Friday, January 4, 2019

EPUKA KAULI HII MWAKA MPYA 2019, " FEDHA SIYO KILA KITU " ILI UWE WA MAFANIKIO MAKUBWA KIFEDHA KWAKO.

Usemi huu ni maarufu sana kwa wengi, hasa masikini, kwamba usijisumbue sana na fedha kwa sababu fedha siyo kila kitu. Hii kauli siyo sahihi kwa asilimia 100, ni kweli kuna vitu muhimu kwenye maisha ambavyo tunavipata bura, kama hewa tunayopumua. Lakini ukiwa mgonjwa na huwezi kuvuta hewa mwenyewe, utauziwa hewa hiyo kwa bei ya juu sana.
Usitumie kauli hii ya fedha siyo kila kitu, kiri kwamba fedha ina mchango mkubwa sana kwenye maisha yako na kazana kuipata ili maisha yako yawe bora.
Vitu kama mahusiano yako na wengine unaweza kuona havihitaji fedha, lakini unapokuwa huna fedha ndiyo unagundua ni vigumu kiasi gani kuendesha mahusiano yako na wengine.

Tuesday, January 1, 2019

MAMBO 18 YA KUFANYA KILA SIKU ILI KUPATA MAFANIKO MAKUBWA SANA.

1. Amka asubuhi na mapema sana, angalau masaa mawili kabla ya muda wako wa kuanza kazi.


2. Unapoamka cha kwanza kufanya shukuru, kwa sala au tahajudi.


3. Andika malengo yako makubwa kila siku unapoamka, malengo ya mwaka, miaka 5, miaka 10 na hata miaka 50. Lazima uwe na malengo ya aina hii.


4. Ipangilie siku yako kabla hujaianza, weka vipaumbele vyako kwa siku husika, viwe kati ya 3 mpaka sita. Andika kabisa nini utafanya na kwa muda gani wa siku hiyo.


5. Soma kitabu au pata maarifa yoyote chanya na ya hamasa kabla hujaianza siku yako. soma angalau kurasa kumi za kitabu kila siku.


6. Fanya mazoezi ya viungo kabla ya kuianza siku yako, mazoezi bora kabisa ni kukimbia.


7. Epuka habari au kitu chochote hasi muda wa asubuhi. Usisikilize redio, wala kuangalia tv au kusoma magazeti.


8. Unapoingia kwenye kazi au biashara yako, fuata vipaumbele ulivyoweka vya kufanya kazi, na unapokamilisha jukumu weka alama ya vema kisha nenda kwenye jukumu jingine.


9. Fanya jambo moja kwa wakati, usifanye mambo mengi kwa wakati mmoja, unapoteza nguvu na umakini.


10. Unapofanya kazi, akili na mawazo yako yote yawe kwenye kile unachofanya, usiwe unafanya kazi huku unafikiria vitu vingine.


11. Kula kwa afya, punguza sana vyakula vya wanga na sukari, kula matunda na mbogamboga kwa wingi na kunywa maji mengi zaidi, angalau lita tatu kwa siku nzima.


12. Ondoka kwenye mitandao yote ya kijamii unayotumia kama haikuingizii fedha moja kwa moja. Sheria ya kutumia mitandao ya kijamii iwe hii, iwe inakuingizia fedha moja kwa moja. Kama hakuna fedha inayoingia kupitia mitandao hiyo, achana nayo mara moja.


13. Acha kabisa kutumia kilevi cha aina yoyote ile, kuanzia pombe, sigara, madawa ya kulevya na hata viburudisho kama kahawa.


14. Kwenye kila kipato unachoingiza, sehemu ya kumi ya kipato hicho usitumie kwa namna yoyote ile, hicho ni kipato ulichojilipa na utakitumia kwa kuwekeza kwa ajili ya baadaye.


15. Imarisha sana mahusiano yako na watu wote wa karibu kwako, kuanzia familia yako, ndugu, jamaa na marafiki na pia wale unaohusiana nao kwenye kazi au biashara.


16. Imalize siku yako kwa kutafakari yale uliyofanya, matokeo uliyopata, makosa au changamoto ulizokutana nazo na namna unavyoweza kufanya kwa ubora zaidi siku inayofuata.


17. Lala mapema ili uweze kuamka mapema, kama hufanyi kazi za usiku, saa nne inapaswa kukukuta kitandani ukiwa umeshalala.


18. Tumia neno HAPANA mara nyingi uwezavyo, neno hapana ndiyo litakupa uhuru wako. Kama kitu hakikuwezeshi kufika kule unakotaka kufika, sema hapana bila ya kuona aibu.
Ndimi  MWL  JAPHET   MASATU, DAR  ES  SALAAM , TANZANIA.
MOBILE  PHONE: WhatsApp +255 716924136 / +255 755400128 /   +255 688 361 539
EMAIL: japhetmasatu@gmail.com
 

Tuesday, December 25, 2018

WEKA MALENGO YAKO MWEZI DISEMBA KABLA MWAKA HAUJAANZA.

Watu wengi wanakosea kuweka malengo kwa sababu wanayaweka kipindi ambacho siyo sahihi. Wakati wa mwaka mpya, watu wengi huwa wanakuwa na hisia kali za upya wa mwaka na kwa kuwa kila mtu anasema mwaka mpya mambo mapya, basi na wao wanajiunga na msafara huo.
Wengi wanajikuta wanaweka malengo ambayo siyo yao, wanapoona wengine wameweka malengo fulani basi na wao wanaona wanapaswa kuwa na malengo ya aina hiyo. Kitu kinachowapelekea kushindwa sana kwenye maisha yao.

Wakati sahihi wa kuyaweka malengo yako kwa mwaka mpya ni kabla mwaka haujaanza. Hivyo mwezi huu wa disemba, tenga muda na ukae chini ili kuweka malengo yako kwa mwaka unaofuata. Kupitia tafakari ya mwezi ulioisha uliyofanya, kupitia vipaumbele vya mwaka ulivyojiwekea, unaweza kuweka malengo ambayo ni bora sana kwako.

Weka malengo yako ya mwaka mpya mwezi disemba na wakati wengine wanakimbizana na malengo mwanzo wa mwaka, wewe unakuwa upo kwenye utekelezaji.

HERI  YA   X--MASS  NA  MWAKA  MPYA.

WEKA VIPAUMBELE ( PRIORITES ) MWEZI DISEMBA VYA MWAKA UNAOFUATA.

Kabla hujaweka malengo yoyote, anza kwanza na vipaumbele. Watu wengi wanakosea kwenye kuweka malengo kwa sababu hawajui na pia hawana vipaumbele kwenye maisha yao. Hilo linawapelekea kuweka malengo ambayo hata hawajui wanayafikiaje, kwa sababu yanakuwa hayaendani na hayajapangiliwa vizuri.

Chagua vipaumbele vichache kwa mwaka unaofuata, angalia yale maeneo ambayo ni ya muhimu zaidi kwenye maisha yako, ambayo ukiyasimamia vizuri na kuyafanyia kazi, utaweza kupata matokeo bora sana kwenye maisha yako.
Kwa kujua vipaumbele vyako, utaweza kuweka malengo ambayo ni sahihi kwako na yanafikika.

HERI  YA  X--MASS NA  MWAKA  MPYA.

KUWA MAKINI NA MSIMU WA SIKUKUU USIKUACHE MWEUPE PEPEEE !!

Mwezi disemba ni mwezi ambao huwa kuna sikukuu nyingi, ni mwezi ambao wengi wana mategemeo makubwa ya kupumzika na kusherekea. Lakini unapaswa kuwa makini sana na kipindi cha sikukuu kwa sababu wengi hujisahau na kuuanza mwaka wakiwa kwenye madeni makubwa.

Hakikisha unajiwekea bajeti ya matumizi yako kwenye msimu wa sikukuu, na usizidishe kabisa bajeti hiyo. Hakikisha unaamua mapema kabisa ni vitu gani utagharamia kwenye msimu huo wa sikukuu na vipi utaachana navyo.

Na kama kuna sherehe ambazo hazina ulazima, zisikuumize kichwa, achana nazo. Hakuna utakachokikosa kwa kuachana na baadhi ya sherehe na mapumziko. Pia kama utaanza kufanyia kazi malengo yako mapema, utakuwa bize kupiga hatua na sikukuu hazitakuwa na madhara kwako.

HERI  YA  X--MASS  NA  MWAKA  MPYA.

UTAFAKARI MWAKA UNAOKWENDA KUUMALIZA.

Watu wengi huwa wanauanza mwaka kwa matumaini makubwa, wanaweka malengo makubwa lakini huwa hayamalizi mwezi, wanaachana nayo na kurudi kwenye maisha ya kawaida.

Unapofika mwezi disemba ni wakati mzuri wa kuutafakari mwaka unaokwenda kuumaliza, kuangalia yale malengo na mipango uliyojiwekea na pia kuangalia kwa kiasi gani umeweza kutekeleza.

Kwa yale malengo uliyoachana nayo, jua tatizo ni nini, uliyaweka vibaya au uvivu na uzembe wako ndiyo umekufanya uachane nayo?
Angalia pia fursa mbalimbali ulizokutana nazo kwenye mwaka wako mzima, zile ulizofanyia kazi na zile zilizokupita.

Kwa kuutafakari mwaka unaokwenda kuumaliza, utaweza kuona wapi umefanya vizuri, wapi umekosea na marekebisho yapi ya kufanya.

HERI  YA  X--MASS  NA  MWAKA MPYA.

JIKUMBUSHE KUSUDI LA MAISHA YAKO MWEZI DISEMBA.

Kwa kelele za dunia ni mihangaiko yetu ya kila siku ni rahisi sana kusahau kusudi la maisha yako. Na ukishasahau kusudi la maisha yako, huna tofauti na meli ambayo haina uelekeo. Unaweza kwenda kasi sana, lakini haitakusaidia, kwa sababu unakuwa tayari umeshapotea.

Unapofika mwisho wa mwaka jikumbushe kusudi la maisha yako, jikumbushe kwa nini upo hapa duniani, jikumbushe nini kinakusukuma kutoka kitandani kila asubuhi.

Kusudi la maisha yako ndiyo linapaswa kukupa msukumo wa kufanya makubwa. Na unapolikumbuka mara zote, linakuwezesha kuchukua hatua sahihi ili kuweza kulitimiza.
Jikumbushe kusudi la maisha yako na jiulize yale unayofanya yanachangiaje kwenye kufikia kusudi la maisha yako.

HERI  YA  KRISMASI  NA  MWAKA  MPYA !