Wednesday, December 5, 2018

TEGEMEA NGUVU ZAKO NA SIYO HURUMA ZA WENGINE.

Kwenye MAISHA, kwa chochote unachochagua kufanya basi unapaswa kutegemea zaidi nguvu zako, uimara wako na siyo kutegemea huruma za wengine. Kila unapoanza kutegemea huruma za wengine, ndipo unapoingia kwenye shimo zaidi na kukosa uhuru wako.
 
Kila unapokuwa unategemea wengine wafanye kitu ndiyo wewe uweze kupata unachotaka, utajikuta unakosa uhuru wa kuishi maisha yako kwa namna unavyotaka wewe.
 
Kwa sababu yeyote yule unayemtegemea sana, ambaye huwezi kupiga hatua fulani bila yeye, anageuka na kuwa kikwazo kwako, kwa sababu asipofanya kama unavyotegemea, basi wewe hutaweza kupata kile unachotaka kupata.
 
Unapaswa kuyatengeneza maisha yako kwenye msingi huu wa KUJITEGEMEA binafsi kwenye mambo mengi ya maisha yako, kujua namna ya kutumia uwezo mkubwa uliopo ndani yako na kutoruhusu mtu mmoja au watu wachache wawe na maamuzi ambayo yanaweza kuathiri sana maisha yako.
 
Kama maisha yako yanategemea sana maamuzi ya mtu mmoja au watu wachache, utakosa uhuru mkubwa kwenye maisha yako, kwa sababu hata kama mtu huyo hakusumbui, bado ndani yako utakosa amani, kwa sababu hujui ni namna gani mtu huyo anaweza kubadilika siku za mbeleni.
 
Maisha ya uhuru kamili, maisha ya kupata kile unachotaka ni kuweza kutumia uwezo wako mkubwa, kutengeneza maisha ambayo hayana utegemezi mkubwa kwa mtu mmoja au watu wachache. Hilo linajumuisha hata wewe binafsi.
 
Kwa mfano kama kipato chako kinategemea wewe ufanye kazi, bado hujawa huru, kama huwezi kuingiza kipato hata kama wewe hufanyi kazi, unaendelea kuwa mfungwa kwenye upande wa kipato. Lazima uwe na mfumo huru unaoweza kutengeneza kipato iwe unafanya kazi au la.
 
Una uwezo mkubwa sana ndani yako, una nguvu kubwa sana ambazo kama utaanza kuzitumia, utayabadili sana maisha yako, utawafanya wengine wakutegemee wewe zaidi kuliko unavyowategemea wao. Na kadiri wengi wanavyokutegemea wewe, ndivyo unavyokuwa huru zaidi.
 
Na hili ni zuri na muhimu sana kwa wale watu ambao wanapenda kufanya kazi zao za ajira, lakini wanapenda kuwa huru. Kwa mfano mtu anaweza kuwa anapenda kufanya kazi fulani, lakini ataifanya vizuri kama atakuwa ameajiriwa sehemu fulani. Kwa mtu huyu kutumia vizuri uwezo wake mkubwa na nguvu zake, anajitengenezea hali ya kutegemewa kwenye kile anachofanya, kitu ambacho kinamfanya aheshimiwe na kuwa na uhuru zaidi kuliko wale ambao hawategemewi na badala yake wanategemea zaidi kazi wanayofanya

PATA MUDA WA KUKAA MWENYEWE KWENYE CHUMBA KWA UTULIVU. USIJIOGOPE WEWE MWENYEWE.

Mwanasayansi na hisabati Blaise Pascal aliwahi kusema matatizo yote ya binadamu yanatokana na mtu kushindwa kukaa mwenyewe kwenye chumba kwa utulivu.
 
Na hili ni sahihi kabisa, kinachowafanya watu wengi kuingia kwenye matatizo mbalimbali, ni kushindwa kutulia na mawazo yao, kukosa ujasiri wa kukaa na kutafakari chochote walichonacho kwenye mawazo yao.
 
Mimi nakwenda mbali na kusema kwamba watu wengi tunajiogopa sisi wenyewe. Ndiyo maana tukikutana na upweke tu tunakimbia haraka sana.
 
Kama unabisha jiangalie tu tabia yako, huwa unafanya nini pale unapojikuta upo mwenyewe. Lazima utatafuta kitu cha kuchukua muda wako na kushika mawazo yako. Labda utaanza kuchezea simu, utaanza kusoma kitu au hata kuwatafuta watu ambao hukuwa umepanga kuwatafuta.
 
Yote hayo ni kuepuka tu kuwa peke yako, upweke umekuwa hofu kubwa kwetu, hatutaki kabisa kukaa wenyewe, tukiwa tumeachwa na fikra zetu.
 
Rafiki, hebu acha kujiogopa, hebu rudisha urafiki kwako binafsi. Unapopata nafasi ya kuwa na upweke, itumie hiyo kuyatafakari maisha yako, itumie hiyo kujijengea taswira ya kule unakoenda.
 
Usijiogope na kukimbia kila unapojikuta mpweke, badala yake tumia nafasi hiyo kujenga urafiki na wewe binafsi na hata kujijua zaidi na kujua kwa kina kule unakokwenda.

Friday, November 30, 2018

SAFARI YA MAFANIKIO INAANZA NA WATU WENGI SANA. WENGI HUISHIA NJIANI, KWANINI ??


Watu wengi wanakata tamaa kwenye safari ya mafanikio kwa sababu ya kutokujua kwamba mafanikioo yanataka muda mrefu. Katika kipindi cha kutafuta mafanikio yako unatakiwa ujitoe hasa, kuvumilia na kutoa kila ulichonacho hadi ufanikiwe.
Kwa mfano, ilichukua muda wa miaka 11 hadi program ya ‘Microsoft’ ya bilionea mkubwa duniani kuanza kufanya kazi na kuleta mafanikio makubwa. Mafanikio yake hayakutokea tu ghafla kuna miaka ilikataika hapa katikati.
Pia ilimchukua miaka 29 kwa Abraham Lincoln hadi kuweza kuwa Rais wa marekani. Ipo mifano mingi inayoonyesha kwamba mafanikio si kitu cha mara moja tu, unatakiwa kuwekeza muda ili uweze kufanikiwa kwenye mafanikio hayo uyatakayo.
Kwenye akili yako sasa weka wazi, mafanikio ni safari ya muda mrefu. Unatakiwa kabisa utenge miaka angalau kuanzia 5 hadi 15 ya kutafafuta mafanikio yako ya kweli na ya kudumu. Ukikurupuka na kutaka mafanikio ya chapu chapu utakwama.
Kama utakuwa ni mtu wa kutaka mafanikio na halafu ukategemea mafanikio hayo yakatokea ghafla ghafla kwa muda mchache ni rahisi sana kwako kuweza kukata tamaa na kuona ni kitu ambacho hakiwezekani au mafanikio ni ya watu wa aina fulani tu lakini si wewe.

JIWEKEE MUDA WA UKOMO KWA CHOCHOTE UNACHOPANGA KUFANYA.

Mtu mmoja amewahi kusema kwamba jukumu huwa linachukua muda uliopangwa lifanyike. Akimaanisha kama kuna jukumu ambalo linapaswa kufanywa kwa masaa mawili, litakamilika ndani ya masaa mawili. Jukumu hilo hilo likipangwa kufanyika ndani ya masaa matano, litachukua masaa matano.
Huwa tunasukumwa kufanya zaidi pale ambapo muda unakuwa mdogo, na tunaahirisha mambo pale muda unapokuwa mwingi. Ndivyo maana wanafunzi ni vigumu sana kusoma siku za kawaida, lakini mtihani unapokaribia, hamasa ya kusoma inakuwa juu.
Jiwekee muda wa ukomo kwa chochote unachopanga kufanya, na muda huo uwe mfupi kuliko muda uliozoeleka. Kwa kuwa na muda huu na kuufuata, utaweza kujisukuma kufanya zaidi. Kadiri unavyokuwa na muda mfupi wa kutekeleza jambo, ndivyo mawazo ya kuahirisha yanavyopotea kwenye akili yako. Waahidi watu kwamba jukumu litakamilika mapema kuliko kawaida, na tekeleza hilo uliloahidi.

KUWA NA MAMBO YAKO MATANO KWA SIKU AMBAYO UTAYATEKELEZA.

Kila siku unayoianza, ainisha mambo matano muhimu ambayo ukiyafanya siku hiyo yatakusogeza karibu na mafanikio unayotaka kuyafikia. Mambo hayo matano unapaswa kuyafanyia kazi bila ya kujali mazingira yapoje. Inyeshe mvua au liwake jua, hayo matano ni muhimu kwa siku yako na unapaswa kuyafanyia kazi.
Kwa kuwa na tano za siku, unajiweka kwenye nafasi ya kutekeleza yale muhimu na kuepuka kupotezwa na kelele ambazo zimekuzunguka kila mahali.

TUMEZOEA KUSIMAMIWA : KUWA NA MTU WA KUKUSIMAMIA.

Sisi binadamu ni wabaya sana kwenye kujisimamia wenyewe, huwa tunajionea sana huruma na ni rahisi sana kujidanganya. Unaweza kuwa na orodha yako ya siku, umepanga mambo yako matano muhimu na hata kujiwekea ukomo. Lakini katikati ya siku yako ukawa hujisikii kuendelea na yale uliyopanga, ni rahisi kujihalalishia kwamba labda umechoka au ni kitu hakiwezekani.
Lakini unapokuwa na mtu wa pembeni, mtu ambaye jukumu lake ni kuhakikisha umekamilisha uliyopanga na hapokei sababu bali matokeo, utalazimika kufanya kile ulichopanga kufanya.
Tafuta mtu wa karibu kwako, ambaye hakuonei huruma kisha mtake akusimamie kwa karibu ili utimize unachotaka. Kama huwezi kupata mtu wa karibu basi kuwa na kocha au menta ambaye atakusimamia kwa karibu.

JIAMBIE HIVI " NAFANYA SASA , MUDA HUU ".

Kuna wakati unakuwa umeshapanga kabisa nini utafanya na kwa wakati gani. Lakini inapofika muda wa kufanya, mawazo ya kuahirisha yanaanza kukuingia. Unaanza kuona labda hujawa tayari au ni bora kusubiri.
Ni katika wakati kama  huu ndiyo unapaswa kujiambia kauli hii, NAFANYA SASA HIVI, rudia kauli hiyo mara nyingi uwezavyo na utajikuta umeanza kufanya. Kila unapofikiria kuahirisha kufanya kitu, jiambie kauli hiyo kwamba unafanya. Kila unapoanza kujiambia kwambe umechoka, anza kujiambia kauli hiyo.
Kwa kurudia rudia kujiambia kauli hiyo, unaanza kuiamini na kujiamini wewe mwenyewe na kuanza kufanya.