Friday, February 8, 2019

MWAMSHE SHUJAA ALIYE NDANI YAKO.

Kila mmoja wetu ana shujaa aliye ndani yake. Shujaa huyu ni uwezo mkubwa na wa kipekee ambao mtu anao, uwezo usio na ukomo na ambao hakuna mwingine anao hapa duniani.

Njia ya kumwamsha shujaa aliye ndani yako ni kujijengea kujiamini. Tatizo la wengi ni kutokujiamini, kushindwa kusimamia kile wanachotaka, hasa pale ambapo wengine hawakubaliani nao.

Katika kujijengea kujiamini, zingatia vitu vitatu muhimu; uthubutu wa kufanya kitu kipya, dhamira ya kufanya kitu hicho na kutumia uwezo wa ndani yako kufikia kile unachotaka kufikia.

Watu wengi hawajui kwamba ndani yao wana uwezo mkubwa wa kufanya chochote wanachotaka. Wengi huangalia nje na kukosa msaada. kama utaanza kuangalia ndani yako utapata msaada mkubwa kwako kufika unakotaka kufika.

TENGENEZA HADITHI YENYE NGUVU KWAKO.

Kila mmoja wetu kuna hadithi ambayo anaiishi, hadithi ambayo umekuwa unajiambia kila siku na imekuwa kikwazo kwako kupiga hatua. Kwa mfano kama umetokea familia masikini na huna elimu, hadithi yako inaweza kuwa kwamba wewe huwezi kufanikiwa kwa sababu umetoka familia masikini na huna elimu kubwa.
Lakini hadithi hiyo ni uongo, ni kweli unaweza kuwa umetoka familia masikini na huna elimu kubwa, lakini hicho siyo kinachokuzuia kufanikiwa. Wapo wengi waliotoka kwenye umasikini mkubwa kuliko wako na hata hawakupata elimu kabisa lakini wamefanikiwa.
Hivyo badili hadithi inayokuzuia kufanikiwa na tengeneza hadithi mpya ya mafanikio yako ambayo itakusukuma kufanikiwa zaidi. Hadithi yako ya mafanikio iguse yale maeneo ambayo una uimara na uyatumie kama sababu ya wewe kufanikiwa.
Hadithi yako mpya iwe ni kinyume kabisa na ile iliyouwa inakuzuia. Ukishaandika hadithi hii jiambie na kujikumbusha kila siku mpaka iwe sehemu ya fikra zako.

MSINGI MKUU WA MAFANIKIO YOTE.

Changamoto kubwa ya zama hizi ni kwamba kila mtu anakwenda kasi, lakini cha kushangaza hajui anakwenda wapi. Kila mtu yupo bize kila siku, anaamka asubuhi na mapema na kuchelewa kulala, lakini hajui wapi anayapeleka maisha yake.

Haijalishi unakwenda kiasi gani, kama hujui unakokwenda, kasi uliyonayo inakupoteza tu.

Msingi mkuu wa mafanikio yote ni kujua nini hasa ambacho unakitaka, kuwa na maono ya kile unachotaka kwenye maisha yako. Ukishajua kwa hakika nini unachotaka, hutasongwa tena na mambo ambayo siyo muhimu kwako.

Kama kila siku upo bize na huna muda wa kukamilisha mambo yako, ni dalili kwamba hujui unachotaka au hujui unakokwenda.

Anza kwa kujua nini hasa unachotaka, wapi hasa unakotaka kufika, kisha jua hatua zipi muhimu za kuchukua ili kufika unakotaka kufika, kisha puuza mengine yote ambayo hayachangii wewe kufika unakotaka kufika

Wednesday, January 30, 2019

UKIONA DALILI HII KATIKA MAHUSIANO JUA MAHUSIANO YANAELEKEA KUVUNJIKA.


Mara nyingi tumekuwa tunakaa kwenye mahusiano ambayo baadaye yanaishia kuvunjika bila ya sisi kujua nini kimepelekea mahusiano hayo kuvunjika.
 
Tunaona kama kila kitu kinakwenda vizuri mpaka pale changamoto zinapoanza kuonekana wazi kwenye mahusiano hayo na yanaishia kuvunjika.
 
Ni rahisi kuamini kwamba mahusiano yamevunjika ghafla na sababu haijulikani, lakini ukiwa mwangalifu na kufuatilia kila mahusiano uliyonayo, ni rahisi kuziona dalili za awali kabisa zinazoonesha mahusiano yanayoelekea kuvunjika.
 
Kuna dalili moja na ya awali ambayo inaonesha kwamba mahusiano uliyonayo na mtu yanaelekea kuvunjika. Na sababu inaweza kuwa wewe, mwingine au wote kwa pamoja.
 
Dalili hiyo moja muhimu ni kuhesabu yale ambayo umemfanyia mwingine na yeye hajakufanyia. Ukishaanza kuona kwenye mahusiano, wewe au mwingine anaanza kuhesabu mazuri aliyofanya ambayo mwingine hajayalipiza jua hayo mahusiano hayana tena muda mrefu.
 
Inapofikia kwenye mahusiano unafanya vitu kwa kuhesabu, basi huenda hufanyi kwa moyo mmoja au yule uliyenaye kwenye mahusiano hajali chochote unachofanya. Kwa vyovyote, mahusiano hayo hayataweza kudumu, na kama yataendelea changamoto zitakuwa nyingi.
 
Na hii ni kwa mahusiano yoyote yale, kuanzia mahusiano ya kimapenzi na ndoa, mahusiano ya kindugu na kirafiki na hata mahusiano ya kikazi na kibiashara.
 
Mkiishaanza kuhesabu nani kafanya nini na nani hajafanya nini, hapo mambo yameshaanza kwenda mrama.
 
Mahusiano bora na yenye afya ni yale ambayo kila aliyepo kwenye mahusiano hayo anakazana kufanya kilicho sahihi na bora kwa mwingine kwa sababu ndiyo amechagua kufanya na anajali. Na siyo pale ambapo mtu anafanya kwa sababu mwenzake kafanya au inabidi na yeye aonekane kafanya.
 
Boresha mahusiano yako kwa kufanya kile kilicho sahihi na kutokuhesabu, na kama upande wa pili haujali basi jenga mahusiano mengine bora na wale wanaojali zaidi.
 

Tuesday, January 29, 2019

JE, WEWE NI MJASIRIAMALI ? TAMBUA KUKABILIANA NA HOFU.

Wale wanaofanikiwa si kwamba ni watu ambao hawana hofu kabisa, ni watu ambao wana hofu kama wewe ila wanaamua kukabiliana na hofu zao hivyo hivyo pasipo kujali nini kinaendelea ndani mwao juu ya hofu hizo.
Hata wewe unaweza kukabiliana na hofu hizo hivyo hivyo kila siku. Kuna wakati utakutana na mambo yatakayokuwa  magumu kwako lakini unatakiwa kujifunza jinsi ya kukabaliana nayo na uatafika wakati utakuwa mshindi kweli.

JE , WEWE NI MJASIRIAMALI ? TAMBUA KUNA HALI HATARISHI.


Zipo hali hatarishi nyingi sana au ‘risk’ hasa pale unapochagua kuingia kwenye ulimwengu wa biashara. Hali hizi hatarishi unatakiuwa kupambana na kukabiliana pasipo na hofu yoyote kwani kwa kuzishinda huko ndiko unafanikiwa.
Kama umeamua kuingia kwenye biashara  au ujasiriamali na ukawa mwoga na hali hizi hatarishi basi utakuwa unapotea. Kwa kujua kuna hali hatarishi basi itakuwa ni njia sahihi ya namna ya wewe kuongozwa kwentye njia ya mafanikio ya ujasiriamali wako.

JE, WEWE NI MJASIRIAMALI ? TAMBUA JINSI YA KUKABILIANA NA HALI YOYOTE ILE.

Unapoingia kwenye biashatra na huku ukaingia na mawazo ya aina moja tu kwamba mimi naenda kupata, basi utakuwa unajiweka kwenye wakati mgumu sana. Kwa kuwa umechagua kuingia kwenye biashara ujie kabisa kuna kupata na kukosa.
Inapotokea umepata unashukuru Mungu, lakini inapotokea umekosa pia unashukuru Mungu kwa matokeo hayo na kuchukua uamuzi wa kusonga mbele. Usiingie kwa akili ya kupata moja kwa moja utapotea.