Saturday, April 4, 2020

MFANYABIASHARA / MJASIRIAMALI : TOA ELIMU NA USHAURI SAHIHI KWA WATEJA WAKO,

Kwenye mlipuko unaoendelea sasa, kila mtu ni mwalimu, mshauri na mtaalamu wa magonjwa ya mlipuko. Hata mtu ambaye mwezi mmoja uliopita alikuwa hajui (na huenda mpaka sasa) hajui kwamba kirusi siyo kiumbe hai kamili, ni mshauri mzuri sana kwa wengine kuhusu mlipuko unaoendelea.

Wewe wape wateja wako elimu sahihi, ambayo umeitoa kwenye vyanzo sahihi. Usilete ujuaji wako au kukusanya taarifa za mtandaoni na kufikiri hiyo ni elimu. Nenda kwenye vyanzo vya uhakika, na kwa hili la Corona, sikiliza taarifa za serikali na tembelea tovuti ya Shirika la Afya Duniani (WHO), kwa anuani www.who.int kupata elimu sahihi kuhusu mlipuko huu wa Corona.
Mfano; kuna vitu vingi ambavyo watu wanashauriana kufanya, ambavyo siyo sahihi. Kwenye tovuti ya WHO, kuna kipengele wanakiita MYTH BUSTERS ambapo wanatoa ukweli kuhusu vitu visivyo sahihi wanavyoshauriana watu. Kama ulaji wa vitunguu hauzuii maambukizi ya Corona. Ingia kwenye tovuti hiyo, pata taarifa sahihi na kisha washauri wateja wako kwa usahihi.

MFANYABIASHARA / MJASIRIAMALI : USITUMIE NAFASI HII KUNUFAIKA ZAIDI.

Katika hali ya mlipuko kama huu, ambapo watu hawana uhakika wa lini hali itarudi kama kawaida, wanakimbilia kufanya manunuzi makubwa. Hapa mfanyabiashara unapata tamaa ya kuongeza bei kwa sababu uhitaji ni mkubwa. Watu wanaweza kununua kwa bei juu kwa sababu hawana namna.
Lakini tambua kwamba huu mlipuko utapita, na kama unataka biashara yako iendelee kuwepo na iwe na wateja waaminifu hata baada ya mlipuko huu, usiutumie kujinufaisha zaidi.
Usiongeze bei kwa sababu tu kila mtu anaongeza bei na uhitaji ni mkubwa. Kama ulikuwa na mzigo wa kutosha kabla ya janga hili kuanza, endelea kuuza kwa bei zile zile. Na kama uhitaji ni mkubwa, wape kipaumbele wale wateja ambao umekuwa nao kwa muda mrefu.
Kama mlipuko umepelekea gharama za wewe kupata unachouza kuwa juu, waeleze wazi wateja wako kuhusu mabadiliko hayo. Usikimbilie tu kupandisha bei, jua wateja hawatasahau hilo na watavunja uaminifu kwenye biashara yako baada ya janga hili kupita.

Mfano; wauzaji wa vitu muhimu kama dawa, vifaa vya kujikinga, vyakula na vitu vingine wamekuwa wanapandisha bei katika nyakati kama hizi, wewe usifanye hivyo.

MFANAYABIASHARA / MJASIRIAMALI : JIKINGE WEWE NA TIMU YAKO.

Wewe mfanyabiashara ukiumwa au wasaidizi wako wakiumwa, biashara itaathirika zaidi. Hivyo wewe na timu yako mnapaswa kuwa mstari wa mbele katika kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huu.
Hakikisha njia zote za kujikinga zinajulikana na kutumika na kila anayehusika kwenye biashara yako. Njia kuu zinafahamika, kunawa mikono kwa maji safi na sabuni, kuepuka kushikana, kuepuka kushika uso. Hivi vyote vinapaswa kufanyiwa kazi.
Pia eneo la biashara liboreshwe kwa namna ambayo linapunguza maambukizi. Ukaribu baina yako au watoa huduma na wateja unapaswa kupunguzwa. Maeneo ya kunawa mikono yanapaswa kuwepo au dawa za kusafisha mikono kupatikana kwa urahisi.
Usiache kujilinda wewe na timu yako kwa kuepuka gharama, ukiugua wewe au timu yako, ni tiketi ya kifo kwa biashara yako.

Mfano; kwenye kila eneo la biashara kunapaswa kuwa na sehemu ya watu kunawa mikono kwa maji na sabuni au kwa dawa maalumu. Pia kama biashara inahusisha watu wengi, kuwekwe utaratibu wa kupunguza msongamano wakati huu. Kwenye huduma za afya, watoa huduma wanapaswa kuwa na vifaa vya ziada vya kujilinda wao wenyewe.

MFANYABIASHARA / MJASIRIAMALI : BADILI MFUMO WA BIASHARA KUENDANA NA MABADILIKO YANAYOTOKEA.

Maisha ya watu yamebadilika katika wakati huu wa mlipuko wa ugonjwa wa Corona. Biashara yako pia inapaswa kubadilika ili kuweza kuwahudumia vizuri wateja wako.
Kama watu wanatumia muda mwingi nyumbani kuliko kutoka, usiendelee kusubiri wateja waje kwenye biashara yako, badala yake wafuate huko majumbani.
Badili mfumo wa biashara yako kutoka kusubiri wateja waje eneo la biashara na kufanya wateja waweze kuagiza wakiwa nyumbani na kupelekewa au kutumiwa kile walichoagiza.
Hatujui lini hali hii itaisha kwa hakika, hivyo usijiambie unasubiri mambo yatulie, badala yake chukua hatua sahihi ili uendelee kuwahudumia wateja wako.

Mfano; biashara ambazo zimekuwa zinategemea wateja waje kwenye biashara, ni wakati sahihi sasa kuweka mfumo wa wateja kuweza kuagiza wakiwa nyumbani na kisha kupelekewa au kutumiwa walichoagiza.

MFANYABIASHARA / MJASIRIAMALI : WAPE WATEJA WAKO MATUMAINI SAHIHI.

Wakati wa mlipuko kama huu, hakuna anayejua nini kitatokea kesho, na kadiri mambo yanavyozidi kuwa mabaya, ndivyo watu wanaendelea kutabiri kwamba mambo yatakuwa mabaya zaidi.
Watu wanatishana na kupeana wasiwasi mkubwa. Wapo wanaosema huu ndiyo mwisho wa dunia. Kila mtu ana maoni yake. Lakini tunajua kitu kimoja kuhusu maoni, siyo ukweli.
Hakuna aliyeweza kutabiri ujio au madhara ya mlipuko huu, na hakuna anayeweza kutabiri kwa uhakika mambo yataendaje. Tunachojua ni kwamba tutavuka hili, kama ambavyo jamii ya binadamu imevuka mengi siku za nyuma.
Hivyo wewe kuwa chanzo cha matumaini sahihi kwa wateja wako. Katika hali ya wasiwasi kama hii, watu wanapenda kuwasikiliza wale wanaoleta habari njema, lakini siyo habari njema hewa. Bali habari njema sahihi.
Usiwe mtu wa kutoa habari mbaya kwa wateja wako, utawatisha na kuwafanya waahirishe kununua. Badala yake kuwa mtu wa kutoa habari njema, mtu wa kuwapa wateja wako moyo na hapo watajisikia vizuri na kununua. Ukiweza kuwaonesha jinsi kile unachouza kinawasaidia kupunguza makali ya mlipuko, wateja wanakujali zaidi.

Mfano; biashara za ushauri na mafunzo zinapaswa kuwa chanzo cha matumaini kwa wateja wake. Kwa kuwaonesha kwamba hili linaloendelea siyo mwisho wa dunia na mambo yatakwenda vizuri baada ya hili.

MFANYA BIASHARA / MJASIRIAMALI : JUA THAMANI NA WAELEZE WATEJA WAKO

 BIASHARA  pekee zitakazovuka kipindi hiki cha Mlipuko wa ugonjwa wa   CORONA salama ni zile ambazo zinatoa thamani kubwa kwa wateja wake na jamii kwa ujumla. Zile biashara ambazo watu hawawezi kuishi bila ya kuwa na kile kinachouzwa.
Hivyo huu ni wakati wa wewe kukaa chini na kujiuliza ni thamani gani unayoitoa kwa wateja wako. Huenda umezoea kuuza na kupokea fedha na umesahau thamani ipi unatoa.
Jiulize ni tatizo au hitaji gani la wateja ambalo biashara yako inatoa. Kisha waeleze wateja thamani hiyo vizuri, waoneshe jinsi ambavyo wanaihitaji thamani hii wakati huu wa mlipuko.
Mfano; biashara za huduma za kifedha zinatumia nafasi hii kuonesha jinsi ilivyo salama kutuma na kupokea fedha kwa mtandao na siyo fedha taslimu. Hii ni thamani kubwa ambayo mteja au mfanyabiashara hakuwa anaiona, lakini kwa sasa iko wazi.