Kwenye maisha yetu ya kila siku, vitu vyote muhimu huwa hatuvifanyi mara moja na kuachana navyo, bali huwa tunavifanya kila siku. Na hakuna hata siku moja ambayo tunajiambia tumechoka na hivyo hatufanyi.
Fikiria
yale tunayofanya kila siku ili maisha yetu yaende, unakula kila siku,
unapumua kila siku, unasafisha mwili wako kila siku, na hata nyumba au
nguo zako, unasafisha kila mara.
Lakini inapokuja kwenye kazi na biashara, huwa tunajipa kila aina ya sababu kwa nini tusifanye kwa baadhi ya siku. Huwa tunachukulia kazi na biashara zetu kama kitu cha ziada kwenye maisha yetu na siyo maisha yetu.
Kadhalika
vitu kama kujifunza, mfano kusoma vitabu. Utasikia watu wakisema kabisa
kwamba hawasomi vitabu kwa sababu hawana muda. Lakini hutawasikia watu
hao wakisema wana siku mbili hawajala kwa sababu hawajapata muda.
Kwa kila kilicho muhimu kwenye maisha, huwa tunapata muda wa kukifanya, hata kama tumebanwa kiasi gani.
Hivyo
ninachotaka uondoke nacho hapa rafiki yangu ni hiki, chagua vitu
ambavyo lazima kila siku utavifanya na uvifanye kweli bila ya kusingizia
muda au kuchoka. Na
ukiacha vile ambavyo tayari unafanya ili uwe hai, kama kula na
kadhalika, ongeza vitu kama kujifunza, kufanya majukumu yako na kukuza
vipaji au kile unachopenda.
Kama wewe ni mwandishi basi hakikisha kila siku unaandika, usikubali siku ipite hujaandika. Na wengine kwa nafasi zao za kazi au biashara, hakikisha kila siku kuna kitu unakifanya cha kukufanya uwe bora zaidi.