Rafiki yangu mpendwa, mdau wangu
Ugunduzi wa mtandao wa intaneti yalikuwa ni mapinduzi makubwa mno kwenye maendeleo ya binadamu.
Kwani mtandao huo ulileta uhuru wa kila mtu kuweza kuwasiliana na yeyote akiwa popote.
Watu waliamini mtandao wa intaneti utaleta demokrasia na uhuru wa kweli, ambapo kila mtu anaweza kujifunza chochote anachotaka, anaweza kuwasiliana na yeyote na anaweza kushirikisha maoni yake bila kuzuiwa na yeyote.
Lakini ndoto hizo zimekuja kuyeyuka baada ya kugunduliwa kwa mitandao ya kijamii na simu janja.
Mitandao
hii ambayo ilianza kama vitu tu vya watoto na vijana, sasa imepenyeza
kwenye maisha ya walio wengi na imekuwa na madhara makubwa.
Mitandao
ya kijamii imeharibu akili za wengi kwa njia mbalimbali, leo tunakwenda
kuangalia njia moja ambayo ina madhara makubwa kwako na kikwazo kwa
mafanikio yako.
Njia hiyo ni kutaka raha ya haraka (instant gratification).
Iko hivi rafiki, ili uweze kufikia mafanikio makubwa, lazima uwe tayari kuchelewesha raha (delayed gratification). Uweze kuweka juhudi kubwa mwanzoni na kuwa na subira kabla hujaanza kupata raha.
Hilo linajengwa na ukomavu wa kiakili, ambapo unaweza kuweka umakini wako kwenye jambo moja kwa muda mrefu bila ya kuhama hama.
Hicho
ndicho ambacho mitandao ya kijamii inakwenda kuvunja na kukufanya uwe
na uteja kwenye mitandao hiyo, kwa sababu unaitegemea ili kupata raha ya
muda mfupi.
Muuzaji
mkubwa wa madawa ya kulevya ambaye aliachana na biashara hiyo baada ya
kufungwa kwa muda mrefu aliulizwa ni jinsi gani walikuwa wanapata wateja
wengi wa kuwauzia madawa ya kulevya.
Muuzaji huyo alijibu walikuwa wakienda kwenye mji, wanawakusanya watumiaji wengi wa madawa kisha wanawapa ofa ya bure.
Haichukui muda watu hao wanakuwa wateja wao wa kudumu, kwa sababu madawa yanajenga uraibu kwao.
Hivyo pia ndivyo mitandao ya kijamii inaharibu akili yako, kwa kujenga uraibu wa kulata raha ya haraka.
Kabla
ya ujio wa mitandao ya kijamii, watu waliweza kuweka muda wa kutosha
kwenye kusoma vitabu au kufanya mazungumzo na wengine.
Lakini sasa
mtu hawezi kusoma hata kurasa kumi kabla hajagusa simu yake. Watu
wanaweza kuwa hawajaonana miaka lakini wanapokutana baada ya salamu kila
mtu anahangaika na simu yake.
Kukufanya
utake raha ya muda mfupi na kuwa tegemezi kwa mitandao hiyo kupata raha
hiyo ndiyo madhara makubwa sana ya mitandao ya kijamii kwenye akili
yako.
Hili linavunja kabisa ustahimilivu wako, ambao unahitajika sana ili uweze kufanikiwa kwenye maisha yako.
Akili yako ikishaharibiwa na mitandao ya kijamii, uwezo wako wa kuweka vipaumbele sahihi kwenye maisha yako unaharibiwa kabisa.
Unakuwa huwezi tena kuweka umakini wako kwa muda mrefu kwa yale ambayo ni sahihi kwako.
Mitandao
hiyo inakujengea hofu ya uongo, hofu ya kwamba kuna kitu unakosa kama
hujaingia kwenye mitandao hiyo hata ndani ya muda mfupi tu.
Tatizo kubwa zaidi ni kwamba hakuna anayeliona na kulizungumzia tatizo hili wazi wazi. Wanasema kulijua tatizo ni nusu ya kulitatua. Wengi ambao akili zao zimeshaharibiwa na mitandao ya kijamii hawajui hata kama wana tatizo. Wao wanaona ni sehemu ya kawaida ya maisha yao, kumbe wameshageuzwa kuwa tegemezi kwenye mitandao hiyo.
Tatizo
hilo halizungumziwi kwa sababu wengi hawana uelewa na wale wanaomiliki
mitandao hiyo wanapima mafanikio kwa idadi ya walio tegemezi kwenye
mitandao hiyo.
Hivyo hili linabaki kuwa wajibu wako mwenyewe kama hutaki liendelee kuwa na madhara kwako.
Mitandao ya kijamii imeajiri watu wenye elimu kubwa kwa lengo moja tu, kuteka umakini wako na kukufanya kuwa tegemezi.
Ni wakati wa kuwa huru sasa na kushika hatamu ya maisha yako ili uweze kufika kwenye mafanikio makubwa.
Chukua hatua sasa maana kadiri unavyochelewa, ndivyo mitandao hiyo inavyozidi kutawala na kuharibu akili yako. JIUNGE SASA NA " DARASA ONLINE " uanze kubadili maisha yako.
Rafiki yako mpendwa
KOCHA MWL. JAPHET MASATU , DAR ES SALAAM, TANZANIA
WASILIANA NAMI SASA
( WhatsApp + 255 716 924136 ) / + 255 755 400 128
No comments:
Post a Comment