Friday, June 14, 2019

KILA HATUA UNAYOPIGA HUZALISHA KIKWAZO

Kwenye fizikia, kuna kanuni tatu kuu za mwendo ambazo mwanasayansi Isaac Newton alizigundua.
 
Kanuni ya kwanza inasema kitu kilichopo kwenye mwendo kinaendelea kuwa kwenye mwendo mpaka nguvu ya nje itakapotumika kukizuia.
 
Kanuni ya pili inasema nguvu ya kitu kilichopo kwenye mwendo inategemea uzito wake na mwendokasi wake.
 
Na kanuni ya tatu inasema kila mwendo huwa unazalisha upinzani.
 
Ni kanuni ya tatu ambayo tunakwenda kuijadili hapa kwenye dakika moja ili uelewe kwa nini baadhi ya vitu vinatokea kwenye maisha yako na hatua sahihi kwako kuchukua.
 
Kila mwendo unaoanzisha, kuna mwendo mwingine utakaoanzishwa kuzuia mwendo huo.
 
Unapojaribu kwenda mbele, kuna mtu atajitokeza kukurudisha nyuma.
 
Hii ndiyo inasababisha mafanikio kuwa magumu. Kwa sababu siku unayoamua kwamba unataka kufanikiwa, zitaibuka kila aina ya nguvu kukupinga, kutaibuka kila kikwazo kwenye njia yako ya mafanikio.
 
Unapojua hili, unajipanga kwa upinzani kwa kila hatua unayopanga kupiga na hujidanganyi kwamba mambo yataenda vizuri yenyewe kama wengi wanavyofanya.
 
Usishangae pale ambapo marafiki ulionao sasa watageuka kuwa maadui zako pale unapotangaza kwamba unataka kufanikiwa sana. ulipokuwa kawaida mlikuwa marafiki, unapopanga kupiga hatua zaidi wanakuwa maadui, hiyo ni kanuni ya asili, huwezi kupingana nayo.
 
Usikubali kipingamizi chochote kikuzuie wewe kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako, jua kwa kila hatua utakayopanga kuchukua kuna kipingamizi kitaibuka na hivyo jiandae kukivuka.

KILA MTU ATAKUFA , NI BORA UULIWE NA KAZI !


Kila mtu atakufa, hilo halina ubishi. Hii ni hukumu uliyoipata siku unayozaliwa, ambacho hujui ni siku gani hukumu hiyo itakamilika.
 
Lakini kuna kitu kingine muhimu sana kuhusu kifo ambacho wengi tumekuwa hatukitafakari, ambacho tukikielewa kitatusaidia sana.
 
Kila mtu kuna kitu kitakachomuua. Ndiyo, kuna kitu ambacho kitakuua, yaani kitachangia kwenye kifo chako.
 
Kuna ambao ulevi utawaua, kwa kuendekeza sana ulevi mwili unachoka na kupata magonjwa ambayo yanachangia kifo chao.
 
Kuna ambao chakula kitawaua, kwa kushindwa kula kwa nidhamu wanakuwa na afya mbovu ambayo inaleta magonjwa yanayowaua.
 
Kuna ambao wasiwasi na hofu vitawaua, kwa kuwa na wasiwasi na hofu mara zote kunaufanya mwili uwe haifu na hivyo kushindwa kuhimili magonjwa mbalimbali.
 
Kuna ambao mapenzi yatawaua, kwa kushindwa kudhibiti hisia zao za mapenzi na ngono wanajikuta kwenye hatari zinazoondoa maisha yao.
 
Kuna ambao kazi zitawaua, kwa kuweka muda na nguvu zao nyingi kwenye kazi zao kunachosha miili yao na kuibua magonjwa yatakayowaua.
 
Kuna ambao uvivu utawaua, kwa kukaa muda mrefu na kutokuwa na majukumu makubwa, mwili unakuwa mzembe na kushindwa kupambana na magonjwa na hilo kupelekea kifo.
 
Ndugu  yangu, hakuna atakayetoka hapa duniani akiwa hai, na kila mtu kuna kitu ambacho kitamuua.
 
Wito wangu kwako, chagua sumu yako vizuri, kile ambacho kitakuua, basi kiwe na maana kwako na hata wengine pia. Kuliko uuliwe kwa pombe, ulevi au ngono, ni bora uuliwe na kazi, maana kazi hiyo itakuwa na maana kwako na kwa wengine pia.

TABIA ZA WATU WALIOFANIKIWA SANA

(1). HAMASA.

Sifa ya kwanza ambayo watu waliofanikiwa wanaitaka kuwepo kwenye kile wanachofanya na chenye maana kwao ni hamasa. Wanapokuwa na nafasi ya kuchagua kipi cha kufanya, wale waliofanikiwa sana wanachagua kile ambacho wana hamasa kubwa ndani yao ya kukifanya.

Kitu hicho wanakuwa wanakipenda kutoka ndani ya mioyo yao na hivyo kusukumwa kukifanya vizuri kuliko wengine. Wanakuwa tayari kukifanya muda wote bila ya kuchoka na hawaangalii sana ni kiasi gani wanalipwa katika kukifanya.

Unapofanya kile unachopenda kufanya, kile ambacho una hamasa kubwa ndani yako kukifanya, unakuwa hufanyi kazi, bali unafanya maisha na hivyo nafasi ya wewe kufanikiwa inakuwa kubwa zaidi.

Kila siku jiulize swali hili muhimu; ni kitu gani kinanipa hamasa kubwa kwenye maisha yangu, kazi yangu na biashara yangu? Kisha nenda kafanye hicho, utazalisha matokeo bora zaidi kuliko wengine na hilo litakuwezesha kufanikiwa zaidi.


( 2 )MAHUSIANO.
Mahusiano ya kijamii ni muhimu sana kwenye maana ya maisha. Wale wanaokuwa wametengwa na watu wengine huwa wanaripoti maisha yao kupoteza maana. Maana ya maisha yetu ni matokeo ya vile ambavyo wengine wanapokea kile tunachofanya.

Watu waliofanikiwa sana wamekuwa wakichagua kwa umakini watu wanaojihusisha nao kwenye kazia au biashara wanazofanya. Wanafanya kazi au biashara zinazowawezesha kutengeneza mahusiano bora na wale ambao wanawapenda, wale ambao tabia walizonazo zinaendana nao.

Watu waliofanikiwa pia huwa wanapenda kuzungukwa na watu wanaowapa changamoto ya kupiga hatua zaidi. Hivyo wanafanya kazi au biashara ambayo wamezungukwa na watu wanaofanikiwa na wanaopiga hatua kufanikiwa zaidi. Watu hawa wanakuwa msukumo kwao kupiga hatua zaidi.

Usikubali kufanya kazi au biashara ambayo wengi unaoshirikiana nao hamuendani kitabia wala kimtazamo, itakuwa kikwazo kikubwa kwako kufanikiwa. Lakini pia kazana kuzungukwa na watu ambao wanakusukuma uwe bora zaidi, zungukwa na watu ambao wanapiga hatua zaidi ili iwe chachu kwako kupiga hatua zaidi.

Mahusiano yako na wengine kwenye kazi au biashara unayofanya yanapokuwa mabovu, maisha yako yanakuwa mabovu pia na hilo linachangia maisha yako kukosa maana.

( 3 ).KURIDHIKA.

Maisha yanakuwa na maana pale ambapo kile unachofanya kinakuridhisha, pale moyo wako unaporidhika na kile unachofanya unafurahia maisha yako na kuona yana maana kubwa.

Watu waliofanikiwa sana wamekuwa wanachagua kufanya kazi au biashara ambayo inawapa hali ya kuridhika, na hilo limekuwa linawawezesha kufanikiwa zaidi kupitia kile wanachofanya.

Kuridhika kwenye kile tunachofanya kunachangiwa na vitu viwili;

Moja ni ukuaji binafsi. Huwa tunaridhika pale ambapo kile tunachofanya kinatusukuma kukua zaidi ya pale tulipo sasa. Kama unajiona ukipiga hatua kadiri unavyokwenda, unaridhika zaidi.

Mbili ni mchango kwa wengine. Huwa tunaridhika pale ambapo kile tunachofanya kinakuwa na mchango kwa wengine. Pale wengine wanapotushukuru kwa kile tunachofanya, tunaridhika sana.

Hivyo chagua kazi au biashara ambayo inakupa nafasi ya kukua zaidi, ambayo unapiga hatua kadiri unavyokwenda na siyo kudumaa au kushuka chini. Pia kazi au biashara hiyo iwe inagusa maisha ya wengine, inaongeza thamani kwa wengine na kuwafanya kuwa bora kuliko walivyokuwa. Watu hao wanapokushukuru kwa mchango ambao umekuwa nao kwao, unaridhika sana na maisha yako yanakuwa na maana.

( 4 ). UMUHIMU.

Kila tunachofanya au kinachotokea kwenye maisha yetu, huwa tunakilinganisha na maeneo mengine ya maisha yetu. Kama kitu hicho kinaendana na maeneo mengine ya maisha yetu, basi tunaona maisha yetu yanakuwa na maana kubwa. Lakini kama kinachotokea hakiendani na maeneo mengine ya maisha yetu, maana inakosekana.

Watu waliofanikiwa sana wamekuwa wanachagua kufanya vitu ambavyo ni muhimu kwao, ambavyo vinaendana na haiba zao, sifa zao na hata maeneo mengine ya maisha yao.

Kama mtu anajichukulia kuwa mwaminifu, kazi au biashara inayojenga mazingira ya uaminifu inakuwa muhimu zaidi kwake na kuleta maana kwake. Lakini mtu huyo akafanya kazi ambayo haina uaminifu, anaweza kupata fedha, lakini ndani yake atakosa maana, kwa sababu kile anachofanya hakiendani na vile yeye alivyo.

Chagua kufanya kazi au biashara ambayo inaendana na wewe, ambayo inatumia na kukuza zile sifa binafsi zilizopo ndani yako na pia inachangia katika kuyakamilisha maisha yako. Yaani ukiangalia kila unachofanya, kinachangia maisha yako kukamilika.

Rafiki, hizo ndiyo sifa nne za kuangalia wakati unachagua kazi au biashara ya kufanya ili iwe na maana kwako na uweze kufanikiwa zaidi.

Kama tayari upo kwenye kazi au biashara ambayo unaona haina maana kwako, una hatua mbili za kuchukua ili uweze kupata maana na kufanikiwa zaidi.

Hatua ya kwanza ni kutafuta maana kwenye kazi au biashara hiyo. Huenda hujapata maana kwa sababu hujaitafuta, umekuwa unafanya tu kwa mazoea siku zote na hivyo hujawahi kutafakari na kuona maana. Anza kwa kuangalia sifa hizi nne kwenye kile unachofanya, jiulize ni kitu gani kinakupa HAMASA sana kwenye kazi au biashara unayofanya. Angalia wale ambao UNAHUSIANA nao kupitia kazi au biashara hiyo na ona ni watu gani bora zaidi unaoweza kutengeneza nao mahusiano. Tafuta KURIDHIKA kwa kukua zaidi na kufanya maisha ya wengine kuwa bora kupitia kazi au biashara unayofanya. Na mwisho angalia ni jinsi gani kazi au biashara hiyo ina UMUHIMU kwenye maisha yako, angalia inayakamilishaje maisha yako kwa kuendana na sifa zako nyingine.

Hatua ya pili ni kuondoka kwenye kazi au biashara hiyo na kwenda kufanya ile yenye maana kwako. Kama umejifanyia tathmini na hujaweza kupata maana kwenye kazi au biashara unayofanya sasa, kuendelea kubaki hapo hakutaleta maana kwenyewe. Badala yake chukua hatua ya kuondoka kwenye kazi au biashara hiyo na kwenda kufanya ile ambayo ina maana kwako. Hata kama hutaweza kuondoka kwa haraka, lakini lengo linapaswa kuwa kutengeneza maisha yenye maana.

FURSA YA KILIMO CHA MAPARACHI---------- " Fursa Afrika Mashariki Blog "

Wednesday, June 12, 2019

JE, WAJUA BIASHARA NI KAMA KIUMBE ?? HUZALIWA , HUKUA , HUDUMAA NA KUFA ?

" BIASHARA "  ni kiumbe hai, ambacho kinazaliwa, kinakua au kudumaa na mwishowe kinakufa. Biashara ni kitu ambacho kina maisha yake ya kujitegemea na jinsi ambavyo kinapewa uhuru wake ndivyo inavyofanikiwa zaidi.
Lakini pia biashara huwa inakuwa na tabia zake, ambazo zinaweza kuifanya ifanikiwe zaidi au kuizuia isifanikiwe. Tabia hizi za biashara huwa zinatokana na tabia ambazo mwanzilishi wa biashara hiyo anazo

Na hii ndiyo maana kwenye kila biashara kuna utaratibu na utamaduni fulani uliopo, ambao huwa ni mgumu sana kubadilisha. Hata wafanyakazi wapya wanapokuja kufanya kazi kwenye biashara hiyo, baada ya muda hujikuta wameshavaa utamaduni huo wa biashara.

Utaratibu na utamaduni uliojengeka kwenye biashara nyingi huwa ni matokeo ya tabia za mwanzilishi wa biashara, huwa siyo kitu ambacho kimetengenezwa kwa makusudi ambacho kinaweza kuwa na msaada kwenye biashara hiyo.

Hivyo unakuta biashara imejijengea tabia ambazo siyo nzuri na zinakuwa kikwazo kwa maendeleo ya biashara hiyo. Ukiangalia tabia za biashara hiyo, zinakuwa zinaendana sana na tabia za mwanzilishi wa biashara hiyo.

Mfano kama mwanzilishi wa biashara ni mzito kwenye kufanya maamuzi, basi ufanyaji wa maamuzi wa kila mtu kwenye biashara unakuwa ni mzito sana. Maamuzi hayafanyiki kwa wakati na biashara inazikosa fursa nzuri za kukua zaidi.

Kama mwanzilishi wa biashara hawezi kupangilia vitu vyake vizuri kwenye maisha yake binafsi, unakuta biashara nayo haina mpangilio mzuri, vitu vipo hovyo hovyo na hakuna utaratibu wowote unaotumika kwenye kufanya vitu.

Kama mwanzilishi wa biashara ana tamaa, biashara nzima inaendeshwa kwa tamaa, kila aliyepo kwenye biashara hiyo anakuwa na tamaa na kujali mambo yake zaidi kiliko ya biashara.

Hivyo popote ambapo biashara imekwama, kwa hakika ndipo ambapo mmiliki wa biashara hiyo amekwama. Biashara haiwezi kukua zaidi ya ukuaji wa mmiliki wa biashara hiyo.