateja wako na wasiliana nao kwa njia ambayo siyo ya usumbufu kwako.

VIII. KUWEKA AKIBA.
Kwa lengo lako la kufika kwenye mafanikio makubwa kibiashara, unapaswa kuweka akiba kwenye kila faida unayoingiza kwenye biashara yako.
Wakati biashara inafanya vizuri, usibweteke na kuona mambo yataenda hivyo wakati wote.
Weka akiba ambayo itakusaidia wakati biashara haiendi vizuri.
Akiba hiyo ndiyo itakusaidia kwenye ukuaji wa biashara yako.

IX. KUKUZA BIASHARA.
Kwa kuwa una maono makubwa ya biashara yako, kila wakati angalia fursa za ukuaji zaidi.
Kila wakati piga hatua kuikuza biashara yako zaidi.

X. KUJIFUNZA KILA SIKU.
Kujifunza kila siku ni hitaji muhimu la ukuaji wa biashara yako.
Kila siku hakikisha unajifunza kitu kwenye kuikuza biashara yako.
Biashara inahitaji ubobezi maeneo mbalimbali kama masoko, mauzo, fedha, ushawishi na uongozi.
Soma vitabu mbalimbali vya biashara yako na  unayojifunza yafanyie kazi.

Saturday, July 10, 2021

MITANDAO YA KIJAMII INAELEKEA KUWAGAWA WATU KATIKA MAKUNDI HAYA.

Umakini wako ndiyo utajiri wako, kama utaweza kuweka umakini wako wote kwenye kile unachofanya, kwa hakika utaweza kuongeza kipato chako maradufu.

Mtaalam Mmoja Aliwahi Kusema Hivii.Siku zijazo, kutakuwa na makundi makuu mawili ya watu duniani.

Kundi la kwanza litakuwa la wale ambao wanaruhusu umakini wao kudhibitiwa na watu wengine, ambao wanaruhusu kila aina ya usumbufu kuwaingia. Kundi hili litakuwa na watu wengi sana, na mara zote watakuwa wamevurugwa na wasiweze kufanya makubwa kwenye maisha yao.

Kundi la pili litakuwa la wale ambao wanadhibiti umakini wao na kutoruhusu usumbufu wa aina yoyote ile kuwavuruga. Kundi hili litakuwa na watu wachache sana, na hawa ndiyo watakaoweza kufanya makubwa na kufanikiwa sana.”

Swali kwako, je kwa hali inavyokwenda sasa kwenye maisha yako, unajiona ukielekea kwenye kundi lipi kati ya hayo mawili?

Na je ungependa kuwa kwenye kundi lipi? Kama ungependa kuwa kwenye kundi la kwanza huna cha kufanya, endelea kufuata mkumbo na kila aina ya kelele.

Lakini kama ungependa kuwa kwenye kundi la pili, basi yale yote ambayo umejifunza kwenye kitabu cha juma hili yafanyie kazi.

Jua usumbufu wako wa ndani na wa nje na tenga muda wa kufanya yale muhimu na kuepukana na usumbufu.

Maarifa tayari unayo, kama hutachukua hatua huna wa kumlaumu, utakuwa umechagua wewe mwenyewe.

Tuko kwenye vita, adui mkuu anajua yuko vitani ila wanaolengwa hawajui.

Hivyo unapaswa kuwa na maandalizi mazuri ya kupambana na vita hii ili uweze kutoka salama na siyo kuwa mfungwa.


KAMA UNATAKA MAFANIKIO MAKUBWA , USIWE " FAIR " KWENYE MAENEO HAYA KUMI ( 10 ).

Rafiki yangu mpendwa,
Kuna vitu waliofanikiwa sana wanavijua, lakini huwa hawaviweki wazi.

Wanafanya hivyo kwa sababu jamii huwa haielewi vitu vingi kuhusu mafanikio, na hivyo huishia kuwashambulia waliofanikiwa pale wanapojaribu kuwa wakweli.

Mara ngapi umesikia masikini wakiwasema matajiri kwamba ni freemason au wamepata utajiri wao kwa njia za giza?
Umewahi kumwona tajiri akibishana na masikini juu ya hilo?

Jibu ni hapana, tajiri anajua masikini hawezi kuelewa na hata kuamini mengi yaliyomsaidia yeye, hivyo anamuacha aamini anachochagua kuamini.

Leo nakupa siri kubwa, nakupa ukweli mchungu ambao ukiweza kuupokea na kuuishi, utaweza kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako.

Ukweli huo ni kama unataka mafanikio makubwa, basi usiwe ‘fair’.
Neno fair yaani usawa limekuwa linatumika sana.
Wengi wamekuwa wanalalamika kwamba maisha hayapo fair, pamoja na juhudi wanazoweka bado hawapati wanachotaka.

Leo nakwenda kukushirikisha maeneo 10 ambayo upaswi kuwa ‘fair’ kama unayataka mafanikio makubwa.
Kwenye maeneo hayo, unapaswa kuwa tofauti kabisa na wengine walivyo ili uweze kupata matokeo ya tofauti.




Kama unataka mafanikio makubwa, usiwe fair kwenye maeneo haya 10.

(1). USIWE  "FAIR"   KWENYE  KAZI.
Watu wengi wanafanya kazi kwa mazoea na kwa viwango vya chini sana. Wewe nenda kinyume nao, fanya kazi kwa juhudi kubwa na kwa viwango vya juu sana.
Anza kwa kufanya kazi muda mrefu kuliko wengine.
Kama wanaanza kazi saa mbili asubuhi na kumaliza saa 10 jioni, wewe anza saa moja asubuhi na kumaliza saa 12 jioni.
Kila siku weka masaa 2 mpaka 4 ya ziada kwenye kazi unayofanya.
Na unapofanya kazi  weka umakini wako wote kwenye kile unachofanya na usiruhusu usumbufu wowote ukuvuruge.

( 2 ). USIWE  "FAIR"  KWENYE  MUDA.
Watu wengi huwa wanachezea muda kama vile ni kitu ambacho hakina ukomo.
Lakini muda una ukomo, kuna masaa 24 tu kwenye siku, ukishayatumia huwezi kupata tena mengine.
Kuwa bahili sana wa muda wako, usikubali upotee hovyo kwa mambo yasiyo na tija.
Kila siku unayoianza pangilia muda wako, weka vipaumbele vyako vya siku na vifuate hivyo.
Kuwa na orodha ya mambo utakayoyafanya kwenye siku yako na ifuate hiyo.
Usiruhusu usumbufu au mahitaji ya wengine yaingilie ratiba yako muhimu ya siku.

( 3 ). USIWE  "FAIR"  KWENYE  FEDHA.
Watu wengi wakipata fedha huwa wanakimbilia kuzitumia mpaka ziishe na hata zikiisha hawaishii hapo, badala yake wanakopa ili waendelee kutumia zaidi.
Wewe usiwe hivyo, unapopata fedha yoyote ile, tenga kwanza akiba kabla hujatumia. Usitumue kisha inayobaki ndiyo uweke akiba, fedha huwa haibaki. Badala yake weka akiba kwanza kisha inayobaki ndiyo utumie.
Na akiba unayoweka, iwekeze mahali inapozalisha na kukua zaidi. Hiyo ndiyo njia ya uhakika ya kuondoka kwenye umasikini na kwenda kwenye utajiri.

(4). USIWE  " FAIR "  KWENYE  KUSUDI.
Watu wengi wanaishi maisha ya bendera kufuata upepo, hawalijui kusudi la maisha yao na hivyo ni rahisi kushawishiwa na chochote kinachopita mbele yao.
Wewe usiwe na maisha ya aina hii, pambana ulijua kusudi la maisha yako na kuliishi kila siku.
Jua kwa nini uko hapa duniani, maisha yako yanapaswa kuacha alama gani na jipe wajibu mkubwa unaokusukuma kuchukua hatua kila siku.
Ukiwa na kusudi unakuwa na msimamo.

( 5 ). USIWE " FAIR " KWENYE   NDOTO.
Watu wengi hawana ndoto kubwa, wanaishi maisha ya mazoea, wanafanya shughuli zao, wanapata pesa ya kula na wanaridhika na hayo.
Wewe usiwe mtu wa kuridhika na mambo madogo unayopata sasa.
Kuwa na ndoto kubwa sana, ndoto ambazo wengine wakizisikia wanaona kama umechanganyikiwa na wanakuambia haiwezekani.
Ni ndoto kubwa unazoziamini bila ya shaka zinazokusukuma kufanya makubwa zaidi kwenye maisha yako.

( 6 ). USIWE " FAIR "  KWENYE  KUJIFUNZA.
Watu wengi wakishahitimu shule, hawajifunzi tena vitu vipya wala kusoma vitabu. Watu hawasomi kabisa vitabu, wakiamini hakuna kipya wanachoweza kujifunza, tayari wanajua kila kitu.
Wewr usiwe hivyo, kuwa mtu wa kujifunza vitu vipya kila siku. Kuwa mtu wa kusoma vitabu kila siku.
Hakikisha kila mwezi unasoma angalau kitabu kimoja na kwa kila kitabu unachosoma chukua hatua za kuyabadili maisha yako.
Hilo pekee linatosha kukupa fursa nyingi na kukuwezesha kupiga hatua kuliko wengine.

(7).USIWE  " FAIR "  KWENYE  MAHUSIANO.
Walio wengi wanazungukwa na watu hasi, watu waliokata tamaa na wanaowakatisha tamaa pia. Mahusiano yao mengi yanakuwa kikwazo kwao kupiga hatua.
Wewe kuwa makini sana na mahusiano yote uliyonayo, hakikisha yanakuwa mahusiano bora na yanayokusukuma uwe bora zaidi.
Waepuke watu hasi na waliokata tamaa kama ukomo, usijenge ukaribu na watu wa aina hiyo, kwani watakuambukiza waliyonayo.
Ulivyo ni wastani wa watu watano wanaokuzunguka, chagua watano bora ambao watakusukuma upige hatua zaidi.

( 8). USIWE " FAIR "  KWENYE  KUJIAMINI.
Watu wengi hawajiamini, wanaweza kuwa na ndoto kubwa ila wanapowaambia wengine na wakawakatisha tamaa, wanawasikiliza na kukubaliana nao.
Ndiyo maana kundi kubwa la watu kwenye jamii hawawi na maisha wanayoyataka, maana hawajiamini kiasi cha kuwashinda wale wanaowakatisha tamaa.
Wewe jiamini kupitiliza, amini ndoto kubwa ulizonazo utaweza kuzifikia bila ya kujali unaanzia wapi sasa.
Hata kama wengine wanakuambia haiwezekani, hata kama wanakuonesha na mifano kabisa, usiwaamini zaidi ya unavyojiamini wewe. Jifunze yote muhimu na endelea kusimama kwenye ndoto zako kubwa.

( 9 ). USIWE  " FAIR " KWENYE  UNG"ANG"ANIZI.
Ili ufanikiwe lazima uwe king’ang’anizi sana, ujitoe kweli kweli na ukomae mpaka upate kile unachotaka.
Utakutana na magumu, vikwazo na kushindwa, lakini usiruhush hayo kuwa mwisho wa safari yako.
Jipe kiapo kwamba utapata kile unachotaka au utakufa ukiwa unakipambania, hakuna mbadala wa hilo.

( 10 ). USIWE " FAIR " KWENYE  KUTOA  KAFARA.
Ili upate kile ambacho hujawahi kupata, lazima uwe tayari kupoteza kile ambacho tayari unacho sasa. Kuna vitu vizuri unavyo sasa lakini ni kikwazo kwako kupata mafanikio makubwa unayotaka.
Wengi wanataka mafanikio lakini hawapo tayari kutoa kafara, kuachana na vile vizuri walivyonavyo sasa ili kupata vilivyo bora zaidi.
Ukiweza kuvuka hilo, utaweza kupata makubwa.

Ukiondoa usawa kwenye maeneo haya 10 muhimu, utakuwa na maisha ya tofauti kabisa na utaweza kufanya makubwa sana.
Lakini utakapokua na maisha ya tofauti wengi watakushambulia, hivyo utakuwa kama mpweke katikati ya kundi kubwa la watu.

Nakukaribisha ujiunge kwenye " DARASA  ONLINE " UJIFUNZE  MENGI  USIYOYAJUA.

Usikubali tena kuendelea kuwa fair kwenye mambo yanayokurudisha nyuma.
Chagua kushika hatamu ya maisha yako ili uweze kufanya makubwa.

Ndimi  rafiki yako  mpendwa,
KOCHA  MWL.  JAPHET   MASATU , DAR  ES SALAAM, TANZANIAW

 

WASILIANA  NAMI   SASA  KWA

 

 ( WhatsApp + 255 716 924136    )  + 255 755 400 128 

 

KILA MTU ANA KIU YA KUTENDEWA UKARIMU / MEMA---" UKARIMU NI MGUSO WA PEKEE KWA KILA BINADAMU.

Maisha yetu sisi binadamu yanahitaji mguso. Mguso wa kutendewa mambo mazuri hata kama sisi tunawatendea wengine mabaya au tu wabinafsi. Ile kiu ya kutendewa mambo kwa ukarimu huwa kunatugusa sana. Kiu hii au njaa hii imo kwa kila mtu katika moyo wake kutamani kuona anapata kutendewa mema na mazuri. Licha tunaweza kuishi katika nyakati ambazo zimejaa watu wenye chuki, wasio na upendo bado mioyo yetu inatafuta wapi itapata ukarimu, wapi upendo ulipo, wapi furaha ilipo na wapi pa kupata matumaini.

Jamii zetu zina upungufu mkubwa wa watu ambao wana mioyo ya majitoleo. Kila mtu anapambana kuona ni kwa vipi atafaidika kuliko namna atakavyosaidia wengine wafaidike kwanza. Hili linajenga watu wakose ukarimu, wakose kusaidia wengine na wengine hata kuzuia wengine kupata vitu vizuri. Ukarimu imekuwa bidhaa adimu katika maisha tunayoishi maana kila mtu anajifikiria yeye mwenyewe tu na kusahau kuangalia wengine.

Usijekushangaa pale mtu mkarimu anapoonekana ni bidhaa adimu sokoni anapokuwa ni mtu anayewajali wengine, anayewatanguliza wengine, anayejitoa kwa faida ya watu wengine, anayejitosa kuingia gharama kwa ajili ya watu wengine. Si jambo rahisi kupatikana kwa kila mtu kuwa tayari kuingia gharama katika kujisahau yeye kwanza na kuwafikiria wengine kuwa kwa kuwafanyia wengine ukarimu ni yeye mwenyewe kujifanyia ukarimu. Ni vile mtu anavyojitoa kusaidia wengine ni yeye anajisaidia, ni kama vile mtu anavyoona kuwanyima nafasi wengine kufanikiwa ndivyo na yeye anavyojinyima kufanikiwa. Lolote lile tunalowafanyia wengine si kuwa wanaathirika wao tu bali hata sisi tunaathirika iwe moja kwa moja au njia nyingine.

Watu waliojeruhika ni wengi katika mioyo yao, watu walipitia mateso na taabu ni wengi, watu walopita manyanyaso ni wengi. Tendo la ukarimu kwa makundi haya ya watu ni jambo kubwa lisiloweza kupimika. Watu hawa wana kiu na njaa ya kuona hata kidogo wapate kuona matendo mema na ya ukarimu yakifurika katika maisha yao. Tendo jema lina mguso na huacha alama kubwa kwa maisha ya watu.

Tunaishi sasa na ipo siku ambayo tutayaacha maisha haya ya mwili na kufa. Kumbukumbu la maisha yetu itaanzia kwanza katika wema tulotenda kwa wengine au ubaya kwa wengine. Matendo mema huliliwa sana na watu ambao walitenda katika siku za uhai wao. Matendo ya ukarimu hugusa mioyo ya watu na huacha alama njema ya jina la mtu duniani. Tafuta nafasi hata ndogo ya kuonesha matendo ya ukarimu kwa watu wanaokuzunguka. Utaacha mguso usiofutika katika maisha yao na hii ni maana njema ya kuishi kikamilifu na kuishi kwa umoja kwa kuhesabu watu wanaokuzunguka ni sehemu ya viungo vya mwili wako.

UJUMBE : TAFUTA   NAFASI YA  KUTENDA  TENDO   LA  UKARIMU. MUNGU  AKUBARIKI  SANA.

Ndimi  KOCHA   MWL.  JAPHET   MASATU , DAR  ES  SALAAM , TANZANIA.

 ( WhatsApp + 255 716 924136 ) / + 255  755 400 128 

 

TUMIA MBINU HIZI SIKU ZOTE KUPAMBANA NA CHANGAMOTO YOYOTE MBELE YAKO.

HAKIKISHA! Siku Zote Unapopambana Na Changamoto Yoyote Ile Usisahau Kutumia Mbinu Hizi Muhimu Zenye Matokeo Ya Haraka…!

Rafiki yangu mpendwa,

Katika maisha lazima ujue kila wakati unaweza kukutana na changamoto.

Na watu wanasema kila ukitoka kwenye changamoto moja utaingia kwenye changamoto nyingine, duniani hapa kama hauko kwenye changamoto basi utakuwa umetoka kwenye changamoto au unaelekea kwenye changamoto nyingine.

Shida sio changamoto unazokutana nazo, tatizo kubwa ambalo watu linawakabili ni namna ya kushughulika na changamoto ambazo zile zinatokea katika maisha yao.

Na Leo lingependa nikwambie namna ambavyo unaweza kutoka kwenye changamoto yoyote inayokukabili, inawezekana leo upo kwenye changamoto kwenye taaluma yako inawezekana leo upo kwenye changamoto ya mahusiano yako au upo kwenye changamoto ya kiuchumi, au upo kwenye changamoto ya kazi, kazi unayofanya au eneo lako la kiofisi au kwenye biashara yako.

Bila kujali upo kwenye changamoto ipi kuna maeneo manne ukiweza kuyazingatia yatakusaidia sana kutoka kwenye changamoto yako tena kwa haraka.

Kumbuka tena washindi ni wale ambao wakipita kwenye changamoto wanaondoka kwenye changamoto zao kwa haraka sana bila kuchelewa.

Jambo La Kwanza; Ambalo unatakiwa kulifahamu katika maisha yako ni kwamba unapopitia changamoto USIKUBALI ile hali ya kujiambia changamoto yako ni SPESHO.

Changamoto SPESHO, maana yake ni kuna watu wanafikiri wanapopitia matatizo ni wao ndio wa kwanza kupitia katika matatizo hayo na hakuna mtu mwingine yeyote aliyepitia katika changamoto hiyo.

SI KWELI, ukiwa na fikra ya namna hiyo utashindwa kabisa kukabiliana na changamoto yako.

Changamoto yoyote leo unayokutana nayo, cha kwanza ambacho ningependa nikuambie. Kuna mtu ameshawahi kukutana na changamoto kama hiyo, na katika wale waliokutana na changamoto kama hizo hakika wako ambao wameshinda hizo changamoto.

Lakini kuna mtu leo anapitia changamoto kama ya kwako na hakika anaweza akashinda pia, wewe ukajua na kufikiri kwamba changamoto yako ni SPESHO na hakuna mtu ambaye anachangamoto kama ya kwako, hakika hautavuka, hautatoka katika hiyo changamoto.

Kuna watu ambao wakipitia matatizo wanaona changamoto yao hakuna mtu mwingine yeyote mwenye nayo. Wanaona kama lile tatizo ndio mara yao ya kwanza wanalipitia duniani yaani ni kama limevumbuliwa hakuna mtu mwingine ambaye amekutana nalo.

SI KWELI, usikubali hata siku moja kwamba changamoto yako ni SPESHO hakuna mtu mwenye changamoto kama hiyo, ukiwa na fikra kwamba changamoto yako ni spesho , hautapata uvumbuzi mapema na utaona hakuna msaada.

Cha kwanza kabisa kataa fikra inayokuambia changamoto yangu ni spesho hakuna mtu kama mimi, mtu aliyopo kama mimi, hakuna mtu aliyepata matatizo kama mimi.

SI KWELI, wako wengi na wameshinda na wewe unaweza kuishinda.

Jambo La Pili; Unalotakiwa kulifahamu ni kwamba changamoto yoyote unayopitia ni SAIZI YAKO, watu wengi ambao changamoto zinawazidi sio kwa sababu wanashindwa kuzitatua kwa sababu walikata tamaa.

Ningependa nikuambie changamoto yoyote ile unayokabiliana nayo leo ya KIFEDHA, ya KIMAHUSIANO, ya KITAALUMA, KAZINI KWAKO au kwenye BIASHARA, inawezekana kabisa umekosa usingizi kabisa kwa sababu ya changamoto inayokukabili.

Ninachotaka nikuhakikishie ni kwamba changamoto hiyo unayokutana nayo leo ni SAIZI YAKO.

Ukiwa na fikra ya namna hiyo tafsiri yake ni kwamba utafanya kila unachoweza, kuweza kukabiliana nayo, unapokubali kwamba changamoto hii ni SAIZI YAKO. Unaulazimisha ubongo wako kutafuta suluhisho unaposema changamoto hii imenizidi umri unauambia ubongo wako ila tu kwa sababu hakuna kitu ninaweza kufanya.

Ninachotaka kukuambia ni kwamba changamoto ni saizi yako, ya mambo unayopitia leo.

Jambo La tatu; Ambalo ni la msingi sana, kulijua katika kutoka kwenye changamoto unayokutana nayo ni kujua katika kila changamoto KUNA MLANGO WA KUTOKEA, kuna njia za wewe kutoka kwenye changamoto ukweli ni kwamba hukuuona huo mlango wakutokea.

Ukweli ni kwamba haujaona njia za kutoka kwenye changamoto zinazokukabili haimaanishi kwamba changamoto yako imekosa suluhisho, kuna suluhisho kwenye changamoto yako inawezekana haujaiona ndio maana tunasema kama leo unapitia changamoto usikubali tu kukaa nyumbani, usikubali tu kukaa ndani, usikubali kujifungia, tafuta watu uzungumze nao, nenda mahali toka nje fuatilia kitu fulani utapata suluhisho.

Hakuna changamoto ambayo haina suluhisho katika maisha hata ya kwako, iwe inawezekana umefika sehemu unasema kwamba nimejaribu kila nilichofanya kupata suluhisho.

SI KWELI, changamoto uliyonayo ina suluhisho kama hutokata tamaa utapata suluhisho ya changamoto yako.

Jambo La Mwisho; Ambalo litakusaidia kutoka kwenye changamoto ambayo inakukabili sasa hivi kwa haraka sana nikijua kwamba changamoto zinapokuja saa zingine zinatuepusha na mabaya makubwa ambayo hatuyaoni.

Kuna watu wengi sana wanapitia changamoto za mahusiano na kusema yule nilimpenda sana, nikajitolea na leo hayupo tena kwenye maisha yangu, kuja kugundua kwamba hapana kumbe ni sababu ya wao kupata watu sahihi zaidi, kuna watu walifukuzwa kazi, kuna watu waliondolewa ofisini kwa kudhalilishwa lakini leo wanamiliki makampuni yao au wengine wamepata kazi kubwa zaidi.

Kwa hiyo kila wakati unapokutana na changamoto uwe na jicho la ziada la kuangalia usiangalie kile tu ulichokosa lakini pia kuna kitu ambacho kiko leo.

Kwa nini inakuwa hivyo mara nyingine tukiambiwa tuache vya sasa hivi tulivyonavyo ili tupate bora, tulivyoandaliwa mbele yetu hatutakuwa tayari kufanya maamuzi magumu ya namna hiyo kwa sababu yanatuumiza, lakini changamoto zinakuja pia kutuepusha na mabaya ambayo kwa macho ya kawaida hatuyaoni, ndio maana changamoto unayopitia leo ni mbaya na inakuumiza sana.

Lakini kesho utamshukuru mungu na kusema afadhali nimepitia hii changamoto. Kwa sababu imenisaidia kuwa hivi nilivyo sasa.

 KAZI   KWAKO   MDAU  WANGU .

TUWASILIANE   KWA 

 ( WhatsApp  + 255 716924136 )  kwa  USHAURI NA  MAONI  YAKO   WEWE  UNASEMAJE ??

JINSI MITANDAO YA KIJAMII INAVYOHARIBU AKILI YAKO NA JINSI YA KUEPUKA HILO.

Rafiki yangu mpendwa, mdau  wangu 
Ugunduzi wa mtandao wa intaneti yalikuwa ni mapinduzi makubwa mno kwenye maendeleo ya binadamu.
Kwani mtandao huo ulileta uhuru wa kila mtu kuweza kuwasiliana na yeyote akiwa popote.

Watu waliamini mtandao wa intaneti utaleta demokrasia na uhuru wa kweli, ambapo kila mtu anaweza kujifunza chochote anachotaka, anaweza kuwasiliana na yeyote na anaweza kushirikisha maoni yake bila kuzuiwa na yeyote.

Lakini ndoto hizo zimekuja kuyeyuka baada ya kugunduliwa kwa mitandao ya kijamii na simu janja.
Mitandao hii ambayo ilianza kama vitu tu vya watoto na vijana, sasa imepenyeza kwenye maisha ya walio wengi na imekuwa na madhara makubwa.




Mitandao ya kijamii imeharibu akili za wengi kwa njia mbalimbali, leo tunakwenda kuangalia njia moja ambayo ina madhara makubwa kwako na kikwazo kwa mafanikio yako.
Njia hiyo ni kutaka raha ya haraka (instant gratification).

Iko hivi rafiki, ili uweze kufikia mafanikio makubwa, lazima uwe tayari kuchelewesha raha (delayed gratification). Uweze kuweka juhudi kubwa mwanzoni na kuwa na subira kabla hujaanza kupata raha.

Hilo linajengwa na ukomavu wa kiakili, ambapo unaweza kuweka umakini wako kwenye jambo moja kwa muda mrefu bila ya kuhama hama.
Hicho ndicho ambacho mitandao ya kijamii inakwenda kuvunja na kukufanya uwe na uteja kwenye mitandao hiyo, kwa sababu unaitegemea ili kupata raha ya muda mfupi.

Muuzaji mkubwa wa madawa ya kulevya ambaye aliachana na biashara hiyo baada ya kufungwa kwa muda mrefu aliulizwa ni jinsi gani walikuwa wanapata wateja wengi wa kuwauzia madawa ya kulevya.
Muuzaji huyo alijibu walikuwa wakienda kwenye mji, wanawakusanya watumiaji wengi wa madawa kisha wanawapa ofa ya bure.
Haichukui muda watu hao wanakuwa wateja wao wa kudumu, kwa sababu madawa yanajenga uraibu kwao.

Hivyo pia ndivyo mitandao ya kijamii inaharibu akili yako, kwa kujenga uraibu wa kulata raha ya haraka.
Kabla ya ujio wa mitandao ya kijamii, watu waliweza kuweka muda wa kutosha kwenye kusoma vitabu au kufanya mazungumzo na wengine.
Lakini sasa mtu hawezi kusoma hata kurasa kumi kabla hajagusa simu yake. Watu wanaweza kuwa hawajaonana miaka lakini wanapokutana baada ya salamu kila mtu anahangaika na simu yake.

Kukufanya utake raha ya muda mfupi na kuwa tegemezi kwa mitandao hiyo kupata raha hiyo ndiyo madhara makubwa sana ya mitandao ya kijamii kwenye akili yako.
Hili linavunja kabisa ustahimilivu wako, ambao unahitajika sana ili uweze kufanikiwa kwenye maisha yako.

Akili yako ikishaharibiwa na mitandao ya kijamii, uwezo wako wa kuweka vipaumbele sahihi kwenye maisha yako unaharibiwa kabisa.
Unakuwa huwezi tena kuweka umakini wako kwa muda mrefu kwa yale ambayo ni sahihi kwako.
Mitandao hiyo inakujengea hofu ya uongo, hofu ya kwamba kuna kitu unakosa kama hujaingia kwenye mitandao hiyo hata ndani ya muda mfupi tu.

Tatizo kubwa zaidi ni kwamba hakuna anayeliona na kulizungumzia tatizo hili wazi wazi. Wanasema kulijua tatizo ni nusu ya kulitatua. Wengi ambao akili zao zimeshaharibiwa na mitandao ya kijamii hawajui hata kama wana tatizo. Wao wanaona ni sehemu ya kawaida ya maisha yao, kumbe wameshageuzwa kuwa tegemezi kwenye mitandao hiyo.

Tatizo hilo halizungumziwi kwa sababu wengi hawana uelewa na wale wanaomiliki mitandao hiyo wanapima mafanikio kwa idadi ya walio tegemezi kwenye mitandao hiyo.
Hivyo hili linabaki kuwa wajibu wako mwenyewe kama hutaki liendelee kuwa na madhara kwako.

Mitandao ya kijamii imeajiri watu wenye elimu kubwa kwa lengo moja tu, kuteka umakini wako na kukufanya kuwa tegemezi.

Ni wakati wa kuwa huru sasa na kushika hatamu ya maisha yako ili uweze kufika kwenye mafanikio makubwa.

Chukua hatua sasa maana kadiri unavyochelewa, ndivyo mitandao hiyo inavyozidi kutawala na kuharibu akili yako. JIUNGE   SASA  NA  " DARASA  ONLINE "   uanze  kubadili maisha yako.

Rafiki yako mpendwa

KOCHA  MWL.  JAPHET  MASATU , DAR  ES  SALAAM, TANZANIA

 WASILIANA   NAMI  SASA

 

 ( WhatsApp + 255 716  924136  )  / + 255 755 400 128