Monday, December 30, 2019

PUNGUZA SANA AU ACHA KABISA KUTUMIA MITANDAO YA KIJAMII KAMA HAIKUINGIZII KIPATO

Mitandao ya kijamii imekuwa chanzo cha wengi kupoteza muda mwingi wa maisha yao. Pia imekuwa chanzo cha wengi kupata msongo na sonona kutokana na kufuatilia maisha ya wengine na kujilinganisha nao, kitu ambacho siyo sahihi kwa sababu wengi huigiza kwenye mitandao hiyo.
Hivyo ili kuepuka kupoteza MUDA  na  UTULIVU wako, na ili kupata AMANI ya moyo na kuepukana na msongo na sonona, acha kabisa kutumia mitandao ya kijamii. Jaribu hili , ile mitandao ambayo inachukua muda wako mwingi na kila ukiingia unatoka ukiwa unawaonea wengine wivu kwa mambo mazuri yanayoendelea kwenye maisha yao, acha kuitumia mara moja.
Ukiacha kutumia mitandao hii utajikuta ukiwa na muda mwingi wa kufanya kazi zako, kujifunza kupitia kusoma vitabu na hata muda wa kukaa na wale watu wa karibu na muhimu kwako.
Tumia mitandao hii ya kijamii kama tu inakuingizia KIPATO, kama unafanya biashara na unatangaza kupitia mitandao hii na inakuletea wateja, basi endelea kutumia kwa madhumuni ya biashara. Tofauti na hapo achana nayo.
Mitandao ya kijamii inaingiza fedha kupitia wewe, wewe ndiyo bidhaa inayouzwa na mitandao hii kwa wale wanaotangaza biashara zao. Hivyo kama na wewe huingizi fedha kupitia mitandao hii, achana nayo, usikubali kuuzwa kwa wengine.
Wapo wanaosema kama siyo mitandao ya kijamii hawawezi kukutana na maarifa mazuri kama haya. Hilo siyo kweli, maarifa mazuri yanapatikana pale unapoyatafuta, na mitandao ya kijamii siyo sehemu nzuri kwako kujifunza.
Hivyo acha kutumia mitandao ya kijamii 2020, labda kwa lengo la kibiashara pekee.

TOFAUTI KATI YA TAJIRI NA MASIKINI KATIKA KUJIFUNZA NA KUKUA...

MATAJIRI huwa wanajifunza kila siku na kuendelea kukua zaidi. Wanajisomea vitabu na kutafuta maarifa mbalimbali yanayowawezesha kupiga hatua. Wanaamini kuna mengi hawajui hivyo kujifunza zaidi, na hilo linawafanya wafanikiwe.
 
MASIKINI wao hawana muda wa kujifunza, wanaamini tayari wanajua kila kitu. Hawasomi vitabu ila habari za udaku na mitandao ya kijamii ndivyo wanapenda kufuatilia. Kwa njia hii wamekuwa hawajifunzi na hivyo kubaki kwenye umasikini wao.

Wednesday, December 25, 2019

TOFAUTI YA TAJIRI NA MASKINI KATIKA KUDHIBITI FEDHA.


MATAJIRI  wana uwezo wa kudhibiti fedha zao na hivyo kuweza kupiga hatua zaidi. Hawana ulimbukeni kwenye fedha, hawabadili maisha yao kwa sababu wamepata fedha zaidi. Na pale wanapopata fedha zaidi, wanaiwekeza. 

MASKINI  hawawezi kudhibiti fedha zao, wana ulimbukeni mkubwa kwenye fedha. Wakipata fedha zaidi wanabadilika, wanaanza kununua vitu visivyo muhimu mpaka fedha hiyo iishe. Kwa namna hii, wanashindwa kupiga hatua na kila wanapopata fedha zaidi, ndiyo wanapotea zaidi.
Acha ulimbukeni kwenye fedha, jifunze jinsi ya kudhibiti fedha zinazokuja kwako ili uweze kuzitumia kupiga hatua zaidi.