Tuesday, February 12, 2019

WEKA KIPAUMBELE KWA FAMILIA--NI SIRI YA KUKUWEZESHA KUISHI ZAIDI YA MIAKA 100.


Wote ambao wameweza kuishi kwa miaka zaidi ya 100, wamekuwa na kipaumbele kikubwa kwa familia zao. Wengi wanakuwa wanaishi na familia zao, na hata wale ambao wanaishi wenyewe, wana muda wa kuwa pamoja na familia zao. Tafiti zinaonesha wazee ambao wanaishi na watoto wao wanaishi kwa muda mrefu kuliko wale wanaoishi wenyewe au wanaoishi kwenye vituo vya kulea wazee.

Familia ndiyo msingi mkuu wa maisha bora, ya kiafya na mafanikio. Wale wanaoweka kipaumbele cha kwanza kwenye familia wanakuwa na maisha marefu.

Mambo muhimu ya kuzingatia ili kuweka kipaumbele kwa familia;

Weka mazingira ya kuwa karibu na familia. Kwa kuishi kwenye nyumba moja kunawafanya muwe karibu zaidi kama familia. Pia kuishi kwenye nyumba ambayo ni ndogo, ambayo wote mnaweza kuonana kila siku kuna manufaa zaidi.
Kuwa na utaratibu wa familia, utaratibu ambao unawaleta pamoja. Mfano kuwa na mlo mmoja kila siku ambao mnakula kwa pamoja kama familia kunawafanya kuwa karibu kuliko pale ambapo kila mtu anakula kwa muda wake.
Tengeneza eneo la kumbukumbu ya familia. Mnaweza kuwa na chumba au eneo ambalo kumbukumbu mbalimbali za kifamilia zinatunzwa. Mnaweza kuweka picha za matukio mbalimbali ya kifamilia. Mtu anapokuwa kwenye eneo hilo anapata kumbukumbu ya umoja wenu wa kifamilia.
Weka familia yako mbele. Tenga muda wa kukaa na wale wa muhimu kwako, watoto wako, mwenza wako na hata wazazi wako. Mahusiano bora yanajengwa kwa muda na kujali.

Saturday, February 9, 2019

TUSIOGOPE WALA KUKIMBIA MAGUMU TUNAYOPITIA . NI KIPIMO CHA UWEZO MKUBWA ULIOPO NDANI MWETU.

Mara nyingi tumekuwa tunakwepa magumu kwenye maisha yetu, tumekuwa tunaomba tusikutane na magumu, kwa sababu tunaona magumu ndiyo kikwazo cha sisi kuwa na maisha tunayoyataka. Lakini hilo siyo sahihi, kama tusingekutana na magumu kabisa kwenye maisha yetu, maisha yangekosa maana na tusingeweza kuwa watu ambao tumekuwa sasa.
Magumu ambayo tumekutana nayo kwenye maisha ndiyo yametufanya tuwe watu ambao tumekuwa sasa. Hivyo badala ya kukataa na kukimbia magumu, tunapaswa kuyakaribisha kwa mikono miwili. Kwa sababu kupitia magumu ndiyo tunakua, na ndiyo tunafikia uwezo mkubwa uliopo ndani yetu.
Kufukuzwa au kukosa kwako kazi huenda kumekufanya ukaweza kuanza biashara yako. Kusumbuliwa kwenye mahusiano yako ya mwanzo na yakavunjika ndiyo kumekupelekea kutengeneza mahusiano mengine bora. Na hata kupata hasara na kufa kwa biashara yako ya mwanzo kumekuwa funzo la wewe kufanikiwa kwenye biashara nyingine.
Tusiogope wala kukimbia magumu, na wala tusiombe kutokukutana na magumu. Badala yake tuombe kuwa imara zaidi ili kuweza kukabiliana na kila gumu tunalokwenda kukutana nalo.

NGUVU YA FURAHA KATIKA SAFARI YA MAFANIKIO.

Wengi wamekuwa wanafikiri kwamba wakifanikiwa ndiyo watakuwa na furaha. Lakini ukweli ni kwamba furaha ndiyo inaleta mafanikio.
Mwandishi  Dean anatushirikisha hatua muhimu za kuchukua ili kujijengea furaha ambayo itatuwezesha kupata mafanikio makubwa;
  1. Jua nini maana ya furaha kwako, kinachokupa furaha wewe siyo kinachowapa furaha wengine.
  2. Ishi kwenye wakati uliopo saa, siyo wakati uliopita wala wakati ujao.
  3. Acha kufikiria sana kuhusu vitu, hasa vile ambavyo hakuna hatua unazoweza kuchukua.
  4. Angalia upande chanya wa kila jambo, hata kama jambo ni baya kiasi gani, lina upande ambao ni mzuri, angalia huo.
  5. Linda amani na utulivu wako wa ndani, ondokana na hali zote hasi.
  6. Elewa kwamba kuteseka ni kuchagua, chagua kutokuteseka.
  7. Pokea kushindwa kwa mikono miwili na chukua hatua ili kuwa bora zaidi.
  8. Usiwe na kinyongo na yeyote, samehe kila mtu.
  9. Usiweke matarajio makubwa na kutegemea kila kitu kitaenda kama ulivyopanga.
  10. Shukuru kwa kilichopo mbele yako.
  11. Usiridhike na kile ulichozoea, usifanye mambo kwa mazoea.
  12. Kuwa sehemu ya kitu kikubwa, jijenge zaidi kiroho na kiimani.

Friday, February 8, 2019

MVUTO NA USHAWISHI KATIKA SAFARI YA MAFANIKIO.

Mvuto na ushawishi ni vitu viwili ambavyo kila anayetaka kufanikiwa na kutengeneza kipato kikubwa anapaswa kuwa navyo. Dean anaita vitu hivi viwili kichocheo cha utajiri, vikikosekana huwezi kufikia mafanikio makubwa na utajiri.
 
Mvuto na ushawishi ni njia nyingine ya kusema MASOKO NA MAUZO. Kila tunachofanya kwenye maisha ni masoko, na kila kinachotuingizia kipato ni mauzo.

Hivyo tunaweza kusema kazi zetu kubwa kwenye maisha ni mbili, MASOKO NA MAUZO. Tunapaswa kujiweka kwa njia ambayo watu wayajua uwepo wetu, na pia tuweze kuwashawishi watu hao kutupa kile ambacho tunataka watupe.

Katika kuboresha masoko na mauzo kwenye biashara zetu, kazi zetu na hata maisha yetu kwa ujumla, Mwandishi Dean anatushirikisha hatua zifuatazo za kuchukua;

------Kuwa muwazi na mwaminifu mara zote. Uaminifu unalipa.
------- Kuwa wewe na kuwa na hamasa, usijaribu kuingiza kuwa mtu mwingine.
--------Amini kwenye utele na siyo uhaba, amini kuna wingi wa chochote kwa ajili ya kila mtu.
------Wape watu kile wanachotaka na siyo wanachohitaji.
-----Tumia hadithi, watu wanaelewa na kusukumwa zaidi na hadithi na mifano kuliko maelezo pekee.
------Usiwe mwongeaji sana, ukishaeleweka nyamaza.
Kuwa na msukumo wa ndani wa kile unachofanya.
-------- Endelea kutengeneza mahusiano na wale ambao unawauzia au wameshakubaliana na wewe.
-----Tengeneza mtazamo wa shukrani.
-------Zingatia zaidi kujenga mahusiano kuliko kipato, fanya kile ambacho kitaboresha mahusiano yako na unayetaka kumuuzia au akubaliane na wewe.

MWAMSHE SHUJAA ALIYE NDANI YAKO.

Kila mmoja wetu ana shujaa aliye ndani yake. Shujaa huyu ni uwezo mkubwa na wa kipekee ambao mtu anao, uwezo usio na ukomo na ambao hakuna mwingine anao hapa duniani.

Njia ya kumwamsha shujaa aliye ndani yako ni kujijengea kujiamini. Tatizo la wengi ni kutokujiamini, kushindwa kusimamia kile wanachotaka, hasa pale ambapo wengine hawakubaliani nao.

Katika kujijengea kujiamini, zingatia vitu vitatu muhimu; uthubutu wa kufanya kitu kipya, dhamira ya kufanya kitu hicho na kutumia uwezo wa ndani yako kufikia kile unachotaka kufikia.

Watu wengi hawajui kwamba ndani yao wana uwezo mkubwa wa kufanya chochote wanachotaka. Wengi huangalia nje na kukosa msaada. kama utaanza kuangalia ndani yako utapata msaada mkubwa kwako kufika unakotaka kufika.

TENGENEZA HADITHI YENYE NGUVU KWAKO.

Kila mmoja wetu kuna hadithi ambayo anaiishi, hadithi ambayo umekuwa unajiambia kila siku na imekuwa kikwazo kwako kupiga hatua. Kwa mfano kama umetokea familia masikini na huna elimu, hadithi yako inaweza kuwa kwamba wewe huwezi kufanikiwa kwa sababu umetoka familia masikini na huna elimu kubwa.
Lakini hadithi hiyo ni uongo, ni kweli unaweza kuwa umetoka familia masikini na huna elimu kubwa, lakini hicho siyo kinachokuzuia kufanikiwa. Wapo wengi waliotoka kwenye umasikini mkubwa kuliko wako na hata hawakupata elimu kabisa lakini wamefanikiwa.
Hivyo badili hadithi inayokuzuia kufanikiwa na tengeneza hadithi mpya ya mafanikio yako ambayo itakusukuma kufanikiwa zaidi. Hadithi yako ya mafanikio iguse yale maeneo ambayo una uimara na uyatumie kama sababu ya wewe kufanikiwa.
Hadithi yako mpya iwe ni kinyume kabisa na ile iliyouwa inakuzuia. Ukishaandika hadithi hii jiambie na kujikumbusha kila siku mpaka iwe sehemu ya fikra zako.

MSINGI MKUU WA MAFANIKIO YOTE.

Changamoto kubwa ya zama hizi ni kwamba kila mtu anakwenda kasi, lakini cha kushangaza hajui anakwenda wapi. Kila mtu yupo bize kila siku, anaamka asubuhi na mapema na kuchelewa kulala, lakini hajui wapi anayapeleka maisha yake.

Haijalishi unakwenda kiasi gani, kama hujui unakokwenda, kasi uliyonayo inakupoteza tu.

Msingi mkuu wa mafanikio yote ni kujua nini hasa ambacho unakitaka, kuwa na maono ya kile unachotaka kwenye maisha yako. Ukishajua kwa hakika nini unachotaka, hutasongwa tena na mambo ambayo siyo muhimu kwako.

Kama kila siku upo bize na huna muda wa kukamilisha mambo yako, ni dalili kwamba hujui unachotaka au hujui unakokwenda.

Anza kwa kujua nini hasa unachotaka, wapi hasa unakotaka kufika, kisha jua hatua zipi muhimu za kuchukua ili kufika unakotaka kufika, kisha puuza mengine yote ambayo hayachangii wewe kufika unakotaka kufika