Tunangoja kuishi tukijua kuwa watu wengi wanatufikiria kumbe hakuna anayekufuatilia watu wanahangaika na maisha yao pia. Pia wengi wameshindwa kuanzisha vitu kwa kuhofia namna watu watakavyowasema. Hii hofu imeua ndoto nyingi za watu wasijue kuwa hakuna aliyekuwa anajali au kuwafuatilia. Watu wana asili ya kusahau kadri muda unavyosogea.
Falsafa inatufikirisha namna miaka 100 ijayo watu wanaokuzunguka wengi hawatakuwepo na kumbuko la wengi litasahaulika kabisa. Jinsi ambavyo walowahi kuishi wamesahaulika ndivyo hata sisi tutakavyosahaulika. Kwanini uogope kuishi sasa ukiwa hai, kwanini uogope kutumia kipaji au kwanini uogope kuziishi ndoto zako wakati miaka 100 ijayo hakuna atakayekuwepo ?.
Hofu ya kuwafikiria watu wakati hawakufikirii wewe ni upotevu wa muda katika zawadi ya maisha. Watu wengi wanaishi wakihofu hofu kubadili maisha yao na kupata mafanikio kwa hofu za wale wanaowazunguka. Hili linanyima nafasi ya watu wengi kujitambua kuwa maisha ni ya mtu mwenyewe na kila mtu anapitia changamoto mbalimbali katika maisha kiasi kwamba hawatakuwa wanakuwazia wewe tu masaa yote 24 katika siku.
Anza kuishi, anzisha vitu, weka mpango wa kubadili maisha yako huku ukiondoa hofu kabisa juu ya watu watakuchukuliaje. Ikiwa ni kitu kizuri na kitakuwa na manufaa kwako na wale wanaokuzunguka hata kama si sasa basi ivuke hofu ya watu watasemaje. Usikubali kuishi kwa kuwapendeza watu huku unajiumiza ndani yako. Kuwa huru kuishi katika uhalisia wako, ishi wajue uhalisia wako na hili ndo jambo muhimu kulifanya. Wengi wanaishi maisha ambayo si yao kwa kuogopa watu ingawa wangependa kuishi vizuri kwa nafsi zao.
Kila wakati ambao utakuwa unafikiria kuwa watu sijui watanionaje katika mambo mazuri jikumbushe kuwa miaka 100 watu wote ambao unaona sasa watanionaje hawatakuwepo na pengine na wewe hutakuwepo. Kuhofia hilo ni kupoteza nafasi hii ya maisha ulopata. Ishi kwa uhalisia pasipo kuogopa watu maana hakuna atakayekukumbuka miaka 100 ijayo.
NA KOCHA MWL. JAPHET MASATU , DAR ES SALAAM , TANZANIA.
( WhatsApp + 255 716924136 ) / + 255 755 400128 / + 255 688 361 539
EMAIL : japhetmasatu@gmail.com