Watu wengi tumekuwa na maisha ambayo tunakosa hata muda mzuri wa kutulia na kuangalia hatua zetu zilivyosogea na kufanya tafakari. Tunakosa kuyajua mengi yanayoendelea maishani mwetu hadi tunapokuja kugundua maisha yamefika sehemu mbaya ndo tunakumbuka kuwa tungekuwa na utamaduni wa kujichunguza mara kwa mara jioni huenda tungeanza kuona hatari inayokuja mbele yetu.
Wengi huwa hatuna utamaduni wa kuweka muda angalau dakika 30 kila jioni kujiuliza maswali namna siku zetu zilivyoenda na kufanya tathimini ya kesho itakavyokuwa. Jioni huenda zinapofika tayari tumechoka sana na shughuli za siku na hatukumbuki umuhimu wa kujifanyia tathimini. Wengine jioni wanaishia kuwa ni saa za kujiburudisha, kula na kustarehe kutokana na kazi za siku. Wanaokumbuka umuhimu wa kutenga muda kuangalia siku ilivyokwenda huenda ni wachache.
Umuhimu wa kuichunguza siku upo katika kutambua mabadiliko yaso kawaida ambayo huanza kujitokeza na kuwa rahisi kuyarekebisha. Unapokuwa na utaratibu wa kufanya tathimini kila siku lazima utagundua vitu fulani ambavyo kwa haraka utaviepuka ili isije kutokea madhara makubwa baadaye endapo vikiachwa au kuendelea kuchukuliwa kiwepesi. Wakati wa jioni unakupa kuona makosa yalojitokeza katika siku, unagundua ushindi ulofanikisha na unagundua maeneo ya kuyaboresha kwa siku zinazokuja.
Falsafa ya Ustoa inahimiza sana juu ya umuhimu wa tafakari za jioni na huwa zinajulikana kama “Evening meditation”. Kuwa ni tahajudi za jioni ambazo zinakupa picha ya kuangalia siku yako kama mchezaji na mtazamaji. Inakupa kuangalia yale uloyafanya, ulokosea na yepi ya kwenda kuboresha siku nyingine ikijitokeza. Wastoa hili wanahimiza ili uweze kuwa na udhibiti na usishangazwe na chochote maishani endapo kitatokea.
Sisi binadamu tuna mapungufu yetu ambayo hatuwezi kuyaona mpaka pale ambapo tunakuwa na wasaa wa kujitafakari, kujiuliza maswali na kutenga muda wa utulivu na kuyatazama maisha yetu. Tunapokuwa na tafakari tunagundua namna tusivyo imara katika matukio yanayojitokeza, wadhaifu katika tamaa za mwili au tusio na udhibiti wa hasira zetu pale ambapo tunatukanwa au kupishana kimawazo na wengine. Huwezi jua haya endapo hujipi wasaa wa kujitafakari hasa hasa muda wa jioni.
Dakika 30 ambazo utaanza kuzitenga kuanzia sasa na ukaweka uendelevu kila siku haijalishi mambo gani unapitia za kujitafakari itakuwa ni kujiwekea mazingira mazuri ambayo yatakusaidia kuyaelewa maisha yako kwa kina, kuishi kitoshelevu na zaidi kuishi bila kushangazwa na chochote katika maisha yako.
Dakika hizi zitenge katika mambo makubwa matatu. Moja ni kuandika mambo uloweza kuishi vizuri na watu au kukabiliana na tukio fulani. Pili ni kuandika mambo uloshindwa kufanya kama mwanafalsafa na Tatu andika njia ya kwenda kuwa mtu bora kutokana na yale ambayo ulishindwa na ulienda tofauti na misingi ulojiwekea. Unaweza kufanya hili zoezi ukiwa na sehemu ya kuandika, unaweza kufanya ukiwa eneo tulivu lisilo na usumbufu wowote au kelele. Kadri utakavyokuwa ukiendelea kufanya zoezi hili bila kuacha ndivyo utakavyokuwa unaweza kuona matokeo yake.
NA KOCHA MWL. JAPHET MASATU
WhatsApp +255 716 924 136 / ( + 255 755 400 128 )