Sunday, March 24, 2019

ENEO LA KAZI : Ulipo Sasa, Unakotaka Kufika, Viwango Vya Kujiwekea , Kitabu Cha Kusoma.

Kazi au biashara unayofanya ni eneo muhimu sana la maisha yako. Hili ni eneo ambalo unapaswa kuwa unakua kadiri muda unavyokwenda. Kwa sababu kubaki pale pale, ni kurudi nyuma. Katika kazi au biashara unayofanya, lazima uweze kupima ukuaji wako.

ULIPO SASA; unaielezeaje kazi? Je unafurahia kazi au biashara unayoifanya? Je unajiona kuwa kwenye nafasi ya kufanikiwa kupitia kazi au biashara unayofanya. Je unakua kwa kiasi gani ukijipima kikazi na kibiashara?

UNAKOTAKA KUFIKA; ni ubobezi gani unajiona kuwa nao kwenye kazi unayofanya? Ni mabadiliko gani ungependa kuleta kupitia kazi au biashara unayofanya. Kuwa na picha ya mchango wako mkubwa na mabadiliko unayotaka kuleta na ifanyie kazi kila siku.

VIWANGO VYA KUJIWEKEA; jiunge na kundi la kitaalamu kulingana na taaluma au ujuzi ulionao. Shiriki mikutano na mafunzo mbalimbali yanayoendana na taaluma na ujuzi ulionao. Pia jipime jinsi unavyokua kupitia kazi au biashara unayofanya.

KITABU CHA KUSOMA; kitabu ORIGINALS cha Adam Grant ni kitabu kitakachokuwezesha kuwa na ubunifu mkubwa kwenye kazi yako na kufikiria nje ya boksi, kuuza mawazo yako na kuleta mapinduzi.

ENEO LA MAZINGIRA : Ulipo Sasa, Unakotaka Kufika, Viwango Vya Kujiwekea, Kitabu Cha Kusoma.

Mazingira yako yana mchango mkubwa sana kwenye mafanikio yako. Kuanzia nyumbani kwako, gari lako, eneo lako la kazi au biashara na eneo lolote ambalo unakuwepo unaposafiri.
ULIPO SASA; ni katika mazingira gani unajisikia furaha? Je umeridhika na pale unapoishi sasa na jinsi unavyoishi? Je unaamini unastahili kuwa na mazingira bora na ya kifahari, kuanzia nyumbani mpaka kwenye kazi zako?
UNAKOTAKA KUFIKA; tengeneza picha ya mazingira bora kwako, kuanzia nyumbani, kazini na popote unapokuwa. Kama usingekuwa na kikwazo chochote, hasa kifedha, ungeishi nyumba ya aina gani, ungeendesha gari ya aina gani na eneo lako la kazi lingekuwaje? Beba picha hii kila siku ya maisha yako na ifanyie kazi kuifikia.
VIWANGO VYA KUJIWEKEA; yafanye mazingira yako kuwa safi na yanayokupa hamasa zaidi. Fanya chumba chako kuwa safi, nyumba safi, mazingira masafi na hata eneo lako la kazi liwe safi na vitu vipangiliwe kiasi cha kuwa rahisi kupata chochote unachotaka kutumia.
KITABU CHA KUSOMA; soma kitabu kinachoitwa THE MAGIC OF THINKING BIG kilichoandikwa na David Schwarrz. Kitabu hiki kitakusukuma kuboresha maisha yako na kuwa na ndoto kubwa kuhusu nyumbani kwako, ofisini kwako na mengine mengi.

ENEO LA SAFARI : Ulipo Sasa, Unakotaka Kufika, Viwango Vya Kujiwekea, Kitabu Cha Kusoma.

Safari mbalimbali za kujifunza na kubadili mazingira ni muhimu sana kwa mafanikio yako. Unapotoka pale ulipozoea na kwenda maeneo mengine, unajifunza zaidi na hata kupata mtazamo wa tofauti na ule uliozoea.

ULIPO SASA; unapofikiria kuhusu safari, ni picha gani unaipata kwenye akili yako. Je unaamini unahitaji kujipanga sana na kuwa na fedha nyingi ndiyo uweze kusafiri? Je unaona hakuna kipya cha kujifunza katika kusafiri bali kujichosha tu?

UNAKOTAKA KUFIKA; pata picha ya wale ambao unaona wana safari na burudani, kisha jione na wewe ukiwa na safari na burudani kwenye maisha yako. Ni maeneo gani ambayo ungependa kutembelea kwa ajili ya kujifunza na hata kupata burudani? Orodhesha maeneo yote ambayo unasukumwa sana kuyatembelea ili kujifunza zaidi na ifanye hii kuwa ndoto unayoifanyia kazi.

VIWANGO VYA KUJIWEKEA; jiwekee viwango vya safari utakazofanya kwa mwaka na hata mapumziko ambayo utayachukua kwenye kazi au biashara yako. Panga kusafiri na kujifunza zaidi kupitia tamaduni za wengine.

KITABU CHA KUSOMA; soma kitabu kinachoitwa LOSING MY VIRGINITY kilichoandikwa na Richard Branson. Kitabu hiki kitakupa hamasa ya kuishi maisha bora kwa kuwa na safari matukio ya burudani wakati unafanyia kazi ndoto zako.

ENEO LA UBUNIFU :Ulipo Sasa, Unakotaka Kufika, Viwango vya Kujiwekea, Kitabu Cha Kujisomea.

Unapaswa kuwa na kitu cha kibunifu unachofanya kwenye maisha yako. Kitu hiki kinachochea akili yako kufikiri zaidi na kukuwezesha kukua zaidi. Inaweza kuwa uandishi, uchoraji, uimbaji, upigaji vifaa vya muziki, uigizaji na kadhalika.
ULIPO SASA; je unaamini kwamba wewe ni mbunifu? Je kuna mtu mbunifu ambaye unapenda sana kuwa kama yeye? Ni mambo gani ya kibunifu ambayo unafanya sasa kwenye maisha yako? Je ni vipaji gani ulivyonavyo na unavitumiaje?
UNAKOTAKA KUFIKA; ni ubunifu gani ambao ungependa kuwa nao na kubobea zaidi siku zijazo? Ni jinsi gani unaweza kutumia ubunifu huo kuwasaidia wengine zaidi. Chagua ubunifu unayotaka kuwa nao na jiendeleze kila siku na kutoa mchango kwa wengine.
VIWANGO VYA KUJIWEKEA; chagua aina ya ubunifu ambao utakuwa unajihusisha nao na kila siku tenga muda wa kujiendeleza kwenye ubunifu huo. Unaweza pia kujiunga na wengine au kushiriki madarasa yanayokuwezesha kukuza zaidi ubunifu wako.
KITABU CHA KUSOMA; soma kitabu THE WAR OF ART cha Steeven Pressfield ambacho kitaamsha na kuchochea ubunifu uliopo ndani yako na kuweza kufanya kazi za kibunifu.

ENEO LA FAMILIA :Ulipo Sasa, Unakotaka Kufika, Viwango vya Kujiwekea, Kitabu cha Kusoma.

Familia yako ni mahusiano ambayo ni muhimu sana kwenye maisha yako. Haya ni mahusiano ambayo yana mchango mkubwa sana kwenye mlinganyo wako wa mafanikio. Kadiri mafanikio haya yanavyokuwa bora, ndivyo unavyokuwa bora.

ULIPO SASA; je unafurahia kurudi nyumbani baada ya siku yako ya kazi kuisha? Je unajua lipi jukumu lako kuu kwenye familia? Na je familia kwako ni watu gani? Unaamini familia ni mzigo kwako au kichocheo kwako kufanikiwa?

UNAKOTAKA KUFIKA; pata picha ya familia bora kwako, inawahusisha watu gani, mahusiano yapoje na kila mtu ana mchango gani kwenye familia hiyo? Weka juhudi katika kujenga familia hii bora kwako na siyo kuishi kwenye familia usiyoifurahia.

VIWANGO VYA KUJIWEKEA; weka lengo la kutenga muda wa kufanya mambo ya kifamilia. Tenga muda wa kuwa pamoja na familia, mfano mzuri ni kuwa na chakula cha pamoja, kutoka pamoja au kwenda kutembelea ndugu na jamaa kama familia. Haya yanaimarisha mahusiano ya kifamilia.

KITABU CHA KUSOMA; kitabu MASTERY OF LOVE cha Don Miguel Ruiz kitakupa msingi mkuu wa mafanikio kwenye familia ambao ni upendo.

ENEO LA MAPENZI : Ulipo sasa, Unakotaka Kufika, Viwango vya Kujiwekea . Kitabu cha Kusoma.

Hili ni eneo linalohusu mahusiano yako ya kimapenzi na mwenza wako. Ni eneo muhimu sana kwa sababu hili linagusa kila eneo la maisha yetu. Kama mahusiano yako ya kimapenzi yako vizuri basi maisha yako yanakuwa vizuri. Lakini kama eneo hili lina matatizo, hutaweza kutuliza akili yako kwenye jambo lolote.

ULIPO SASA; Tafakari pale ulipo sasa kwenye mahusiano yako ya kimapenzi, je umeoa au kuolewa au upo peke yako? Na je kwenye hali ya mahusiano uliyopo, unayafurahia? Unayaelezeaje mapenzi? Ni kitu gani unatoa na kipi unapokea kutoka kwenye mahusiano yako ya mapenzi? Je unaamini mapenzi yanaleta maumivu? Je upo tayari kumpenda kweli mwenzako na kumwonesha kwamba unampenda? Je unajiona ni mtu unayestahili kupendwa kweli? Jiulize na kujipa majibu ya maswali hayo na yatakupa picha ya pale ulipo sasa.

UNAKOTAKA KUFIKA; Katika kuboresha zaidi mahusiano yako ya kimapenzi, unapaswa kuwa na picha ya wapi unataka mahusiano hayo yafike. Katika kutengeneza picha ya unakotaka kufika, jiulize na kujipa majibu ya maswali haya; je mahusiano bora ya kimapenzi kwako unataka yaweje? Pata picha ya mahusiano yenye mafanikio, mnawasilianaje, kuchukulianaje, vitu gani mnafanya pamoja na jinsi mnavyoyafurahia maisha pamoja. Kuwa na picha hii kila wakati na ifanyie kazi, itakusukuma kuwa bora zaidi.

VIWANGO VYA KUJIWEKA; Katika eneo la mapenzi unapaswa kujiwekea viwango ambavyo utavizingatia ili kuimarisha eneo hili. Viwango vya kujiwekea ni muda wa kuwa pamoja wewe na mwenza wako, inaweza kuwa kwenye mtoko mnaofanya pamoja, kufanya mazoezi pamoja na hata kuwa na ratiba ya kuwa na faragha nyinyi wawili pekee kwa ajili ya yale muhimu kwenu. Zingatia sana hili la kupata muda wa kuwa na mwenzako na weka kiwango cha muda huo.

KITABU CHA KUSOMA; Kujiweka vizuri kwenye eneo la mahusiano ya mapenzi soma kitabu kinachoitwa MEN ARE FROM MARS, WOMEN ARE FROM VENUS Kilichoandikwa Na John Gray. Kitabu hiki kitakufundisha jinsi ya kuishi na mwenzako.

Thursday, March 21, 2019

LIPE TATIZO LAKO MUDA KAMA NJIA ZINGINE ZIMESHINDIKANA.

Wenye busara walisema muda ni tiba ya kila kitu. Kwamba hakuna kitu ambacho muda haukiathiri, hivyo kama kuna kitu kinakusumbua, ambacho unaona kimekushinda, uachie muda ufanye kazi yake.
 
Hakuna kitu ambacho muda unakiacha jinsi ulivyo bila ya kukiathiri, kadiri muda unavyokwenda, tatizo linakosa nguvu au njia bora za kulitatua inapatikana.
 
Hata kama kwa sasa huoni kabisa namna ya kuvuka ugumu unaopitia, usikate tamaa, jua muda uko upande wako. Unachohitaji ni uvumilivu na kusahau tatizo hilo kwa muda, kwa kutoruhusu likutawale wakati huna cha kufanya.
 
Kila ugumu unaopitia, jua kwamba utaupatia jawabu au muda utatoa jawabu. Hivyo kama umeshafanya kila unachoweza kufanya na zaidi, lakini hupati majibu, hapo siyo mwisho, muda una nafasi kubwa ya kuhangaika na tatizo hilo. Kubali na songa mbele na mengine yaliyo ndani ya uwezo wako, na muda utahangaika na hilo lililokushinda.