Kama unataka kufurahia biashara yako, basi unapaswa kufanya kazi nje ya biashara na siyo ndani ya biashara. Kufanya
kazi ndani ya biashara ni pale ambapo unakuwa bize na shughuli za kila
siku za biashara hiyo, kuuza, kuwahudumia wateja na kuzalisha au kuandaa
bidhaa na huduma unazouza. Japokuwa
unaweza kuona hilo ni muhimu na hata kupenda sana kulifanya, linakuzuia
kuikuza zaidi biashara yako, maana unapofanya kazi ndani ya biashara,
unachoka sana na hupati nafasi ya kuona mbali zaidi ya kile unachofanyia
kazi kwenye biashara hiyo.
Kufanya
kazi nje ya biashara yako ni pale ambapo unaiangalia biashara yako kama
mtu baki, kuangalia kila kitu kinavyofanyika na kuona uimara na udhaifu
wako. Ni sawa na kupanda juu angani kisha kuangalia biashara yako kwa chini, na kutathmini kila kinapofanyika. Unapofanya
kazi nje ya biashara, hufikirii yale majukumu ya kila siku ya biashara,
bali unaangalia kule ambako biashara inakwenda na uwezo wa kufika huko.
Kama
unataka biashara yako ikue, lazima uweze kufanya kazi nje ya biashara
yako, uweze kuiangalia biashara kama mtu wa pembeni na kupata picha ya
pale ilipo sasa na inapoweza kufika.