Monday, March 22, 2021

UNAPOMALIZA KUTATUA CHANGAMOTO MOJA NI MWANZO WA CHANGAMOTO NYINGINE.

Kutambua kuwa maisha ni mfululizo wa matukio, magumu na masumbuko kunarahisisha zaidi kuyaelewa maisha mbali na yule ajuaye maisha huenda yatakuwa rahisi kadri anavyoishi. Mapambano katika maisha ni mchezo endelevu unaokomea tu pale mtu anapofika ukomo wa maisha yake. Ukiwa hai basi mapambano hayaishi bali hupokezana gumu moja na kuja lingine. Ukweli huu wengi hawapendi kusikia au kuamini ila kadri muda unavyokwenda na matukio katika maisha yanavyojitokeza ukweli huu unaanza kuwa wazi kwa mtu na kujua kuwa ni kweli mapambano hayakomi katika maisha ya kila siku.

Ukirejea maisha yako nyuma kidogo kuna kipindi umewahi pitia cha magumu kweli na hadi ukafikiria huenda gumu hili halitapita au ni gumu zaidi hayatatokea mengine magumu zaidi ya hayo. Ila muda unapopita unakuja kukutana na jambo lingine ambalo ni gumu kuliko lile la awali. Hili hujitokeza katika maisha yetu ya kila siku namna tunavyokabiliana na mambo. Latoka hili laja hili na mzunguko huendelea hivi bila kuachana.

Zipo nyakati za maisha zinazojitokeza ambazo mtu hufikiria gumu linalojitokeza likiisha litampa mapumziko ila isiwe hivyo. Kuna watu wanafikiria kuwa watakapofanikiwa basi matatizo yataisha yote ila hujawahi ona watu licha kuwa wana utajiri ila wanakutana na ugumu wa namna wanakosa muda na familia zao. Kweli utajiri wameupata ila wanapoteza muda wa kuwa na familia kwa sababu ya muda mwingi kupambana na biashara zao. Wangapi umewasikia namna familia zimelaumu kuwa licha baba au mama kuwa na mafanikio ila wanakosa muda kuwa na wazazi wao wapo bize au kutingwa na mambo ya biashara. Hili limechangia watoto kukosa ukaribu na wazazi na hata malezi kuwa hafifu.

Kuna mwingine anaweza kuona akishapata umaarufu basi magumu yataisha ila umaarufu unakuja na gharama zake au magumu yake. Kuna mambo ambayo mtu akifanya ni ya kawaida ila akifanya mtu mwenye umaarufu haiwi kawaida. Hili linawatesa watu wengi walio maarufu kukosa uhuru wa kuishi maisha ya kawaida hata kama wanayatamani kuyaishi. Ila wanakabiliwa na ugumu wa vipi watu watanionaje, vipi watanifikiriaje ?. Maisha haya ni magumu mno kwao na huwa mabaya zaidi pale wanapokutana na hali za kushuka kimaisha au kiuchumi.

Mifano ni mingi namna maisha ni mapambano na mfululizo wa magumu katika kuishi kwetu. Kila panapojitokeza mafanikio basi magumu nayo yapo karibu. Magumu na mafanikio yapo pamoja hayaachani. Mtu anapofanikiwa kwa kitu fulani basi ina maana ni mshindi wa mambo fulani magumu aloyakabili iwe kwa watu kumwona au yeye mwenyewe kuyapitia kimya kimya. Huu ni ukweli wa maisha ambao mtu akiutambua mapema hatachukia magumu au kuyakimbia bali kuyakabili na kuyafurahia maana ni kupitia magumu ndipo palipo na maana ya maisha na mafanikio.

KOCHA  MWL.  JAPHET   MASATU.

WhatsApp + 255  716924136  /  + 255 755  400  128 

EMAIL : japhetmasatu@gmail.com

 

Saturday, March 20, 2021

KWANINI UKIPATA PESA MAWAZO MAZURI YANAPOTEA ?

Naamini umewahi kujikuta kwenye hali hii, unakuwa na mawazo na mipango mizuri sana.

Unapanga vizuri kwamba utakapozipata fedha, basi utakamilisha vizuri mipango hiyo.

Lakini pia unawashangaa sana wale wenye fedha kwa jinsi wanavyozitumia hovyo, unajiambia kama ungezipata basi ungefanya mambo ya tofauti kabisa.

Inatokea na wewe unazipata fedha, na hapo unasahau kabisa mipango mizuri uliyokuwa nayo, unazitumia fedha vibaya mpaka pale zinapoisha ndiyo unakumbuka ile mipango yako mizuri.

Na ukitaka kudhibitisha hilo, angalia wale watu ambao wanapata fedha nyingi kwa wakati mmoja.

Labda ni kushinda bahati nasibu, au kupata mafao au kufanya biashara yoyote ambayo inaleta kipato kikubwa kwa mara moja.

 Wengi huwa kama akili zinahama , wanafanya mambo ya ajabu, na fedha zinapoisha ndipo akili zinarudi na wanaanza kujutia walivyozitumia vibaya.

Siyo kama watu hao akili zao zinahama, bali kinachotokea ni fedha wanazokuwa wamezipata , zimepitiliza kiwango cha fedha walichonacho kwenye akili.

Hivyo akili inashindwa kufikiri kwa usahihi na kufanya kile ambacho ni rahisi.

Wanatumia fedha hizo mpaka zikiisha ndipo akili zinaanza kutafuta fursa za kufanya.

Watu hao hawana tofauti kabisa na wewe, ambaye ukipata pesa mawazo mazuri yanapotea.

Ndio mnafanana.

Umekuwa unajizuia wewe mwenyewe kupata fedha zaidi, kwa sababu kiwango chako cha kifedha kwenye akili ni kidogo.

Umeridhika sana na mshahara unaoupata, au faida unayopata kwenye biashara yako ya sasa.

Na umeyajenga maisha yako kuhakikisha mambo yanaenda hivyo.

Maana angalia hata wale wanaokuzunguka, utaona wote mna viwango vya fedha vinavyofanana.

Mnaishi maisha ya aina moja, hadithi mnazopiga zinafanana na hata changamoto za kifedha kwenu ni zilezile.

Ni mpaka pale utakapoamua kuongeza kiwango chako cha kifedha kwenye akili, ndipo unaweza kutoka hapo ulipo sasa.

Ndipo utakapoweza kuacha kujizuia kupata fedha zaidi ya unavyopata sasa. 

Hili litakuondoa kwenye mazoea na utajisukuma kuchukua hatua zaidi.

Utaanza kuongea hadithi tofauti, utaanza kujichanganya na watu tofauti na utaanza kutafuta taarifa tofauti , ambazo zitakusukuma wewe kuwa zaidi.

 

STADI ZA KAZI---DARASA LA SABA ( STD 7 )----MUZIKI--Kusoma na kuandika Muziki , Utunzi na Uimbaji Nyimbo , Ala za Muziki---NUKUU ZA SOMO----NOTES----KWA SHULE ZA MSINGI---TANZANIA-----( PDF )

 

Sunday, March 14, 2021

MAPUMZIKO NI KAMA KUJICHAJI KAMA BETRI , ILI UREJEE TENA KAZINI.

Maisha yana matukio mengi ambayo yanatuchosha na kufanya miili yetu iwe imeishiwa nguvu wakati mwingine. Tunapopata mapumziko au kulala basi tunajikuta kama tumeongezewa nguvu tena ya kuendelea na kazi. Nafasi ya mapumziko imekuwa ni njia inayofanya watu wapate kuchangamka na kuwa na ari mpya tena. Tunaona namna vipindi vya mapumziko vipo mashuleni, semina, michezo mbalimbali na hata sehemu za kazi ili watu wapate kurejea tena mara baada ya kazi au kufanya jambo kwa muda mrefu.

Watu wanapotoka kutoka katika mapumziko huwa na nguvu za kuendelea na nafasi nyingine ya mambo. Huwa nafurahia sana ninapoona wachezaji wa mpira wanapopata dakika chache za mapumziko na marejeo yao ya dakika nyingine 45 huwa na ari mpya, nguvu na kasi mpya. Hivi ndivyo ilivyo nguvu ya mapumziko inapofanywa kwa kiasi ili kurejesha nguvu.

Zama tuishizo sasa watu huzidisha mapumziko na kufanya zaidi ya mapumziko. Mapumziko haya hupelekea uzembe na uvivu ambao watu hujisahau kuwa faida ya mapumziko ni muda mfupi kisha unarejea kazini. Wengine wamefanya mapumziko ya kazi hadi wamepoteza kazi, wapo ambao wamefanya mapumziko hadi wamesahau tena kurejea kusoma na wapo ambao walifunga biashara wakaishia katika mapumziko ambayo yaliwaletea hasara baada ya faida.

Mapumziko ni sawa na pale ambapo betri limeishiwa chaji basi linachajiwa na likishajaa basi linatumika kufanikisha tena kazi. Likijaaa halafu lisitumike kuna nafasi ya kuharibika baada ya muda kupita. Kitu kinachopumzika muda mrefu huanza kuharibika. Jaribu kuangalia vitu kama magari yakiachwa muda mrefu bila kufanyiwa chochote huanza kuharibika tairi na kutu huwa inaanza kushambulia maeneo ya gari. Mapumziko yakidumu bila kuangalia muda ni kutayarisha kufa kwa kitu.

Fanya kazi kweli kweli ila jipe nafasi fulani ya muda kupumzika kwa lengo kuikuza afya na nguvu na si kufanya ulevi wa mapumziko. Mstoa Marcus anasema “Rest is for recharging, not for indulgence. Take only what is sufficient for your health and vitality. Too much rest—like too much food or drink—defeats its purpose, weakening the body and dulling the spirit”. Ikiwa na tafsiri “Mapumziko ni kwa kujichaji, sio ulevi. Chukua mapumziko kwa kutoshea afya na nguvu. Mapumziko ya kuzidisha ni sawa na ulaji au unywaji ulopitiliza moja kwa moja huondosha fokasi, hudhoofisha mwili na kuitia kiza roho”.

Muda wa mapumziko husisha kutuliza akili yako, kulala kwa muda wa kiasi, kuwa mbali na mitandao, tafuta eneo zuri la asili au fanya matembezi ya maeneo tulivu. Utulivu huu husaidia mapumziko yawe imara na kumsaidia mtu kumaliza likizo au muda wake wa mapumziko akiwa na nguvu na ari mpya ya kurudi ulingoni. Maisha ni mapambano kuna wakati unatoka kidogo kupumzika kupata amsho jipya la kupambana.

KOCHA   MWL.  JAPHET   MASATU , DAR  ES  SALAAM.

WhatsApp + 255 716924136  /  + 255  755 400128

 

 

WAZA SASA , FANYA SASA , IJAYO HAIPO ISIKUSUMBUE SANA.

Wasiwasi au hofu ambazo huingia ndani ya maisha yetu ni pamoja na kufikiria wakati ujao utakuja na mambo gani tusoyajua. Mabadiliko yanayoweza kujitokeza wakati ujao ni chanzo kikubwa cha kutawaliwa na hofu na wasiwasi. Tunajawa na wasiwasi namna maisha yetu ya baadaye namna uchumi utakuwa, afya, magonjwa na mabadiliko mbalimbali ya mambo.

Si rahisi kusema usiwazie wakati ujao ikiwa sasa una mambo magumu unapitia, kipato ni kidogo, misiba inatokea, biashara zinaanguka, umaskini na habari za kutisha kama milipuko ya magonjwa na maeneo mengine yanakabiliwa na vita na njaa. Ni ngumu sana mtu kukuelewa kuwa achana kuifikiria kesho wakati hofu na wasiwasi upo juu ya hali zitakavyokuwa baadaye. Wakati wa sasa huachwa hivi hivi kwa wasiwasi ambao mtu anakuwa anatarajia namna mambo yatakavyokuwa mabaya siku zijazo.

Hofu na wasiwasi ni hali za kawaida zinazotutokea maishani ila zinapokuwa zimezidi hili ni tatizo la udhibiti wetu wa kujua mambo yepi yapo katika uwezo wetu na yepi yalo nje ya uwezo wetu. Habari kuhusu wakati ujao ni jambo usiloweza kulizuia kutokea ila una nafasi ya kuitumia sasa ikaweza kusaidia kukabiliana na mambo yatakavyotokea baadaye. Inawezekana mtu akawa na wasiwasi juu ya maisha yake kiuchumi yatakavyokuwa ila unaloweza kufanya sasa ni kufanya maandalizi ya uchumi wako, kuweka akiba, kuweka dharura na kufanya uwekezaji. Ijayo itakuja na tusiwe na udhibiti nayo ila nafasi ya sasa au wakati wa sasa tunaweza kufanya kitu au jambo.

Kujifunza jambo ambalo hujazoea kulifikiria siku za awali jua itakuwa ngumu sana kuliweza. Hivi ndivyo inavyokuwa ngumu kwa watu wengi kutoacha kuiwazia baadaye na wakapoteza kuitumia kabisa leo. Unajifunza kuipa uzito sasa kwa kujifunza kuituliza akili yako yote kufanya kitu kwa umakini wako wote bila kufikiria kuwa ipo kesho. Weka umakini katika maisha yako ya sasa, furahia mchakato wa maisha sasa bila kufikiria hadi upate kitu fulani siku moja. Ishi kwa wakati wa sasa na ijayo usiiwazie bali ije ikukute unaendelea kuishi kwa kuipa uzito sasa. Wakati ujao ni kiini macho maana unaposema utaikuta ijayo au kesho hutaikuta bali utaihesabu ijayo kama sasa. Kwanini upoteze uzito wa nafasi ya muda ulonayo sasa kwa kuwazia hali isiyo ya kweli bali kiinimacho ?.

Unapoacha kuiwazia ijayo unapata muda wa utulivu wa kufanya kitu kwa umakini na ufanisi. Unapokuwa na wasiwasi mkubwa wakati mwingine hufanyi chochote kile, wengine utakuta hali ya hofu inawafanya washindwe kutuliza akili, wanatetemeka, wanapoteza hamasa maana muda wote wanashindwa kufanya chochote wakitawaliwa na namna mambo siku za baadaye yatakavyokuwa mabaya au hatari. Ukiishinda hii hali unajenga nafasi ya kutumia wakati wa sasa vizuri na unakuwa imara zaidi.

Jifunze kuanzia leo kuwa kwa kila utakachokuwa unakifanya weka akili yako iwe sasa. Hili litakujengea nguvu na kuondoa hofu na wasiwasi wowote kuhusu wakati usio sasa. Mstoa Marcus anasema “Don’t worry about the future. By doing your best today, you’ll build the strength and resources to handle whatever tomorrow may bring”. Hii ikiwa na tafsiri “Usiwe na wasiwasi kuhusu ijayo. Ila Fanya kwa uzuri sasa, hili litakujengea nguvu na rasimali za kutosha kukabiliana na kesho itakavyokuja.

KOCHA  MWL.  JAPHET  MASATU , DAR  ES SALAAM.

WhatsApp + 255  716924136 /   + 255 716  924136


 

HIVI NDIVYO UNAVYOWEZA KUTAJIRIKA-----ANZA HAPO ULIPO.

Utajiri ni kitu ambacho kila mtu anakipenda, kwa sababu fedha ni hitaji muhimu kwenye maisha yetu ya kila siku.

Ila kwenye jamii yoyote ile, ni wachache sana wanaofikia utajiri, kwa sababu wachache hao kuna siri wanazozijua kuhusu fedha na utajiri, ambazo wengi hawazijui.

Je ungependa kuzijua siri hizo ili na wewe uweze kufikia utajiri kwenye maisha yako? Kama jibu ni ndiyo basi kaa hapa, maana umefika mahali sahihi.

Kabla hatujaendelea nikukumbushe kwamba kinachowatofautisha tajiri na masikini siyo umri, kuna matajiri vijana na wazee, na wapo masikini vijana na wazee.

Na wala siyo kiwango cha elimu, kuna matajiri ambao hawajasoma kabisa na waliofika viwango vya juu ambao ni masikini.
Na wala hawatofautiani kwa rangi, kabila au jinsia.

Kwenye kila kundi la watu, kuna matajiri na masikini.

Hivyo kitu pekee kinachowatofautisha matajiri na masikini ni kile wanachojua na hatua wanazochukua.

Hayo mawili tu, WANACHUJUA na WANACHOFANYA.

Hiyo ina maana kwamba kama ukijua kile matajiri wanachojua na ukifanya wanachofanya, lazima na wewe uwe tajiri.

Je upo tayari kujua, ili uweze kufanya na utoke hapo ulipo sasa? Kama jibu ni ndiyo, basi karibu ujue kile matajiri wanajua na kikusaidie kufanya wanavyofanya na uwe tajiri.

Kuna maeneo kumi kuhusu fedha ambayo matajiri wanajua tofauti na masikini na hatua wanazochukua kwenye maeneo hayo ni tofauti na wanazochukua masikini.

Eneo la kwanza ni dhana halisi ya fedha, wanavyoichukulia fedha matajiri ni tofauti kabisa na masikini.

Eneo la pili ni kipato, matajiri wanajua jinsi ya kuingiza kipato hata wakiwa wamelala.

Eneo la tatu ni matumizi, masikini ni wazuri kwenye matumizi na hapo ndipo wanaachwa nyuma.

Eneo la nne ni madeni, matajiri wanajua madeni mazuri na mabaya na wanayatumia kwa umakini mkubwa.

Eneo la tano kutengeneza kipato kisicho na ukomo, vipato vya matajiri huwa havina ukomo.

Eneo la sita ni kuweza kuendelea kuingiza kipato hata wanapokuwa wamestaafu, matajiri wanajua kujiandaa kwenye hilo mapema.

Eneo la saba ni kodi, matajiri huwa wanalipa kodi ndogo kuliko masikini na wanafanya hivyo kisheria kabisa.

Eneo la nane ni kulinda utajiri usipotee, kupata utajiri ni jambo moja, kuuliza usipotee ni jambo jingine ambalo wengi hawalijui.

Eneo la tisa kuwaandaa watoto kuridhi na kukuza utajiri waliotengeneza, matajiri wa kweli wanawaandaa watoto wao vizuri ili mali walizopata zisipotee.

Eneo la kumi ni utoaji, matajiri wanajua utajiri wao siyo wao peke yao, hivyo wamekuwa wanatoa kwa jamii na wanapotoa ndivyo wanavyopata zaidi.

MAAMUZI MAGUMU YANA GHARAMA , NDIO NJIA YENYE MATOKEO BORA KATIKA MAISHA.

Ukiangalia maisha yako utajishukuru kuwa katika maamuzi magumu ulowahi kuyafanya ndio yalokujengea uimara au kukupa mabadiliko makubwa maishani mwako. Ukiangalia unaona namna bila kuamua maamuzi magumu pengine usingekuwepo ulipo sasa. Maamuzi magumu hayaanza kufanyika sasa ila toka zama zilizopita miaka 2000 huko Ugiriki ambapo tunakutana na habari za Mgiriki aitwaye Demosthenes.

Demosthenes alizaliwa mwaka 384 kabla ya Kristu huko Ugiriki ya Zamani. Utoto wake alizaliwa mtu ambaye alikuwa si imara katika mwili wake, alikuwa na tatizo la kutamka au kigugumizi na tatu alipoteza wazazi wake ambapo walezi walipora mali za urithi zote alizoachiwa na baba yake ambazo zilkuwa dola milioni 11 za Kimarekani sawa na shilingi bilioni 25 na milioni 454 kwa sasa. Walezi walichomwachia ni nyumba ndogo tu na pesa wakaondoka nazo. Hali hii alopitia Demosthenes hata leo inajitokeza ambapo watoto wanaachiwa mali na wazazi wao ila ndugu au walezi wanatumia nafasi kudhulumu haki zao.

Maisha ya Demosthenes yangetosha kukata tamaa na pengine kutoona mwelekeo wa siku zijazo. Akiwa katika huo huo umri mdogo kabla ya miaka 20 alifanya maamuzi magumu ambayo yamebakia historia katika maandiko ya Kigiriki na hata leo tunamsoma kujifunza kwake. Maamuzi makubwa matatu aloyafanya ambayo yalimwinua kuwa moja ya wazungumzaji nguli kuwahi kutokea huko Ugiriki huwezi msahau Demosthenes na pia inasemekana ni moja ya waanzilishi wa sanaa ya uzungumzaji Duniani.

Demosthenes alipenda sana uzungumzaji licha kuwa na kigugumizi ila hilo halikuzuia kuamua kujifungia chini ya handaki na kunyoa nusu ya nywele katika kichwa ili asitoke nje. Ndani ya handaki alikuwa akisoma kwa kina vitabu kuhusiana na siasa, tamaduni za kigiriki na maarifa mengi.

Pili aliamua kujifunza kuzungumza huku akiwa na vijipande vidogo vidogo vya mawe mdomoni huku akikimbia. Zoezi hili halikuwa jepesi kwake kuwa unarudia rudia sentensi za kuzungumza huku na vijimawe na unakimbia katika upepo mkali. Maamuzi haya yalichangia kuzalisha mzungumzaji bora kuwahi kutokea Ugiriki. Zoezi lingine alikuwa akizungumza na huku anajitazama katika kioo mara kwa mara.

Maamuzi magumu aloyafanya Demosthenes ni mwaliko wa maisha tunayoishi sasa kuwa ili tuvuke hatua fulani kubwa katika maisha lazima tuwe tayari kulipa gharama ya kufanya maamuzi magumu ambayo yanaweza kutugharimu kwa muda ila yakazalisha matokeo makubwa siku zijazo. Unaweza kuwa unatamani kuwa na maisha bora ila unaogopa kufanya maamuzi magumu kuhusu maisha yako kwa kuanzisha mfumo wa maisha wenye kuhitaji ujitoe, ujitose, ujikaze na usijihurumie ili kuzalisha matokeo bora.

Maamuzi magumu yatakutisha na kukuogopesha sasa ila utakapoweza kuvuka njia ya maamuzi magumu hutabakia mtu wa kawaida. Fanya maamuzi magumu kwa chochote kile ukijua kwa kufanya maamuzi magumu hayo kuna mchakato utapitia utakaokuwa na maumivu ya muda ila wenye matokeo mazuri baadaye. Changamoto ni njia kwa watu wanaishi falsafa na changamoto hazikimbiwi.

KOCHA  MWL.  JAPHET   MASATU , DAR  ES  SALAAM , TANZANIA.

WhatsApp + 255 716 924136 /  + 255 755  400 128