Na mazoezi ambayo yanakuwezesha kuishi miaka mingi siyo mazoezi magumu sana, bali mazoezi madogo madogo ambayo yanaufanya mwili utumie vyakula unavyokuwa umekula.
Katika kuiishi siri hii ya kuweka mwili kwenye mwenzo, zingatoa yafuatayo;
- Ondoa urahisi kwenye maisha yako. Hapa jisukume kutembea na kufanya kitu badala ya kutumia urahisi uliopo. Kwa mfano kama kuna ghorofa unapanda na kuna lifti na ngazi, wewe panda ngazi badala ya lifti. Kama unaangalia tv na uko mbali nayo, kama unataka kubadili chaneli au kuongeza sauti, badala ya kutumia rimoti amka na uende ukabadili mwenyewe. Mazoezi madogo madogo kama haya yanakusaidia sana.
- Fanya mazoezi kuwa kitu unachofurahia. Usifanye mazoezi magumu na ya kukuumiza, badala yake fanya mazoezi ambayo unayafurahia, kama kuna eneo la karibu unaloenda, badala ya kutumia gari basi tembea au nenda kwa baiskeli. Kadiri unavyopata nafasi kama hizi za kuupa mwili wako mazoezi, zitumie.
- Kuwa na muda wa matembezi kwenye siku yako. Kuwa na matembezi ya peke yako au pamoja na wengine kunaufanya mwili wako kuwa kwenye mwendo.
- Kuwa na mkutano wa kutembea. Kama kuna mtu ambaye unataka kuwa na mazungumzo naye, iwe ni ya kikazi, kibiashara au hata ya kindugu na kirafiki, unaweza kutumia mkutano huo kuwa sehemu ya mazoezi. Mnaweza kufanya mazungumzo yenu mkiwa mnatembea eneo tulivu na hii itakuwa msaada zaidi kwenu.
- Kuwa na bustani. Kwa kuwa na bustani ambayo unaihudumia kila siku ni zoezi tosha kwa mwili wako. Kupanda, kupalilia na hata kuvuna mazao kwenye bustani yako kunatosha kuupa mwili wako zoezi.
- Jiunge na darasa la yoga. Yoga ni mazoezi ya mwili yanayouwezesha mwili wako kuweza kuwa na usawa. Ukiweza kufanya zoezi hili la yoga angalau mara mbili kwa wiki inakusaidia sana.