Sunday, May 5, 2019

WEWE NA BIASHARA YAKO NI VITU VIWILI TOFAUTI

Hiki ni kitu ambacho kila mfanyabiashara anapaswa kuambiwa, tena kupigiwa kelele kila mara mpaka aelewe. Kwa sababu kama wafanyabiashara wakielewa hili, nusu ya matatizo ya biashara yatatoweka yenyewe.
 
Sehemu kubwa ya matatizo ya biashara yanasababishwa na mfanyabiashara kufikiri yeye ni biashara yake, kitu ambacho siyo kabisa.
 
Biashara nyingi hazikui kwa sababu hakuna mpaka baina ya biashara na mmiliki wa biashara. Mtu anaweza kutoa fedha kiholela kwenye biashara kwa sababu anaona biashara ni yake. Kitu ambacho kinakuwa na athari kubwa sana kwenye ukuaji wa biashara hiyo.
 
Ndugu , naomba nikusisitizie hili, na liandike mahali ambapo utaweza kulisoma kila siku; WEWE SIYO BIASHARA YAKO, wewe na biashara yako ni vitu viwili tofauti kabisa.
 
Wewe una maisha yako, ndoto zako na mahusiano yako, biashara ina maisha yake, ndoto zake na mahusiano yake. Kinachowaunganisha wewe na biashara yako ni mtaji ambao umeuweka kwenye biashara hiyo, mtaji huo umeikopesha biashara, na njia pekee ya kunufaika kupitia biashara hiyo ni pale inaopata faida baada ya kufanyika kwa biashara.
 
Ukiweza kuelewa hili, kwamba wewe siyo biashara yako, ukaiheshimu biashara yako na kuiacha ikue bila ya kuiingilia, ukaiendesha kwa misingi ya ukuaji wa biashara, utaiwezesha biashara hiyo kukua zaidi.

FURSA 20 ZA KUFANYA KIPINDI CHA MVUA----Maisha Na Mafanikio Blog ( Life & You )

Saturday, May 4, 2019

FURSA ZA KUFANYA UKIWA NYUMBANI KWAKO ( A ) / BIASHARA ZA KUFANYA NYUMBANI-------Maisha Na Mafanikio Blog ( Life & You )

KILA BIASHARA INA CHANGAMOTO ZAKE . USIPUUZE AU KUKWEPA IKABILI KILA CHANGAMOTO INAPOJITOKEZA.

Ni changamoto zipi unazokutana nazo na unazoweza kukutana nazo mbeleni?
Kila biashara ina changamoto zake, hakuna biashara isiyokuwa na changamoto kabisa. Lakini watu wengi huwa hawapendi kukutana na changamoto, na hivyo huwa hawapo tayari kuzikabili.
Wanachofanya wafanyabiashara wengi pale wanapokutana na changamoto ni kuzipuuza au kuziacha wakiamini zitaondoka zenyewe. Changamoto hizo huwa haziondoki, badala yake zinakua na kuota mizizi, na hizo ndiyo huja kuua biashara.
Unapaswa kujua zipi changamoto kubwa zinazoikabili biashara yako sasa na hata siku za mbeleni. Kisha kuwa na mkakati sahihi wa kukabiliana na kila changamoto pale inapojitokeza. Usijaribu kupuuza au kukwepa changamoto, badala yake ikabili kila changamoto inapojitokeza, na siyo tu utaitatua, bali pia utapiga hatua zaidi kwenye biashara yako.

KUWA NA MKAKATI WA MASOKO YA BIASHARA YAKO.

Upi mkakati wa masoko unaofanyia kazi wa  biashara     yako ?
Biashara ni wateja, bila ya wateja, haijalishi una bidhaa au huduma bora kiasi gani, huna biashara. Na njia pekee ya kuwaleta wateja kwenye biashara hiyo ni mkakati wa masoko.
Wafanyabiashara wengi wadogo huwa hawajisumbui kabisa na masoko. Huwa wanaendesha biashara zao kwa mtazamo wa kizamani kwamba ukijenga biashara wateja watakuja wenyewe. Lakini zama hizi ambazo wafanyabiashara ni wengi, hakuna mteja atakayekuja kwako, bali unapaswa kuwatafuta wateja.
Unawatafuta wateja kupitia mpango mkakati wa masoko unaokuwa nao kwenye biashara yako.
Hii ni kusema kwamba ili biashara yako ifanikiwe, lazima iwe na mkakati wa masoko, ambao unawatambua wateja wa biashara hiyo, kuwafikia kule waliko na kuwashawishi kununua.
Mkakati wako wa masoko unapaswa kuzingatia vitu vinne muhimu sana;
  1. Kuwatabua wateja sahihi wa biashara yako, wale ambao wanaweza kunufaika na bidhaa au huduma unazotoa.
  2. Kutambua vitu vitatu vinavyokutofautisha wewe na wafanyabiashara wengine wanaofanya biashara kama yako. Kama huna utofauti wowote na wafanyabiashara wengine, hakuna sababu ya mteja kuja kwako.
  3. Mchakato sahihi wa ufanyaji wako wa biashara, jinsi mteja anavyohudumiwa na hatua zote zinazochukuliwa kwenye biashara yako.
  4. Uhakika unaowapa wateja wako. Wateja wamepata fedha zao kwa shida, hawataki kuzipoteza, hivyo wanahofia sana kufanya manunuzi mapya. Unapaswa kuwapa uhakika kwamba wakinunua kwako hawapotezi fedha bali wanapata thamani.
Tengeneza mkakati wako wa masoko ambao unajumuisha vitu hivyo vinne na utaweza kuwafikia wateja wengi na kuwashawishi kununua kwako.

WEKA MALENGO YA MUDA MREFU ( MIAKA MITANO , KUMI ........... !! ) YA BIASHARA YAKO.

Ni lengo lipi kubwa unataka kufikia ndani ya miaka MITANO ,  KUMI ?  YA  BIASHARA   YAKO ?

Kabla sijaendelea hapa, hebu tafakari hilo swali na jipe majibu sahihi. Ni lengo lipi kubwa unalofanyia kazi ambalo unataka kulifikia miaka MITANO , KUMI  ijayo? Watu wengi wanaweza kushangaa unapangaje miaka kumi ijayo, wengi kupanga mwaka mmoja tu ni shida.

Huwezi kufanikiwa kwenye biashara kama huna malengo ya muda mrefu. Na hata kinachofanya wafanyabiashara wengi kukimbizana na fursa mpya zinazojitokeza ni kwa sababu hawana malengo yoyote ya muda mrefu, hivyo chochote kinachojitokeza wanaona ni sahihi kwao kukimbizana nacho.

Unapaswa kuwa na lengo kuu la miaka MITANO , KUMI  ijayo ya biashara yako, wapi unataka kufika na kwa kiwango gani. Lengo hili ndiyo litakusukuma kila siku, ndiyo litakuwa mwongozo wako na ndiyo litaathiri kila maamuzi unayofanya.

Kama huna lengo la miaka MITANO , KUMI  ijayo ya biashara yako, hujajitoa kufanikiwa kweli kwenye biashara hiyo. UNATANIA  NDUGU !  BADILIKA !  NA  AMKA !

WEKA KIPAUMBELE KIKUU CHA BIASHARA YAKO .

JIULIZE  Kipi kipaumbele kikuu cha biashara Yangu ?

Hakuna kitu kinachowapoteza wafanyabiashara wengi kama fursa mpya na nzuri zinazojitokeza kila wakati. Iwapo mfanyabiashara atakuwa mtu wa kukimbizana na kila fursa inayojitokeza, hawezi kufanikiwa kabisa kwenye biashara.

Hii ni kwa sababu fursa mpya huwa ni nyingi na haziishi, na ili upate mafanikio kwenye jambo lolote, unahitaji kuweka muda na kazi.

Jukumu lako kama mfanyabiashara ni kuweka kipaumbele kikuu cha biashara yako, yaani ni aina gani ya biashara utafanya na kisha kuachana na kelele nyingine zozote.

Ukishachagua biashara utakayofanya, funga masikio kuhusu biashara nyingine zisizoendana na biashara hiyo. Hata uambiwe kuna biashara mpya na yenye faida kubwa, usidanganyike kuondoka wenye vipaumbele vyako na kwenda kwenye biashara hiyo mpya, utajipoteza mwenyewe.

Ukichagua nini unataka na kuweka nguvu zako zote kwenye kitu hicho, lazima utakifikia. Lakini ukigawa nguvu zako kwenye kila kitu kipya kinachojitokeza, unajizuia mwenyewe kufanikiwa.

Kama biashara uliyoanzisha imekuwa na unaona fursa ya kuingia kwenye biashara nyingine, fanya hivyo kwa mipango na maono yako na siyo kwa kusukumwa na tamaa zako na za wengine.