Wednesday, May 1, 2019

USISUBIRI KUSTAAFU, NDIO UFANYE UJASIRIAMALI USIJE UKAFA MAPEMA.

Wengi wameingia kwenye mtego huo, kazi wanaifanya kweli, na wanafikia umri wa kustaafu, wanastaafu, mafao wanayapata, lakini maisha hayawi mazuri bali yanakuwa yamejaa msongo. Na wengi, hawavuki miaka mitano, wanafariki ndani ya miaka mitano baada ya kustaafu.
 
Hivyo kama hutaki kufa mapema, basi usikubali kustaafu. Kila siku ya maisha yako ifanye kuwa siku ya kazi, na kadiri mwili unavyokuwa kwenye kazi, unakuwa imara zaidi ya mwili uliopumzika.
 
Hivyo chagua kufanya kazi au biashara ambayo utaendelea kuifanya hata ukiwa na miaka 80, 90 na hata 100. Chagua kufanya kazi mpaka siku unayokufa, na utakuwa na maisha marefu, na yaliyo bora zaidi.
 
Kama umeajiriwa na ukifika miaka 60 au 65 ni lazima ustaafu, hakikisha unatengeneza mazingira ya kukuwezesha kuwa na kazi ya kuendelea kufanya hata baada ya kustaafu kwenye ajira. Na hapo siyo ukatafute tena ajira za muda, badala yake uwe umeshajenga kitu chako ambacho utakifanyia kazi kwa miaka yako yote.

Friday, April 26, 2019

JIWEKE KWENYE VIATU VYA MWINGINE HUTAKUWA NA SABABU YA KUUMIZWA NA CHOCHOTE TOKA KWA WENGINE


Njia ya kuondokana na msongo na kupata utulivu kwenye maisha yako ni kujiweka kwenye viatu vya wengine, kukaa kwenye nafasi ya mwingine ili kuweza kuelewa kwa nini mtu amefanya kile ambacho amefanya.

Chanzo kikubwa cha hasira, msongo na hata migogoro kwenye maisha yetu ni mahusiano yetu na wengine. Pale wengine wanapofanya vitu ambavyo hatukutegemea wafanye, tunapatwa na hasira na msongo. Tunaona kama wamefanya kwa makusudi au wamepanga kutuumiza kwa namna fulani.

Lakini mara nyingi sana watu wanafanya vitu kwa nia njema, hasa kwa upande wao. Ni wachache sana ambao wanafanya kitu kwa makusudi ili kumuumiza mtu mwingine. Ukitaka kuelewa kwa nini mtu amefanya kile alichofanya, jaribu kwanza kujiweka kwenye nafasi yake.

Kila mtu huwa ana sababu nzuri ya kufanya kile ambacho amefanya, iwe ni kizuri au kibaya kwako. Ukichukua nafasi ya kuelewa sababu hiyo, hasa kwa kujiweka kwenye nafasi yako, utagundua huna sababu ya kuwa na hasira au msongo. Kwa sababu huenda na wewe ungekuwa kwenye nafasi kama yake ungefanya kama alivyofanya yeye.

Tambua kwamba watu wana mitazamo tofauti, vipaumbele tofauti, uelewa tofauti na hata imani tofauti. Ukichukua nafasi ya kuelewa hayo kuhusu wengine, utaona huna sababu ya kuumizwa na chochote ambacho wengine wanafanya.

BADILI MPANGILIO WA VIPAUMBELE PALE MAMBO YANAPOKWENDA TOFAUTI.

Njia ya kuondokana na msongo na kuwa na utulivu kwenye maisha yako ni kubadili mpangilio wa vipaumbele vyako kulingana na mazingira unayojikuta upo. Kila mmoja wetu ana mpangilio wake wa vipaumbele, na tunapenda mpangilio huo uende hivyo bila ya kubadilika. Inapotokea hali inayobadili mpangilio huo tunapatwa msongo na kuona hatuna udhibiti wa maisha yetu.

Hatua bora za kuchukua hapa ni kubadili mpangilio wa vipaumbele vyako. Mfano inawezekana familia kwako ni kipaumbele cha kwanza, kazi au biashara ni kipaumbele cha pili. Sasa unajikuta kwenye kazi au biashara ambayo inataka muda wako mwingi na kukunyima muda wa kukaa na familia, ambayo ndiyo kipaumbele cha kwanza. Hali hii inaweza kukuletea msongo mkubwa na kukosa utulivu, kwa sababu vipaumbele vyako vinavurugwa. Lakini unaweza kuchukua hatua ya kubadili mpangilio wa vipaumbele vyako kulingana na hali uliyonayo. Kwa kipindi fulani kuweka kipaumbele cha kwanza kuwa kazi au biashara kabla ya familia, na baada ya kujijengea msingi mzuri ukarudi kwenye vipaumbele vyako vya awali.

Hilo pia linakwenda kwa vipaumbele vingine kwenye maisha, mfano kama umekuwa unapendelea kufanya kazi mwenyewe, lakini ukajikuta kwenye kazi inayokutaka ushirikiano na wengine, kama hutabadili kipaumbele kuwa kufanya kazi na wengine utakuwa na msongo kipindi chote cha kazi. Kadhalika kwenye mahusiano na maeneo mengine ya maisha, pale mazingira yanapobadilika au unapokutana na uhitaji tofauti, kuwa tayari kubadili vipaumbele vyako.

Unapobadili vipaumbele kulingana na mazingira au hali inapobadilika, unakuwa tayari kutumia kila hali unayokutana nayo badala ya kupambana nayo.

Tuesday, April 23, 2019

KUWA KING"ANG"ANIZI NA MVUMILIVU UTAFANIKWA SANA.

Kila kitabu kinachohusu mafanikio kinasisitiza sana ung’ang’anizi na uvumilivu ili kuweza kufanikiwa. Lakini siyo kila ung’ang’anizi na uvumilivu utakufikisha kwenye mafanikio. Bali unahitaji ung’ang’anizi sahihi, na kukubali pale ambapo umekosea ili kuboresha zaidi.
Tunapaswa kuwa ving’ang’anizi ili kupata utajiri na mafanikio, tunapaswa kujaribu tena na tena na tena kila tunaposhindwa. Lakini tunapaswa kukumbuka kwamba kufanya jambo lile lile kwa njia ile ile halafu kutegemea kupata matokeo tofauti ni maana sahihi ya ujinga.
Tunapaswa kung’ang’ana kwa njia sahihi, tunapaswa kubadili njia tunazotumia, ambacho hatupaswi kubadili ni lengo ambalo tumejiweka. Tunapaswa kuendelea na mapambano mpaka pale tutakapopata tunachotaka.
Wote tunajua jinsi ambavyo dunia ina uangalifu, haikubali kutoa kitu kwa mtu ambaye hajaonesha kweli anakitaka na yupo tayari kulipa gharama kukipata. Jioneshe kwamba wewe unautaka utajiri kweli, kuwa tayari kulipa gharama na ng’ang’ana kwa njia sahihi na utapata unachotaka.

JIAMINI WEWE MWENYEWE.

Kama hujiamini wewe mwenyewe, hakuna yeyote anayeweza kukuamini na hutaweza kufanikiwa kwenye jambo lolote maishani mwako.
Unapaswa kujiamini wewe mwenyewe, unapaswa kuamini kwamba una uwezo mkubwa ndani yako wa kukuwezesha kupata chochote unachotaka, unapaswa kuamini hakuna kinachoweza kukuzuia kupata kile unachotaka. Tunaambiwa imani inaweza kuihamisha milima, na hii ndiyo imani unayopaswa kuwa nayo ili kufanikiwa na kufikia utajiri.
Katika safari yako ya kusaka utajiri utakutana na vikwazo vya kila aina, utapatwa na hofu nyingi, wapo watakaokukatisha tamaa kwa kukupa mifano ya wengi walioshindwa. Kitu pekee kinachoweza kukuvusha kwenye hali hizo ni kujiamini wewe mwenyewe.
Pia hakuna utakachopanga na kikaenda kama ulivyopanga, utashindwa kwenye mambo mengi licha ya kufanya kila unachopaswa kufanya. Kujiamini ndiyo kutakupa nguvu ya kuamka kila unapoanguka ili uweze kuendelea na safari ya mafanikio.
Jiamini wewe mwenyewe na hakuna kitakachoweza kukuzuia kufanikiwa.

AMINI SAUTI YAKO YA NDANI.

Kila mmoja wetu ana sauti iliyopo ndani yake, hisia fulani unazozipata ambazo huwezi kuzielezea, ambazo zinakuashiria kama kitu ni kibaya au kizuri, kama ni sahihi au siyo sahihi. Mara nyingi huwa tunapuuza sauti hii na matokeo yake tunafanya makosa makubwa. Kuna wakati ndani yako unapata msukumo wa kufanya au kutokufanya kitu, lakini ushawishi wa nje unakufanya uende kinyume na sauti hiyo na unakuja kugundua ungejisikiliza ungekuwa sahihi zaidi.
Jifunze kuamini sauti yako ya ndani, hata kama inaendana na uhalisia wa nje. Kuna kitu kwa nje kinaweza kuonekana ni sahihi, lakini sauti yako ya ndani ikakuambia siyo sahihi, au kitu kwa nje kikaonekana siyo sahihi, lakini sauti yako ya ndani ikakuambia ni sahihi. Jifunze kusikiliza sauti yako ya ndani, inajua zaidi kuliko wewe na itakuongoza kwa usahihi mara zote.
Watu wote ambao wamefikia utajiri na mafanikio makubwa, kuna hatua ambazo wamewahi kuzichukua, ambazo watu wa nje waliwaambia wanakosea, lakini wao walifanya, kwa sababu sauti ya ndani iliwaambia ndiyo kitu sahihi kufanya.
Unapojikuta njia panda na hujui hatua ipi sahihi kuchukua, isikilize sauti yako ya ndani, inajua njia sahihi na utaweza kufanya kilicho sahihi.

SIKILIZA NA JIFUNZE.

Kusikiliza ndiyo silaha yenye nguvu sana katika safari ya mafanikio. Ukiwa msikilizaji mzuri, utajifunza mambo mengi sana kwa watu wengine. Kuanzia wale unaofanya nao kazi na hata wale ambao inabidi upatane nao kwenye makubaliano mbalimbali.
Kusikiliza ni kugumu sana, na wengi hawawezi kusikiliza kwa umakini ndiyo maana hawajifunzi, hawajui watu wanataka nini na kuweza kuwapatia. Ukiwa mtu wa kusikiliza kwa umakini, kwa lengo la kuelewa na kujifunza, utajua mengi na pia utazijua tabia za watu, ambazo utaweza kuzitumia kwa mafanikio zaidi.
Ukiwasikiliza wateja wako utayajua mahitaji yao hata kama hawajakuambia wazi na kuweza kuwatimizia. Ukiwasikiliza wafanyakazi wako utajua kinachowahamasisha na ukiwapatia watajituma zaidi. Ukiwasikiliza unaotaka kufikia nao makubaliano, utajia udhaifu wao uko wapi na kuweza kuutumia.
Katika safari ya mafanikio na utajiri, kusikiliza na kujifunza ni hitaji muhimu sana. Hata watu wanawaheshimu sana wale ambao wanachukua muda na kusikiliza. Tumia nguvu hii kwa manufaa yako na ya wengine pia.