Sunday, January 6, 2019

JINSI UTAJIRI UNAVYOKUJA KWAKO.

 Utajiri unakuja kwako kwa njia ya thamani. Unapaswa kutoa thamani kubwa zaidi ya matumizi kuliko thamani ya fedha ambayo mtu anakupa. Ili kupata zaidi lazima uwe tayari kutoa zaidi.
 
Usiwalangue watu, wala usitumie mbinu kuwashawishi wanunue kitu ambacho hakitawasaidia. Wape watu kitu ambacho kitakuwa na msaada kwenye maisha yao na wewe utaweza kupata kile unachotaka.

USIWE MTU WA KULALAMIKA AU KUKOSA SHUKRANI.

Tumeona kwamba kuna mfumo wa fikra ambao unatupa kila ambacho tunakifikiri kwa muda mrefu. Njia pekee ya kushirikiana na mfumo huu ni kuwa na shukrani.
 
Kwa kushukuru, mfumo huu wa fikra unajua kwamba upo tayari kupokea zaidi na hivyo kukuwezesha kupata zaidi.
 
Usiwe mtu wa kulalamika au kukosa shukrani, mara zote shukuru na utaweza kupata zaidi. Shukuru kwa kidogo na utafungua milango ya kupata kikubwa zaidi.

NAMNA FULANI YA KUFIKIRI ILI KUVUTIA UTAJIRI.

 Hatua muhimu ya kupata kile unachotaka ni kujua kwa hakika nini hasa unachotaka. Huwezi kupata kile usichokijua, hivyo lazima ujue kwa undani kile unachotaka na kukifikiria kwa ukamilifu wake ndiyo uweze kukipata.

Unapaswa kutengeneza picha kwenye fikra yako ya kile unachotaka, kwa namna unavyokitaka kisha weka picha hii kwenye fikra zako mara nyingi. Kila unapokuwa na muda ambao huna kazi, tumia muda huo kufikiria picha hiyo na kujiona tayari umeshapata kile unachotaka.
Unapoifikiria picha ya kile unachotaka, unapaswa kuwa na imani kwamba tayari umeshakipata kwa namna unavyokitaka. Ona kama tayari unacho. Kwa njia hii, mfumo wa fikra unaoongoza dunia utakuwezesha kupata kile unachotaka.

JINSI YA KUTUMIA MATAKWA YAKO ILI KUVUTIA UTAJIRI.


Katika kutumia sayansi ya kupata utajiri, hupaswi kutumia matakwa yako kwa kitu chochote kilichopo nje yako. Usitumie nguvu ya matakwa yako kuwaendesha wengine kama unavyotaka wewe.


Sayansi ya kupata utajiri haitaki wewe uingilie maisha ya wengine, na pale unapofanya hivyo, kwa kutumia matakwa yako kuingilia maisha ya wengine, unaharibu mfumo mzima unaopaswa kutengeneza utajiri kwako. Kadiri unavyohangaika na ya wengine, ndivyo unavyopoteza ya kwako.



Tumia nguvu ya matakwa yako katika kufikiri na kutenda kwa namna ambayo itakuwezesha wewe kupata kile unachotaka. Na katika kuweka nguvu ya matakwa yako kwenye kupata utajiri, usijihusishe kwa namna yoyote na umasikini, usiufikirie umasikini, usitake kujua kwa nini watu ni masikini na wala usisome au kusikiliza vitu vinavyoeleza kuhusu umasikini. Ukatae umasikini kabisa na fikra zako zielekeze kwenye namna bora ya kufikiri ili kutengeneza utajiri.

PELEKA MAWAZO NA AKILI ZAKO ZOTE KWENYE UTAJIRI.

Huwezi kutengeneza na kutunza maono ya utajiri kama unahamisha mawazo yako kwenda kwenye picha inayokinzana mara kwa mara. Hupaswi kufikiria kitu kinachopingana na utajiri unaotaka kwenye maisha yako. Muda wako wote fikiria ile picha ya utajiri uliyojitengenezea.
 
Usizungumzie kuhusu umasikini uliokuwa nao au wazazi wako waliokuwa nao, usizungumzie kuhusu hali mbaya ya uchumi au mabaya yoyote yanayoendelea. Hata kama mambo ni magumu kiasi gani, hayo yanapita, hayadumu milele. Hivyo usiharibu fikra zako kwa kuyafikiria au kuyazungumzia.
 
Peleka mawazo na akili zako zote kwenye utajiri na ipe picha unayotaka kufikia na waache wengine wahangaike na hayo mengine.

NAMNA FULANI YA KUFIKIRI NA KUTENDA / KUCHUKUA HATUA ILI KUVUTIA UTAJIRI..

Fikra zina nguvu kubwa sana ya kuumba, pale unapofikiri kwa namna fulani, unatumia nguvu ya mfumo wa fikra unaoongoza dunia katika kukuletea kile unachotaka. Lakini kile unachotaka hakitatokea kwa muujiza, badala yake kitatokana na matendo na hatua unazochukua.
Ipo namna fulani ya kutenda ambayo inakuwezesha kupata kila unachotaka kwenye maisha yako. Na bila ya kuchukua hatua kwa namna fulani, hata kama ungekuwa na fikra bora kiasi gani, hazitaweza kuleta unachotaka.
Chochote unachokitaka sasa, kipo kwenye mikono ya wengine, na ili hao wengine wakupe hicho unachotaka, lazima wewe uwape kwanza kile wanachotaka. Hivyo lazima uwe na namna bora ya kuchukua hatua, namna inayoendana na fikra ulizonazo na kuchukua hatua ukiwa na imani na uhakika wa kupata unachotaka na utakipata.
Unapaswa kuchukua hatua sasa, kwa kuweka nguvu zako zote kwenye kile unachofanya kwa wakati huo, usifikirie kuhusu jana wala kesho, badala yake fikiria kuhusu kile unachofanya kwa wakati husika, hili litakuwezesha kufanya vizuri kile unachofanya.

CHUKUA HATUA ZENYE UFANISI ILI KUVUTIA UTAJIRI.

Kama pale ulipo sasa hapakuridhishi, kama unataka kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako na kwa kile unachofanya, unapaswa kukua zaidi ya pale ulipo sasa. Unapaswa kuijaza ile sehemu uliyopo sasa kiasi kwamba hakuna tena nafasi kwa ajili yako na hivyo inakubidi ukue zaidi.
 
Chochote unachofanya sasa kifanye kwa viwango vya juu sana kuliko ilivyozoeleka. Na unapofanya kwa viwango vya juu, mfumo wa fikra unaoendesha dunia utakupeleka kwenye hatua za juu kuliko hapo ulipo sasa.
 
Kila siku fanya kile unachopaswa kufanya bila ya kuahirisha, na kifanye kwa ufanisi mzuri. Usifanye kitu chochote kwa haraka au njia ya mkato. Mafanikio kwenye maisha ni kufanya vitu kwa ufanisi wa hali ya juu.
 
Kwa kila hatua unayochukua, kuwa na picha ya matokeo unayotaka kupata na fikiria picha hiyo mara zote. Hili litaweka fikra zako kwenye kile unachofanya na utaweza kupata matokeo bora.