(1). WATEJA.
Wateja
ndiyo kipande cha kwanza muhimu sana cha biashara yako. Kama hakuna
wateja basi hakuna biashara. Lazima uchague biashara yako inakwenda
kuwahudumia watu gani, wanaopatikana wapi na unawafikiaje. Biashara
lazima ijenge wateja ambao wanaotegemea kwa kile inachofanya.
Unapoingia
kwenye biashara anza na kitu ambacho tayari watu wanajihitaji, hivyo
wewe unakuja na suluhisho na kuhakikisha watu wanajua uwepo wako kwenye
biashara hiyo. Hivi ndivyo unavyoweza kutengeneza wateja wa biashara
yako.
(2). MAHITAJI YA WATEJA.
Ukishachagua
aina ya wateja ambao biashara yako inawahudumia, unapaswa kujua yale
mahitaji yao ya msingi. Yale mahitaji yanayowasukuma kununua kile
ambacho wewe unauza. Ukishayajua mahitaji hayo, jipange kuyatimiza kwa
namna ambayo hakuna mfanyabiashara mwingine anayeweza kuyatimiza hivyo.
Kuna
vitu viwili muhimu sana unapaswa kujua kuhusu mahitaji ya wateja wako,
hofu na tamaa. Wateja wa biashara yako wanafanya maamuzi kwa kutumia
hisia hizo mbili, labda wana tamaa ya kupata kitu fulani au wana hofu ya
kupoteza kitu fulani. Jua hisia hizo mbili za wateja na zitumie katika
mauzo.
(3). NAFASI YAKO KATIKA SOKO.
Biashara
yoyote unayofanya, kuna nafasi ambayo upo kwenye soko, unaweza kuwa
ndiyo namba moja yaani wateja wanakufikiria wewe kwanza au ukawa haupo
kwenye namba za juu, yaani wateja hawakufikirii kabisa. Ili kukuza
biashara yako, unapaswa kuwa kwenye nafasi ya juu kwenye soko lako.
Unapaswa kuwafanya wateja wako wakufikirie wewe kwanza inapokuja kwenye
mahitaji yao.
Matangazo,
alama za kibiashara, rangi za kibiashara, kauli mbiu na hata utamaduni
wa tofauti wa biashara yako ni vitu vinavyowafanya wateja wakukumbuke na
kukufikiria muda mrefu. Tengeneza picha ya tofauti ya biashara yako
ambayo inawafanya wateja wakufikirie wewe mara zote.
(4). UBOBEZI WA BIASHARA YAKO.
Je
biashara yako imebobea kwenye nini? Biashara yako inajulikana kwa kipi?
Je ni kitu gani wateja wanapata kwako ambacho hawawezi kupata kwa
wafanyabiashara wengine?
Hayo
ni maswali muhimu ya kupima ubobezi wa biashara yako. Biashara
iliyobobea kwenye kile inachofanya ndiyo biashara ambayo inapata
mafanikio makubwa sana.
Jua
ni aina gani ya biashara unayofanya, na kipi cha tofauti unachotoa kwa
wateja wako kisha kazana kutoa kitu hicho kwa namna ambayo wateja
hawawezi kupata sehemu nyingine na utaweza kufanikiwa sana kwenye
biashara unayofanya. Bobea kwenye vitu vichache na hilo litakufanya
kinara kuliko kung’ang’ana kufanya vitu vingi.